MaxShimba
JF-Expert Member
- Apr 11, 2008
- 35,772
- 4,054
MCHUNGAJI wa Kanisa la EAGT lililo Mtaa wa Ichenjezya kwenye mji mdogo wa Vwawa mkoani Mbeya Simon Kitwike, 48, amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya kukataa kuapa mahakamani kutokana na imani ya dini yake.
Mchungaji huyo, ambaye alifika mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi katika kesi ya wizi kwenye nyumba yake iliyovunjwa mwishoni mwa mwaka jana na kuibiwa mali kadhaa, aliishangaza mahakama baada ya kukataa kuapa kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake.
Hakimu wa mahakama ya wilaya, Kajanja Nyasige alimtaka asome kifungu katika Biblia kinachomtaka asiape mahakamani, ndipo mchungaji huyo alipofungua kitabu hicho kitakatifu na kusoma Mathayo 5: 35 akisema mistari hiyo ndiyo inayompa msimamo huo.
Mstari huo ambao alisema unamzuia unaanzia Mathayo 5:34 na kuendelea hadi 5:35 na unasema:
"Lakini mimi nawaambia, usiape kabisa; hata kwa Mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yaje; wala kwa Yerusalem, kwa maana ndio mji wa Mfalme Mkuu."
Baada ya kusoma kifungu hicho, Hakimu Nyasige alimuuliza tena mchungaji huyo kama alikuwa tayari kuapa ili aweze kuendelea na kutoa ushahidi wake mahakamani, hata hivyo mtumishi huyo wa Mungu aliendeleza msimamo wake wa kukataa kuapa.
Kitendo hicho kilifanya hakimu huyo kumsomea kifungu cha sheria na 198 (1) kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 kinachokataza mtu kudharau mahakama na kumwambia kuwa kuendelea kukataa kuapa ni kuvunja sheria na hivyo anatenda kosa la jinai.
Hata hivyo, Hakimu Nyasige aliendelea kumvumilia mchungaji huyo ili aweze kubadili msimamo wake kwa kumwamuru asome Biblia hiyo tena katika kitabu cha Warumi 13:1- 5, lakini baada ya kusoma kifungu hicho, mchungaji huyo hakubadili msimamo wake na hivyo kumpa mwanya Hakimu Nyasige kutoa hukumu yake.
Hakimu Nyasige alisema anamtia hatiani mchungaji huyo kutokana na kosa la kuidharau mahakama na hivyo kumhukumu kwenda jela miezi sita na kuwa atatakiwa kurufi mahakamani kutoa ushahidi wake kwa kesi ya msingi Machi 2.
Akiongea na Mwananchi, mchungaji aliyejitambulisha kwa jina la Mwakasaka alisema amepokea hukumu hiyo kwa masikitiko na mshangao mkubwa kwani mchungaji huyo amenukuu vibaya Biblia, akisema kuwa kitabu hicho kinakataza mtu kujiapiza yeye mwenyewe lakini inaruhusiwa kuapishwa kwa mamlaka iliyo ya duniani.
Matukio ya waumini wa madhehebu kupingana na sheria yamekuwa yakitokea mara kadhaa wilayani hapa. Wanafunzi wa madhehebu ya Mashahidi wa Yehova wamekuwa na mgogoro na serikali kutokana na kukataa kuimba Wimbo wa Taifa shuleni.
Pia wakati fulani mgonjwa aligoma kuongezewa damu na kuna wakati wanafunzi sita waligoma kufanya mtihani wa darasa la saba kutokana na imani ya dhehebu lao.
Habari hii nimeipata kutoka Gazeti la Mwananchi.
Last edited by a moderator: