Mchungaji atembezwa uchi, saba wakimbia nyumba

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
WACHUNGAJI wanane wa makanisa ya Kipentekoste wanaotoka jamii ya wafugaji wa Kimasai wilayani Arumeru wamezihama nyumba zao na kwenda mafichoni wakihofia kukamatwa, kuvuliwa nguo, kutembezwa mitaani na kutozwa faini dume la ng’ombe baada ya kudaiwa kwenda kinyume na mila, desturi na taratibu za jamii hiyo kuhusu sherehe za tohara kwa wanaume.

Waliokimbia nyumba zao kwa hofu hiyo ni pamoja na Mchungaji Edward Supeeti, Simon Sivai, Joel Hamisi na Loi Langasi huku wengine wakiwa ni Loishinde Mollel, Jonas Lebulu na Geofrey Jacob.


Hofu hiyo imewakumba wachungaji hao kutokana na vitisho dhidi yao baada ya mmoja wao, Julius Lukumay (34) kukamatwa na vijana wanaojiita jeshi la mila na kumtembeza mitaani kwa siku mbili akiwa uchi akidaiwa kukataa kuhudhuria kikao cha mila cha rika la Korianga.

Lukumay, baba wa watoto wanne alikamatwa Novemba 17 mwaka huu na kutembezwa katika vijiji vinne tofauti baada ya kukataa kutoa faini ya ng’ombe au Sh500,000 kwa kosa la kuwashitaki wazee wa mila kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Siwandate, Kata ya Kiranyi wilayani Arumeru, ambao waliagiza vijana wakamate tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 100 lililokuwa nyumbani kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuokolewa na askari polisi waliofika eneo la tukio, siku ya pili tangu alipokamatwa na jeshi la mila, Lukumay alisema licha ya kuvuliwa nguo zote, watekaji wake walimvalisha bati iliyotobolewa sehemu ya kichwa pamoja na mfuko aina na kiroba ulioishia tumboni na kumwacha sehemu zake za siri zikiwa wazi.

“Mimi nimeokoka, ndiyo maana sihudhurii vikao vinavyohusiana na matambiko ya kimila. Cha ajabu, nilishangaa watu wanaoujua ukweli huo kufika nyumbani kwangu na kuchukua tanki langu eti kwa nini sikuhudhuria kikao cha rika na nilipofuatilia wakanikamata, kunivua nguo na kunitembeza uchi mitaani,” alilalamika Lukumay.

Alisema watekaji hao walimtembeza katika vijiji vya Ngaramtoni, Mringaringa, Kenyaki, Olevelosi, Kiranyi na Elerai huku wakimwimbia nyimbo za kumkejeli hadi saa sita usiku walipomrudisha kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Olchoki .

Mwathirika huyo wa sheria za mila alizungumza akiwa Hospitali ya Seliani, eneo la Ngaramtoni alikokimbizwa baada ya kuokolewa na polisi ambapo daktari aliyemchunguza aligundua kuwa alipigwa na kupata majeraha yaliyomsababishia maumivu makali.

Daktari aliyemtibu na kusaini PF3 iliyotolewa Kituo cha polisi Ngaramtoni ambaye alitambuliwa kwa jina moja tu Swai alibainisha kupitia maelezo yake kuwa majeraha na maumivu aliyoyapata Mchungaji Lukumay yalisababishwa na kupigwa kwa fimbo na rungu.

Katibu wa Umoja wa Wachungaji wa Madhehebu ya Kipentekoste mkoani Arusha, Joseph Kaondo alilitupia lawama jeshi la polisi kwa kushindwa kuwahakikishia usalama, wao na waumini wao dhidi ya vitisho na manyanyaso wanayopata kutoka kwa wazee wa mila na vijana wa jeshi la mila akitolea mfano tukio la kukamatwa kwa Lukumay ambaye aliokolewa zaidi ya saa 22 tangu tukio hilo liliporipotiwa polisi.

Mbele ya wachungaji wenzake, katibu huyo alisema jeshi la polisi linasuasua kuchukua hatua kwa maelezo kuwa hayo ni mambo ya mila yanayostahili kumalizwa na vikao vya mila, licha ya ukweli kwamba wao hawaishi kwa kufuata mila na desturi baada ya kuokoka.

Alisema hata mtendaji wa kijiji aliyepokea malalamiko ya Lukumay kukamatiwa tanki lake maji , Rafael Laizer alikataa kutatua mgogoro huo akidai kuhofia usalama wake na kuwataka wahusika wakayazungumze mambo hayo kwenye vikao na wazee ambao waliagiza Lukumay atembezwa uchi akiimbiwa nyimbo za kejeli au alipe dume la ng’ombe kwa ajili ya
chakula cha jeshi la mila kwa kosa la kuwashtaki ofisi ya Mtendaji.

Baada ya kutembezwa, Lukumay alipelekwa mto Ngarenaro ambako aliogeshwa Saa 11 asubuhi kabla ya kupelekwa nyumbani kwake ili akatoe ng’ombe lakini ikashindikana baada ya mkewe Happines kuhamisha mifugo iliyokuwepo nyumbani kwake, jambo lililowaudhi jeshi la mila waliamua kumchukua mkewe na kuvisha salfeti na kumuunganisha na mumewe huku wakimtelekeza nyumbani mtoto wao, Bezaleli mwenye umri wa miezi saba.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alikiri kufahamu tatizo hilo alilodai linatokea mara kwa mara kipindi cha tohara za mila kwa jamii ya Wamasai.

Alisema baada ya kumuuokoa kijana huyo walikubaliana Mkuu wa Wilaya ya Arumeru , Mercy Silla kuwa vifanyike vikao vya mapatano kati ya viongozi wa mila na wale wa madhahebu ya dini.

Mkuu huyo wa wilaya pia alikiri kuwepo jambo hilo, lakini amekana kupata taarifa za wachungaji hao kukimbia nyumba zao kwa kuhofia usalama wao baada ya mmoja wao kutekwa na jeshi la mila.

Hata hivyo, alisema baada ya mchungaji aliyetekwa kuokolewa, walikubaliana na viongozi wa mila kuheshimu imani ya wengine wasiokubaliana na matambiko yao.

Alisema wamewaagiza viongozi wa pande zote mbili kuheshimu makubaliano yao ya Februari 22 mwaka jana yaliyofikiwa mbele ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Arusha , Isdory Shirima ikiagiza viongozi wa dini na mila kutoingiliana katika utekelezaji wa shughuli zao .

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa dini akiwemo askofu Leonard Mwizarubi ambaye ni mwenyekiti wa makanisa ya kipentekesto mkoani hapa, Askofu wa kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer, kiongozi wa mila wa kimasai Amani Lukumay, mkuu wa wilaya ya Arusha , Raymond Mushi , mkuu wa wilaya ya Siha , Silla , maaafisa
kutoka vyombo vya ulinzi na usalama mkoani hapa.
Gazeti la Mwananchi
 
watekaji wameenda kinyume na uhuru wa kuabudu hauwezi kumlazimisha mtu kuabudu/kuamini itikadi ya dini unayoifuata.
 
Back
Top Bottom