Mitandao inavyogeuka tishio maisha ya watu

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,830
4,585
Licha ya ujio wa mitandao ya kijamii kuwa na faida nyingi katika nyanja mbalimbali, ikiwamo ya kiuchumi, ukweli usio na shaka ni kwamba imekuwa na hasara zake lukuki.

Yapo mengi lakini kubwa linaloweza kuonekana kwa urahisi ni lile la baadhi ya watu kukiuka utumizi sahihi wa mitandao hiyo na badala yake kushambulia na kudhalilisha wengine bila kujali athari zinazoweza kujitokeza hapo baadaye.

Kauli za vitisho, picha na video za kushusha hadhi za watu zimekuwa sehemu ya utumizi wa mitandao ya kijamii, licha ya mamlaka za kila nchi kujaribu kwa kadri ya uwezo wake kuweka mikakati ya kudhibiti.

Katika utafiti wa hivi karibuni uliopchapishwa kupitia tovuti ya Visual Capitalist, imebainika kuwa asilimia 22.5 ya udhalilishaji wa huko mitandaoni hufanywa kupitia ‘komenti’ wanazotoa watu juu ya picha au video.

udhalilishaji.png
Aidha, asilimia 20.1 ya udhalilishaji hufanyika kupitia usambazaji wa taarifa za uzushi. Ni kama utafiti ulivyobaini kuwa asilimia 70 ya watu 20,000 (waliohusika katika utafiti) walidhalilishwa kupitia taarifa za uzushi zilizosambazwa dhidi yao. Vilevile, asilimia 12.1 hufanyika kwa picha na video za ngono.

Kujuana tatizo kubwa
Kwa upande mwingine wa utafiti huo, umebaini kuwa asilimia 64 ya wanaofanya hivyo si kwa bahati mbaya, bali huwalenga watu wanaowafahamu kabisa. Vilevile, inaelezwa kuwa mmoja kati ya vijana sita, sawa na asilimia 15, wamewahi kukumbwa na udhalilishaji huo wa mitandaoni.

Katika hilo, utafiti ukaonesha kuwa asilimia 61 ya waliokumbana na waliodhalilishwa ilitokana na mionekano yao (sura au umbo). Katika hilo la mwonekano, asilimia 17 ya wanaodhalilishwa huko mitandaoni ni kwa misingi ya ubaguzi wa rangi.

Pia, ubaguzi wa kijinsia nao unachukua nafasi kubwa katika matukio ya kushambuliwa mitandaoni, ikielezwa kuwa asilimia 15 ya wale wanaochafuliwa ni kwa sababu tu ni wanawake au wanaume. Wakati huo huo, asilimia 11 ya udhalilishaji wa mitandaoni hutokana na dini.

Takwimu zinaonesha janga la watu kudhalilishwa, kutishiwa mitandaoni limeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Vijana kaa la moto, wasichana hatarini
Kuanzia mwaka 2007 hadi 2016, ni asilimia 32 tu ya vijana waliokiri kukumbana na matukio hayo. Kwa mwaka 2019, hali ilikuwa mbaya zaidi kwani waliongezeka na kufikia asilimia 43.

Ikabainika pia, asilimia 73 ya vijana wanaoendelea na masomo katika shule za sekondari nao wanatumia mitandao ya kijamii na kukumbana na kadhia ya kudhalilishwa.

Utafiti unaeleza kuwa wasichana wanateseka zaidi kwa udhalilishaji au vitisho vya mitandaoni. Ni asilimia sita tu ya vijana wa kiume wanaokumbana hali hiyo, huku wenzao (wasichana) wakiwa ni wengi (15%).

Udhalilishaji Mitandaoni.png
Facebook majanga zaidi
Hata hivyo, asilimia 56 ya walioripoti kukutwa na majanga hayo walisema hayo yaliwakuta kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook. Hiyo inaweza kuwa inatokana na ukweli kwamba Facebook ndiyo mtandao wa kijamii uliobamba zaidi ukiwa na watumiaji wa kila mwezi wanaofikia bilioni 2.5 duniani kote.

Mitandao mingine iliyoonekana kuwa na kiwango kikubwa cha matukio ya aina hiyo ni Instagram (42%), Snapchat (31%), WhatsApp (12%), YouTube (10%), na Twitter (9%).

Athari za matukio hayo
Kudhalilishwa au kutishiwa maisha mitandaoni humfanya muhusika kupoteza hali ya kujiamini, msongo wa mawazo, kuingia kwenye ulevi na wakati mwingine kushuka kwa kiwango cha ufanyaji kazi.

Utafiti wa mwaka 2017 ulibaini kuwa asilimia 66 ya wanawake waliodhalilishwa mitandaoni walisema walipoteza hali ya kujiamini, huku asilimia 63 wakisema walishindwa kupata usingizi kwa siku kadhaa.

Kuanzia mwaka 2008 hadi 2015, asilimia 37 ya watu waliofanyiwa ‘unyama’ mitandaoni walikiri kuangukia kwenye msongo wa mawazo, wakati wengine (26%) walijaribu kujiua.

Nchi zinazoongoza udhalilishaji mitandaoni
Kwa mwaka 2018, India ndiyo iliyokuwa kinara wa matukio ya watu wake kukutwa na udhalilishaji wa mitandaoni. Zaidi ya asilimia 37 ya wazazi nchini India wanakiri watoto wao waliwahi kukutwa na kadhia hiyo, likiwa ni ongezeko la asilimia tano ukilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2016.

Lakini, elimu juu ya matukio ya aina hii ni kubwa katika nchi mbili; Sweden na Italia, ambazo kila moja ina asilimia 91. Pia, Saudi Arabia nayo inafanya vizuri (37%) katika kutoa elimu kwa raia wake juu ya udhalilishaji wa mitandaoni.
 
Back
Top Bottom