Miaka 57 ya Umoja wa Nchi Huru Afrika: Je, kuna matumaini ya amani, diplomasia na demokrasia Afrika?

bigmukolo

JF-Expert Member
Mar 6, 2012
597
2,225
Umoja wa nchi huru za Afrika ndio kimbilio na tegemeo la kutatua changamoto mbalimbali za Afrika ikiwemo vita, ukame, njaa, maradhi na viashilia vya uvunjifu wa amani na ustaraabu wa maisha ya waafrika, kiujumla siasa za kimajumui ni falsafa zenye mawazo ya kuitaka Afrika kuungana pamoja ili kudhibiti ubeberu na uliberali, Afrika tunataka iungane ili kutengeneza Dola yenye nguvu kisiasa, kiuchumi na kijeshi.

Mawazo haya yalianza hata kabla ya umoja wa Afrika kuanzishwa mnamo tarehe 25/5/1963 nchini Ethiopia ambapo zaidi ya nchi thelathini zilikutana na kuanzisha umoja wa nchi huru Afrika kwa malengo ya kuondoa ukoloni Afrika, umoja wa Kiuchumi na biashara, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi na mambo kadhaa ambayo yalikuwa kikwazo kwa ustawi wa Afrika.

Tangu mwaka 1961 Mkutano wa Casablanca mjini Morocco ambapo nchi za Algeria, Misri, Ghana, Guinea, Libya, Mali na Morocco zilianza harakati za kuunganisha bara zima la Afrika lakini walikwama kutokana na tofauti za kimtazamo, itikadi na propaganda za mataifa ya Magharibi hasa Marekani na Urusi.

Baadhi ya viongozi wazalendo na wanamajumui walitaka Afrika kuungana ili kuifanya Afrika iwe na sauti moja, nguvu za kijeshi, kiuchumi na kisiasa, Kwame Nkrumah, Haille Selasie, Ahmed Sekou Toure na Gamal Abdel Nasser na viongozi mbalimbali walijadili Afrika kuungana ili kuunda United States of Africa, lakini kuna viongozi wengine walimuogopa Kwame Nkrumah kwa kudhani angekuwa Raisi wa Afrika labda kwa sababu alikuwa amesoma sana kuliko wenzake au alikuwa ana ushawishi wa kujenga hoja na kujiuza kisiasa na kiitikadi Ulimwengu mzima.

Hoja za Kwame Nkrumah zilipingwa na wadau kama Mwalim Nyerere huku akisema kwamba ni vyema tujiunge kikanda kabla ya kufikiria kuungana Afrika nzima, ndoto za Kwame Nkrumah zikafa baada ya juhudi za mabeberu hasa Marekani na Israel kufanya njama za kulihujumu Jeshi la Ghana na hatimae mwaka 1966 Generali Joseph Arthur Ankrah alimpindua Dr Kwame Nkrumah.

Tarehe 25 /5/2020 Umoja wa nchi huru Afrika utatimiza miaka 57 tangu kuanzishwa kwake ingawa kuna mabadiliko mbalimbali ya kikatiba na mfumo wa uendeshaji mfano mwaka 1991 Viongozi wa umoja wa mataifa ya Afrika walikutana Abuja Nigeria kubadilisha katiba, pia tarehe 9/9/1999 viongozi wa mataifa ya Afrika walikutana mjini Sirte Libya nyumbani kwa mbabe wa kivita Muammar Mohammed Abu Minyar Gaddafi kwa lengo la kubadilisha baadhi ya vifungu na kanuni za kisiasa. Mwaka 2002 Umoja wa nchi huru za Afrika ulibadilishwa na kuwa Umoja wa Afrika.

Je miaka 57 ya umoja wa nchi za Afrika kuna matumaini ya amani, ustawi na ustaraabu wa Afrika? Hilo ni swali la msingi kwa sababu Afrika haiwezi kusonga mbele ili kushindana na jumuia ya ulaya kama amani na utulivu utakuwa mdogo, Afrika ni yetu sote hivyo majadiliano ya kina na juhudi za kidiplomasia zinahitajika ili kuifanya Afrika kuwa sehemu salama kwa kila mtu ukiachilia mbali tofauti zetu za kisiasa, kijiografia, kijamii, kiuchumi, kidini na kihaiba.

Tangu mwaka 1968 umoja wa Afrika umekuwa ukitatua mizozo na machafuko ya kisiasa barani Afrika kuna mizozo ambayo umoja huo ulifanikiwa na kuna baadhi ya mizozo ni kitendawili mpaka leo mfano suala la Sahara Magharibi na Morocco, pia mzozo wa kisiasa nchini Congo tangu kifo cha Patrick Lumumba mwaka 1961 hali si shwari mpaka leo. Kuna nchi zaidi ya 55 kwenye umoja wa Afrika lakini nchi 50 zimeshaingia na kukumbwa kwenye vita au machafuko ya kisiasa au hata kuongozwa kidikteta ama kijeshi huku utawala bora, sheria na haki za binadamu zikiminywa kwa kiwango cha hali ya juu, baadhi ya nchi zimeonesha ukomavu wa kisiasa tangu uhuru mfano Sao Tome and Principals, Botswana na Namibia.

Nchi zingine zote zimewahi kuwa na sifa zifuatazo, mwelekeo wa vita, utawala wa mabavu, maandamano na vurugu zenye kuonyesha chuki, uasi na dhulma.

Nchini Tanzania mwalim Nyerere (1922_1999) Katika uongozi wake kuanzia mwaka 1961_1985 alikumbana na vikwazo vingi sana mfano mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli na kudhibitiwa zaidi ya mara saba, changamoto za Muungano na hekaheka za Generali Iddi Amini Dada, Kuna nchi mpaka leo kuna changamoto za amani na demokrasia ingawa kuna vikosi mbalimbali vya kulinda amani chini ya umoja wa Afrika na umoja wa mataifa mfano Somalia, Darfur Sudan kaskazini, Sudan kusini, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Mali, Misri, Jamhuri Ya Afrika ya kati, Nigeria, na Libya. Vikosi vya umoja wa Afrika vinalipwa pesa nyingi ambazo mataifa ya Magharibi na umoja wa mataifa huchangia kwa kiasi kikubwa huku umoja wa Afrika ukichangia kwa kiasi kidogo, swali la msingi je kuna haja ya kuweka vikosi mbalimbali vya kulinda amani bila kutatua chanzo cha migogoro hiyo? Kwanza inatakiwa pande zinazokinzana ziwekwe chini halafu wataalamu wa diplomasia na intelijensia wasuluhishe mizozo hiyo kwa sababu hata waasi au wapinzani wa serikali wana hoja za msingi ambazo kimsingi zimewaingiza kwenye uhaini, ugaidi na uhujumu wa nchi zao.

Kuna baadhi ya mizozo barani Afrika imekwisha kulingana na juhudi za umoja wa mataifa na umoja wa Afrika mfano Liberia kuanzia mwaka 1980-2003 kulikuwa na machafuko na vita tangu Utawala wa Samuel Kanyoni Doe, Prince Johnson na Charles Taylor. Nchi zingine ni mzozo wa kisiasa nchini Sierra Leone na ivory Coast ambapo mwaka 2012 mcheza soka wa Chelsea na timu ya Taifa ya ivory Coast Didier Drogba aliwaomba waasi kuweka silaha chini ili kuleta amani na ustaraabu nchini ivory Coast.

Umoja wa Afrika Unapaswa kutambua kwamba suala la amani ni jukumu la waafrika wote na mizozo ya Afrika inapaswa kutatuliwa na waafrika wenyewe na sidhani kama umoja wa Afrika umeshindwa kusuluhisha matatizo ya Afrika kwa sababu nguvu na mamlaka inayo kitu cha ajabu ni kwamba inaonekana kwamba umoja huo una kasoro nyingi ndio maana baadhi ya wanazuoni na wanafalsafa hawauamini umoja huo huku wakidai kwamba tume ya usuluhishi ya umoja wa Afrika inatafuna fedha za bure bila kufanikisha mchakato wa amani, ustawi na ustaraabu wa Afrika.

Ali Amini Mazrui (1933_2014) Mwanafalsafa kutoka Mombasa Kenya ambaye alitawafu mwaka 2014 , amewahi kuainisha changamoto kadhaa za umoja wa Afrika, moja fedha za kuendesha vikao na usuluhishi hazitoki Kwa waafrika mara nyingi zinatoka ughaibuni na Magharibi. Hivyo fedha hizo zina masharti kadhaa, pili waafrika wengi wamekosa imani na umoja huo hasa kwa baadhi ya migogoro mfano mzozo wa kisiasa nchini Mali ambapo waasi wa Tuareg wanataka kutengeneza nchi yao ndani ya Mali, tangu mwaka 1995 waasi hao wamekuwa wakifanya fujo na mauaji makubwa ya wananchi.

Umoja huo upo Mali na uasi unaendelea. Cha tatu ambacho Profesa Mazrui alisema ni kwamba umoja wa Afrika una shikwa masikio na umoja wa mataifa hivyo basi ni vigumu kuwa na msimamo na kauli moja Kuhusu hatma na mwelekeo wa amani barani Afrika. Cha nne kuna suala la rushwa miongoni mwa viongozi mbalimbali wa umoja huo ndio maana kuna baadhi ya nchi ziliamua kugoma kutoa michango yao mfano Ghana kipindi cha Generali John Rawlings.

Cha mwisho ambacho Marehemu Profesa Mazrui alisema ni kwamba mataifa ya Magharibi kama Marekani, uingereza na Ufaransa wananufaika kwenye baadhi ya migogoro barani Afrika hivyo basi ni vigumu kuwa na amani, utulivu na ustaraabu wa Afrika mfano mzozo wa kisiasa nchini Angola kuanzia mwaka 1975-2002 Marekani ilimuandaa Jonas Savimbi ili kuhujumu serikali ya kijamaa ya Augustine Neto na Jose Eduardo Dos Santos.

Changamoto hizo zimesababisha vita na mazingaombwe yenye visa bandia kuwa sehemu ya maisha ya waafrika kwenye nchi zao,pia Ongezeko la wakimbizi ni moja kati ya matokeo makubwa ya machafuko ya kisiasa barani Afrika nchi kama Rwanda, Uganda, Kenya, Burundi, Congo, Somalia na Libya watu wa nchi hizo wamewahi kukimbia nchi zao kisa vita.

Nchini Congo hasa mji wa Goma Jeshi la Tanzania linalinda amani huko dhidi ya waasi wa ADF wenye asili ya Uganda, Jeshi la kulinda amani kutoka Tanzania lilidhibiti eneo la Goma na kuwafukuza waasi, kituko cha karne ambacho wasomi na wanazuoni waliziba vinywa vyao ni pale umoja wa mataifa ulipoliomba Jeshi la Tanzania kuondoa silaha kali Congo kwa sababu wananchi walikuwa wanashtuka, baada ya kufanya hivyo waasi wa ADF walirudi tena kushambulia mji wa Goma, Hii ni biashara kichaa, Tanzania inaweza kuumaliza mzozo wa kisiasa nchini Congo na kuwamaliza waasi wote tatizo ni kwamba umoja wa mataifa, Marekani na nchi za Magharibi zinataka mzozo huo uendelee kwa sababu kuna maslahi mapana.

Hivyo waafrika tunapaswa kuamka kwa sababu hatma ya Afrika iko mikononi mwetu itakuwa ni ujinga kutegemea mizozo ya Afrika kutatuliwa na mataifa ya Magharibi huo ni utata kwa sababu historia inaonyesha kwamba Marekani, Urusi, uingereza, Ufaransa na Uberigiji wamechangia mizozo mingi kutokea barani Afrika hasa kipindi cha vita baridi kuanzia mwaka 1945_1990. Hivyo basi nchi hizo hatupaswi kuziamini katika mchakato wa kuleta amani na ustaraabu wa Afrika.

Nchini Somalia hali ni tete tangu Marekani walipompiga fitina Comred Generali Mohammed Siad Barre, huyu alikuwa kiongozi wa Somalia kuanzia mwaka 1969_1991, tangu atolewe madarakani na Marekani hali ni tete nchini Somalia ndio maana kuna baadhi ya wataalamu wanasema kwamba kundi la wanamgambo wa AL_Shabab ni kutoka ukoo wa Marehemu Siad Barre hivyo wanataka mmoja kati ya ukoo ule awe Rais wa Somalia, kitu kingine ni kwamba waasi hao hawataki serikali ya Kenya kuingilia mizozo ya Somalia mfano Raisi wa Somalia Mohammed Farmajo analindwa na askari kutoka Kenya ndio maana kuna uhasama mkubwa kati ya waasi wa AL Shabab na serikali ya Kenya.

Nchini Libya kuna vita tangu mwaka 2011 baada ya kufanyika makosa ya kiufundi ya kumuondoa Kanali Muammar Mohammed Abu Minyar Gaddafi, leo hii Libya ni tishio kwa usalama na ulinzi, Libya ilikuwa nchi nzuri sana huku ikizishinda baadhi ya nchi za ulaya, kwa sasa hivi Libya ni soko la utumwa, magendo, silaha na ugaidi, Kuna serikali mbili yaani serikali ya Tripoli inayoongozwa na Generali Khalifa Belqasim Haftari na serikali ya Tobruk ya ustadhi Fayez EL Sarraji. Je umoja wa Afrika unahaja ya kuwa na imani na Marekani Kuhusu kumalizika kwa mzozo wa kisiasa nchini Libya?

Nini Kifanyike ili Kuleta amani na ustaraabu wa Afrika kwenye nchi zenye machafuko ya kisiasa?
Kuna mbinu, njia na mikakati mbalimbali inapaswa kufanyika ili kuleta amani, ustaraabu, demokrasia na mshikamano barani Afrika.

Mosi, njia za kidiplomasia na Majadiliano ya kina yanapaswa kufanyika kwa sababu matumizi ya silaha sio mazuri. Kuna maridhiano, mijadala na kongamano mbalimbali. Mfano mzozo wa kisiasa nchini Sudan kusini Rais Salvaar Kiir anapaswa kutambua kwamba yeye hajaumbwa kuwa Raisi wa nchi hiyo milele, madai ya kiongozi wa waasi Riek Mashar ni kutaka kuwa Raisi wa nchi hiyo kwa sababu walikubaliana kwamba atampisha, historia inaonyesha kwamba tangu Torit Mutiny mwaka 1952 watu wa Sudan kusini walianza harakati za kujitenga kutoka Sudan ya khartoum baadae ikaja vita ya Anya-anya yaani Anya-anya ya kwanza, pili na tatu. Mwaka 2011 walifanikiwa kupata uhuru wao baada ya kura za wazi.Tangu mwaka 2011 mpaka leo hakuna amani nchini Sudan kusini kati ya Dinka na Nuer. Hii ni hasara sana kwa Afrika.

Pili, mahusiano mazuri kati ya viongozi wa Afrika na wapinzani hasa watu wenye mawazo tofauti na serikali, Hii huongeza vita na machafuko Afrika kwa sababu ya ubinafsi, uroho wa madaraka na hulka ya viongozi wa kiafrika kujiita miungu watu mfano Raisi wa pili wa Kenya ndugu Daniel Arap Moi (1924_2020) alikuwa anajiita mtukufu Moi katika utawala wake kuanzia mwaka 1978-2002 watu wengi waliteswa na kupotea hasa waliompinga, Afrika ukikosoa serikali unaonekana sio mzalendo au unatumwa na mabeberu hii huminya uwezo wa watu kuhoji dhulma na ukandamizaji, watu wameamua kuwasifu na kuwaabudu viongozi madikteta ili kuepuka kufa, kuteswa na kufilisiwa Mali zao, umoja wa Afrika katika vikao vyao Unapaswa kuhimiza mahusiano bora kati ya viongozi wa kiafrika na wapinzani ili kuleta chachu na ushindaji wa hoja, na huo ndio ulimwengu wa waelevu na wajivu.

Tatu, Nguvu za kijeshi katika jamii zinapaswa kupunguzwa kwa sababu operesheni za kijeshi uraiani ni hatari sana kwa afya ya wananchi, mfano mwaka 2008_2015 vikosi vya Ufaransa ambavyo vilikuwa vinalinda amani Jamhuri ya Afrika ya kati vilituhumiwa kubaka wanawake na kulawiti watoto wadogo kwa sababu ya hongo ya chakula na maji. Hoja za Mazungumzo na upatanishi kati ya waasi na serikali ni muhimu sana kuzingatiwa ingawa kuna baadhi ya mahitaji ya waasi ni vigumu serikali kutekeleza, hapa tunapaswa kufikiri kwa kina kama kobe na kuona mbali kama tai, viongozi wakiweka maslahi ya nchi zao mbele hasa maslahi mapana ya Afrika lazima amani itarejea kwenye nchi zenye machafuko kama Congo, Mali, Chad Somalia, Sudan na Libya. Ni vyema tujiunge bara zima ili kuwa na sauti moja, itikadi moja na falsafa moja Kuhusu utu, ustaraabu na ustawi wa Afrika.

Nne,Chaguzi mbalimbali Afrika zinapaswa kuwa za huru, haki na uwazi, ili kuepusha malalamiko na wizi wa kura, mfano mwaka 2016 nchini Zambia Raisi Edgar Chagwa Rungu alikuwa ameshindwa na Mpinzani wake ndugu Hakainde Hichilema, tume ya Taifa ya uchaguzi Zambia ilidai kwamba ndugu Edgar Rungu kashinda kwa asilimia tano, baada ya miez miwili Hakainde Hichilema alipanga kwenda mahakamani kukata rufaa ya matokeo cha ajabu akafungwa jela kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa kosa la uhaini, eti alivamia msafara wa Raisi Edgar Chagwa Rungu.

Kuna malalamiko mbalimbali na kashfa za wizi wa kura barani Afrika mfano mwingine ni uchaguzi Mkuu nchini Zimbabwe kati ya Raisi Emmerson Dambuzo Mnangagwa na mpinzani wake mwanasheria machachari ndugu Nelson Chamisa, wananchi wa Zimbabwe walimchagua Nelson Chamisa lakini tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Zimbabwe ikamtangaza Emmerson Mnangagwa. Afrika kuna maajabu mengi sana kwa sababu mgombea anaweza kupata kura nyingi kuliko idadi kamili ya wapiga kura, Hii iliwahi kutokea nchini Liberia miaka ya 1950. Uhuru, uwazi, haki na usawa ni muhimu katika Chaguzi mbalimbali Afrika ili tupate viongozi bora kwa maslahi mapana ya Afrika.

Tano, Katiba mbalimbali za nchi za kiafrika ni za kihafidhina hivyo mabadiliko mengi yanahitajika kwa sababu katiba hizo zinampa Rais mamlaka makubwa na hatimae tunazalisha viongozi wengi miunguwatu, mfano nchini Tanzania mihimili ya serikali haina usawa hata kidogo mfano katibu wa Bunge anateuliwa na Rais hii ni mbaya sana kwenye usawa na uhuru wa Bunge, jaji Mkuu na majaji mbalimbali Rais ndio mwenye jukumu la kuwapitisha hivyo uhuru wa mahakama unakuwa na ukakasi mwingi sana, pia wasisamizi wa uchaguzi ni wakurugenzi wa halmashauri ambao wanateuliwa na raisi hii ni hasara kubwa kwa Taifa na Afrika kwa ujumla.

Ndio maana kuna tuhuma na kashfa nyingi za wizi wa kura kwenye Chaguzi mbalimbali Tanzania tangu mwaka 1995 mpaka leo. Mabadiliko mbalimbali ya katiba ni muhimu ili kukuza demokrasia, uzalendo, utu na usalama wa Afrika. Kuanzia Afrika kusini mpaka Dakar Senegal lazima katiba zibadilishwe ili kuwa na hatma bora ya Afrika miaka Mia moja ijayo.

Sita, Umoja wa Afrika Unapaswa kusimama wenyewe katika kuleta amani Afrika, pia kuna umuhimu mkubwa kwa umoja huo kutengeneza vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuepuka fedha za mabeberu ambazo kimsingi zinaongeza tamaa na uasi, matajiri wa Afrika wako radhi kuchangia fedha ili kuleta amani kama zikitumika kwa usahihi bila rushwa na ubadhilifu. Kutegemea umoja wa mataifa, umoja wa Ulaya, Marekani na Uingereza ili kutatua mizozo ya kisiasa Afrika ni sawa na kutafuta mto Saudi Arabia.

Hitimisho, Mwanafalsafa na nguri wa historia kutoka Gambia Alhaji Profesa Alieu Ebrima Cham Joof (1924_2001) aliwahi kusema kwamba"matatizo ya Afrika ni ya waafrika wenyewe hivyo juhudi za utatuzi zinapaswa kufanywa na waafrika wenyewe na ikitokea kwamba waafrika tumeshindwa kumaliza tofauti zetu basi tutakuwa watumwa wa kifikra milele".
Je, tutaendelea kuwa watumwa wa fikra mpaka lini? Vijana wa Afrika mawazo yao yanasikilizwa kwenye vikao mbalimbali vya umoja wa nchi huru Afrika nchini Ethiopia? Kuna vituko vingi vimewahi kufanyika kwenye umoja wa Afrika mfano mwaka 1974 viongozi wa umoja wa Afrika walimchagua Iddi Amini Dada kuwa Mwenyekiti wa umoja huo, pia Generali Joseph Desire Mobutu Sese Seku Kuku Ngendu Wa Zabanga(1930-1997) amewahi kuwa Mwenyekiti wa umoja huo mwaka 1967-1968. Hii ni ishara kwamba kuna masihara mengi katika umoja wa Afrika.
 
Ubinafsi na uroho wa madaraka wa baadhi ya wakuu wa nchi bado ni changamoto kubwa sana kwa umoja huu.
 
United state of Africa..
Hapo viongozi wangekuwa hawatoki madarakani,
Ingevunjika kama ilivyo vunjika U.S.S.R
Suala la changamoto ingawaji tunajitahidi kukabiliana nazo lakinj hatuna nguvu..
Huu umoja wa Africa hauna Nguvu kabisa ni jina tu maana angalia kama Libya walikuja wamarekani kumtoa Gadaffi umoja wa Africa ulikaa kimya, kwa nini mwanzo huu umoja wa Africa hukuweza kumshauri Gadaffi kama alikuwa anaenda tofauti,
Gadaffi pia alikuwa anahitaji umoja wa Africa wenye nguvu.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom