Mambo Usiyo yajua Kuhusu Hayati Mwl.J.K.Nyerere

mchawi wa kusini

JF-Expert Member
Apr 18, 2018
805
810
Habari Ya Usiku huu Wana JF njoo tuungane na Mimi Twende Kwa Baba Wa TAIFA nisiwachoshe Sana let's go

MAMBO USIYOYAJUA KUHUSU HAYATI MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE:

Tarehe 14 ni siku maarufu sana hapa Tanzania,siku ya Nyerere Day! 14.10. Ya kila mwaka

Najua mnajua mengi kuhusu Mwalimu, lakini pia najua kuna machache ambayo wengi hawajui.

Mwalimu Julius Nyerere alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa nchi huru ya Tanganyika, baadaye Tanzania na hatimaye Rais wa kwanza pia wa Tanzania. Alikuwa mtu mwenye maono yake, ambayo yalikuwa ni pamoja na kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki na umoja wan chi zote za kiafrika.

Kwa hiyo alikuwa mwanachama dhahiri wa vuguvugu la muungano wa Afrika, Nyerere aliiongoza Tanganyika kupata uhuru kutoka Uingereza na baadae akaiunganisha na Visiwa vya Zanzibar na kuunda Tanzania ya leo. Sera yake ya kipekee ya Ujamaa inasifiwa kwa kuipa nchi yetu ya Tanzania utambulisho wa kitaifa.Nahisi bila ujamaa tungekuwa tu kama nchi zingine na tungesambaratika kuliko hata nchi hizo, kwa sababu tunamakabila mengi mno.

Nyerere aliishi wapi?

Alizaliwa mwaka 1922 katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoani Mara katika iliyokuwa Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania. Baba yake alikuwa ni Chifu na alikuwa na wake 22!

Ndugu wengine wa Mwalimu kwa upande wa Baba ni Joseph Kizurira Nyerere (JK Nyerere), na John Kiboko Nyerere (JK Nyerere), hawa ni ndugu wa tumbo moja. Alisomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na baadae alisomea Uchumi na Historia katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uskochi.

Alijulikana kwa kitu gani?

Alijulikana zaidi kwa jina lake la "mwalimu". Nyerere kwa hakika alisomesha Baiolojia na Kiingereza kwa miaka mitatu kabla ya kuiongoza Tanganyika katika kupata uhuru na baadaye kuwa rais wa kwanza wa Tanzania.

Alipenda sana kuiona Afrika inaungana na kuwa moja. Lakini alipingana na Kwame Nkrumah wa Ghana katika suala hilo. Nyerere alitaka hatua ya kwanza iwe kuungana kwa nchi za Afrika Mashariki, wakati Nkrumah akigombania kuungana kwa nchi zote za Afrika kwa wakati mmoja. Kwa kushirikiana hata hivyo, waliunda Umoja wa nchi huru za Afrika, OAU. Nyerere aliwakaribisha wapiganaji wa uhuru. Baaada ya kupata uhuru wa nchi yake, aliwakaribisha na kuwaunga mkono waasi waliokuwa wakizipinga serikali za Msumbiji, Afrika Kusini, Namibia na nyinginezo. Mwalimu ni shujaa wa Afrika.

Julius Nyerere alikuwa anajulikana sana kwa kitu gani kingine?

Mwalimu Nyerere alitafsiri katika lugha ya Kiswahili vitabu vya mwandishi gwiji wa Kiingereza, William Shakespeare-Ulijua hili?

Nyerere alikuwa mkaidi kiasi gani?

Katika kipindi cha vita baridi, Nyerere hakuegemea upande wowote. Wakati Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani iliiomba Tanzania kuachana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani kulingana na Kanuni zake za “Hallstein” lakini Nyerere alikataa, akiwa tayari hata kupoteza misaada ya kimaendeleo iliyokuwa ikitoka Ujerumani, alisisitiza juu ya umuhimu wa uhuru wa Tanzania. Alisema nchi yake "haitakubali msaada kwa masharti" - na hatimaye aliwashinda. Nchi yake iliimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Ujerumani zote mbili za wakati huo.

Mwalimu alianzishaje Ujamaa?Ni nini hasa?

Kutokana na kwamba alitoka katika familia kubwa, na mfuasi ya jumuiya ya watu wenye kuunga mkono falsafa ya ujamaa nchini Uingereza (British Fabian Society), Nyerere alianzisha mfumo wa Ujamaa wa Afrika uliojaribu kujumuisha mfumo wa maisha wa Kiafrika wa kuishi kwa pamoja.

Alijadiliana na Jomo Kenyatta, na kuna wakati alikuwa tayari kumpa nafasi Kenyatta kuwa kiongozi wa Afrika Mashariki yote. Alikuwa tayari hata kuusogeza mbele uhuru wa Tanganyika, na kuziongoza nchi nyingine tatu za Afrika Mashariki kupata uhuru wao kwa matumaini ya kuungana pamoja baadae. Viongozi wengine wa nchi hizo za Afrika Mashariki walikuwa wabinafsi, walimuendea kinyume lakini hilo halikumrudisha nyuma Nyerere.

Alielekeza juhudi zake katika kuyaunganisha pamoja makabila mbalimbali ya Tanzania, mfano moja ya mbinu alizozitumia ni kuhakikisha lugha ya Kiswahili kinazungumzwa na wote kama lugha rasmi ya taifa.

Nini maana ya jina lake la Kambarage?

Kwa mila na tamaduni za kizanaki na hata tamaduni za makabila mengi barani Afrika,mtoto hupewa jina kulingana msimu,muda na tukio wakati anazaliwa. Kambarage ni jina apewalo mtoto aliyezaliwa siku ya mvua. Mwalimu Julius Nyerere alizaliwa usiku wa mvua kali, Aprili 13, 1922 hivyo akaitwa Kambarage. Kambarage maana yake ni mzimu wa mvua. Kama angekuwa mjaluo angeitwa “Okoth.”

Mwalimu alipataje jina lake la Julius?

Aliendelea kulitumia jina la Kambarage mpaka mwaka 1942 alipobatizwa na kuwa mkristo rasmi. Alilichagua jina la Julius akivutiwa na mtawala wa zamani wa milki ya Roma, Julius Kaizari (Caesar) na ndipo akaitwa Julius Kambarage Nyerere kwa sababu hakutaka kuliacha kabisa jina lake la asili.

Alichelewa sana kubatizwa kwa sababu wamisionari walihisi angerithi uchifu wa baba yake. Baba yake, alikataa Ukristo kata kata! Wamishenari walipomshawishi kuachana na dini asili na kujiunga na Ukristo, aliwauliza Ukristo una nini ambacho dini za asili hazina. Walimjibu, upendo, amani, unyenyekevu, uii na haki, naye aliwajibu tena kwa mifano hai jinsi wanavyohubiri upendo, amani, unyenyekevu, utii na haki. Mwaka 1942, baba yake, Chifu Burito Nyerere alifariki, na uchifu ukarithiwa na kaka wa Kambarage aliyeitwa Edward Wanzagi. Wamisionari wakapata nafasi ya kumbatiza. Alibatizwa akiwa anasoma Tabora.

Kwa nini Mwalimu alichelewa sana kuanza shule?

Alianza shule ya msingi 1934 akiwa na miaka 12. Alichelewa kuanza kwa sababu baba yake hakutaka mwanaye asome. Akiwa na miaka 11, alicheza bao na kumfunga mzee mmoja, rafiki wa baba yake. Huyo mzee akamshauri Chifu Burito kumpeleka mwanaye shule, mzee akakubali. Alianza mwezi Aprili wakati wenzake walianza tangu Januari.

Na vipi kuhusu umahiri wake wa lugha za Kiswahili na Kiingereza?

Wakati anaanza shule Mwalimu Nyerere hakujua kabisa lugha ya Kiswahili. Lakini alikuwa mtu mwenye akili san ana mtu mwenye uwezo mkubwa wa kujifunza haraka sana, haikupita muda akajua lugha ya Kiswahili,na ndo maana hata lugha ya Kiingereza alikuwa na uwezo nayo vizuri sana.

Wakati huo, shule zilianzia darasa la kwanza mpaka la nne baada ya hapo kunakuwa na shule nyingine ya kuanzia darasa la tano mpaka la nane. Kwa hiyo alitakiwa asome miaka minne halafu afanye mtihani wa taifa lakini kutokana na uwezo wake mkubwa, alisoma miaka mitatu pekee kwani alipomaliza darasa la pili 1935, alirushwa mpaka la nne na kufanya mtihani wa taifa mwaka1936 ambao aliongoza Tanganyika nzima (Genius)

Mwalimu alikuwa mkorofi au mtetezi tu wa haki?

Mwaka 1937 alianza darasa la tano Tabora. Akiwa huko, alikuwa ni mtoto mkaidi sana!. Adui zake wakuu walikuwa ni “Makaka”. Walimu wakaamua kumpa cheo cha kaka(kiranja) ili kumnyamazisha. Kulikuwa na utaratibu wa makaka kupata upendeleo wa kujigawia chakula. Alipopewa cheo hicho, akaanzisha harakati za kuleta haki sawa kwa wote. Katika kutekeleza hilo, aliitisha mgomo kwa wanafunzi wote mpaka upendeleo ule uondolewe na akafanikiwa.

Pia alishitakiwa mara kadhaa kwa mwalimu mkuu na ukafikia wakati mwalimu mkuu akaamua Julius afukuzwe shule!. Mwalimu wake wa darasa licha ya utundu wake, alimpenda sana kwa sababu alikuwa na akili sana, hivyo akamnusuru kufukuzwa.

Mwalimu alichukia sana ukabila na ubaguzi wa aina yoyote ile!

Misemo maarufu ya Mwalimu Nyerere:

1. Uhuru na kazi.
2. Hakuna taifa lenye haki ya kufanya maamuzi juu ya taifa lingine, wala hakuna mtu mwenye haki ya kumfanyia maamuzi mtu mwengine.
3. Umoja hautatufanya tuwe matajiri, lakini itaifanya vigumu kwa Afrika na Waafrika kupuuzwa na kufadhaishwa.
4. Elimu sio njia ya kuepukana na umaskini, ni njia ya kupambana nao.
5. Ili kupata maendeleo ya kweli, watu lazima wahusishwe.

Pumzika kwa amani shujaa.

#GodBlessTanzania
#GodBlessAfrica
 
Back
Top Bottom