Maulid ya mfungo sita viwanja vya Mnazi Mmoja 1963

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,268
Mzee Kissinger baada ya miaka 16 kupita toka ilipotoka tafasiri ya Kiswahili cha kitabu cha Abdul Sykes ndiyo kwanza kakisoma sasa na ananieleza kuwa amekuwa akikisoma usiku hadi amekimaliza.

Lakini kuna kipande katika historia ya Sharif Badawy na kaka yake Sharif Hussein sikueleza chote kwa ukamilifu wake.

Inawezekana kuwa Shariff Hussein Badawy na nduguye Mwinyibaba wakawa ndiyo Waafrika wa kwanza Tanganyika kupigwa PI yaani Prohibited Immigrants – Wahamiaji Wasiotakiwa.

Nini kisa cha ndugu hawa wawili kufukuzwa Tanganyika mwaka wa 1963, miaka miwili tu baada ya Tanganyika kupata uhuru wake?

Katika Maulid ya Mfungo Sita mwaka wa 1963 Mwinyibaba alipanda jukwaani kujibu hotuba. Majibu kutoka kwa kijana mdogo Mwinyibaba yalikuwa makali sana kama ilivyo ada ya vijana.

Damu zao zinachemka na hawachagui maneno lile linalokuja ndipo hilo litatoka kinywani.

Mzee Kissinger alikuwapo katika maulid yale pale Mnazi Mmoja usiku ule na yeye pia kama alivyokuwa Mwinyimababa, pia alikuwa kijana.

Katikati ya khutba ya Mwinyibaba iliyokuwa inaunguruma katika vipasa sauti vilivyoenea pale uwanjani ilisikika sauti ikitokea sehemu ya nyuma karibu ya Hospitali ya Mnazi Mmoja ikipiga ukelele, ‘’Unachanganya dini na siasa.’’

Sauti hii ilikuwa sauti maarufu hakuna katika mji wa Dar es Salaam mtu ambae alikuwa haijui sauti hii.
Hii ilikuwa sauti ya Rashid Sisso.

Mpigania uhuru, mmoja wa vijana wa mwanzo kuingia TANU na kufanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi kujiunga na TANU na kubwa zaidi Rashid Sisso alikuwa rafiki wa Mwalimu Nyerere sasa Rais wa Tanganyika.

Katika watu waliokwenda uwanja wa ndege kumsindiza Mwalimu Nyerere katika safari yake ya kwanza UNO, Rashid Sisso alikuwa mmojawapo pamoja na Idd Faiz Mafungo, Bi. Tatu bint Mzee, Bi. Titi Mohamed, John Rupia, Zuberi Mtemvu, Robert Makange, kuwataja wachache.

Katika mikutano ya TANU Rashid Sisso akisimama nyuma ya Mwalimu Nyerere wakati akihutubia. Mwalimu Nyerere akampachika jina akawa anamwita, ‘’Afisa,’’ Hakuna ajuaye kwa nini alimpa jina hilo.

Sauti ya Rashid Sisso ili ilikuwa sauti ya onyo kali na Rashid Sisso hakuwa mtu wa kupuuzwa. Mwinyibaba alipuuza zauti ile na aliendelea na khutba yake kali hadi alipomaliza.

Watu walijua kuwa Mwinyibaba tayari alikuwa matatani.

Baada ya Maulid kumalizika walimwendea wakamwambia asisubiri hadi asubuhi akimbie aende kwao usiku ule ule kwani asubuhi taarifa itafika katika vyombo vya usalama na hakuna shaka yoyote askari watamfuata kumkamata.

Mwinyibaba hakupuuza ushauri ule.

Usiku ule ule majira ya saa sita usiku Mwinyibaba akapanda lori la mizigo lililokuwa linakwenda Tanga na hata kabla jua halijapanda siku ya pili Mwinyibaba alikuwa keshavuka mpaka wa Horohoro anaelekea kwao Mombasa.

Asubuhi siku ya pili mapema Mzee Kissinger anapita Msikiti wa Badawy Kisutu anaelekea kazini kwake African Printers, anawaona maofisa wa Uhamiaji Wazungu wawili wanaingia na viatu ndani ya msikiti wa Badawy kuwatafuta Sharif Hussein na nduguye Mwinyibaba kuwapa notisi za PI kuwa wanafukuzwa Tanganyika hawatakiwi kuwapo nchini.

Mzee Kissinger akasimama pembeni na watu wengine wakistaajabu kuwaona maofisa Wazungu wakiwa katika sare zao za kazi wakiingia msikitini bila ya kuvua viatu.

Notisi ile aliipokea Sharif Hussein peke yake.

Ilikuwa siku ya Ijumaa na alikwenda Msikiti wa Kitumbini kusali sala ya Ijumaa na baada ya sala alisimama na kuwaaga Waislam.

Hali ilikuwa ya simanzi sana kwani Sharif Hussein alikuwa na madras maarufu hapo msikitini akisomesha vijana na watoto na sifa kubwa ya madras ile ilikuwa usomaji wa tajwid, nyuradi na kasda za kupendeza katika maulid.

Kundi kubwa la Waislam lilimsikindikiza hadi kutoka Msikiti wa Kitumbini Masjid Badawy na baada ya hapo Sharif Hussein akaondoka kurudi kwao Kenya.

Haya ndiyo aliyonieleza mwalimu wangu Mzee Kissinger ambayo alinambia yalistahili niyaeleze katika kitabu cha Abdul Sykes.

Katika picha ya safari ya Mwalimu Nyerere UNO 1955 wa kwanza kushoto aliyeshika kikapu cha ukili ni Rashid Sisso.

SAFARI YA JULIUS NYERERE UNO 1955.jpg
 

Attachments

  • MWINYIBABA NA MOHAMED SAID.jpg
    MWINYIBABA NA MOHAMED SAID.jpg
    19.7 KB · Views: 1
  • MZEE KISSINGER, MWINYIKHAMIS MUSSA NA MUHARAM KOBE.jpg
    MZEE KISSINGER, MWINYIKHAMIS MUSSA NA MUHARAM KOBE.jpg
    11 KB · Views: 1
Mzee wangu Mohamed Said

Kwa sasa wote hao wanakuja sana Tanzania.
Je amri ya kuondolewa zuio la kuingia
Tanzania liliondolewa kipindi gani?

Niliwahi kusikia Sheikh Nurdin Hussein aliwahi kuzuiwa kutoka maeneo ya Mgombezi?

Je ni kweli? Kama ndio sababu ni nini?

Ntashukuru kupata majibu
 
hujatueleza hiyo hotuba ya mwinyibaba ilikuwa inasemaje, alizungumza nini cha kumfanya aingie matatani
 
hujatueleza hiyo hotuba ya mwinyibaba ilikuwa inasemaje, alizungumza nini cha kumfanya aingie matatani
Laki...
Huwa sielezi kila kitu kwa kuwaonea huruma baadhi ya watu ambao wengine wametangulia mbele ya haki.

Lakini ukisoma kitabu cha Abdul Sykes yote yaliyopitika siku ile pale Mnazi Mmoja nimeyaeleza.
 
Usjl mzee wangu tupo vijana ambao tunataka kurudisha hizza wa mababu wetu waliochangia asilimia kubwa katika uhuru wa tanganyika ila kwa chuki za watu flani flani historia na ukwel ukazimwa kama mshumaa.
 
Back
Top Bottom