Kwa Lowassa, mwenye macho haambiwi tazama

Mbase1970

JF-Expert Member
Jun 11, 2015
6,053
4,595
Baada ya kusoma comment na mada nyingi zinazomhusu aliyekuwa Waziri Mkuu wa serikali ya MUungano wa Tanzania Mheshimiwa E Lowasa nimeona ni busara kupitia nini tulizungumza kuhusu EL huko nyuma.
Hii Makala ilitolewa na Ndugu KAUMIZA May 10, 2013 kabla mheshimiwa hajawa kipenzi cha watu wa mitandaoni.

Kwa Lowassa, mwenye macho haambiwi tazama
Katika uwanja wa siasa, hasa siasa za moja kwa moja (active politics) kuna aina mbili ambazo hutumiwa na wanasiasa ili kupata ridhaa ya kuongoza. Iwe ni uongozi wa nchi, jimbo, kata, mtaa ama taasisi yoyote ile ambayo kiongozi wake hupatikana kwa njia ya kuchaguliwa.

Njia ya kwanza ni kwa mtu kujipima mwenyewe kama unazo sifa stahiki za kuweza kuongoza katika nafasi unayotaka kugombea. Iwapo utajipima na kuona kuwa unazo sifa za kutoshabasi unaweza kufuata taratibu zilizowekwa katika kuomba ridhaa kwa wale unaotaka kuwaongoza ili wakupe ridhaa kwa utaratibu uliopangwa.


Njia ya pili huwa ni kwa kuombwa na watu wanaokufahamu baada ya wao kuridhika kuwa unavyo vigezo vya kutosha vya kuweza kuwaongoza.

Nimetangulia kutoa maelezo haya kutokana na joto la siasa za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 linavyozidi kupanda. Wakati tukielekea mwaka 2015, mwaka ambao tutakuwa na uchaguzi mkuu akili yangu inanituma kuwa uchaguzi huo unaweza kuweka historia katika siasa za Tanzania kwa sababu zifuatazo.

Kwanza, kama mambo yatakwenda kama tunavyopenda, huu utakuwa ni uchaguzi wa kwanza utakaofanyika chini ya katiba mpya. Kutokana na katiba mpya, inawezekana mabadiliko na fursa mbalimbali zikaonekana na kushuhudiwa. Si ajabu tukashuhudia uwepo wa wagombea binafsi katika ngazi zote za kiuongozi jambo ambalo limekuwa ni kilio kikubwa sana na cha muda mrefu hasa kwa wanaharakati wa siasa na demokrasia pamoja na wasomi.

Ikumbukwe kuwa mwa mwaka 1993 Mchungaji Christopher Mtikila alishinda kesi yake aliyoifungua katika mahakama kuu kanda ya Dodoma ambapo Jaji Kahwa Lugakingira alilitaka Bunge kutunga sheria kuruhusu mgombea binafsi.

Lakini pia katika hukumu yake mahakama kuu ilimpa Mwanasheria mkuu wa serikali kuanzia katikati ya mwaka 2006 hadi uchaguzi mkuu uliopita awe amewasilisha bungeni sheria inayotoa fursa ya mgombea binafsi.Kwa hali hii si ajabu mwaka 2015 tukashuhudia uwepo wa mgombea binafsi.

Pili, iwapo upepo utaendelea kuvuma kwa kasi na uelekeo huu wa sasa basi tutashuhudia mpambano mkali sana kati ya vyama vikuu vinavyotawala siasa na kuhodhi siasa za Tanzania katika ngazi zote zitakazoshindaniwa.

Takribani, miaka miwili na nusu imebakia kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu. Baadhi ya wanasiasa wanatajwa kuwa wanaweza kugombea urais. Katika siasa za CCM wanatajwa wengi, lakini zaidi wanatajwa Waziri mkuu mstaafu Mhe Edward Lowassa (MB) na waziri wa Mambo ya nchi za Nje na ushirikiano wa Kimataifa Mhe Benard Membe (MB).

Ingawa wenyewe hawajaweka wazi iwapo wataingia katika kinyang'anyiro cha urais ushahidi wa kimazingira unaonesha wazi kuwa kwa sasa wanazichanga karata zao na kuna uwezekano mkubwa kwa viongozi wetu hawa kuingia katika kinyang'anyiro hicho.

Mathalani, Mbunge wa Kilindi Beatrice Shelukindo aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari katika harambee ya kuchangia kanisa la Kilutheri Monduli akieleza kuwa zawadi kubwa kwa wanachi wa Monduli ni yeye kujitoa katika kuhakikisha Mbunge wao anakuwa Rais katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Kwa upande wa Mhe Membe, yeye alikwishawaaga wapiga kura wake kuwa amewatumikia kwa mihula mitatu na kwamba mwaka 2015 hatagombea tena ubunge. Na alipohojiwa katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV mhe Membe alieleza kuwa bado hajaoteshwa kugombea nafasi ya Urais, na kwamba ikitokea akaoteshwa kuna baadhi ya watu ambao itabidi watafute mahali pa kwenda.

Hizi ni baadhi ya kauli ambazo zinaonesha wazi kuwa wanasiasa hawa wamedhamiria. Na kwa kuwa hawajawahi kukanusha kuwa hawana nia ya kugombea urais baada ya Jakaya, basi nina kila sababu ya kuamini kuwa wana nia ya dhati kabisa ya kumrithi rais wa sasa.


Katika makala haya nitamzungumzia zaidi Mhe Lowassa. Kwa nini hasa nimemchagua Lowassa ni kutokana na kwamba inawezekana jina lake likawa ndilo linatajwa sana kuliko mwanasiasa mwingine yeyote.

Kwa miaka miaka mingi sasa, haiwezi kutokea siku ikapita bila kukuta mjadala katika kurasa za mitandao ya kijamii iliyo maarufu kwa mada za siasa bila kukuta jina la Lowassa. Na inawezekana, jina la Lowassa likawa ni jina linaloongoza kwa kujadiliwa sana kuliko jina la mwanasiasa yeyote katika mitandao hapa Tanzania.


Mfano katika mtandao wa Jamiiforums, mada yoyote (wenyewe hupenda kuziiita mada hizo "uzi") unaomzungumzia Lowassa huwa unapata idadi kubwa ya wachangiaji na hata wasomaji. Uwe ni uzi wa kumsifia au hata wa kumponda, lazima utabeba mamia ya wachangiaji.


Nilianza kulisikia jina la Edward Lowasa mwanzoni mwa miaka ya 1990 kipindi akiwa Waziri wa nchi katika ofisi ya makamu wa rais na katika mwaka 1995 pale alipojitosa katika kuomba ridhaa ya jina lake kupitishwa na chama chake kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kipindi hiki nyota ya Lowassa ilikuwa inang'aa kweli kweli kama ilivyokuwa nyota ya rafiki yake ambaye ni rais wa sasa wan chi yetu Mhe Jakaya Kikwete. Kuthibitisha hili ni kauli aliyoitoa Rais Ali Hassan Mwinyi wakati akilihutubia bunge mwaka 1995. Mzee Mwinyi alieleza kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya viongozi na akawataja Jakaya Kikwete na Edward Lowasa kuwa ni hazina kubwa katika taifa letu(nina uhakika ukitembelea maktaba za TBC au katika Hansard za bunge unaweza kuipata nakala ya hotuba hiyo)

Baada ya hotuba hiyo ya Mzee Mwinyi nilianza kuwafuatilia hawa watu ili kuweza kujua ni kwa nini wameitwa hazina ya Taifa. Hapa napo nitamzungumzia Lowassa.

Edward lowassa ni mojawapo ya aina ya viongozi ambao taifa hili linawahitaji. Ni kiongozi imara na asiyeyumbishwa na mawimbi au upepo. Ni mvumilivu na mwenye staha.

Kwa nini nimempa sifa za uimara na uvumilivu. Hili nitalifafanua! Katika kipindi cha miaka mine mfululizo kuanzia 2008 mwanzoni hadi mwaka 2012, Edward Lowasa alikuwa katika kipindi kigumu sana kisiasa hata kumlazimu kujiuzulu nafasi yake ya waziri mkuu kutokana na kashfa ya mitambo ya kufua umeme maarufu kama Richmond.


Pamoja na kashfa nyingi alizotupiwa na matope yote aliyomwagiwa nyota yake imeendelea kung'aa na kuthibitisha kuwa kiongozi imara. Amekuwa kimya siku zote na hajibizani na wale wanaomtupia uchafu na ikitokea ameongea, basi huongelea mambo ya kitaifa na yenye manufaa kwa taifa bila kumlaumu ama kumhutumu mtu yeyote.

Pamoja na kwamba wapinzani wake wa ndani ya chama chake na nje ya chama chake wamekuwa wakimpatia majina mabaya na yenye kuchukiza, kamwe hajawahi kuwarudishia. Hii imemjengea heshima kubwa, kwani watanzania wamezidi kuwa na imani naye kwa kiasi kikubwa.

Katika uislam huwa tunaambiwa kuwa kama kuongea ni fedha, basi kukaa kimya ni dhahabu. Lowasa aliamua kuwa dhahabu kwa kukaa kimya, nadhani lengo likiwa kuwapa watanzania nafasi ya kusikiliza, kutafakari, kupima na kuamua.

Ukimya wa Lowasa umemfanya awe lulu kama siyo dhahabu na ndio maana inapotokea akasema, basi umma mzima wa Tanzania huzizima.

Kashfa zote anazotupiwa ni hisia tu na inaweza kuwa ni chuki binafsi au hata uoga wa wapinzani wake ambao inaonesha wanaogopa kivuli au hata kishindo chake. Hatuwezi kumhukumu kwa hisia tu, kwani hakuna mahakama au chombo chochote kilichothibitisha hatia juu yake. Wanasheria wana msemo wao wa kilatini usemao "Neminem oportet esse sapientiorem legibus" wakimaanisha kuwa hakuna mwenye busara na mjuzi zaidi ya sheria. Kwa hiyo kama sheria haijamtia mtu hatiani na hakuna sauti yoyote kutoka kwa yeyote itakayosikika.


Wapo watu wanaosema kuwa Lowasa ni tajiri mkubwa hivyo hastahili kuwa kiongozi. Binafsi sifahamu kuhusu utajiri wake na nisingependa kujiingiza katika mjadala wenye kuongozwa na hisia. Labda ninachoweza kujadili hapa ni je, tajiri hafai kuwa kiongozi?


Kwa mujibu wa maandiko ya Mwalimu Nyerere, hasa hotuba yake maarufu iliyopewa jina la Ujamaa ni Imani iliyotolewa mwaka 1978 na hata katika kitabu chake cha Freedom and Socialism, Mwalimu Nyerere anaeleza kuwa "Ujamaa ni imani. Hata tajiri anaweza kuwa mjamaa ilimradi anaamini katika usawa wa watu"

Mantiki tunayoipata hapa ni kwamba, mtu unaweza kuwa masikini lakini mwenye moyo/roho ya kibepari. Roho ya kibepari huambatana na choyo, ubinafsi na makuzi. Wakati roho ya kijamaa huambatana na upendo na kuthamini utu wa watu. Mjamaa huwa anaumizwa na shida za watu wengine.


Lakini pia Lowasa ni kiongozi jasiri na mwenye uoni wa hali ya juu (Visionary person). Ni kiongozi wa kwanza nathubutu kusema aliyesimama kidete kuoneshwa kukerwa na hatimaye kulizungumzia tatizo la ajira miongoni mwa vijana wasomi na wasio wasomi. Na si kuzungumzia tu, bali ameweza kutoa hata namna ya kulitatua.


Katika maeneo mengi anapopata fursa ya kuongea, iwe ni katika nyumba za ibada au katika mikutano ya hadhara amekuwa akiomba mashirika ya umma na ya binafsi na taasisi za dini kujaribu kulitatua tatizo la ajira kwa vijana kwa kutengeneza fursa za vyuo vya ufundi na ujasiriamali.

Binafsi siamini kama Lowasa ni mchafu kiasi hicho. Hii inathibitishwa na imani kubwa waliyonayo watu juu yake. Mathalani katika siasa za chaguzi mbalimbali ambazo ameshiriki katika kipindi hiki huku akichafuliwa na kushambuliwa kutoka kila kona, amekuwa akiibuka na ushindi wa hali ya juu kiasi cha kushangaza.

Katika kura za maoni za mwaka 2010 ili kumpata mgombea wa ubunge kupitia CCM katika jimbo lake, alipata kura 40,000 na mpinzani wake kupata kura 300 na katika uchaguzi wa ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama chake mwaka 2012 aliibuka na ushindi mzito wa kura 709 huku mpinzani wake aliyemfuatia akiambulia kura 44 tu. Hii yote ni kielelezo cha namna wananchi walivyo na imani kubwa sana juu yake.

Nimalizie makala haya kama nilivyoianza. Mrithi wa Rais Kikwete anaweza kujitazama mwenyewe na kijipima kama ana sifa lakini hata sisi wananc tuna dhima ya kumshawishi mtu iwapo tunaona kuwa ana sifa ya kutupeleka katika Tanzania tunayoitaka baada ya kumalizika kwa ngwe ya awamu ya nne. Naanza kwa kumshawishi Edward Lowassa kuwa, sifa alizonazo zinaonesha kuwa anatufaa.


Kazi zake zimeonekana katika kila dhamana aliyopewa. Iwe katika nafasi ya ubunge wa Monduli ama wizara ya Ardhi, wizara ya Maji na mifugo na hata alipokuwa waziri mkuu wa nchi yetu.

Kwa Lowassa, mwenye macho haambiwi tazama

nimeiweka hii kuonyesha jinsi gani sisi watanzania tulivyokuwa wanafiki na vinyonga tusio kuwa msimamo. Kama baadhi yetu tunaona kama Mheshimiwa alionewa ni wakati sasa kumuomba msamaha na siyo kujifanya kuwa tumemsamehe ama kumvika kilemba cha ukoka.

Mjadala wa kiutu uzima unatakiwa siyo matusi pamoja na kutokukubaliana naye bado alilitumikia hili taifa hivyo ni vizuri kumpatia heshima yake kama tunavyompatia Mwl Nyerere maana naye alikua na mapungufu zaidi ya Lowasa kwa kuminya demokrasia.
 
Back
Top Bottom