Maajabu ya tanzania haya

Parata

JF-Expert Member
Jul 26, 2011
3,090
675
Tanzania inajulikana ulimwenguni kote kwamba ni nchi ya maajabu. Ndio maana watu kutoka pande zote za dunia husafiri umbali mrefu na kutumia fedha nyingi ili kuja kujionea maajabu mengi yaliyosheheni nchini. Maajabu hayo ni pamoja na mbuga na hifadhi kubwa zenye wanyama wengi ambao hawapatikani mahali pengine popote duniani, milima mingi na mabonde ya kushangaza ikiwa ni pamoja na mlima Kilimanjaro ambao pamoja na kuwa karibu sana na ikweta huwa na theluji mwaka mzima.

Ipo pia mito mirefu yenye maji matamu, na maziwa makubwa yanayo izunguka Tanzania na kuifanya ionekane kama mwanamwali anaelindwa na majemedari wa vita. Ndege, samaki, nyoka na viumbe vingine vya ajabu vyote vimeweka makazi yake nchini Tanzania kana kwamba ndio nchi pekee yenye rutuba.

Tanzania imejaliwa pia kuwa na vito vya thamani ikiwa ni pamoja na almasi, dhahabu, yaspi, yakuti, yakuti manjano, yaspi na zabarajadi. Vyote hivyo vimelundikana katika ardhi kubwa ya nchi hii kiasi cha kuwafanya wataalam washindwe kujua waanzie wapi kuvichimba.


Si hivyo tu, tanzania imejaliwa pia kuwa na mfumo wa siasa na uchumi wa ajabu kuliko nchi nyingine yoyote duniani. Mfumo unaotoa mwanya kwa wageni kuwa mamilionea kwa rasilimali za watanzania huku wazawa wakiendelea kuwa masikini katika nchi yao; na huku serikali yao ikiendelea kuwa ombaomba siku baada ya siku.Si ajabu kwamba nchi hii ya ajabu inaongoza kwa kuwa na viongozi wa ajabu walio tayari kufanya lolote ili kulinda maslahi yao binafsi, lakini wasio tayari kufanya jambo lolote la maana ili kuinua maisha ya wananchi wao, na kuwafanya wapate japo milo mitatu ya uhakika kwa siku.

Zaidi ya yote Tanzania imebarikiwa mno kuwa na raia wa ajabu, wasiojua kulalamika wala kupiga kelele wanapo onewa, au kudhulumiwa mali yao. Ni raia wa ajabu sana, wepesi kulaghaiwa kwa maneno matupu na walio tayari kuuza KURA yao kwa sahani ya pilau, fulana za rangirangi, doti za kanga na hata kwa burudani nzuri tu za wakata viuno na waimba taarab. Ni watu wa ajabu mno ambao hufurahi na kupiga makofi hata pale wanapoambiwa "kila mtu abebe msalaba wake mwenyewe..." Nchi nzuri sana hii.

Acha wazungu walipe mamilioni ya dola kuja kutuona maana kwa kuambiwa hawawezi kuamini. Wakati wenzetu walioendelea walianzia chini na kujikokota taratibu kuelekea juu hadi kufikia mahali walipo leo hii, sisi tumeanzia juu na kujivurumisha kuelekea chini kwa kasi ya fataki. Wakati wenzetu walianza na usafiri wa punda,(miaka 3,500 iliyopita) baadae wakaunda merikebu, magari ya stima, aeroplane, na sasa wanaenda kwenye mwezi na sayari ya Mars; sie tumeanzia kwenye mabasi ya icalus (UDA) tukaja kwenye DCM, chai maharage, vipanya, bajaji na sasa bodaboda. Bila shaka tunaelekea kwenye punda...Ndio! lazima tutoe mfano wa kutunza mazingira maana magari yanaongeza uharibifu wa ozone.

Acha wazungu wamiminike kuja kuona maajabu yetu. we uliona wapi ambulance za pikipiki? unampakia mama mjamzito kwenye ambulance ya pikipiki akifikia muda wa kujifungua wakati hajafikishwa hospitali inakuwaje? Acha hiyo, mgonjwa akizidiwa wakati safari inaendelea, huyo muuguzi (nurse) anamuhudumia vipi? Na mvua ikinyesha je! nani atakae mshikia mgonjwa mwamvuli ili asilowane? Halafu cha kushangaza ghalama ya ambulance hizo inakaribiana kabisa na gari aina ya Toyota Hiace ambayo inaweza kufanyiwa ukarabati kidogo kuwa ambulance bora zaidi.

Hata kama ni msaada wa bure MIMI ningeukataa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba "mtu akikupa ushauri wa kipumbavu, nawe ukaukubali ushauri huo huku ukijua kuwa ni ushauri wa kipumbavu...mtu huyo anakudharau. Hivi kwa nini hatukuchukui sehemu ya posho za wabunge tukanunulia ambulance za kweli?

Sishangai Kenya wanapoongoza duniani kwa kuuza vinyago vya mpingo wakati mti huo haumei kwao, wanauza tanzanites kwa wingi wakati mashimo yako Tanzania tu, wanasambaza kahawa na chai ya Tanzania wakati mazao hayo yanalimwa nchini mwetu. Hainishangazi kuona kwamba wageni wengi wanajua mlima Kilimanjaro uko Kenya, maana wenzetu walishauhodhi siku nyingi wakati sie tunacheza dogoli. Na sasa wanataka kujenga uwanja wa ndege Taveta, hivi KIA itapata mtu kweli?

Sioni ajabu kwamba tumeamua kugawa shahada za udaktari kwa kila mtu bure, maana hakuna haja ya kwenda shule! Kwanza nani kasema mtu akisoma ndio anaelimika au kuwa kiongozi mzuri? Shauri yao akina Salim Ahmed salim walioupata udaktari kwa kuutolea jasho. Kizazi chetu sie ukipata udiwani na udaktari huo unakufata nyuma. Labda usiutake.

Hapa nilipo nasubiria 'ankal' issa michuzi apewe udaktari wake. Ndio, nani asiyejua kuwa blog yake ina mafanikio kuliko blog nyingine yoyote? Kwa nini asipewe udaktari wa kublog? kwani tumewapa wangapi? Tumejidai kuwakataza kina Profesa Vulata, Maji Marefu na Dr Remmy wasijiite maprofesa eti wanaharibu sifa na heshima ya wadhifa huo kumbe na sie tunautamani...ajabu sana, tena ya Mwajabu kuolewa na Rajabu.

Namuomba sana Mungu anipe uhai na kuendelea kulilinda Taifa hili la ajabu na hasa tunapoelekea uchaguzi ujao. Nina hakika huo utakuwa uchaguzi wa AJABU sana.
 
jamani duniani hapakosi mishangao ila Tanzania tumezidi hata tooth pick tunaagiza hii hatari sana
 
Hahaha nimeipenda hii. Kila mtu anajua kua taifa hili limefikia hatua hii kwa uongozi m'baya wa ccm. Embu watu wa vijiji vya ndani kabisa munaojua kua hakuna chama kingine tanzania zaidi ya ccm badirikeni. I hope M4C inafanya kazi nzuri sana. Ingeanza kipindi kile cha 1995 ccm ingekua mabwepande ikijizika yenyewe kwa mapande ya miti muda huu.
 
Hahaha nimeipenda hii. Kila mtu anajua kua taifa hili limefikia hatua hii kwa uongozi m'baya wa ccm. Embu watu wa vijiji vya ndani kabisa munaojua kua hakuna chama kingine tanzania zaidi ya ccm badirikeni. I hope M4C inafanya kazi nzuri sana. Ingeanza kipindi kile cha 1995 ccm ingekua mabwepande ikijizika yenyewe kwa mapande ya miti muda huu.


Mkuu hapo kwenye red nadhani umekosea. Taifa halijafika hapo lilipo kwa sababu ya uongozi wa CCM, bali kwa sababu ya mimi na wewe kutokujua mchana na usiku. Kwa kuendelea kuamini kuwa uongozi wa chama cha siasa ndiyo ukombozi wa Taifa la Tanzania bado tutaendelea kuwa taifa la maajambu kwa miaka zaidi ya 200 ijayo. Ila tukiamini chanzo cha Tanzania kuwa nchi ya ajabu ni sisi wenyewe, then tunaweza kutafuta suluhisho na siyo CHADEMA, CCM, CUF N.K funguka na uelewe ukweli wa maisha na namna ya kujikomboa ujamaa ulikufa siku nyingi. Maendeleo hayataletwa na chama cha siasa au serikali bali na mimi na wewe.
 
Ila chama kinahodhi michango yetu ya kimaendeleo! Sawa na mtu kukushika miguu uckimbie
 
Mkuu hapo kwenye red nadhani umekosea. Taifa halijafika hapo lilipo kwa sababu ya uongozi wa CCM, bali kwa sababu ya mimi na wewe kutokujua mchana na usiku. Kwa kuendelea kuamini kuwa uongozi wa chama cha siasa ndiyo ukombozi wa Taifa la Tanzania bado tutaendelea kuwa taifa la maajambu kwa miaka zaidi ya 200 ijayo. Ila tukiamini chanzo cha Tanzania kuwa nchi ya ajabu ni sisi wenyewe, then tunaweza kutafuta suluhisho na siyo CHADEMA, CCM, CUF N.K funguka na uelewe ukweli wa maisha Kajisemea jenerali ulimwengu KILA MTU NA KAMHOGO KAKE. sababu za kuukataa mfumo huu na makando kando yake tunazo. njia tunaonyeshwa lkn wapi tupo kimya. madaktr waligoma kimya hatukuungana.walimu wamegoma imya hatukuungana.ulimboka wamemlimboka kimya hatukuungana.tuungane ili iwe nini??maana KILA MTU NA KAMHOGO KAKE.
 
Mkuu Nimeipenda hii. Lakini pia maajabu yanatokana na wewe na sisi ambao tunayajua haya lakini hatujafanya jitihada kuwaelimisha wale mbumbumbu waliopumbazwa na kuona mambo yanakwenda kama inavyotakiwa kumbe ni kiini macho!Maajabu wewe na sisi kuishia kuweka machapisho JF na kuwagusa wachache tu ambao kimsingi wanayajua haya na kuwabagua brothers and sisters wasojua haya na wanahitaji kuelemishwa tena na tena kabla hatujafika 2015!
Ni kweli hii ni nchi yenye maajabu Mkuu!
 
[QUOTE

Sishangai Kenya wanapoongoza duniani kwa kuuza vinyago vya mpingo wakati mti huo haumei kwao, wanauza tanzanites kwa wingi wakati mashimo yako Tanzania tu, wanasambaza kahawa na chai ya Tanzania wakati mazao hayo yanalimwa nchini mwetu. Hainishangazi kuona kwamba wageni wengi wanajua mlima Kilimanjaro uko Kenya, maana wenzetu walishauhodhi siku nyingi wakati sie tunacheza dogoli. Na sasa wanataka kujenga uwanja wa ndege Taveta, hivi KIA itapata mtu kweli?
/QUOTE]


Kama kawaida kulialia tu na kulaumu watu wengine bila utatuzi wa matatizo,sasa ulitaka wakajenge wapi Kiwanja, si wanajenga ndani ya mipaka yao tatizo liko wapi?

Halafu kusema kwamba Tz ni nchi sijui ya maajabu Duniani ni propaganda tu, Dunia nzima imejaa maajabu na nchi nzuri na za kuvutia ajabu labda hujabahatika kutembea tu, na ukitembea utagundua kwamba vitu ilivyo navyo TZ ni vya kawaida sana na karibu kila nchi ina maajabu yake kwa hiyo hamna uspecial wowote zaidi ya propaganda tu!

Vyote ulivyoviandika hamna jipya na wala havitokei TZ tu, labda tofauti tu kwamba sisi tunalialia tu kama watoto kwa hiyo ningekushauri urudi ujitafakari na uje na posti inayoelezea jinsi ya kwenda mbele na kutatua matatizo na sio kuliailia tu kama watoto kila siku!

 
Back
Top Bottom