CHANZO: ALASIRINa Emmanuel Lengwa
30th October 2009
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mheshimiwa Maria Hewa, leo amejikuta akikosa vipindi vya maswali na majibu na pia kuweza kushiriki katika michango mbalimbali baada ya kuugua ghafla bungeni na kukimbiziwa hospitalini.
Mbunge huyo, amekutwa na masahibu hayo leo asubuhi, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Bunge, tayari kwa kuungana na wenzie katika shughuli za leo.
Akizungumza baada ya kipindi cha maswali na majibu, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Samwel Sitta, amesema Mheshimiwa huyo alifika mwenyewe bungeni, lakini aliugua ghafla na hivyo kuwahishwa katika Hospitali ya Mkoa huu (Dodoma) kwa ajili ya matibabu zaidi.
Amewataka wabunge watakaotaka kumjulia hali mheshimiwa huyo kufanya hivyo katika hospitali hiyo ya mkoa.
Hata hivyo, hakukuwa na taarifa za chanzo cha kuugua huko ghafla kwa Mheshimiwa huyo, ambaye alikuwa akihudhuria vyema bungeni tangu Jumanne na jana alionekana yu mzima wa afya.
Katika Bunge lililopita, Naibu Waziri wa Miundombinu, Mheshimiwa Hezekiel Chibulunje, aliwahi kukutwa na tatizo kama hilo la kuugua ghafla bungeni.
Yeye alikutwa na mkasa huo wakati akijibu swali la Mbunge mmojawapo kabla ya kusaidiwa na wenzie na kukimbiziwa hospitalini ambako alitibiwa na kuruhusiwa.