Mishikaki ya kinana yazua mjadala mpya

peno hasegawa

JF-Expert Member
Feb 24, 2016
12,830
21,460
Dar es Salaam. Kauli ya Makamu Mwenyekiti CCM-Bara, Abdulrahman Kinana ya kushangazwa na sheria inayozuia bodaboda kubeba mishikaki (abiria zaidi ya mmoja), imewaibua wadau wakionya kuingiza siasa kwenye usalama wa watu.

Julai 27, 2023 akizungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho waliojitokeza kumpokea akiwa ziarani wilayani Bariadi mkoani Simiyu, Kinana alihoji kwa nini waendesha pikipiki, maarufu bodaboda wazuiwe kupakia abiria zaidi ya mmoja ilhali wanapanda kwa hiari yao.

Huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo, Kinana alisema bodaboda akibeba abiria zaidi ya mmoja atapata hela nyingi.

“Wakipanda watatu si kwa hiari yao? Nitakwenda kuzungumza na wahusika wafute hiyo sheria, lazima tuwasikilize watu wanataka nini, wakisema wanataka wapande wawili sawa, watatu sawa, si mnabeba mishikaki sasa mishikaki iendelee,” alisema.

Serikali ilisisitiza marufuku hiyo
Kauli ya Kinana imekuja ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini alipokataa ombi la Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni alilolitoa Juni 28, 2023 bungeni Dodoma akiitaka Serikali kutoa tamko kuruhusu bodaboda kubeba abiria zaidi ya mmoja vijijini kwa kuwa zinatumika kubebea wagonjwa.

“Naomba hili lichukuliwe kama dharura, kule viijijini usafiri mkubwa wa wananchi kubebea wagonjwa ni bodaboda, na mgonjwa hawezi kubebwa mwenyewe, lazima kuwe na mtu wa kumshikilia, lakini sheria hairuhusu hili, naomba angalau basi iruhusiwe vijijini,” alisema Kanali Mageni.

Akijibu swali hilo, Sagini alisema sheria ya usalama barabarani inaeleza bayana ni kosa pikipiki kubeba abiria zaidi ya mmoja kwa kuwa ni hatari kwa usalama wa abiria hao.

“Pikipiki ikibeba abiria wengi ni hatari kwao kutokana na kasi yake. Ningeshauri watumie baiskeli kubebea mgonjwa kwa kuwa inatembea taratibu,” alihitimisha.

Wadau waonya
Akizungumza na Mwananchi jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latra CCC), Leo Ngowi alisema kauli hiyo ya kutaka bodaboda kupakia mishikaki inakiuka usalama wa watu.

“Bodaboda imeundwa kubeba abiria mmoja au mzigo, kwa hiyo kubeba zaidi za hapo ni kinyume cha sheria na mpaka hapo haki ya mtu hailindwi tena, kama tunataka bodaboda ibebe idadi kubwa ya watu lazima muundo wa pikipiki ubadilishwe, kwani ajali ikitokea mwili ndio kinga, hivyo athari za moja kwa moja kwa mtu ni kubwa,” alisema.

Kauli hiyo ya Kinana ilimuibua Balozi wa usalama barabarani, Rama Msangi aliyesema suala la usalama barabarani bado ni changamoto kutokana na watu wengi kufahamu dhana hiyo ukubwani.
“Bado hatuyachukulii madhara ya barabara kwa ukubwa wake, mfano bodaboda anapopata ajali akapelekwa hospitali ana watoto, mke na wazazi ambao walikuwa wanamtegemea watakosa msaada.

“Hapo familia itaanza kuteseka kumhudumia majeruhi na watu kuanza kupitia wakati mgumu, matokeo yake ni watoto kuanza kukimbilia mitaani kujitafutia, hili ni jambo ambalo ukimuuliza bodaboda hawezi kukueleza kwa upana huo,” alisema.

Msangi alisema ni jambo la hatari kwa waendesha bodaboda kuanza kuishi kwa matamko ya kisiasa kuliko kuangalia uhalisia.

“Baraza la usalama barabarani lilipaswa kufanya tafiti nyingi ili kuleta takwimu za kuonyesha ajali za bodaboda nchini zinaumiza maisha ya wananchi kwa ukubwa gani,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, Dk Rajab Mlaluko kutoka Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya, alisema ajali ya bodaboda ni hatari kuliko ya gari kutokana na chombo hicho kutomkinga abiria kunapotokea ajali.
“Vyombo hivyo havina mkanda wa kumkinga abiria ajali inapotokea,” alisema Dk Mlaluko.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi Tanzania (Uwamata) Majura Kafumu, alisema ni muhimu wanasiasa kuheshimu sheria zilizopo, kwani matamko ya kisiasa yanagharimu maisha ya wananchi.

“Hizi siasa ndizo zimetufikisha hapa, hatujui nchi inakwenda wapi, kwa nini tunafanya majaribio kwenye maisha ya watu walio hai.

“Kila siku tunasikia ajali zinaongezeka, tunaishi kwa takwimu, tusigeukie huko, dunia sasa inajikita kupunguza matukio ya ajali, lakini sisi tunatengeneza mifumo ajali ziongezeke, mimi hili wazo sikubaliani nalo,” alisema.

Naye Wakili Jebra Kambole alisema ni muhimu wanasiasa kuwa makini na kauli wanazotoa hata kama zitawanufaisha, ni muhimu kuupa kipaumbele usalama wa raia.

“Hakuna sababu za msingi za kusema sasa bodaboda waanze kupakia abiria mishikaki japo wanapakia kutokana na sheria kutosimamiwa vyema na ajali zinaongezeka kila siku na watu wengi wanapoteza maisha, ni muhimu kutafuta njia za kutatua tatizo na si kuliongeza,” alisema.

Hata hivyo, mtazamo huo umeonekana wenye manufaa kwa madereva bodaboda, ambapo Ramadhani Hamasi, maarufu King Rama, mkazi wa wilayani Temeke alisema kwa maeneo yenye adha ya usafiri waruhusiwe kubeba abiria zaidi ya mmoja. “Maeneo ya mijini sawa wasiruhusu mishikaki, vijijini na maeneo mengine kuna adha ya usafiri, huwezi kubeba mtu mmoja ukaenda umbali mrefu halafu urudi ubebe mwingine, ni hasara kwa kweli,” alisema.

Kwa upande wake Ombeni Stephano, dereva bodaboda eneo la Mbagala Kizuiani, alisema kama Serikali itaruhusu mfumo huo kwao ni neema, lakini lazima sheria iwe kali juu ya madereva wanaoendesha vyombo hivyo vya moto kwa mwendokasi. “Tatizo linakuja kwenye mwendo wa dereva, unaweza kupakia abiria zaidi ya mmoja hata ukianguka ukiwa kwenye mwendo mzuri hawawezi kuumia, sasa mwendo wa dereva lazima uangaliwe kwa sababu huwa ndio tatizo la kwanza la sisi kuonekana tunajitawala,” alisema.

Takwimu za ajali
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) Machi mwaka huu ilieleza kuwa majeruhi wa bodaboda tisa hadi 10 wanapokelewa kwenye taasisi hiyo kwa siku.

Hiyo ni sawa na kusema majeruhi 70 hupokelewa kwa wiki na 280 kwa mwezi wanapokelewa kwenye taasisi hiyo kutokana na ajali za bodaboda.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani, Julai 2021 hadi Machi 2022, Tanzania ilikuwa na matukio 1,594 ya ajali za barabarani ambapo ajali 300 zilisababishwa na madereva wa bodaboda.
Ripoti ya Tanzania in Figures 2021 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha ajali zilizosababisha vifo mwaka 2020 zimeongezeka kutoka 1,031 hadi kufikia 1,038 mwaka 2021.

Mwaka 2021 vifo vilivyoripotiwa kutokana na ajali vilikuwa ni 1,368, sawa na wastani wa kila ajali kusababisha kifo cha mtu mmoja, huku idadi ya majeruhi nayo ikiongezeka kutoka 2,362 mwaka 2020 kufikia 2,452 mwaka 2021.

Kauli ya Lema
Mapema Machi mwaka huu, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alizua mjadala mkali baada ya kueleza kuwa bodaboda ni ajira ya laana kutokana na changamoto wanazokutana nazo, zikiwamo ajali na ujira mdogo.

Baadhi ya madereva wa bodaboda na wadau wengine waliunga mkono kauli hiyo na wengine wakipinga na kumtaka Lema aombe radhi kwa kuwadhalilisha. Hata hivyo, Lema aligoma kuomba radhi na kusisitiza ajira hiyo kutotumika kisiasa.

Jeshi la Polisi
Mwananchi ilipomtafuta Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura kuzungumzia kauli hiyo alielekeza apigiwe Msemaji wa jeshi hilo, David Misime ambaye simu yake iliita bila kupokewa.

Na alipotafutwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyesema yupo kikaoni.
 
KINANA ANAOMBA KURA KWA VIJANA HAPO MWAKANI Kwa sababu vijana wengi ni wajinga watashangilia bila kujua CCM ukivunjika miguu Kwa bodaboda wanakukata miguu Kwa sababu hawajali wananchi wao wanajali uchaguzi tu
 
Suala la bandari .....hatuliachi....kamwe waache mkataba fake huo unauza nchi
 
Back
Top Bottom