Mjadala wa wadau wa Demokrasia: Lipumba asema Demokrasia iliporomoka sana awamu ya tano

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
1692694626547.jpeg


Mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji 2024 na uchaguzi mkuu 2025
===
Demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania ilianzishwa mwezi Julai 1992. Tangu wakati huo, serikali imejitahidi kukuza utawala wa kidemokrasia kupitia marekebisho ya kisheria na mikataba ya kukuza demokrasia. Hata hivyo, kuna changamoto za kidemokrasia.

Kuna makubaliano kati ya wadau wa kisiasa juu ya umuhimu wa kufanyia marekebisho Katiba ya 1977, Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Uchaguzi, na masuala ya vyombo vya habari na ushiriki wa kijinsia. Hatua zimechukuliwa kuanzisha Katiba mpya, lakini mchakato ulisitishwa mwaka 2014. Mikutano ya kisiasa ilipigwa marufuku kati ya 2016 na 2023.

Hata hivyo, mwaka 2022, Rais Samia Suluhu alianzisha Kikosi Kazi kwa ajili ya marekebisho ya kidemokrasia. Kufuatia ripoti ya kikosi hicho, marufuku ya mikutano ya kisiasa iliondolewa na kuanzia Januari 3, 2023. Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa yaliongezwa kwenye ajenda, na mkutano uliitishwa kuandaa marekebisho.

Hali ya sasa inahitaji mazungumzo ya kitaifa kuimarisha makubaliano ya kitaifa. Ingawa wadau wanaweza kutofautiana katika mitazamo, wanaweza kukubaliana kuhusu maslahi ya kitaifa. TCD inaendesha mkutano wa wadau kujadili demokrasia na uchaguzi, kufuatia juhudi za Rais Samia. Mkutano utafanyika Agosti 2023.

Mkutano wa awali wa TCD ulijadili marekebisho ya uchaguzi, matokeo yake yalipendekeza marekebisho ya Sheria za Uchaguzi na Vyama vya Siasa, na kuimarisha ushirikiano wa vyama vya siasa. Mkakati wa kudumisha amani ya kisiasa ulijadiliwa pia.

Mkutano wa wadau wa kitaifa utalenga kukuza demokrasia katika nchi. Malengo yake ni kujenga jukwaa la mazungumzo, kujadili mafanikio na changamoto za demokrasia, kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa awali, na kutoa mapendekezo kwa mustakabali. Washiriki watakuwa viongozi wa vyama vya siasa, wanazuoni, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wadau wengine.

Mkutano huu ni wa siku mbili na wazungumzaji wa siku ya kwanza ni pamoja na
Prof. Ibrahim Lipumba, na Jaji Francis Mutung, msajili mkuu wa vyama vya siasa

Uchaguzi wa serikali za mtaa 2019
Uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika 2019 umeshuhudia vyama kadhaa vya upinzani vikijitoa, hatua inayoweka swali la demokrasia nchini. Vyama vya upinzani vililalamika dhidi ya chama tawala, CCM, kwa madai ya kuvuruga uchaguzi. Vyama kama Chadema, ACT-Wazalendo, CUF, na wengine walijitenga na uchaguzi huo, wakidai kwamba mazingira yasiyofaa yameundwa na CCM.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, uchaguzi wa serikali za mitaa ni msingi wa demokrasia na uwajibikaji wa serikali kwa wananchi. Lakini vyama vya upinzani vilibainisha kuwa wasimamizi wa uchaguzi wameondoa wagombea wengi bila sababu za msingi, na hivyo kudhoofisha mchakato wa kidemokrasia.

Waziri aliyekuwa anasimamia uchaguzi huo, Seleman Jaffo, alijaribu kuvuta upinzani kuendelea na uchaguzi huo, lakini juhudi hizo hazikufua dafu. Vyama vya upinzani vinasisitiza kwamba hawawezi kushiriki katika uchaguzi ambao hauna uwazi na haki.


Aliyozungumza Prof Lipumba
Demokrasia ni adili la vyama vyote, Lipumba amesema hayo akimnukuu mchumi Amartya Sen aliyesema Democracy is universal value, ambapo amesema hata Mwl Nyerere anatambua umuhimu wa demokrasia na kasoro zilizokuwepo ni kutowapa wanawake haki ya kupiga kura.

Msaada wa nchi za nje katika kukuza demokrasia sio katika kukuza utamaduni wa nje bali kukuza ushirikiano wa kidiplomasia. Lipumba ametoa wito kwa balozi zote kushirikiana na TCD katika kukuza demokrasia nchini huku wakihifadhi mazingira. Aidha amesema katika mkutano huu, mgeni rasmi atakuwa Rais Hussein Mwinyi ambaye atahudhuri amkutano huu siku ya pili ya mkutano huu ambayo ni August 23.

Lipumba amesema mwaka huu tunaazimisha miaka 75 ya kuazimisha Universal Declaration of human Rights, kifungu cha kwanza cha tamko la haki za binadamu kitambua usawa wa watu, na kifungu cha 20 kinatambua haki ya kila mwananchi kushiriki katika mambo ya nchi yake na serikali.

Lipumba amesema tamko la haki za binadamu la ulimwengu ndio chimbuko la ahadi za TANU na chimbuko la imani ya TANU ambayo imetokana na tafsiri ambayo mwl Nyerere aliifanya kwa Universal Declaration of human Rights ambayo aliiandika kwa kiswahili ili kueleweka.

Lipumba amemsifu Nyerere kuwa alikuwa ni muumini wa demokrasia ambapo baada ya uhuru ilibidi apambane na changamoto za ujenzi wa taifa. Hata hivyo suala la kama Nyerere alitumia demokrasia ni mjadala mwingine.

DEMOKRASIA ILIPOROMOKA AWAMU YA TANO
Tanzania inakabiliwa na changamoto mbili, kujenga uchumi na kujenga misingi imara ya kidemokrasia. Lipumba amesema hadi sasa Tanzania haijafanikiwa kujenga demokrasia ya kweli, amesema demokrasia iliporomoka sana katika awamu ya tano, ambapo ametolea mfano wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019.

Aidha amesema uchaguzi mkuu wa 2020 haukuonesha hali nzuri ya demokrasia. Katika uchaguzi wa 2020 vyama vya upinzani vilipata viti 8 ambapo Tanzania bara vilipata wabunge 2 katika viti 264 hali ambayo mwanzo haikuwa hivyo. Aidha Kilimanjaro haikuwahi kuwa na mbunge wa CCM lakini mwaka 2020 ilipata mbunge wa CCM. Hivyo amesema 2020 ilikuwa Tsunami, na hali ile haikuwa njema.
1692694742116.jpeg

Mjadala wa Kwanza
Moderator:
Deus Kibamba
Wazungumzaji:
NCCR-Mageuzi - Joseph Selasini
ACT-Wazalendo - Juma Duni Hajji
CUF - Maftah Machuma
CHAUMMA - Hashim Rungwe
CHADEMA - John Mnyika
CCM - Abdulrahman Kinana


Swali linalojadiliwa: Tathmini ya hali ya demokrasia nchini. Je demokrasia imekuwa?

Aliyozungumza Joseph Selasini
Demokrasia inashuka kwa sababu tunakwenda kwenye uchaguzi unaosimamiwa na upande mmoja. Uchaguzi wa sasa unasimamiwa na watendaji wa serikali, na sio watu wa serikali tu bali ni kada wa chama fulani.

Kwa sasa tunaenda kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, wangapi tunajua kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa hauna sheria bali unasimamiwa na TAMISEMI ambaye pia ni mchezaji.

Bahati nzuri tuna maandiko mengi kama ya Jaji Nyalali, Jaji Kisanga hapa inabidi kujua tunaingiaje kwenye demokrasia. Kwanza cha kujua kuwa na uchaguzi sio sawa na kuwa na demokrasia, kwenye uchaguzi tunapigwa na polisi tunafukuzwa na polisi.

Kwa hiyo swali la kama tumefanikiwa kidemokrasia, jibu langu ni kuwa hatujafanikiwa, kwanza tunarudi nyuma. Hatuwezi kuingia kwenye uchaguzi wakati vyama vingine vina mabilioni, vingine vina mamilioni na vingine havina pesa. Kuna vyama havina hata ofisi, hawana hata fedha ya kufika Kibaha kutangaza sera zao.

Kuna watanzania wengi ambao ni viongozi ila hawana uwezo wa kuingia kwenye uchaguzi. Wengi hawawezi kuomba uongozi kwa sababu kwa sasa kuomba uongozi kinaonekana ni kitu cha mtu mwenye fedha nyingi au chama chenye uwezo mkubwa wa kifedha.

Aliyozungumza Juma Duni Hajji
Tumeshafanya Uchaguzi mara kwa mara, ukiniuliza kama tuna demokrasia nitakuambia tuna demokrasia ndooogo. Tatizo tulilonalo, demokrasia inasimamiwa na dola, na kama CCM ingesimama kama CCM na wao wangelalamika kama sisi. Amesema sheria zinatunga na dola.

Amemnukuu tena Amartya Sen kuwa ili kuwa na demokrasia lazima watu wawe huru na wawe huru, pia serikali inayotawala iwe serikali ya watu iliyochaguliwa na watu kwa ajili ya watu, na suala la tatu kuwe na taasisi inayolinda haya mawili ya awali. Hapo hatujafika, hatujawaha huru kuchagua serikali tuitakayo.

Sheria tumetunga wenyewe, katiba tumetunga wenyewe hatuzifuati, matokeo yake tunafanya uchaguzi na wanajeshi wanaingia mitaa. Kama tunataka demokrasia vile tulivyotunga kwenye sheria zetu tuvifuate. Sheria za uchaguzi na polisi zibadilishwe ziwe zile zinazotulinda na kuilinda demokrasia yetu na sio hivi vilivyo hivi sasa.

Aliyozungumza Maftaha Machuma
Kimsingi hali ya kidemokrasia nchini ni mbaya sana. Alipokuwa akizungumza mwenyekiti (Lipumba) kuwa alivyoingia Magufuli hali ilikuwa vibaya zaidi. Mimi nilikuwa mbunge mwaka 2015 hadi 2020 lakini kilichotokea 2020 sio cha kuzungumza katika ukumbi huu. Vyombo vya kusimamia uchaguzi vilitumika au kwa maamuzi yao kuharibu uchaguzi. Kamati za ulinzi na usalama, zilifanya kazi kubwa ya kuharibu uchaguzi ambao upo kwa mujibu wa sheria. Vyombo vya ulinzi na usalama vilitumika kupanga matokeo ya uchaguzi. Bahati ,baya zaidi vyombo vyetu ambavyo vinasimamia uchaguzi vinatokana na watu ambao wameteuliwa na rais, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Hivyo kama tusiporekebisha mfumo huu, upinzani Tanzania haitaweza kushika hatamu ya uchaguzi. Kama tusipobadili mfumo huu, hii nchi inaelekea kubaya.

Nikizungumza hali inayoendelea, Rais Samia alikuja na maneno mengi ya matumaini. Mambo haya yamezungumzwa sana na viongozi wa ngazi za juu. Tumekutana na serikali na rais na tumeambiwa mambo mengi kuhusu demokrasia, lakini yanayozungumzwa juu na yanayofanyika chini ni vitu viwili tofauti. Mfano mwaka 2020 watu walipiga kura mara mbili hadi tatu. Mtu anapiga kura kituo kimoja na anasindikizwa na vyombo vya usalama kupiga kura kituo kingine. Na ilizungumzwa wazi kwamba hatutakuogopa.

Maftaha amesema CCM wanazunguka mitaani kukusanya vitambulisho vya wapiga kura wakijiandaa na uchaguzi unaofuata. Na wasimamizi wanasema hayo yaliyozungumzwa na viongozi wa juu hayajawafikia kwa kuwa hawajapokea waraka kutoka kwa viongozi wa juu.

Aliyozungumza Mnyika
Ili nchi ielekee kwenye mkondo wa kidemokrasia lazima kuandika katiba mpya kwa sababu katiba ya mwaka 1977 iliundwa kwa chama kimoja, chama dola. Hii ilipendekezwa katika mazungumzo ya awali ya tangu mwaka 1991 hali ya kutathmini hali ya kidemokrasia. Hivyo mimi nizungumzie mkwamo tulio nao,

Kwanza tumechelewa tangu mwaka 2021 kuweka misingi ya Uchaguzi huru, na tumechelewa hadi sasa, Rais aliahidi kuunda kamati ya kuendeleza mchakato wa katiba mpya lakini hadi sasa tumekwama hakuna kamati hiyo. Mkondo uliopo ni kupitia tena mapendekezo ya mwaka 1991, mchakato uliopangwa kufanyika mwezi Septemba, mimi niseme huku ni kurudishana nyuma kwa kuwa maoni yapo tayari. Hivyo ni muhimu kuendeleza mchakato wa katiba ambao umeshafanyika.

Kama taifa tujielekeze kwenye kuharakisha kupeleka bungeni muswada wa bungeni wa katiba mpya. Na hiyo bajeti ya Tsh bilioni 9 iliyoelekezwa kutoa elimu kuhusu katiba iliyopo ingeelekezwa katika mchakato wa kupata katiba mpya.

Mimi rai yangu ni kuwa tutoke kwenye kujadili tulikotoka, tutoke kwenye kujadili matatizo tuliyonayo, tujadili ufumbuzi wa matatizo tuliyonayo. Matatizo tuliyonayo yanafahamika, tujikite kwenye kupata ufumbuzi.

Ukiuliza kuhusu uhuru wa kuzungumza tuwaulize waliokamatwa na kutaka kupewa kesi ya uhaini watakwambia uhuru wa kuzungumza tuko nao ila uhuru wa kuwa huru baada ya kuzungumza.

JOHN MNYIKA: TSH. BILIONI 9 ZA KUTOA ELIMU KUHUSU KATIBA ILIYOPO IELEKEZWE KATIKA MCHAKATO WA KATIBA MPYA

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA amesema, "Kama taifa tujielekeze kwenye kuharakisha kupeleka Bungeni Muswada wa Bungeni wa Katiba Mpya. Na hiyo bajeti ya Tsh bilioni 9 iliyoelekezwa kutoa elimu kuhusu katiba iliyopo ingeelekezwa katika Mchakato wa kupata katiba mpya

Ameongeza,"Mimi rai yangu ni kuwa tutoke kwenye kujadili tulikotoka, tutoke kwenye kujadili matatizo tuliyonayo, tujadili ufumbuzi wa matatizo tuliyonayo. Matatizo tuliyonayo yanafahamika, tujikite kwenye kupata ufumbuzi

Akizungumzia Uhuru wa Kujieleza amesema, "Ukiuliza kuhusu Uhuru wa kuzungumza tuwaulize waliokamatwa na kutaka kupewa kesi ya Uhaini watakwambia Uhuru wa kuzungumza tuko nao ila uhuru wa kuwa huru baada ya kuzungumza"

Aliyozungumza Kinana
Ukiniuliza kama demokrasia imekuwa, nitasema ukifananisha na miaka kadhaa iliyopita demokrasia imekua. Kwanza kwa kuangalia uwakilishi. Je kuna mapungufu? Nakiri kuwa kuna mapungufu katika sheria na kusimamia sheria wakati wa uchaguzi. Uhuru wa kusema kama upo? Mimi nasema upo lakini kila uhuru una mipaka yake. Uhuru bila nidhamu ni wendawazimu, nidhamu bila uhuru ni utumwa.

Kuna hili jambo la katiba, umuhimu wa kuwepo kwa katiba na katiba mpya. Kumekuwa na tume nyingi ikiwa katika juhudi ya kuwa na katiba nzuri kuwafanya watanzania kushiriki kwa uhuru zaidi. Baadhi ya mambo ya tume hizi yametekelezwa na baadhi hayajatekelezwa. Lakini katika awamu hii niseme baadhi ya mambo yameanza kufanyiwa kazi.

Rais Samia ameshazungumza namna ambavyo serikali yake imejipanga kuwa na katiba, ambapo kutakuwa na michakato miwili ambapo katika michakato hiyo mmoja wapo ni kurekebisha mchakato wa katiba, ambapo kutakuwa na marekebisho ya sheria ya tume ya uchaguzi, sheria ya uchaguzi na sheria ya namna vyama vya siasa vitakavyosimamiwa. Nina hakika tutakuwa na uchaguzi huru na wa haki kwa miaka inayofuata ikiwa mapendekezo ya sheria hizi yatapelekwa bungeni.

Demokrasia imekuwa, kwa kuangalia idadi ya wawakilishi wa vyama walivyokuwa wanaongezeka katika bunge. Japo kuna kasoro, lakini dhamira ya kurekebisha sheria hizi ipo hivyo kutakuwa na uchaguzi huru na haki mwaka 2024/25.

Siamini kwamba ili katiba ibadilike lazima sheria ya uchaguzi ibadilike. Siamini! Tunaweza kubadili sheria ya uchaguzi bila kubadili katiba. Sheria itakayopigiwa kura na bunge inaweza kufuta yaliyoandikwa kwenye katiba.

1692695663709.jpeg


Aliyozungumza Hashimu Rungwe
Jamani mimi nimepewa nafasi tena ya kuzungumza na ninyi. Wananchi wanataka mtu aongee akiwa huru na sio mtu akiongea akadhibitiwa. Sasa uhuru wa uchaguzi unategemea na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, sasa bila kurekebisha hizi sheria hakutakuwa na uchaguzi.

Tunasikia hii katiba iliunda na watu wawili kina Pius Msekwa.Pia uchaguzi wa serikali za mitaa unasimamiwa na TAMISEMI ambayo lazima wataipendelea serikali kwa kuwa wanalinda ugali wao. Hivyo tunapaswa kuunda tume ambayo haitakuwa na uhusiano na serikali. Wasiwe watu wanaotegemea kuteuliwa katika nafasi zozote katika serikali.Yaani kuanzia mwanzo tume inachagua watu ambao inajua hawana uhusiano na serikali, sio kwa kujuana.

Ili kusiwe na lawama, lazima tuteue chombo kingine kitakachosimamia na kiwe huru kwelikweli, mimi nafikiri wananchi wanataka tume huru ya Uchaguzi. Nilikuwa Zambia kwenye uchaguzi ilikuwa ni tume huru, kule Polisi anakaa mbali sio aje karibu na kujihusisha na uchaguzi.Tupate tume huru ambayo haipati amri kutoka serikalini au CCM.

Polisi wote ni CCM, hivyo wanavyosimamia wanatetea maslahi ya CCM.

CHEYO: UCHAGUZI WETU TANGU VYAMA VINGI NI MNADA. ANAYETOA FEDHA KUBWA NDIO MSHINDI

Mwazilishi wa TCD na Mwanasiasa Mkongwe, John Cheyo, amesema tatizo moja kubwa lililopo katika Mfumo wa Vyama vingi na katika jambo la Demokrasia ni fedha. Amesisitiza kuwa Fedha sasa ni adui yetu namba moja Tanzania.

Ameongeza "Labda na mimi nijilaumu kidogo, nilisema nikiwa Rais nitawajaza mapesa kibao. Ila siokuwa na nia ya kuwajaza mapesa ili mapesa hayo yatumike nunua vyeo. Uchaguzi wetu tangu Vyama vingi ni mnada"
Amesema leo kama mtu huna pesa usijaribu kuwa Mbunge wala kugombea Uwenyekiti wa Kitongoji kwani watu wanahonga hadi Ng'ombe. Amesisitiza jambo hilo linahitaji mazungumzo.

JENERALI ULIMWENGU: TUMEPOTEZA UWEZO NA UHURU WA KUZUNGUMZA KWA HOJA

Akishiriki katika Mjadala wa Kujadili hali ya Demokrasia Nchini, Mwanaharakati Jenerali Ulimwengu amesema, "hii nchi tumepoteza uwezo na Uhuru wa kuzungumza kwa hoja, tumeona juzi juzi hapa kwenye suala la Bandari lililoibuka limedhihirisha kuwa sisi tumekuwa kama Swala aliyeingia ghafla barabarani na kupigwa na mwanga mkali"

Ameongeza, "Imefikia hatua Watanzania tumekuwa watu wa kujenga hoja kwa kufokeana, kutishana, kukaripiana ilimradi tu hatupati nafasi ya kuzungumza kwa uhuru, hali inayoonesha hata kwenye masuala ya Katiba tuishia kuonyana na kupeana ahadi za uongo"
 
Back
Top Bottom