Maandamano ya kumuunga mkono JK yavunjwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,015
JK agonga mwamba

na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

SASA ni dhahiri kuwa kauli aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete kuhusu hadhi ya Zanzibar katika Muungano haijawaridhisha Wazanzibari.

Taarifa kutoka visiwani humo zinaeleza kuwa imeibuka misuguano ya chini kwa chini baina ya viongozi wa serikali visiwani humo na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yakiibuka makundi miongoni mwao ambao bado hawajaridhika na kile kilichosemwa na Rais Kikwete katika hotuba yake ya kihistoria bungeni wiki iliyopita.

Kwa upande mwingine, msimamo wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ni chama kikuu cha upinzani visiwani humo, wa kuipinga hotuba ya Kikwete katika kipengele cha hadhi ya Zanzibar, umezidi kuleta mfarakano baina ya viongozi wa CCM na SMZ.

Kilele cha kugonga mwamba kwa kauli ya Kikwete, kilijidhihirisha baada ya maandamano yaliyoandaliwa kuiunga mkono hotuba yake hiyo, na kupata baraka za Jeshi la Polisi juzi, kuvunjwa jana katika mazingira ya kutatanisha.

Maandamano hayo yalikuwa yameandaliwa na CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar na yalipangwa kufanyika leo.

Maandamano hayo yalikuwa yaanzie katika viwanja vya Komba Wapya hadi Msikiti wa Ngamia, Amani mjini Zanzibar, na mgeni rasmi alipangwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz.

Kwa kuonyesha kuwa suala hilo linahusisha mgogoro mzito, viongozi kadhaa wa CCM Mjini Magharibi, waliohojiwa na gazeti hili kutaka kujua sababu ya kuahirisha maandamano hayo, walikataa kulizungumzia suala hilo na wengine wakitoa kauli za kutaka kujiweka mbali na mgogoro huo.

Alipohojiwa jana, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Yussuf Mohammed, alisema hafahamu sababu ya kuahirishwa kwa maandamano hayo, kwa vile wasaidizi wake walikuwa bado hawajampa taarifa yoyote.

“Ni kweli nimesikia yameahirishwa, lakini sifahamu hadi sasa sababu ya kuahirishwa kwake, kwa vile wasaidizi wangu bado hawajanipa taarifa juu ya sababu ya msingi ya kuahirishwa maandamano hayo,” alisema mwenyekiti huyo wa mkoa, ambaye kimsingi ndiye alipaswa kuwa na taarifa zote kuhusiana na maandamano hayo.

Hata hivyo, alisema kwamba azima ya kufanyika maandamano hayo na mkutano wa hadhara, bado ipo na ratiba ya kufanyika kwake inatarajiwa kupangwa tena kwa vile muda bado upo.

Taarifa ya CCM Mkoa wa Mjini Magharibi kupitia kituo cha televisheni cha serikali (TVZ) juzi usiku, ilisema kuwa, maandamano hayo yameahirishwa hadi itakapotolewa taarifa nyingine.

Maandamano hayo yamevunjwa siku chache tangu kufanyika kwa maandamano kama hayo kisiwani Pemba na kuwashirikisha wanachama wa CCM kutoka mikoa miwili ya kisiwa hicho.

Taarifa zaidi zilizopatikana jana zilieleza kuwa, kumejitokeza mvutano kutokana na baadhi ya viongozi wa CCM Zanzibar kutaka yafanyike na wengine kupinga.

Haikueleweka wazi kwa nini baadhi ya viongozi wa CCM Zanzibar wanapinga maandamano hayo, lakini habari zaidi zimesema kuna viongozi ambao hadi sasa hawajaridhishwa na ufafanuzi wa Rais Kikwete juu ya hadhi ya Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano, alioutoa alipohutubia Bunge hivi karibuni.

Aidha, kitendo cha CCM kisiwani Pemba kuandaa na kufanya maandamano hayo, nacho kimeanza kulalamikiwa na baadhi ya viongozi wa CCM Unguja.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi, naye alisema hafahamu sababu ya kuahirishwa maandamano hayo, kwa vile hayakuandaliwa na CCM taifa.

“Naomba watafuteni watu wa mkoa ndio walioandaa maandamano hayo, wao watakuwa wanafahamu zaidi sababu za kuahirishwa kwake,” alisema.

Maandamano hayo yameahirishwa yakiwa tayari yamepatiwa kibali na Jeshi la Polisi, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mapema juzi, Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi ilipiga marufuku maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na kikundi cha Wazanzibari, yaliyokuwa yamelenga kuunga mkono tamko la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwa Zanzibar ni nchi.

Polisi katika taarifa yao walisema kwamba walilazimika kuzuia kufanyika kwa maandamano hayo kwa vile tayari kulikuwa na maombi ya wananchi wengine kufanya mkusanyiko kwa siku hiyo, na hivyo ulinzi wa polisi ungeelekezwa huko.

Hayo ni maandamano ya tano kukwama kufanyika katika Kisiwa cha Unguja tangu kuibuka suala la hadhi ya Zanzibar katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Inaonekana kuwa hotuba hiyo ya Kikwete kuhusu hadhi ya Zanzibar, imewagawa Wazanzibari hata ndani ya CCM yenyewe.

Dalili kwamba maandamano hayo yalikuwa katika hatihati zilianza kuonekana juzi, siku moja kabla ya kufanyika kwake. Kwa kawaida, CCM inapoandaa maandamano, kunakuwa na shamrashamra siku moja kabla katika maskani zote za chama hicho.

Lakini hali ilikuwa tofauti juzi ambapo hakukuonekana shamrashamra zozote katika maskani za CCM.

Tayari wanachama wa CCM katika mikoa kadhaa nchini wameshafanya maandamano kama hayo. Waliongozwa na wanachama wa CCM wa mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya, ambao waliandamana mapema wiki hii, kumpongeza rais kwa hotuba yake makini na nzuri bungeni.

Mjini Dar es Salaam, mamia ya wanachama hao wa CCM waliandamana kutoka ofisi ndogo za chama hicho Mtaa wa Lumumba hadi katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Huko Mbeya, mamia ya wanachama wa CCM nao waliandamana mapema wiki hii kuanzia kwenye eneo la Mafiati jijini humo na kutembea umbali wa kilomita moja na nusu hadi katika ofisi za CCM mkoa, wakiwa wamebeba mabango ya kuwapongeza wafanyakazi kwa kuunga mkono hotuba ya rais na kusitisha mgomo.

Akihutubia baada ya kupokea maandamano hayo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Nawab Mulla, alisema hotuba ya rais imejibu maswali mengi yaliyokuwa yanawatatiza wananchi, likiwamo suala la EPA na suala la Muungano, ambalo lilizua mjadala mkubwa katika siku za karibuni.
 
Back
Top Bottom