Maisha yangu ni chaguo langu, maisha yangu yamekuwa ni hadithi ya kusimulia. Kila baada ya mwaka mpya. Heri ya siku yangu ya kuzaliwa

Jumanne Mwita

JF-Expert Member
Nov 18, 2014
424
1,044
picha.jpg

Habari za leo rafiki naitwa Jumanne Mwita,
Leo ni tarehe 06/06/2022 Kila ifikapo siku yangu ya kuzaliwa, huwa naandika moja ya makala kwa ajili yangu, kwa sasa nimetimiza miaka kadhaa ambayo kwangu mimi ni miaka mingi kidogo sihaba hapa nilipofikia pia namshukuru Mungu niko hai bado.

Miaka hii niliyonayo ni michache kwa wengi na mingi kwa wengine. Kwa upande wangu miaka hii imekuwa miaka ya kujifunza mambo mengi sana kuhusu maisha, watu na mafanikio kwa ujumla.
Kila inapofika tarehe ya kuongeza mwaka mwingine kwenye maisha yangu, huwa natenga muda wa kuyatafakari maisha yangu, kuangalia nilipotoka, nilipo na ninapoelekea. Huwa nafanya tathmini ya kina ya kila ninachofanya na kuona ni kwa jinsi gani nachangia au kukwamisha kufika kule ambapo ninataka kufika.
Na kipindi hichi pia nimepata nafasi ya kutafakari kwa kina kuhusu maisha yangu na kila ninachofanya. Katika tafakari hiyo, nimefikia maazimio mengi, ambayo nitakuwa najiwekea kumbukumbu hii ndogo ndogo kadiri nitakavyojaliwa kuwepo hapa duniani.

Kwa sasa ninakwenda kukaribia muongo kwenye maisha yangu, huu ni muongo ambao kwenye maisha ya kila mtu una maana kubwa sana. Katika umri wa miaka kadhaa, najua kila mtu anakuwa na ufanisi mkubwa sana kwenye maisha yake, kipindi ambacho mtu anakuwa ameshajifunza mengi kwa kujaribu jaribu mengi kwenye muongo uliopita na hivyo anakuwa ameshajua nini anataka kufanya na maisha yake.
Ninafanya haya kwa sababu naweka kumbukumbu zangu sawia maana nikikumbuka nilikotokana, bado sifahamu nitaishiawapi ndio Napata ujasiri wa kuwa mwandishi wa Makala kama hizi kila ikifikia siku kama ya leo.

Picha ya familiya.jpg

Historia Fupi Ya Maisha Yangu

Mwaka 2005 nikiwa na familia yangu na huyo mama unaye muona ndiye mama mzazi, aliyepata uchungu siku ya kuja kwangu hapa duniani. Hao wengine kulia ni dada yangu anaitwa Annastazia na kushoto ni kaka yangu anaitwa Machage, wote tuko hai tunashukuru Mungu kuendelea kutupigania mpaka sasa tunaishi.
Mwaka 2000 Tulihamaia Kahama tukitokea Mkoa wa Mara Wilaya ya Bunda, kijijini huko sema vijiji vya huko sivijui kwa sasa ila nakumbuka kata ni GUTA tulipokuwa tukiishi ni sehemu moja inaitwa Nyantare. Kijiji hiki kinaaminika kwa uchawi kipindi cha nyuma palikuwa na wachawi wengi mno unawangiwa mchana kweupe, kwa sasa sijui kama mambo hayo yapo ingawa ni kwetu kabisa ambako mzazi mmoja anatoka ila sikuwahi kurudi toka 2000 mpaka leo hii mwaka 2022.

Nimezaliwa Mkoa wa Mara Wilaya ya Bunda, Kahama tulihamia baada ya babu na bibi kizaa baba kufariki, hivyo baba yetu mkubwa aliyekuwa akiishi Kahama alipokuja kijijini kwenye msiba wa baba yake, ambapo yeye ndio kijana wa kwanza kwao. Siku babu amefariki zilipita siku kama mbili ile ya 3 ndio ilikuwa maziko ya mwili wake, bibi nae alifariki ghafla siku hiyo tunamzika babu. Kwa hiyo tukazika babu na bibi kwa wakati mmoja, hivyo baba yetu mkubwa alipotaka kuondoka kurudi Kahama, aliwaambia baba na mama kwamba inabidi muhame hapa kijijini twende kuishi mjini, ambako ni Kahama. Kwenye ghalama hapo siwezi jua alichangia au tuliuza ng'ombe maana ng'ombe tulihamishia kwa ndugu tukaondoka na vyombo tu, mambo mengine tuliyaacha kijijini.
Hata hivyo baada ya kuwa tumefika Kahama mambo yalikuwa ni magumu na hakukuwa na ahueni yeyote, iwe kwa mama au baba wote hawakuwa na kazi ambayo ingetuingizia kipato na kutufanya tuishi kama watu wengine wanaofurahia maisha hapa duniani.

Mwaka 2002 baba alisafiri kwenda Dar es Salaam kwa mdogo wake aliyekuwa anaishi huko, tulibaki na mama alikuwa ni mtafutaji na ni mpambanaji naweza kumuita kwa jina hilo, maana najua haso anazopitia na alizopitia kututunza mpaka hapa tulipofika. Maisha yetu hayakuwa mazuri sana katika ukuaji wetu, wazazi wote hawakuwa na kazi za kueleweka, hata baada ya baba kwenda Dar es Salaam. Hakuna badiliko lolote wala unafuu wowote kwenye maisha ya nyumbani.
Kule kijijini tulikotoka wote walikuwa wanajishughulisha na kilimo tu, msimu ukifika ni kulima baada ya msimu kuisha. Mama alikuwa akijishughulisha na uuzaji wa togwa/Bhusara kwa lugha ya kikulya huitwa hivyo, alikuwa akipeleka kwenye minada, kule kwetu tunaita "Mtera" ila kwa mjini huita "mnada" mnada ni mchanganyiko wa wauza mifugo, wauza nafaka na wauza nguo n.k.

Baada ya mama kuhangaika kutafuta chakufanya alianza kufanya vibarua vya kualilia nyumba za watu baadae akaacha ikabidi asome upepo wa Kahama maana maisha bado ni magumu. Ilibidi akapige mawe mlimani, palipo na shule ya Rocken Hill kwa sasa ni Shule ya Private Kubwa sana pale Kahama-Nyasubi, kipindi hicho haikuwa hivyo ilivyo palikuwa wazi tu. Mama alipiga kokoto muda mrefu kidogo kabla ya kubadili kazi nyingine, ilifika kipindi akachoka ikabidi ahamie kwenye uuzaji wa mahindi ananunua kutoka kwa mkulima na yeye anauza palepale ilienda hivyoo baadae tukawa tumehama kutoka pale tulipofikia ambako ni kwa baba yetu mkubwa na yeye ndie aliyetutoa kijijini kutuleta mjini, baada ya kuwa yumepata mwanga wapi tutaanzia ilitubidi tuhame pale tujitegemee.
Nitaruka ruka vipengele kwa sababu nataka nitoe vyenye vinagusa zaidi maisha yangu hata na wewe huenda ukawa unaguswa kwa namna moja au nyingine, maana kila mmoja ana mikasa yake mpaka hapo alipofikia.
Nakumbuka ilikuwa mwaka 2004 njaa ilitukumba kwetu, hatukuwa wakulima wala wafanyabiashara, mama yangu ndio namtaja hapa. Maana yeye ndio naona kama nguzo mhimu sana kwangu na hata kufika hapa ni sababu yake ingawa baba alikuwepo.

Mwaka huo tulipatwa na njaa isiyo yakawaida kuna muda tulikuwa tunapika maji, kuonesha kwamba tunapika kumbe tunachemsha maji tu. Hata unga wa kupika uji tukawa tunausikia tu yaani hata kuusikia uji ukoje na unga wake unatoshelezaje kuupika tukawa hatuna. Kwa upande wangu kuacha kaka yangu na dada yangu mimi pekee nilipata njaa ya siku 7 nilichokuwa naambulia ni maji tu, siku ya 5 tulibahatika kuletewa unga wa uji na rafiki yake mama aitwae kwa jina la Mama Ghati tena alituma watoto. Unga ule baada ya kuisha mpango wa uji ukawa umeisha, kilichokuwa kimebakia ni kuangalia namna nyingine maana hamna kitu chochote.
Kilichofuata baada ya kuwa nimekunywa uji baada ya siku kadhaa bila kula chochote, nilienda kwenye shamba la watu walilovuna mahindi wakamaliza, nilienda kwa ajili ya kuokoteza mahindi yaliyodondoka na mengine ambayo huwa yakisahaulika kuchumwa huenda nikapata hata kimfuko cha rambo. Nilijikaza hivyo hivyo, bahati nzuri kweli nilifanikisha kuokota kimfuko cha rambo kama nilivyokuwa nimewaza nikafanikiwa.
Baada ya kuyapata nilirudi nayo nyumbani kuyapukuchua na kuyatengeneza, nilipomaliza kimbembe kilikuja kuyasaga nikajikuta nachoka ghafla mahindi kweli nimepata kazi ikaja kupata hela ya kwenda kusagia?

Naipataje?​

Nilipata wazo nilipokuwa naokoteleza mahindi kwenye lileshamba ndipo palikuwa na mashine ya mafuta ya kusaga unga. Hivyo nilichofanya nilienda moja kwa moja nikapanga foleni na mahindi yangu kwenye rambo ya blue.
Niliona nikimwambia hajasaga hatakubali atakataa kunisagia, hivyo ataomba kwanza hela nilisubili alipo maliza ndipo nikamfuata na kumueleza. Mzee mimi sikuja na hela sikuwa nayo kabisa naomba unisaidie sina chochote nachoweza kukuahidi kwamba nitakuletea naomba nisaidie, alikataa kabisa ila nilimuomba kwa huruma mpaka nikaanza kulia. Baadae sana huruma ilimuingia akaniambia chukua mzigo wako uende siku nyingine uje na hela.
Nilifurahi ingawa nilishalia kabla ya msaada huo sikujali wala nilichokuwa na waza ni unga nipate nikasonge walau ugali nile kwa leo. Baada ya kufikisha unga nyumbani, nilikuta kaka yangu na dada yangu wamerudi, tulipika ugali, hatukujali mboga hamna wala nini tulichojali ni ugali kwanza uive. Baada ya kupika ugali kimbembe kikageukia kwenye mboga! Hapo kwanza mimi nilisha anza kuula kabla hawajaepua, nilikuwa naulia kwenye sufuria, yaani kwa lugha nyingine naumanga bila mboga. Ulipoepuliwa nilichofanya wenzangu muda huo wanawaza walie nini mimi nilisha pata chumvi nilienda kuomba kwa jilani.

Ile chumvi niliyokuja nayo iliiloweka nikaloweka ikawa na radha nzuri tu, nikapiga zangu ugali yaani nilivyomaliza kula tu nilipata na usingizi moja kwa moja palepale kwa sababu sikuwa napata usungizi zaidi ya siku kama 3 silali na kunywa uji nikikosa nakunywa maji nalala siku hiyo niliona shida nimezipiga teke kwa mlo huo mmoja, hata hivyo nilishukuru kuweka chochote tumboni.
Ilipofika jioni muda wa mama kurudi kutoka kwenye kibarua chake, alikuwa dalali wa mazao kwa wakulima wanaoleta mahindi na kuuzia wafanyabiashara. Wanaouza rejareja kwa wateja, mama hakuwa na mtaji wa kumfanya anunue hata gunia moja. Yeye kazi yake ilikuwa kuelewana na mkulima endapo mkulima akikubali kumuuzia, anakwenda kuomba hela kwa mtu ambaye anamtaji wanaungana kwenye ule mzigo, hivyo mwenye mtaji anapata pesa bila ya kutoa jasho.

Hivyo anaweza kupata mkulima wakapatana amuuzie, kama umewahi kufanya biashara utaelewa huwa wakulima wanatabia zipi kukugeuka ni mara moja hawanaga msimamo. Akifika sehemu husika mkulima akiona mteja aliyemuuzia siku za nyuma wewe uliyekujanae anakuacha hapo anaongea na yule aliyemuuzia mzigo alioleta. Hivyo unaweza kupambana siku nzima, usipate mkulima na pesa pia usipate ikifika jioni unaamua kurudi nyumbani. Hiyo ndio kazi mama alikuwa akiifanya sehemu moja inaitwa Rami iko Kahama-Shinyanga, kama kunamtu anafahamu Kahama sehemu hiyo inayoitwa Nyihogo kuna kasehemu panaitwa "rami" kwa sasa sijui kama bado jina lile linatumika au laaah!

Tuendelee, baada ya mama kurudi kutoka kwenye mihangaiko yake na amechoka hajui ataipa nini familia yake, alikuta tumekula na unga upo mwingine wa usiku, mama alifarijika sana kwa kile alichokiona alijikuta akibubujika machozi, huku asijue nini afanye juu ya familia yake. Kumbuka muda huo baba alisafiri kwenda Dar es Salaam kwa mdogo wake hivyo familia ilibaki mikononi mwa mama pekee. Mama alilia alikosa la kutuambia tulipika ila yeye hakula alisema ameshiba ila hakuwa amekula popote, tulijua mama alikuwa anawaza mengi sana ila hakuwa na namna tulipika ugali tena tukala na maji ya kuloweka na chumvi.

Maisha yakaendelea baada ya siku za mbeleni ilikuja njaa nyingine tena hii sasa ilitubidi tujiongeze zaidi ya mwanzo, hii ilitutandika tukakumbuka hapo tulipokuwa tukiishi kwa mbele yetu mita kama 30 hivi kuna sehemu wanafuga nguruwe. Ilitubidi twende tukaombe mabaki ya Nguruwe, yaani yale machakula ya maugali na mawali mchanganyiko humo humo. Tulipoenda kuomba yule mlishaji wa Nyuruwe alikuwa anatufahamu tunapoishi kwa majina simfahamu, siku nikimuona au kukutana naye nitampa chochote kama shukrani. Baada ya kumuomba alituuliza kwanza mnapeleka wapi haya mabaki ya chakula? Tulimwambia hapa tulipo tunanjaa hatujala siku ya 3 sasa!
Hivyo tumeona hatuwezi kufa wakati chakula kipo hapa, hikihiki tunacho kiona kitatufaa, alituuliza maswali lakini. Ila baadae alitupa mabaki mazuri tena yale yaliyofunikwa kwenye pipa kubwa tu ya moto kabisa. Niweke sawa hapa mabaki haya ni kile chakula wanachopikiwa watoto wa shule, makaki haya alikuwa akiyatoa shule inaitwa Rocken Hill. Shule hii ipo Kahama inapokea watoto wa Boarding na Day, alikuwa akienda anachukua yale mabaki watoto wanayokula, mengine alikuwa anapitia kwenye mahoteli yaani na migahawa anaongezea analetea Nguruwe.
Tuliendelea kula yale mabaki tunayopata kutoka kwa yule baba kutoka manguruweni, hapo tukaona unafuu wa maisha tumeupata na nguvu za kwenda na shule tunazo. Tukawa tukitoka shule tunaenda pale kwenye manguruwe, yule baba tunamshukuru alikuwa ameisha elewa hali zetu zikoje alikuwa anatutunzia. Muda mwingine anatuita akituona tupo pale nyumbani, naomba niishie hapo mambo ni mengi nimepitia hicho kilikuwa kionjo tu kuna muda nitaweka hapa maisha yangu yote maana niko naandaa kitabu.

Mpaka sasa kwa mengi niliyopitia nimekuwa napata elimu ya namna gani uishi na watu, nawezaje kuwa mtu mwenye matatizo nikajionyesha ni mtu mwenye furaha. Uaminifu pia nikitu ambacho ninakiweka mbele ya maisha yangu na sihitaji kujaribu kufanya vitu viovu au kuwa mtu tofauti na yule kijana niliyetoka katika maisha duni.
Katika mapito yote niliyopitia na tuliyopitia mama yangu alitujenga kimawazo na namshukuru sana kwa hilo. Maana alipata muda mwingi sana wa kutusihi na kutuambia mambo ambayo tunatakiwa kuyafanya, endapo akiwa hayupo au bado yupo na mpaka sasa nayaishi maneno yake na mpaka hapa nilipo ni sababu yake yeye mama. Namuombea aendelee kuishi maana namtegemea sana bado katika maisha haya.
Katika miaka inayokuja ni kipindi ambacho nitakwenda kujisukuma zaidi, nitakwenda kuweka juhudi kubwa mno kwenye maisha yangu, ili kuweza kupiga hatua kubwa zaidi ya nilivyotarajia kupiga.
Nakusogezea Na Hii Kidogo Maana Leo Ni Siku Yangu Basi Hata Mengine Inabidi Niyakumbuke Soma Hapo Chini.
Juma4 459.jpg

“Hakuna mtu ambaye anaweza kufanikiwa kutimiza malengo aliyonayo kwenye maisha yake kwa kufanya peke yake, kila mtu anahitaji watu wengine ili aweze kufanikiwa”​


Mwaka 2018 tulipiga picha hii tukiwa Bukoba imebeba ujumbe mkubwa sana kwangu ndio maana katika siku hii, imekuwa na nafasi sana hapa na nimeitumia kutoa somo kwa mtu anayepigania maisha yake. Akijua anawatu wanaomsaida au kwa namna moja au nyingine, itakubidi utenge muda wako kujua nini ambacho na maanisha hapa.
Katika harakati za kuyafanya maisha yawe rahisi, mnamo mwaka 2017 mkurugenzi wa kampuni moja hapa Tanzania sitoitaja jina, niliyokuwa nikifanya kazi toka 2013-2017 alituwezesha mimi na wapwa wake wawili. Aliweka wazi nini anafanya kwetu na alicho kikusudia nikiwemo na mimi.

Hata hivyo mambo yalikwenda vizuri ingawa changamoto hazikosekani katika kazi yeyote, huwezi kutegemea mtelemko kila utakacho fanya lazima ule msoto kwanza ndio kipimo cha mafanikio kilivyo endapo hata ukizipata/ukipata ujue namna ya kuitumia kwa adadu/heshima.
Hivyo mategemeo yetu yalikuwa mazuri kulingana na upepo wa biashara mwanzo ulivyo tupokea na wateja katika biashara tuliyoifanya ilionekana kuwa nzuri baada ya wateja kukubali huduma zetu.
Mambo yalianza kwa ugumu baadae tukapata ahueni kiasi flani, tukaona mambo yanaenda kuwa sawa, walau nasi tupate ahueni katika haya maisha. Ila hatukujua yambeleni ni yapi nakumbuka msemo mmoja usemao "jambo usirolijua ni kama usiku wagiza"mambo haya kuwa kama tulivyokuwa tukifikiria na sikuzote kitu ukikitegemea kwa 100% huwa hakifanikiwa kamwe weka 30% hadi 20% hapo umakini utakuwepo zaidi.
Kilichotokea uaminifu ukawa ziro na ndio mwanzo wa kuanguka ulipoanza taratibu, mwisho wasiku tukapata shoti/hasara kubwa ambayo katika ufanyaji wangu wa kazi, sikuwahi kupata hasara kubwa kama ile ambayo jumla ilikuwa Tsh. (7,000,000/= milioni saba). Jambo ambalo niliona kabisa hapa ndoto za kufanikiwa zimeisha yeyuka tayari.

Baada ya kupata pigo hilo na mzunguko wa biashara kukwama ilibidi kufunge, maana kulitokea sintofahamu ya kushutumiana kama nilivyosema hapo juu, biashara ile walikuwemo ndugu wa boss yaani wapwa wake hivyo wazazi walikuja juu na maneno mengi yakasemwa. Wengine hawakutaka mtoto wake ashtumiwe na kumkingia kifua kuwa mtoto wake hakushiriki kuua ofisi, hivyo shutuma nyingi ziliangukia kwangu. Sikuwa na chochote cha kujitetea maana ukweli nilikuwa na ujua na ukitaka mtu aongee ili atoe sumu aliyonayo ni kumuacha aongee usimuingilie niliyeona anaongea kupitiliza nilimuacha aongee. Katika watu waliokua wanafanya kazi kwa kujitoa mmoja wapo nilikuwa mimi, nilifanya kazi kwa juhudi zangu zote nikijua kwamba muda utakapo fika tukafanikiwa matunda hayatakuwa kwangu pekee hivyo ni wote tutafaidika. Ingawa mambo hayakutimia ila kazi niliyofanya tulisogea soegea na kujikuta tunasukuma siku hadi siku na tunavuka vikwazo na mitihani mingi tu.

Bosi alichoka chokochoko na tuhuma za wazazi wanaingilia, ndipo alitoa kauli moja tukusanye madeni tufunge ofisi maneno yamekuwa mengi amechoka nayo.
Baada ya hayo kutokea na kuisha maisha yaliendelea, pia nafanya hivi kufupisha stori ila katika kitabu changu kitakachotoka mengi nitayaweka, ambayo nayaacha hapa nafupisha fupisha, hatimae tulifunga ofisi na mimi nilirudi kwetu nikaanza kuangalia ramani itasomea wapi maana sina inshu tena muda huo.
Nakumbuka nilimrudia boss kumuomba anirudishe kwenye kampuni yake niendelee kufanya kazi ili nipate pesa nimsaidie mama yangu, maisha yetu ni magumu kila mmoja anapambana kivyake na hamna mwenye unafuu atakaye msaidia mwenzake.

Ndipo nilifanya maamuzi nikamtumia boss message kumuomba kazi, nakumbuka majibu aliyonipa yalinivunja moyo sana, nikusihi hata wewe unayesoma makala hii usije ukajibu mtu ukiwa na msongo wa mawazo utajikuta unaharibu hata huo msaada wenyewe. Majibu hayakuwa mazuri kulingana na ile message nilichomjibu mimi nilimwambia "sikuwa na niambaya kama kazi haipo basi" nimenukuu maneno baadhi siyo kwamba nilisema hayo tu. Baada ya hapo nilikaa nyumbani bila kazi muda huo nikitembea maeneo yangu ya zamani kuona namna nitaweza kuisaidia familia yangu pamoja na mama yangu.

Baada ya miezi 2 hivi boss yuleyule alinipigia simu mwenyewe kuwa kazi imepatikana nitume barua ya kuomba kazi, ila anuani tumia ile unayoijua maana alikuwa ananirudisha kwenye kampuni yake. Anasema alinirudisha kwenye kampuni kwa sababu anajua uwezo nilionao,juhudi na kujituma kazini alimwambia mmoja wa ndugu yake mmoja ambaye ndiye aliyeniambia kuwa umerudishwa kazini sababu kuu ikiwa hiyo. Nashukuru maana sikuwa bado nimepata sehemu yeyote, niliandika barua nikatuma baada ya kupokea E-mail yangu ya barua, nilitumiwa nauli kwa ajili ya maandalizi ya safari kesho yake.

Niliporudi kazini kwa mara ya pili muda huu sikufanya makosa, maana hata kazi yetu ya mwanzo sikufanya makosa isipokuwa, malengo yalipishana na wengine. Katika utafutaji kuna watu mtakuwa mnafanya nao kazi ambao wako serius na wengine wapo ilimradi wanakura na wanafanya wanayoweza, hana malengo ya baadae. Mwingine huona ameisha fanikiwa kwa kupata hela ya kununua ngua, kupata msichana anayemtaka mambo ya maendeleo yeye ni kipengele kingine kwake. Kuacha wengine tuliotoka kwenye familia masikini tunapambana ili tutoke hapa tulipo kwenda sehemu nyingine. Hii ni mtihani mkubwa achana na ile mitihani ya kufanya utunukiwe PhDs sijui Degree hii ni zaidi ya hiyo mitihani.

Maisha na mitihani niliyopitia yalinikomaza na nilijifunza maisha na nilijifunza kutumia fulsa, hivyo awamu ya pili niliitumia kama mtu aliye na njaa kwa siku zaidi ya 4-5 ndivyo nilivyo kuwa, nilihakikisha napambana mno na kuweka juhudi, nidhamu na fulsa iliyojitokeza mbele ya utafutaji wangu.

Funzo nililolipata katika maisha yale ni;

Kwenye maisha, kila baada ya muda fulani utakutana na wakati mgumu. Kitu cha muhimu sana ni namna unavyokabiliana na wakati huo mgumu.

Nini Ufanye Unapopitia Wakati Mgumu?.​

INAWEZEKANA unasoma safu hii kwa sababu unajiona kama mtu unayeishi kwenye ukingo wa maisha. Mambo hayaendi kama ulivyotarajia. Umekata tamaa. Ukitazama wapi pa kupata msaada, unaona giza tororo.​

Hakuna tumaini. Ujumbe wangu kwako ni mwepesi. Pamoja na ugumu wa hilo unalopitia sasa, bado lipo tumaini. Muhimu ni kujua kitu gani unaweza kufanya unapopita kwenye nyakati ngumu.​

Ukweli ni kwamba hakuna binadamu anayependa shida. Lakini, hata hivyo, shida hutufundisha mambo ya msingi tunayoyahitaji ili tufanikiwe. Watu wengi waliofanikiwa, kwa mfano, hawakukwepa shida. Hawakutumia shida zao kama kisingizio cha kujihurumia na kuwalaumu wengine. Walizichukulia shida kama mwalimu wa kuwafundisha namna ya kwenda kule wanakotaka kwenda. Ufanye nini unapopita kwenye nyakati ngumu?​

Kuna watu wanapitia wakati mgumu kwa sasa na wanachoona ni aibu iliyo mbele yao. Wanaona kushindwa na kuzomewa na wanaona hawainuki tena. Watu wa namna hii hata maneno yao wanayoongea huwa ni ya kushindwa. Utasikia wanasema “sijui kama nitainuka tena”, . “sijui kama nitapata furaha tena”.​

Usijihurumie Kupita Kiasi​

Kuna mambo ni vigumu kuyakubali yanapotutokea. Ukikubali kilichotokea bila kujali unajisikiaje, hiyo ni hatua ya kwanza inayoweza kuanza kubadili maisha yako.
Changamoto moja wapo inayoweza kukuzuia kukubali hali halisi, ni ile imani kwamba kilichotokea si haki. Ulichotendewa si haki. Unajiuliza, “Kwa nini wengine hawapatwi na kile kinachonitokea mimi?” Pambana na mawazo kama hayo ya kujihurumia. Usipopambana na mawazo kama haya unaweza kuishi na maumivu kwa muda mrefu sana. Wakati mwingine, unapokuwa kwenye magumu kama haya jambo muhimu unaloweza kufanya sio kujiuliza kwa nini kilichotokea kimetokea bali kukubali kwamba ni kweli kimetokea.

Tathmini Kile Ulichojifunza​

Baada ya kukubali kwamba ni kweli sasa huna kazi, kinachofuata ni kile unachojifunza.
Je, inawezekana hukujua namna ya kufanya kazi na mtu asiyekupenda? Je, inawezekana kupoteza kazi ikawa ndio mwanzo wa kufikiri namna ya kuanzisha na kuendesha shughuli zako mwenyewe?
Siku zote kuna upande mzuri kwenye kila kibaya kinachokutokea. Jitahidi kuufahamu upande huo.
Nawafahamu watu wengi waliolazimika kufungua biashara zao na wakapata mafanikio kwa sababu tu walifukuzwa kazi. Wasingefanyiwa fitna kazini na kupoteza kazi, wangeendelea kuajiriwa kwa muda mrefu ujao. Kumbe nyakati ngumu kama hizi ukizitumia vizuri zinaweza kukufungua macho na kubadilisha kabisa uelekeo wa maisha yako.

Usijitenge Na Watu​

Ni kweli, wakati mwingine, kujitenga kunaweza kukusaidia kuwaepuka watu wanaoweza kukufanya ukajisikia vibaya zaidi. Hata hivyo, ukaribu na watu wanaoaminika ni hatua muhimu kuchukua unapopita katika kipindi kigumu. Watu wenye mtazamo chanya, kwa mfano, ndio watakaokusaidia kukutia moyo, kukufariji na kukutazamisha mambo kwa namna itakayochangamsha tena moyo wako.
Kwa vyovyote vile unawafahamu watu katika maisha yako unaoweza kusema unawaamini. Hawa ni watu mnaoaminiana na kuheshimiana. Hawa si watu wepesi kukushambulia, kukuhukumu na kukuonyesha namna gani hali uliyonayo hukupaswa kuwa nayo. Jitahidi kuambatana nao.

Tafuta Msaada Zaidi​

Unahitaji msaada wa mawazo. Mahali pa kuanzia watu ulionao karibu kupitia vikundi vya kijamii ulivyonayo tayari mfano kanisani au msikitini. Hata kama huwafahamu zaidi watu hawa kiundani, bado kwa kule kuwa nao karibu itakusaidia kuyatazama maisha kwa sura ya matumaini. Kaa karibu na vikundi hivi ujijenge kiimani. Nyakati ngumu ziwe kichocheo cha kuwa karibu na Muumba wako.
Lakini pia, ni vizuri wakati mwingine kukutana na watu waliowahi kupitia changamoto yako wanaoweza kukupa mawazo chanya ya namna ya kukabiliana nayo. Kama umepoteza kazi, mathalani, na kuna mtu unayemfahamu aliwahi kupoteza kazi pengine unahitaji kuonana naye kupata uzoefu wa namna alivyoweza kupita kipindi hicho.

Jifunze Katika Haya Maisha Kwa Yale Unayopitia​

Wakati mwingine ugumu wa maisha unatokana na vile maisha yetu yalianza kabla ya sisi kuyafikia. Ndiyo ni sentensi tata, eti maisha kuanza kabla ya kuyafikia.
Wakati unashangaa maisha kuanza kabla ya kuyafikia, inaenda mbali zaidi, yaani yanaweza kuwa yameharibika hata kabla hujayaanza na haupo kabisa katika uso wa dunia. Hayo ndiyo maisha yetu.

MALENGO MAKUBWA NINAYOENDELEA KUFANYIA KAZI BAADA YA KUFELI.


Malengo yangu makubwa kwenye maisha bado ni mengi na ambayo kwa mara ya kwanza nilitamani kuwa nayo ila baada ya haya niliyopitia nimeanza upya na nimefanikiwa mambo kadhaa kuyatimiza.

Lengo kubwa ni kuwa na makazi mazuri katika umri mdogo huu nilionao na hili nimekwisha lianza mapema mnamo mwaka 2020.
Hili ni lengo kubwa sana na wengi hushindwa siyo kwamba hawapendi ni kwa sababu malengo yao yanakinzana na ahadi wanazojiwekea.
Lengo hili lilikuwa ni kupata eneo walau nikipata pesa niweze kujenga taratibu ninapopata vijisenti ninapokuwa na pata. Hata hivyo kiwanja nimefanikiwa kununua tena siyo kimoja nimenunua viwaja viwili. Jingine baada ya kupata kiwanja, nimefikia hatua ya kuwekapo msingi mkubwa tu, wenye vyumba vya kulala 3 sebule, dining, choo cha ndani na choo cha public katika kiwanja kimoja, baada ya kujenga msingi huo nimejenga chumba kimoja ambacho nimeweka familia yangu muda huo najipanga kuinua msingi mkubwa.
Tarehe 11/04/2022 nimejenga tena chumba kingine chenye choondani na jiko la nje ambacho kimeungana na kichumba cha mwanzo ambacho nilijenga kwaajili ya kuanzia maisha muda huo najipanga. Ingawa bado sijakiezeka niko nakusanya nguvu na vipesa kidogo ili niweze kufunika yaani kupiga bati, naimani nitafanikiwa na hili, naamini M/Mungu hawezi kuniacha.

Malengo mengine ni kuwa na biashara, ili ninapotoka kwenye kazi za watu/kuajiriwa niwe na sehemu ya kujishikiza katika biashara yangu hili nalitamani hata kesho ila katika mambo makubwa huwa siyo rahisi kupata mafanikio kwa haraka, lazima usote kwanza. Ni lengo kubwa, lengo ambalo kwa wengi linaonekana kuwapa changamoto mno kufikia au lisiloweza kufikiwa, na kwa wengine wamekuwa wanasema itawezekana lakini lazima uumie. Nakubaliana nao kabisa mafanikio ni magumu kuyapata lazima uumie kabisa, Lakini ni lengo ambalo sitaliacha na wala sina wasiwasi kwenye kulifikia, kwa sababu najua ninaweza na ninajua njia sahihi za kufikia lengo.

Na kama ambavyo nimekuwa napambana katika haya maisha, sita acha kuweka lengo hili kwa sababu ya fedha, bali nimeliweka kama kiwango cha juu kabisa cha kunivusha hapa nilipo na kuwa katika nafasi nyingine, kwa sababu imani yangu kwenye fedha ni kwamba fedha ni zao la thamani, kadiri unavyojituma ndivyo unavyozidi kuona thamani yako. Pia kwa kufikia lengo hilo na hata kabla ya kulifikia, nitaweza kutoa mchango mkubwa kwa wengine, kupitia mchakato wa kuelekea kwenye lengo hilo. Mfano kutoa ajira, kutoa misaada kwa wenye uhitaji na kadhalika. Nikuhakikishie rafiki yangu unayenifuatilia na unayesoma ujumbe huu lengo hili nitalifikia na sitalifikia mwenyewe, lazima wale ninaoambatana nao wafikie hatua kubwa kiasi hicho, nina imani na wewe utakuwa mmoja wao.

Rafiki yangu na ndugu wa karibu kwangu, nilishaacha kusikiliza watu kuniambia nini naweza kufanya au siwezi kufanya, hii ni baada ya kugundua vitu vingi ambavyo watu walikuwa wananiambia siwezi kufanya siyo kwamba haviwezekani, ila ni kwamba wao hawajawahi kufanya na hawajawahi kuona mtu mwingine akifanya.
Kila siku ninapoamka ninayaandika malengo hayo makubwa mawili kwenye kijitabu changu, pamoja na malengo mengine ninayoyafanyia kazi. Kila siku najifunza na kuchukua hatua za kunifikisha kwenye malengo yangu, na mengine makubwa. Na sitakuja kumsikiliza yeyote anayeniambia kuna kitu siwezi kufanya, na huu ni ushauri muhimu sana ninaoutoa kwako, bila ya kujali unataka nini na upo wapi.
Rafiki yangu, katika haya maisha, ninakushirikisha kauli mbili muhimu sana, ambazo zilinifanya nitafakari sana siku za nyuma, na nitakuwa najikumbusha kila siku ili kuchukua hatua kubwa kwa kila siku ya maisha yangu.

KAULI YA KWANZA;
“Set yourself on fire with passion and people will come for miles to watch you burn.” - John Wesley

Ukiwa mahali halafu kwa mbali sana ukaona moto unawaka, lazima utapata hamasa ya kwenda kuangalia moto huo unatokana na nini. Ukiwa unaendelea na shughuli zako ukasikia kuna mtu amejiwasha moto, utaacha kila unachofanya na uende kuangalia nani amejiwasha moto, na kwa sababu gani.
Hichi ndiyo ninachokwenda kufanya na maisha yangu, ninajiwashia moto, na ninakualika utoke popote ulipo, uje uniangalie nikiungua/kuteketea. Na ninaposema najiwashia moto simaanishi kwamba najiweka kwenye moto kweli, au najiunguza, bali namaanisha hatua ninazokwenda kupiga, zitakuwa hatua za tofauti kabisa, hatua ambazo hakuna aliyezizoea na hivyo utapata hamasa ya kutaka kujua ni kwa namna gani hatua hizo zinapigwa na mbona sirudi nyuma.

Namaanisha kwamba hakuna kitakachonirudisha nyuma kwenye malengo ninayofanyia kazi, hakuna nitakachojali kwa yeyote atakayenisema vibaya au kunikatisha tamaa. Maana unapoona mwenzako anapiga hatua jitafakari sana kwanini mimi nishindwe na kwa nini yeye aweze?, chochote anachosema yeyote hakina maana kwako. Nitaendelea kujifunza kila siku, nitaendelea kupiga hatua moja baada ya nyingine kila siku na kuhakikisha kila mwaka kuisha, niangalie nimefanya kitu gani na chenye manufaa katika maisha yangu.
Kujiwashia moto inamaanisha kutokujionea huruma au kujibembeleza, kwa sababu nilichojifunza kwenye haya maisha, lazima kutakuwa na mtu wa kukutawala. Hivyo unapaswa kuchagua kujitawala mwenyewe, au kama huwezi basi uchague mtu wa kukutawala. Kwa malengo makubwa niliyonayo, nikichagua yeyote anitawale sitaweza kuyafikia, hivyo nitajitawala mwenyewe, na nitajiendesha kwa kila linalopaswa kufanyika ili kufika pale ninapopatamani.

KAULI YA PILI;
“Generate so much loving energy that people want to just come and hang out with you. And when they show up, bill them!” — Stuart Wilde

Kitu kimoja ambacho nashukuru sana kwenye maisha yangu ni kujifunza mapema sana msingi wa fedha. Ambapo fedha ni zao la thamani ambayo mtu unatoa kwa wengine. Na tangu nimejifunza msingi huu, umekuwa unafanya kazi kila wakati. Katika kipindi ambacho pesa ninayoingiza ni ndogo, unakuta pia thamani ninayotoa ni ndogo pia. Na kila ninapoongeza thamani ninayotoa, fedha zinaongezeka, bila hata ya kuhangaika sana.
Maisha ni nishati, na nishati huwa haipotei, kwa kanuni za kisayansi. Nikukumbushe kidogo sheria ya nishati, ambayo inasema nishati huwa haitengenezwi, wala haiharibiwi, bali inabadilishwa kutoka mfumo mmoja kwenda mfumo mwingine. Kwa mfano jua linapowaka, linatoa nishati ya manga na joto, mwanga ukifika kwenye mimea unabadilishwa na kuwa nishati ya kemikali, sisi tunapokula mimea, tunapata nishati hiyo ya kemikali. Hivyo unapokula ugali, wali au mboga, unakula nishati ambayo imetoka kwenye jua, lakini kwa mfumo mwingine. Tunaweza kusema wote tunakula jua.

Hivyo fedha pia ni nishati, kadiri unavyotoa nishati kubwa, ndivyo unavyopata fedha zaidi. Ni sawa na mtu anaposema kadiri unavyotokwa jasho zaidi, ndivyo unavyolipwa zaidi. Maana kutokwa jasho ni kubadili nishati, kutoka kwenye kemikali kwenda kwenye nguvu unazoweka kwenye kazi unayofanya.
Katika kipindi cha miaka kumi inayokuja ya maisha yangu, nasambaza nishati kubwa sana ya upendo. Nitafanya kila kinachopaswa kufanywa ili kutoa thamani zaidi kwa wengine, kwa sababu ninapenda kuona wengine wakitoka kwenye magumu, napenda kuona wengine wakipiga hatua na ninapenda kuona wengine wakiwa bora zaidi kila siku.
Nitasambaza nishati hii kwa kiwango cha juu sana, kiasi kwamba popote ulipo utataka kuungana nami, na utakapokuja sasa, utalipia kwa kusoma, Makala mbalimbali na kugusa matangazo yatayotokea hilo ndiyo nilimaanisha utalipia.

HITIMISHO:
Baadhi ya vitu nilivyokuwa nafanya awali huwa naamini muda utaongea kutokana na mambo ambayo nimevuka na kilichonisaidia zaidi ni namna ya kuya mudu na mpaka sasa nimefika hapa nilipo, lakini kwa sababu sitaki kutoka kwenye kusudi nimekuwa nasema lazima nipambane iwe usiku iwe mchana.
Najua kuna wengi wanasema hapana sitaweza kwa sababu nafasi nilizopata kutengeneza maisha ni nyingi na wengu husema nilichezea bahati na wanaenda mbali zaidi wanasema bahati huwa haiji mara mbili. Nataka niwahakikishie kwamba, nyakati nilizopitia zimenijenga mpaka hapa nilipo nimejiona kama nimeshinda hivyo wategemee kuona muujiza ukiwaangukia mbele yangu. Mtu ambae haamini hutegemea kuona kwa macho ya nyama hivyo basi nami nataka niwaonyeshe kuwa nimepambana na nilipo sasa niko namalizia hatua za mwisho. Ndio kwa mambo haya nategemea Kunanigharimu kwa kiasi kikubwa, lakini nikisema ndiyo itanigharimu zaidi baadaye. Juhudi ninazoweka kwenye kusudi langu kwa sasa ninajua zitazalisha matokeo makubwa sana baadaye kuliko nikihangaika na mambo mengine.

Ukishajua kusudi lako, yapangilie maisha yako kwa namna ambayo unaishia na katika harakati zako pia hakikisha huishi nje ya misingi uliyojiwekea vinginevyo hutoweza kuishi kusudi hilo, ndiyo kipaumbele kikubwa kwako na ukisema hapana kwa mengine yote ambayo hayahusiani na kusudi hilo utegemee kuinamisha kichwa chini yaani ukifikia hatua hiyo jua umesalimu amri.

Nikueleweshe vizuri hapo rafiki yangu, nitaweka juhudi kubwa sana kukushirikisha maarifa bora sana kupitia mtandao wa JUMANNE BLOG, ambao ni bure kabisa kuusoma kwenye blog hii utapata fulsa ya kutafuta ajira kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali naya kiserikali fulsa ni nyingi sana katika blog ya www.jumanne255.com. Utakaposoma maarifa hayo na Makala mbalimbali, utatamani sana kupata ushauri na maarifa zaidi.
Nilichojifunza kwa miaka mitano iliyopita, nimefunguka sehemu kubwa sana katika haya maisha na kadiri ninavyondelea mbele thamani yangu naiona kwenye kazi zangu, kwa sasa ndio maana ninaenda na muda ingawa sijachelewa sana ninatumia kila juhudi kujiimalisha na kuimalisha wengine waendelee kujifunza kupitia maisha wanayopitia na wasirudie kufanya makosa tena.

Rafiki yangu, ninakupenda sana, ndiyo maana kila baada ya muda wa kumbukizi hii ya kuzaliwa kwangu najitahidi sana ku-share hapa na wewe kama ushauri n.k.

Jifunze, fanyia kazi yale unayojifunza, kisha uone matunda mazuri. Kipato chako kiongezeke, uwe mtu bora na uweze kulipia huduma zaidi. Hapo sasa ndiyo unaweza kuongea lugha ya wazungu ambayo mimi na wewe hatujui ilipitia njia gani kutufikia Tanzania, katika siku zinavyozidi kusogea ndivyo ambavyo unazidi kukua na unahesabiwa kila unacho kifanya enedelea kupambana maana kadiri siku zinavyokwenda, maisha yako kama unapambana yatazidi kuonekana ya tofauti.

Nikushukuru sana rafiki yangu kwa namna ambavyo tumeendelea kuwa pamoja. Ninajua ni kwa namna gani unaniamini na kufuata kile ambacho tunajifunza kila siku. Nakuahidi tutaendelea kuwa pamoja, na miaka hii mingine mingi inayo kuja naimani utakuwepo na mimi pia nitakuwepo kwa uwezo wa Mungu. Miaka hii ijayo jiandae naujitume kisawa sawa kama ulianguka kama mimi huko nyuma usikumbuke yaliyopita hizo ni kurasa zilizopita funga au delete kabisa uanze kurasa mpya, itakuwa miaka ya kupiga hatua kubwa sana kwako, miaka ambavyo kama na wewe unaweza kujitoa, nakukaribisha sana twende pamoja.
 
Sijasoma yote ni ndefu ila nikukie heri ya siku yako ya kuzaliwa
 
Katika maisha yangu napenda sana kumuuliza Mungu nini cha kufanya na nitumie njia gani.

si njia yakutokomeza shida zote kwani Wokovu pia si lelemama.
lakini, ninalo tumaini, hata nikutane na shida kubwa kiasi gani naamini Mungu yu upande wangu, na ananitia nguvu.

Heri ya siku ya kuzaliwa mkuu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom