Kwaheri 2011, karibu 2012

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,354
33,192
KATUNI(601).jpg

Maoni ya katuni


Leo tunaumaliza mwaka 2011 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2012 ambao tunauanza kesho.

Tunamshukuru mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa baraka zake kutokana na kutuwezesha kuumaliza mwaka 2011 tukiwa wazima. Wako baadhi ambao hawakuweza kufika tarehe ya leo.

Kwaka 2011 tunaoumaliza leo ulikuwa na changamoto nyingi za kiuchumi, kisiasa na kijamii ambazo tumekubana nazo.

Kwa ujumla uchumi wa Tanzania ulikabiliwa na hali ngumu kutokana na mfumuko wa bei na kuporomoka mara kwa mara kwa Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani.
Mdororo wa uchumi ulioikumba dunia na kuathiri sekta nyingi za uzalishaji nchini bado uliendelea kuwa kikwazo cha kukua kwa uchumi wa nchi yetu. Hata nchi tajiri za Ulaya zikiwemo Ugiriki na Italia, mwaka huu tumezishuhudia zikitikishwa na hali ngumu ya uchumi kiasi cha kukumbwa na tishio la kufilisika.

Mwaka huu pia maeneo mengi ya nchi yetu yaliendelea kukumbwa na ukame na matokeo yake kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula. Kutokana na hali hiyo, serikali ililazimika kupeleka tani kadhaa za chakula cha msaada na kuzigawa na kingine kukiuza kwa bei ndogo ili kuhakikisha kwamba wananchi hawafi kwa njaa. Athari hizo za ukame zilitokana na kutonyesha kwa mvua za kutosha mwaka jana ha hivyo kuendelea kusababisha makali mwaka huu.

Kadhalika, katika mwaka 2011 tumeshuhudia nchi yetu ikiendelea kukabiliwa na makali ya nishati ya umeme, hali iliyosabaisha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoa umeme kwa mgawo mara kwa mara katika maeneo yote nchini.

Mgawo huo uliathiri shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi. Kwa mfano, wananchi wanaofanya shughuli za ujasiriamali walilazimika kusimamisha kazi zao na hata baadhi ya wenye viwanda walisimamisha uzalishaji.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wafanyakazi kupoteza ajira na hivyo kusababisha athari katika familia zao na katika jamii kwa ujumla.

Changamoto nyingine kubwa iliyoikumba nchi yetu ni mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuriko katika baadhi ya mikoa nchini. Kwa mfano, katika Jiji la Dar es Salaam, mvua kubwa iliyonyesha kwa siku tatu mfululizo wiki moja iliyopita, ilisababisha maafa makubwa.

Tumeshuhudia jinsi miundombinu kama barabara ikiharibika, madaraja kukatika, makazi ya watu kuzingirwa na maji na kukosa makazi, huku watu 40 wakipoteza maisha. Hadi sasa takribani watu 5,000 wanaoishi katika maeneo ya mabondeni hawana makazi na wanaendelea kuishi katika kambi maalum zilizoko katika maeneo ya shule za msingi na sekondari.

Aidha, ajali za barabarani ziliitikisa nchi yetu na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa. Takwimu za Jeshi la Polisi Kitengo cha Usasama Barabarani nchini, zinaonyesha kuwa matukio ya ajali za barabarani zilizotokea mwaka yalikuwa 24, 665 yaliyosababisha vifo vya watu 3, 582.

Vile vile, ajali hizo zilisababisha watu 20, 656 kujeruhiwa, ambapo kuanzia Januari hadi Desemba 15, mwaka huu, taifa limeshuhudia matukio 23,330 ya ajali yaliyosababisha vifo 3,798 na kuacha wengine 19, 908 wakiwa majeruhi.

Kadhalika, tunakumbuka tatizo la uhaba wa mafuta ambalo limekuwa likitokea mara kwa mara na kusababisha nishati hiyo kupanda bei na kuwathiri wamiliki wa vyombo vya usafiri na umma kwa ujumla.

Hizi zote ni changamoto ambazo sisi kama taifa tunapaswa kujipanga upya kuweka mikakati na mipango kwa ajili ya kukabiliana nazo kikamilifu katika mwaka 2012 ili kuhakikisha kwamba hazitukwamishi katika kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu.

Ni wajibu wa kila mwananchi popote alipo kuhakikisha kwamba anafanya kazi kwa bidii na kwa maarifa zaidi kwa ajili ya kukabiliana na hali ngumu ya maisha kama vile ongezeko la kasi la bei ya bidhaa hususan vyakula, ambalo limetokana na mfumuko wa bei.

Tusijidanganye kwamba kuna mjomba au shangazi atakayekuja kutoa msaada zaidi ya kuchapa kazi kwa bidii. Ingawa serikali haiwezi kutoa msaada wa kila kitu kwa wananchi wake wote, lakini inao wajibu wa kuwawekea raia wake mazingira bora ya kujitafutia riziki na ikiwezekana iwawezeshe kwa namna mbalimbali.

Ni wajibu wa serikali kujipanga kwa kuchukua hatua madhubuti ambazo zitasaidia kukabiliana baadhi ya changamoto kama kasi kubwa ya mfumuko wa bei na kuporomoka kwa shilingi yetu mara kwa mara.

Hatua kama hizo tunatarajia zitachukuliwa kudhibiti bei ya mafuta, matatizo ya umeme na ukame.

Kwa kuwa mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya utapamba moto mwaka 2012, ambapo bila shaka Tume ya kukusanya maoni ya katiba itaundwa na kuanza kukusanya maoni ya wananchi, ni matumaini yetu kuwa mchakato huo utafanyika kwa amani, kwa uvumilivu na kwa kuheshimiana ili mwishowe tupate katiba nzuri.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom