Kwa heri matumaini, karibu majuto

Quadratic

Member
Dec 30, 2010
23
3
MIEZI michache iliyopita, niliandika katika safu hii ya Mchokonozi nikiwaonya wapiga kura wa nchini mwetu waliokuwa wakifurahia kupewa ubwabwa na maharage, khanga, tisheti na kofia wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi ili wawachague waliokuwa wakihonga kuwa, siku chache zijazo watakuwa wakinung'unika, wakilia na hata kufa kwa makosa yao wenyewe ya kutumia kura zao vibaya kwa kuchagua bora viongozi badala ya viongozi bora.
Katika makala ile niliandika kufafanua yale ambayo nilikuwa nikiyaandika kwa wiki mbili mfululizo kabla ya kuandika makala ile. Niliandika kwa lugha nyepesi zaidi ufafanuzi wa maswali ya kufikirisha ya alfu lela na moja niliyokuwa nikimuuliza rafiki yangu Rais Jakaya Kikwete ambayo alifeli yote kwa ujumla wake kwa sababu hakujibu hata moja.
Leo, ikiwa ni siku ya pili baada ya kuuaga mwaka 2010 na kuingia mwaka mpya wa 2011, huku dalili za mateso makali kwa Watanzania walio wengi zikiwa zimeshaanza kuonekana, ninaandika maneno mapesi kabisa huku nikiepuka kugusia mambo mazito yanayoumiza mioyo, kuwakumbusha wapiga kura wa Tanzania kuwa mateso watakayokutana nayo katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia mwaka huu wa 2011 wanayastahili kwa sababu ya uzuzu wao.
Wana kila sababu ya kuishi maisha magumu kwa sababu walikubali kuyauza maisha bora waliyokuwa yakiyachungulia kwa thamani ya ubwabwa na mahagare, khanga, tisheti, kofia na wakati mwingine kwa sh 5,000 au 10,000 baada ya kufanya kazi kubwa ya kuimba kwa sauti kubwa nyimbo za masifu kwa chama chetu cha maulaji.
Ni wapiga kura hawa wanaolia kuwa maisha yanazidi kuwa magumu ndiyo waliokuwa wakichukua shoka na mapanga kwenda kuwashambulia wenzao waliokuwa wakitaka kuking'oa chama cha maulaji madarakani kutokana na kukosa sifa zinazostahili za kuendelea kuiongoza nchi yetu. Wapuuzi kweli kweli, wao na machozi yao.
Wamesahau kuwa kwa makusudi, licha ya makala nyingi za upendo na zilizojaa maonyo nilizokuwa nikiwaandikia kuhusu kutokufanya kosa la kuchagua bora viongozi, walinipuuza. Wakawachagua. Walifanya kosa la kukataa kuyakimbilia maisha yenye matumaini, sasa wanajuta. Nami kwa nafsi nyeupe kabisa namsihi mwenyezi azidi kuwapa maisha magumu yenye kulia na kusaga meno.
Namuomba mwenyezi mungu anisamehe kwa kuwaombea maisha magumu na yenye kila aina ya suluba ndugu zangu ninaokula na kunywa nao kwa jasho la damu. Ninafanya hivi kwa sababu ninaamini ndiyo njia pekee ya kuwafundisha kufikiri sawasawa.
Ninaamini kuwa watakapokuwa wanakufa kwa kukosa huduma ya vidonge vya kutibu maralia katika hospitali zetu za umma huku hao waliowapa kura kwa kughilibiwa na vipande vya khanga na wali na maharage wakienda kutumbuliwa vipele Ujerumani na Amerika, ndipo watapojifunza maana ya kutumia kura zao vizuri kwa kukataa kurubuniwa kijinga.
Ni jambo la ajabu kwa watu walioishi chini ya mfumo wa uongozi wa chama cha maulaji kwa takribani miaka 50 sasa, wanaojua jinsi chama hicho kilivyochoka na kinavyobaka demokrasia kuendelea kukikumbatia kwa kudanganywa kipuuzi kuwa, eti! Bila chama hicho, Tanzania haitakalika.
Kwa watu wanaofikiri sawasawa, ni jambo lisiloingia akili kukiingiza madarakani chama ambacho kina lundo la watu wasiokuwa na sifa za uongozi lakini wanaong'ang'ania madarakani kwa gharama kubwa ya fedha za umma. Watu hawa, hata pale walipojifanya wamesahau walikumbushwa kwa lugha nyepesi kuwa ili kuifikia Tanzania yenye neema tunahitaji mabadiliko ya uongozi, lakini ajabu, waliziba pamba masikioni.
Katika hali ambayo haikutarajiwa na watu wengi wenye akili ambao walikuwa wakifuatilia mwenendo wa kampeni na hata uchaguzi wetu, wapiga kura wa Tanzania walikataa kuwa mfuko wa saruji hauwezi kuuzwa sh 5,000 wala bei ya bati haiwezi kushuka.
Kwa maana nyingine ni kwamba walikubalina na waliokuwa wakiwaambia kwamba bei hiyo ni ndogo kwani kiuhalisia wa biashara ya soko huria, inapaswa kupanda badala ya kushuka.
Leo hata kabla haujapanda, wameanza kupiga kelele za maisha magumu. Naiomba serikali isiwasikilize, izidi kuwahimiza wafunge mikanda kabla ya baa la njaa iliyotangaza kuwa linaweza kuwepo siku chache zijazo halijawadia. Waanze sasa kuzoea maisha yenye ukakasi usiovumilika.
Ni Watanzania wenzangu ambao wengi ninaishi nao huku uswahilini waliowabeza watumishi waliokuwa wakiomba kututumikia ili kwamba kutokana na utumishi wao wenye kutukuka kwa taifa letu, siku moja watoto wetu waweze kusoma bure.
Leo ninapowatizama, wakiwa wanaukodolea macho mwanzo wa mwaka mpya wa 2011 unaowadai walipe kodi za nyumba na karo za watoto wao nawaona wana sura za majuto. Wanasononeshwa na serikali waliyoichagua wenyewe tena siku chache tu zilizopita kwa kushindwa kuwasaidia mizigo hiyo mizito.
Wengine nimesikia wakihoji eti, kama imewezekana kwa Wanyarwanda kuwa maisha mazuri na yenye matumaini kwanini Tanzania isiwezekane. Watu wa ajabu wanajifanya hawajui kuwa haiwezekani kwa sababu ni wao waliokataa iwezekane.
Kwa yeyote asiyesadiki maandishi haya, aje huku uswahilini kwa Wachokonozi asikilize wanavyolia kwa uchungu kuhusu tangazo la serikali la kupandisha bei ya umeme. Wapo ambao wameshaanza kununua vibatari kwa sababu kulingana na kipato chao hawataweza kumudu gharama hizo.
Wameamua kurudi kuishi maisha ya enzi za ujima katika karne hii ya 21 ya sayansi na teknolojia ambapo Tanzania inayoongozwa na serikali inayoimba pambio la ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi!
Katika hali ya halisi ya maisha ya mtanzania kwa sasa, pambio hili ni upuuzi na linatia hasira.Lakini acha kibwagizo chake kiendelee kujirudia masikioni mwa Watanzania ili kiwaongoze katika majuto ya kweli.
Kilio kiko kila mahali kwani hata kwa wale wenye uwezo wa kujikamua na kulipa gharama hizo, umeme umekuwa lulu, unapatikana kwa mgawo na katika sehemu nyingi za uswahili unapatikana usiku.
Mchana shughuli zote zinalala, watu wanashinda wanapiga soga nje ya ofisi zao. Matumaini ya kutekelezwa kwa ahadi lukuki za kusambaza umeme katika sehemu mbalimbali nchini yameyeyuka, yamebaki majuto ya kukosekana kwa umeme na ukali wa mgawo wa umeme.
Majuto haya yanastahili kutokea kwa watu wanaojuta sasa kwa makosa yao ya kuendekeza uroho wa ubwabwa na maharage na kutelekeza haki yao ya msingi ya kutochagua majuto.
Ninapotafakari sana nikiwa katikati ya lundo la watanzania maskini wanaolizwa na kauli ya William Ngeleja, Waziri kijana wa Wizara ya Nishati na Madini, ambaye siku chache baada ya kuteuliwa aliwaambia Watanzania kuwa tatizo la umeme limefikia kikomo, ninaziona mbogo dhaifu za wazee na watu kadhaa wa umri wa makamo zisizokuwa na uwezo wa kifikiri kama walionao vijana wa sasa.
Ngeleja, kwa sisi tunaomfahamu alipotoa kauli ile tulichekea kwapani. Lakini kwa hawa walionyeshwa maji ya bendera walikenua kwa furaha wakitumaini kwamba sasa Tanzania yenye gizaimekoma. Walijidanganya kwa kudanganywa na Ngeleja.
Katikati ya lundo hili la maskini wa kitanzania walio katika majuto baada ya kuyatelekeza matumaini, wanaolia wengi ni wazee na watu wa rika linalokimbilia uzeeni. Wanalalamika kuwa walidanganywa kuwa mambo yatakuwa mazuri baada ya uchaguzi na wakapewa mifano ya jinsi vigogo kadhaa walivyofikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali za ulafi.
Kutoka huko kwa vigogo wanaokabiliwa na tuhuma za ulafi wakageuzwa upande wa pili na kuonyeshwa sinema kadhaa za bunge zilivyokuwa zikichezwa. Wakaonyeshwa tamthilia 'feki' ya Dowans ambayo waigizaji wake wakuu sasa wanafahamika dunia kote kwa umaarufu walionao kama wanavyofahamika akina na Rambo na Van Damme na wakati wakiangalia tamthilia hizo hawakukosa viburudisho vya khanga, fulana, kofia na ubwabwa na maharage vilivyoiharibu kabisa akili yao.
Siku chache baada ya wapigakura kulipa fadhila kwa waliokuwa wakiwahonga khanga hizo kwa kuwapigia kura ya ndiyo, tamthilia ya kweli ya Dowans imeingia Tanzania, hii inaonyesha jinsi watanzania watakavyokamuliwa jasho lao kulilipa dude tulilosadikishwa na serikali kuwa ni 'zimwi.'
Na ukitaka kujua mbivu na mbichi za chama cha maulaji angali tamthilia hizi mbili za Dowans, hii iliyochezwa bungeni na iliyochezwa kwenye mahakama ya kimataifa huko kwa wenzetu walioendelea. Ukitazama vizuri picha hizo ndiyo utajua kuwa bila kukiondoa chama cha maulaji madarakani, chama ambacho watu walioanza kuchoka kiumri wanaking'ang'ania sana,Tanzania italiwa na itakwisha.
Zinajieleza vizuri tu, ukiangalia waigizaji wetu wa hapa nyumbani waliokwenda kuisaka Dowans ughaibuni wanaeleza kuwa Dowans ni zimwi lisiloonekana hivyo hakuna haja ya kuendelea na mkataka nalo ikizingatiwa kwamba liliingia nchini na kuanza kufanya shughuli zake kitaperi.
Tena katika kunogesha igizo lao wakaenda mbali kiasi cha kumtisha mkuu wa kaya kuwa yakiyafumua yote waliyoyabaini kuhusu zimwi hilo basi serikali yake yote yaani na yeye akiwemo itaanguka, lakini kwa sababu wanampenda sana bwana mkubwa, mengine yanayaficha. Akasulubishwa msaidizi wake wa karibu na wenzake wachache.
Lakini huko kwa wenzetu, Dowans imethibitika kuwa ipo, sio zimwi, imekwenda mahakamani imeshinda kesi na sasa tunalazimika kuilipa. Matumaini tuliyopewa yameyeyuka sasa tunajuta kwa kuiamini tamthilia ya waigizaji wetu wa hapa bongo.
Na kama ni kweli kwamba tamthilia hii ya bongo ilichezwa kwa makusudi ya kukomoa baadhi ya watu, kwa sababu mungu yupo, waigizaji wake hawatakwepa mkono wake wakiwa hapa hapa duniani. Lazima watajutia tu igizo lao hilo.
Ninaamini kuwa watajuta kwa sababu mbali na dhambi ya kusababisha majuto kwa watu ambao hawakustahili, watanzania sasa wanalazika kuanza kutoa vijisenti vyao kulipa deni ambalo walidanganywa kuwa haliwezi kuwepo kwa sababu muhusika anayeweza kudai hayupo.
Ni lazima tulipe bila kujali kama tutashinda na njaa, tutakufa kwa kukosa fedha za kununulia dawa kutokana na makali ya kulipa deni hilo au tutashindwa hata kununua chaki za kufundishia watoto wetu huku uswahilini. Laiti tungejua tusingewamini wasanii hawa!
Jambo la msingi ambalo wapiga kura wa Tanzania wanapaswa kulifahamu ni kwamba hivi sasa wanalazima kuishi maishi magumu kwa sababu chama chetu kiko katika mchakato wa kufidia kamasio kurejesha mabilioni ya fedha kiliyoyatumia kuwahonga wao ili wakichague. Hilo ni mbali na maumivu mengine mengi yatakayotukuta kwa kusababishiwa na wasanii wetu.
Ni lazima wengi wetu tule mlo mmoja kwa siku au tulale na njaa kwa sababu tuna deni la kulipia gharama za mabango ya picha za mgombea urais wetu yaliyokuwa yamesambazwa nchi nzima wakati wa kampeni zake za kurejea madarakani. Sote tunajua kuwa gharama hizi zilikuwa za lazima ili kumuwezesha mgombea wetu kushinda na tunaopaswa kuzilipa ni sisi, hivyo asitokee wa kulalamika kwa sababu kinachotekea sasa binafsi niliwahi kuwadokeza Watanzania.
Kama kuna mtu asiyejua hilo nikumbushe hapa kuwa niliwahi kuhoji hivi; 'rais aliyechaguliwa kwa kura nyingi na kukaa madarakani kwa miaka mitano, inakuwaje anahangaika kutumia mabilioni ya fedha ili kuwashawishi wapiga kura wamchague?
'Fedha hizi wangepewa kina Nicholaus Mgaya si wangepunguza kupiga miayo ya njaa na kutishia kugoma kufanya kazi? Matumizi haya ya CCM kumnadi mgombea wao kwa nchi maskini kamahii ambayo ina watu wanaoishi chini ya dola moja kwa siku sio ufisadi?'
Sasa ili haya yaweze kuthibitika na kutimia, mwenendo wa maisha yetu ya kila siku utatuongoza kufika huko kwa kuyafuta matumaini ya maisha bora na kubaki tukijuta kwa kujikosesha kwa makusudi maisha bora katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
 
Back
Top Bottom