Matukio makubwa mahakamani 2012

ndiyomkuusana

JF-Expert Member
Aug 2, 2012
666
421
LEO ni siku ya mwisho kwa mwaka 2012, ambao unaupisha mwaka mpya wa 2013. Makala hii inajaribu kuyatazama baadhi ya matukio makubwa yaliyojiri katika mahakama mbalimbali nchini kwa kipindi cha mwaka mzima.
Desemba 24; Hassanoo anyimwa dhamana
JAJI wa Mahakama Kuu, Zainabu Mruke ametupilia mbali ombi la Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Othman Hassan ‘Hassanoo’ lililokuwa likiomba mahakama impatie dhamana. Jaji Mruke alisema mahakama yake imefikia uamuzi wa kumnyima dhamana Hassanoo ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya sh bilioni 1.1 kwa kusafirisha pembe za ndovu toka Tanzania kwenda Hong Kong nchini China.
Desemba 21: Lema arejeshewa ubunge wake
Mahakama ya Rufaa Tanzania, ilitengua hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 15 mwaka huu, iliyokuwa imemvua ubunge Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), kwa sababu imebaini hukumu ile ilikuwa na upungufu wa kisheria.
Desemba 21: Kesi ya Lulu yahamishiwa Mahakama Kuu
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, aliifunga rasmi kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anayedaiwa kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba na kuihamishia Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Desemba 18: Sangoma anaswa na tunguli
Kifaa maalumu kinachotumiwa na wanausalama kuwapekua watu wanaoingia kwenye eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, siku ya kesi ya uchochezi na wizi wa sh milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49, kilimnasa mganga wa kienyeji, Rajabu Zuberi (30) aliyefika mahakamani hapo akiwa na tunguli.
Novemba 28: Hatiani kwa biashara ya kusafirisha binadamu
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemtia hatiani mfanyabiashara wa ngozi nchini, Salim Ally (61) kwa makosa ya kusafirisha binadamu na kuwatumikisha na kumhukumu kwenda jela miaka 10 au kulipa fidia ya jumla ya sh milioni 17.
Hukumu ya kesi hiyo ya kihistoria na ya kwanza kutolewa katika mahakama hiyo tangu sheria ya usafirishaji haramu binadamu ya mwaka 2008 ilipotungwa na Bunge, ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta.
Novemba 28: Hamad Rashid abwagwa
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitupilia mbali ombi lililotaka mahakama hiyo itoe amri ya kuliita Baraza la Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) na wenzake waje wajieleze ni kwanini walikaidi amri ya mahakama na ni kwanini wasitiwe hatiani kwa kosa la kudharau amri ya mahakama ambalo liliwasilishwa mahakamani hapo na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF) na wenzake 10.
Novemba 23: Maranda, Farijala wahukumiwa tena
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu kwenda jela miaka miwili kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda, na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kughushi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 3.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (EPA).
Novemba 22: Maranda, Farijala wafungwa
Mahakama ya Kisutu imemhukumu kwenda jela miaka miwili Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda, Farijala Hussein na maofisa watatu wa Benki Kuu, waliokuwa wakikabiliwa na makosa ya kughushi, kuisababishia serikali hasara na wizi wa sh bilioni 3.3 katika akaunti ya EPA.
Novemba 20: Askari wa JWTZ wahukumiwa kifo
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa askari wawili wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mmoja wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kusudia, Swetu Fundikira. Askari hao ni MT 1900 Sajenti Roda Robert (42) wa JKT, Kikosi cha Mbweni, MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa JWTZ, Kikosi cha Kunduchi na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni.
Oktoba 18: Sheikh Ponda kortini kwa uchochezi, wizi
Sheikh Issa Ponda na wafuasi wake 49 walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu chini ya ulinzi mkali wa wanausalama kwa kosa la uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya shilingi milioni 59.
Oktoba 15: Shabani Mintanga ashinda kesi
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilimwachilia huru Rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Alhaji Shabani Mintanga, baada ya kuona hana kesi ya kujibu katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya iliyokuwa inamkabili. Mintanga alikabiliwa na kesi ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya kilo 4.8, kupeleka nchini Mauritius mwaka 2008.
Oktoba 9: Rais Mwinyi apanda kizimbani
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi alifuata nyayo za Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, na kupanda kizimbani kutoa ushahidi katika kesi za jinai zilizofunguliwa mahakamani hapo na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Dk. Eliezer Feleshi.
Oktoba 16: Mtoto aliyekojolea Korani kortini
Mtoto (jina tunalihifadhi), alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Devota Kisoka kwa kosa la kudhalilisha na kukojolea kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislamu, Oktoba 10 mwaka huu, huko Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Oktoba 16: Waliochoma makanisa Mbagala watinga kortini
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), alifungua kesi nne kwa mpigo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa washtakiwa tofauti yaliyowakabili na makosa ya kuchoma moto makanisa maeneo ya Mbagala, wizi, uharibu wa mali za watu na unyang’anyi wa kutumia silaha katika vurugu za kidini zilizotokea Oktoba 10 mwaka huu.
Septemba 12: Polisi aliyemua Mwangosi kortini
Polisi Pasificus Cleophace Simon (23) alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Iringa kwa tuhuma ya kumuua mwandishi wa kujitegemea, Daudi Mwangosi katika hafla ya ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, uliofanyika Septemba 2, mwaka huu.
Septemba 5: Serukamba aibwaga CHADEMA
Mahakama ya rufaani nchini, ilitupilia mbali kwa gharama maombi ya kufanyiwa mapitio ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Machi 28 mwaka huu, ambayo ilisema kuwa taratibu za sheria ya uchaguzi na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 yaliyomtangaza Peter Serukamba (CCM), kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, hayakukiuka sheria.
Agosti 21: Ubunge wa Dk. Kafumu watenguliwa
Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ilimvua ubunge aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga, Dk. Dalali Kafumu (CCM) kwa maelezo kuwa taratibu za sheria za uchaguzi zilikiukwa katika kampeni za uchaguzi wa jimbo hilo.
Agosti 10: Papaa Msoffe kortini kwa mauaji
Mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Marijani Abdubakari Msoffe (50) maarufu kwa jina la “Papaa Msoffe” alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Onesphory Kitoli.
Agosti 2: Mgomo wa walimu batili
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi jijini Dar es Salaam, imesema mgomo wa walimu ni batili kwa sababu haukuzingatia matakwa ya kifungu cha 84(1), (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 na uliandaliwa kwa dhamira mbaya. Jaji Sophia Wambura ndiye aliyetoa uamuzi huo ambapo pia aliwataka walimu wote kurejea mara moja kazini.
Julai 24: Maranda, Farijala wafungwa tena
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa mara ya pili tena ilimuhukumu Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na mpwa wake Farijala Hussein kwenda jela miaka mitatu kila mmoja kwa sababu imewakuta na hatia ya makosa sita, likiwemo la kujipatia shilingi bilioni mbili kwa njia ya udanganyifu toka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania.
Julai 13: Aliyemteka Dk. Ulimboka kortini
Raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21) alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na makosa ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Julai 10: Rais wa Madaktari afikishwa mahakamani
Rais wa Chama cha Madaktari nchini (MALT), Dk. Namala Mkopi alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, chini ya ulinzi mkali wa polisi akikabiliwa na makosa mawili, likiwemo la kudharau amri halali ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Julai 23: Lissu ashinda kesi ya kupinga ubunge wake
Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imetupilia mbali kesi ya kupinga ubunge wa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) kwa maelezo kuwa haina mantiki yoyote.
Juni 4: Mbunge Badwel kortini kwa rushwa
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omary Ahmed Badwel, 43 (CCM) alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), akidaiwa kupokea rushwa ya shilingi milioni moja toka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana. Kesi hivi sasa imefikia hatua ya mashahidi wa upande wa jamhuri kuendelea kutoa ushahidi wao.
Mei 7: Mkapa amkaanga JK mahakamani
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, aliikaanga Serikali ya Jakaya Kikwete mahakamani akidai kuwa hakuna ubadhirifu wowote uliofanywa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Prof. Costa Mahalu, katika ununuzi wa jengo la ubalozi nchini humo.
Mei 2: Dk. Mahanga ashinda kesi
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitupilia mbali kesi ya kupinga ubunge wa Mbunge wa Jimbo la Segerea, Dk. Makongoro Mahakanga (CCM) iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya CHADEMA, Fred Mpendazoe kwa maelezo kuwa kesi hiyo haina mantiki kisheria. Mahakama hiyo ilimtangaza Dk. Mahanga kuwa ndiye mbunge halali wa jimbo hilo.
Mei 29: Idd Simba aburuzwa kortini
Hatimaye sakata la ufisadi katika Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), lilifikia tamati kwa serikali kumfikisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Waziri wa zamani, Idd Simba kwa makosa ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kulisababishia hasara ya sh bilioni 2.3. Mbali na Simba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, wengine ni Mkurugenzi Salim Mwaking’inda na Meneja Mkuu wa shirika hilo. Victor Milanzi.
Mei 24: Mnyika ambwaga Ng’umbi
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilipigilia msumari wa mwisho kwa kusema kuwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CHADEMA, John Mnyika ndiye mbunge halali wa jimbo hilo na matokeo ya uchaguzi ya jimbo hilo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Novemba mwaka 2010, yalikidhi matakwa ya kisheria.
Aprili 30: Mahakama yatengua ubunge wa Aeshi
Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imetengua ubunge wa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa tiketi ya CCM, Aeshi Hillali iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CHADEMA, katika uchaguzi mkuu uliopita ambaye alikuwa akiomba mahakama hiyo imvue ubunge kwa sababu alishinda kwa hila.
Aprili 23: Ntagazwa kortini kwa udanganyifu
Aliyekuwa Waziri mwandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa awamu tofauti, Arcado Ntagazwa (65) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa kosa la kujipatia kofia, fulana zenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 74.9 kwa njia ya udanganyifu.
Aprili 5: Lema avuliwa ubunge
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imetoa hukumu ya kumvua ubunge aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Godbless Lema baada ya kumtia hatiani kwa makosa ya kutoa lugha ya udhalilishaji katika kampeni za uchaguzi mkuu wa jimbo hilo mwaka 2010.
Februari 23: Washtakiwa kesi ya ‘Samaki wa Magufuli’ jela miaka 30
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliwatia hatiani washtakiwa wawili wa kesi ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Tanzania, maarufu ‘Kesi ya Samaki wa Magufuli’ na kuwahukumu kwenda jela jumla ya miaka 30 au kulipa faini ya jumla ya sh bilioni 22.
Februari 20: Dowans yaibwaga tena TANESCO
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitupilia mbali ombi la Shirika la Umeme (TANESCO) lililokuwa linaomba iwaruhusu kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa nchini kupinga hukumu yake iliyotolewa Septemba 28 mwaka jana, ambayo iliruhusu tuzo ya Kampuni ya Dowans iliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuhuhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC) isajiliwe hapa nchini. Kwa sababu hiyo haina mamlaka ya kuwaruhusu kwenda katika mahakama hiyo ya juu nchini.
Januari 11: Wanafunzi UDSM waenda jela kwa kukosa dhamana
Wanafunzi wanne kati ya 51 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wanaokabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko haramu, wamepelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana waliyopewa.
Januari 10: Hamad Rashid aitia kitanzi CUF
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), na wenzake 10 waliwasilisha maombi madogo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakiiomba itamke kuwa uamuzi wa Baraza la Uongozi Taifa la chama hicho uliomvua uanachama yeye na wenzake ni batili.
Januari 10: Raia wa Burundi kortini kwa kukutwa na risasi 682
Raia wa Burundi, Ismail Stefano (39) jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka ya kukutwa na silaha mbili aina ya SMG na risasi 682.
 
Back
Top Bottom