Mbinu zinazotumika kutafuna fedha za umma na vigogo serikalini

Benjamini Netanyahu

JF-Expert Member
Aug 7, 2014
80,839
93,626
Dar/Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuwa na imani na Serikali katika mageuzi ndani ya mashirika na taasisi za umma, akiwaonya mawaziri wanaoyatumia kujinufaisha.

Amesema inasikitisha kuona mashirika ya umma katika mataifa mengine duniani yakiongeza tija na mchango kwenye maendeleo, huku nchini hali ikiwa mbaya kutokana na tija ndogo inayosababishwa na uzembe na hujuma.

Rais alisema hayo Jumamosi Agosti 19, 2023 katika hotuba ya takribani dakika 40 aliyoitoa alipofungua kikao kazi cha watendaji wa mashirika ya umma, wajumbe wa bodi, mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) jijini hapa.

Alisema kuna mashirika yanayoingiza faida yakiwamo ya maliasili na utalii, lakini bodi zake zimekuwa na matumizi mabaya ya fedha kupitia vikao vya nje bila tija kwa muda mrefu, huku baadhi ya watumishi wa wizara wakitamani kuhamia mashirika hayo kutokana na mishahara minono na marupurupu.

“Lakini jingine, baadhi tumegeuza mashirika haya kuwa msaada katika pilikapilika za wizara, umekwama kwenye OC (pesa za matumizi) unakwenda kwenye shirika, ‘fanya ulete kidogo’ tusaidie hapa. Pamoja na fedha hizo kuzitumia serikalini, tunazichukua kinyume cha sheria,” alisema na kuongeza; “Yanatakiwa kuleta gawio lakini wizara tunaweka mikono yetu kwenye mashirika, wakati mwingine ofisa mtendaji anaamua kutoa ili asitumbuliwe. Tubadilike, kama tunataka yazalishe, tusiyaingilie.”

Akifafanua mkasa wa namna mawaziri wanavyotumia fedha za mashirika hayo, Rais Samia alisimulia kilichotokea akiwa Waziri wa Utalii na Biashara Zanzibar mwaka 2000 chini ya Rais Amani Abeid Karume.
“Nikiwa Waziri wa Utalii tulikuwa tukitumwa kwenye maonyesho ya utalii kimataifa, UK (Uingereza). Sikuwa na mashirika yenye tija na posho langu nilipewa Dola sijui 3,000 au 4,000 kwa siku zote nitakazokaa, lakini waziri mwenzangu anachukua pia Tanapa, Tawa, Ngorongoro, sijui wapi. Mfuko wake umejaa.”

Rais alimaanisha mawaziri hao kuchukua posho pia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), zilizo chini ya wizara yenye dhamana ya utalii nchini.

“Hata hana nafasi ya kukaa kwenye banda la maonyesho, ni safari madukani. Akirudi anakuuliza, eeh! bado upo kumbe, aah! nilitoka kidogo kuzunguka, nimenunua hivi. Ukijitazama wewe una Dola zako 2,000 kwa ajili ya kula, kulala na usafiri. Sasa hii siyo uendeshaji mzuri na mnajua ni kinyume cha sheria,” alisema.

Rais aliongeza: “Hatuendi hivyo, tuache kuweka mikono kwenye mashirika haya tunayotegemea, huo ni mfano halisi. Najua mawaziri wangu na maofisa wakuu watendaji mnayajua mnayoyafanya huko, yaende yakabadilike.”

Magari ya Serikali
Awali, akitoa mada kuhusu uendeshaji wa mashirika hayo, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad alisema matatizo mengine yaliyopo kwenye mashirika ya umma ambayo yamesababisha yafe au kufanya kazi chini ya kiwango, ni matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za taasisi.
Alisema kuna matumizi mabaya ya fedha za mashirika ikiwemo ununuzi wa magari ya kifahari kama Toyota land Cruiser-V8 ya mwaka 2023 na kwa kila mtendaji wa Serikali kuwa na magari hayo.

"Kuna haja gani kuwanunulia watendaji watano katika taasisi moja magari matano ya kisasa V8 ambao inabidi kuajiri madereva, lazima maeneo ya kuegesha magari wakati si muda wote maofisa hao watakuwa safarini," alisema. Alisema kuna watendaji wa Serikali wanatoa magari ya taasisi kwenda kuwachukua shule watoto wa viongozi wa mashirika jambo ambalo si sawa.

"Hizo gharama za kufuata watoto zinaingia kwenye shirika hapo lazima itaathiri mapato ya taasisi,” alisema na kuongeza: “Kuna hili nimeona wakati tunakuja Arusha kwenye mkutano huu, baadhi ya watendaji wanakuja na ndege na magari yanawafuata Arusha ili waje kutembelea nadhani hii pia ni matumizi mabaya ya rasilimali za mashirika."

Pia alisema kuna tatizo la bodi na watendaji wa mashirika kuingiliwa na viongozi wa juu wa Serikali, hivyo kutolewa uamuzi ambao unaathiri mashirika. Alishauri wajumbe wa bodi za mashirika ya umma wapatikane kwa kuomba kazi hiyo na kufanyiwa usaili kuboresha utendaji kazi wao.

Profesa Assad alishauri katika juhudi za kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) idhibitiwe katika gharama za matengenezo ili kuakisi ushindani uliopo. “Ku-assess (kuchunguza) gari la umma pale Temesa unalipa Sh1 milioni bila kutengeneza. Hii hapana.”

Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na ya Hesabu za Serikali, akitoa mada alipendekeza watendaji wa mashirika ya umma kuajiriwa na bodi. "Rais akiteua mwenyekiti wa bodi, basi bodi ndiyo ipewe jukumu la kuajiri mtendaji mkuu wa shirika ili aweze kuwajibika kwa bodi," alipendekeza.

Zitto alisema kumekuwapo mgongano baina ya bodi na watendaji kwa kuwa kila mmoja ameteuliwa na Rais.
"Bodi ikiajiri mtendaji mkuu ina uwezo wa kumuondoa kama atashindwa kutekeleza majukumu yake na kuajiri mwingine," alisema.

Pia alishauri kuwepo sheria mpya ya mashirika ya umma na kuwa na sera ya mashirika hayo ambayo itasaidia kuleta mwongozo jinsi ya upatikanaji wakurugenzi wa bodi, watendaji wa bodi na masuala ya hisa, uendeshaji na mambo mengine muhimu.

Mageuzi yanakuja
Awali, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu alizungumzia mahitaji ya uwepo wa maboresho ya utendaji katika uendeshaji wa mashirika ya umma ili kuendana na maelekezo ya Rais Samia. Alisema lengo la kuwakutanisha watendaji wa taasisi za umma serikalini ni kuboresha utendaji kazi.

Kuhusu hoja za kamati kuhusu mageuzi ya mashirika na taasisi hizo, ikiwamo kufuta na kuunganisha baadhi, Rais Samia aliagiza viongozi husika washirikishwe.

Alisema endapo hoja za viongozi wa mashirika na taasisi hizo hazitakuwa na mashiko, mapendekezo ya kamati yatatekelezwa kama ilivyo bila kuathiri ajira.

Rais aliagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhakikisha taasisi zote zinaingia mikataba ya utendaji ili kuwachukulia hatua wote watakaoshindwa kutekelezaji mikataba yao. Kuhusu malengo ya uanzishwaji wake, aliagiza ofisi ya msajili wa hazina kuanza kusimamia urejeshaji wa umiliki wa mashirika kwa umma badala ya Serikali.

“Wakati ule wananchi hawakuwa na uwezo wa kununua hisa Serikali ikalazimika kuwa na hisa nyingi, ndiyo sababu yakaonekana kuwa ya Serikali. Kwa kuwa sasa kuna wananchi wana uwezo wa kununua hisa hata kama ni kidogo kidogo, sasa turejee kwenye mwelekeo huo,” aliagiza Rais.

Mwananchi
 
Akitaka tuwajibike ni ukitajwa na CAG tu ni PT mahakamani kesho yake jela tofauti na hapo huku chini hatuwezi jichosha wakati huko juu mnakula bata
Wana mfumo wao wa MUSE umekaa kitapeli sn sababu mtu akilipwa na taasisi nyingine hawezi gundulika kama amelipwa sehemu nyingine siku hiyo hiyo na wakati mfumo ni huo huo, why kusiwe na mfumo ambao ukilipa unahesabu siku ikitokea double payment unakata?
 
Kuhusu malengo ya uanzishwaji wake, aliagiza ofisi ya msajili wa hazina kuanza kusimamia urejeshaji wa umiliki wa mashirika kwa umma badala ya Serikali.
“Wakati ule wananchi hawakuwa na uwezo wa kununua hisa Serikali ikalazimika kuwa na hisa nyingi, ndiyo sababu yakaonekana kuwa ya Serikali. Kwa kuwa sasa kuna wananchi wana uwezo wa kununua hisa hata kama ni kidogo kidogo, sasa turejee kwenye mwelekeo huo,” aliagiza Rais.
Mashirika ya umma yatakuwa na maana ya kuwa ya umma pale yote yatakaposajiliwa kwenye soko la hisa ili wananchi na makampuni yao binafsi wapate fursa ya kununua hisa.

Agizo kama hili liliishatolewa enzi za Mkapa na Kikwete...baadaye kikawa kimya kikuu hadi leo huku soko la hisa wakiilalamikia udogo wa soko letu kwa kuwa na makampuni na mashirika machache yaliyosajiliwa....

Tuone haya maagizo yakitekelezwa kwa dhati sasa.
 
Yawezekana ila kuna asilimia kubwa sana ya kutowezekana. Ngoja tuone
 
Imenishangaza sana kuona posho ya mtumisho wa umma Tanzania kuwa kiwango cha juu kuliko hata nchi zilizoendelea $4000 kwa siku? Kama hayo ndiyo yamekuwa mazoea hakuna namna nchi hii itaendelea kwa mfumo huu. Hata wakianza kusemana hakuna kitakachoweza kubadilika kwa mfumo ule ule, watu wale wale, chama hicho hicho, katiba hiyo hiyo nasisitiza tena hakuna kitu kitaweza kubadilika. Hayo ni maneno tuu!
 
Mashirika ya umma yatakuwa na maana ya kuwa ya umma pale yote yatakaposajiliwa kwenye soko la hisa ili wananchi na makampuni yao binafsi wapate fursa ya kununua hisa.

Agizo kama hili liliishatolewa enzi za Mkapa na Kikwete...baadaye kikawa kimya kikuu hadi leo huku soko la hisa wakiilalamikia udogo wa soko letu kwa kuwa na makampuni na mashirika machache yaliyosajiliwa....

Tuone haya maagizo yakitekelezwa kwa dhati sasa.
Maza anaongea kuliko vitendo
 
Imenishangaza sana kuona posho ya mtumisho wa umma Tanzania kuwa kiwango cha juu kuliko hata nchi zilizoendelea $4000 kwa siku? Kama hayo ndiyo yamekuwa mazoea hakuna namna nchi hii itaendelea kwa mfumo huu. Hata wakianza kusemana hakuna kitakachoweza kubadilika kwa mfumo ule ule, watu wale wale, chama hicho hicho, katiba hiyo hiyo nasisitiza tena hakuna kitu kitaweza kubadilika. Hayo ni maneno tuu!
Ndiyo maana hawataki mifumo isomane, hata kwa hapa ndani kulipwa 250,000 posho kwa siku ni nyingi sn
 
Back
Top Bottom