Kutakuwa na faida gani kurudisha JKT?

still tunahitaji kuwa na jkt kwa sababu naamini wananchi wake watakuwa wakakamavu na watakuwa wamejengewa ujasiri wa kupigania nchi yao.leo hii mgambo tu wakitisha kidogo watu wanakimbiaana na kujificha. je ukitokea uvamizi wa kigeni wataweza kupigania nchi yao kweli! tuacheni kuponda ujio wa jkt kwa sababu zilizo tolewa na watu wachache wazembe na walioponzwa na tamaa zao. huwezi kuwa mkakamavu bila mateso. mwisho wa kuwasilisha.
 
[h=2]Tuesday, August 02, 2011[/h][h=3]Marudio - Miaka Baada ya tukio kaniomba Msamaha![/h]

(Pichani Ukaguzi wa Gwaride Mlale JKT Songea - Picha kwa hisani ya Michuzi Blog)


Naona, kuna 'Anonymous' fulani kagusia hii swala ya yalionipata nikiwa jeshini JKT. Watu wengi wamenitumia e-mail kuulizia details. Nimeamua kuibandika tena. Ni posti ya kutoka April 2006. Lakini mjue enzi za JKT, wasichana wengi walinyanyaswa kijinsia, mimi nilikuwa na bahati maana nafahamu wasichana waliokuwa gang raped. Dada fulani, alimkubali afande, alivyomaliza kaita wenzake kwa kusema, "Njooni, Mboga hii hapa!" Yule dada hakuweza kutembea vizuri kama wmezi baada ya hapo!

*****************************************************************************

Nilipokuwa Jeshi ya Kujenga Taifa (JKT) karibu nibakwe na afande Fulani (jina nahifadhi). Lazima niseme kuwa katika kipindi hicho wanaume wengi waliona makambi ya JKT kama ‘buffet’ ya wasichana. Si maafande wa jeshi tu, bali hata viongozi wa serikali walikuwa wanapitia makambi ya JKT kula tani yao!

Mimi nilikuwa Masange JKT, Tabora. Wakati huo huyo jamaa alikuwa ni Kepiteni wa JKT. Nadhani alidhania kwa vile yeye ni kepiteni basi alikuwa na haki ya kutembea na yeyote aliyemtaka. Kwangu aligonga ukuta! Bila shaka alikuwa hajawahi ‘kunyimwa’ mpaka siku hiyo alipokutana na mimi.

Miaka baada ya tukio nikiwa nafanya kazi Daily News mara nyingi nilikuwa napishana naye Posta Mpya. Basi ananisemesha, na mimi namnunia halafu napita zangu kimya bila kumjibu kwa hasira. Siku moja kanisimamisha kaniambia, "Chemi, naomba msamaha, nisemahe tafadhali, kweli nilikukosea!” Aliongeza kuwa miaka mingi imepita hivyo sina sababu ya kuwa na hasira naye! Na mimi nilimjibu, “Mshenzi sana wewe!” nikaenda zangu.

Ikapita kama mwaka mwiingine. Jamaa anaendelea kunisalimia kila nikimpita njiani na mimi kwa uchungu bado nikashindwa kusema kitu. Basi nikafikiria alichoniambia Posta Mpya. Lakini niliona kama jambo hilo linamsumbua. Na nikasema kama Bwana Yesu aliweza kusamehe watu kwa madhambi yao kwa nini mimi nisimsamehe. Basi baada ya hapo ikiwa nikimwona na akinisalimia naitika na naendelea zangu na nikaona kidogo hata yeye alikuwa na raha.

Lakini bado najiuliza kama kitendo chake kilimsumbua miaka na miaka kama ilivyonisumbua mimi.Unauliza ilikuaje mpaka nikajikuta kwenye situation ya kubakwa. Au mnasema nilitaka mwenyewe. Ngoja niwaelezee ilivyokuwa.

Nilikuwa mhudumu Officer’s Mess, mpishi na msafishaji. Huyo jamaa alikuwa ni mgeni kutoka Makao Makuu ya JKT Dar es Salaam. Kwa kweli sikutaka kufanya kazi pale Mess lakini tulichaguliwa special na Matron, mimi kwa vile niijua kupika vyakula mbalimbali hasa za kizungu. Lakini uzuri wa hiyo kazi ni kuwa uanambulia mabaki ya vyakula (leftovers), na mara nyingine kulikuwa hakuna.

Basi huyo Afande alikaa kambini wiki kadhaa. Katika kumhudumia tukawa tunaongea na mimi nikawa namheshimu kama kaka vile. Wala sikusikia mapenzi yoyote kwake. Basi jioni fulani, kanialika chumbani kwake kunywa soda na biskuti na kwa Maongezi zaidi. Sasa kama ulienda jeshi unajua njaa kali unayokuwa nayo. Nikaenda, kanikaribisha vizuri, nilipewa soda na tukawa tunaongea. Basi nikaona mwenzangu anabadilika ghafla! Mara ananikumbatia kwa nguvu, na kunibusu na mengine. Nikajaribu kuaga lakini jamaa hakuniachia. Baada ya ku-plead naye aniachie, kaniachia. Kaomba msamaha na kaniomba niendelee kukaa nimalize hizo soda alizoninulia.

Kama mjinga nikamwamini, nikakaa nakunywa hizo soda. Tukaendelea na Maongezi, kukaa kidogo huyo kanirukia, najaribu kusimama huyo, kanivuta na kuniangusha kitandani! Mimi saa hizo nikawa naogopa kabisa nia yake!Kaniambia eti, “ukipiga makelele najua nitasema nini! Nyamaza! Huna sababu ya kunikatalia!” LOH! Kanizaba kibao! Nikamwuliza kwa nini anaifanyia hivyo, na mimi nilikuwa namwona kama kaka yangu!Hapo sasa ikaniingia. Nabakwa! Loh!

Nilimpiga mangumi na mateke lakini jamaa alikuwa na nguvu huyo kachana chupi yangu! Baada ya hapo, jamaa kashika miguu yangu huko anafoka kwa sauti kama vile anatoa amri “panua miguu! PANUA MIGUU!” Huko katoa ume wake uliyosimama kwenye suruali! Basi kuona sipanui jamaa kaongeza makofi na kafanikiwa kupanua miguu yangu! Kuona kafanikiwa kupanua huyo kajaribu kupenya. Ilipogusa kwangu nilipiga kelele cha kufa! Nikasema, “Nakuufaaaa!”

Heh! Ghafla jamaa kaniachia kaniambia niende. Alisema, “Nimeigusa na ume wangu, unatosha!” Nenda zako! Na ukimwambia mtu najua nitasema nini!”Loh nilikimbia bwenini na giza lile la Masange huko nalia. Wenzangu wananiuliza vipi, nikashindwa niseme nini! Kwanza niliona haya! Fikiria, niliona haya (shame)!Kesho yake nikaenda dispensary na kujiandikisha mgonjwa. Sikwenda kazini Officer's Mess bali nililala bwenini.

Siku iliyofuatia huyo Afande mshenzi kapita bwenini kwetu kaulizia hali yangu, na mimi huko natetemeka kwa woga nikashindwa niseme nini. Alininunulia Orange squash na biskuti na kuzileta bwenini. Sitasahau alivyonitazama! Ilikuwa kama vile anapanga jinsi gani atanipata. Baada ya hapo alimwopoa msichana mwingine na huyo alimkubali kabisa. Akawa analala kabisa huko Officer’s Mess. Hakuna anayemsumbua wakijua ni bibi wa Afisa. Basi, siku za yule jamaa kukaa kambini zikaisha, na yule binti alienda naye Tabora mjini kwa siku kadhaa. Halafu jamaa karudi zake DSM. Yule binti karudi zake kambini! Kumbe alienda bila pass. Alidhania kwa vile yuko na mkubwa hana haja ya pass. Na yule Afande ndo kaondoka kimoja! Maafande waliobakia wacha wamtese huyo binti alivyorudi kambini! Walimtesa kwa Extra drill na mengine mpaka ikabidi Military Police waombe wakuu wamsamehe la sivyo atakufa. Raha yake iliishia kwa suluba! Sijui yule binti alidhania jamaa atamwoa! Kwa nini alimkubali yule mshenzi.

Anyway, kila mtu na vyake. Alivyotoka kwenye suluba tulimwuguza! Siku haizkupita na mimi nilitolewa kazi Officer’s Mess na kupelekwa kwenye kikosi cha Ujenzi na lazima nisema hapo nilifurahi sana. Basi miaka ilipita. Mimi nilikuwa mwandishi wa habari Daily News, tena nilijenga jina. Sasa nikawa napishana na yule jamaa huko kapandishwa cheo na yuko JWTZ. Jamaa anajaribu kunisalimia na mimi napita zangu kimya, namnunia kabisa.

Nilimwona mshenzi, mnyama, na kila kitu kibaya ndo ilikuwa yeye! Angefanikiwa kuingiza na kunimwagia uchafu wake ningejiona mchafu mpaka leo! Miaka kama 20 imepita sasa na bado nina uchungu naye.Jamani nyie wanaume nawaambia kubaka kinaathari zake kwa wanawake. Unataka raha ya dakika na unamwachia mwenzio na uchungu wa maisha! Wengine mpaka wanakuwa wagonjwa wa akili.

Kwa nini nimeamua kuzungumzia kubakwa kwangu hapa, ni kwa sababu naona wasichana wengi wanabakwa, halafu wanaamua kunyamaza kimya. Kisa wakienda polisi na hospitali wanahofia kuambiwa ni Malaya au walitaka wenyewe! Hata mwamanke mwenzako anaweza kukufokea kuwa ulitaka mwenyewe. Tanzania, wanaume walikuwa na usemi wao kuhusu wanawake na ngono. Walisema eti ukimwomba mwanamke halafu akijibu ndiyo, manake ndiyo atafanya. Akisema labda, manake atafanya, akisema hapana, manake hapana. Lakini jamani tendo si inakuwa tamu kama wote mmekubali? Na kama angefanikiwa kuingiza si angeniumiza sana!

Wengine wanasema ningemshitaki. Je, ningemshitaki ingekuaje? Kwanza jeshini mimi ningepewa Extra Drill mpaka niumie au kufungwa jela ya jeshi iliyojaa maji na mbu kusudi niteswe. Kumbuka ilikuwa Tanzania na yule alikuwa ni Kepiteni wakati huo na mimi nilikuwa Private. Hakuna ambaye angekuwa tayari kunisikia zaidi ya wenzangu maPrivate, na yeye alijua hivyo. SHENZI TAIPU!


Posted by Chemi Che-Mponda at 4:13 PM

Labels: Jeshi, Jeshi la Kujenga Taifa, JKT, Masange JKT, Matron, Ubakaji
kama asinge fata hiyo biskuti na soda yangemkuta hayo!! tatizo tamaa ndio ilimponza.inamaana hakujiuliza kama alikuwa kaka yake kwa nini asingepewa hivo vitu kwenye public places walizokuwa wanakutana kila siku mpaka akampee chumbani kwake. kweli tamaa ni upofu, na dada zetu wengi wameshapofuka hata uwaambiaje hawaachi mpaka yawakute ya kuwakuta'
 
Chemi halikuwa hajui kuwa zamani katika nchni za Kikomunisti wanawake Jeshini walikuwepo kwa ajili ya kustarehesha wanaume na si kama sehemu ya Askali kamili wa kwenda vitani!
 
Kimsingi sina tatizo sana na hoja ya kurejesha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.Ni kweli kwamba ziko faida kadhaa za kupitia kwenye jeshi hilo kama wengi walivyoweza kubainisha. Hatahivyo, si sahihi kupuuza hoja za kuwepo kwa upungufu/udhaifu mkubwa sana katika uendeshaji wa mafunzo hayo.Na moja ni kama walivyoelezea baadhi ya wachangiaji kuhusu unyanyasaji wa kijinsia ulikuwapo wakati huo tunashiriki mafunzo hayo.Wengi tulishuhudia ubabe wa kipuuzi uliofanywa na baadhi ya maafande kwa lengo la kukidhi matamanio ya kingono.Nakumbuka kuna wakati nilimsikia afande mmoja akimuorozeshea afande mwenzie idadi ya wadada aliojirusha nao kwa kipindi cha ukuruta wetu.Maana hiki kipindi cha ukuruta ndio kilikuwa na kashikashi sana, baada ya hapo mtu ukiwa umefikia hatua ya serviceman hali inabadilika.Unakuwa na hadhi ya askari kamili kiasi cha kutoweza tena kuburuzwa na maafande.Hata hii story ya huyu dada imenishangaza kwamba alifanyiwa uhuni huo akiwa kwenye ngazi ya userviceman,hapa nimeshangaa kidogo.
Anyway, haya sasa ni madhaifu ya mafunzo ya JKT ya wakati huo.Sina hakika na sishawishiki kuamini kwamba mafunzo mapya ya JKT yakirudi tena kama yataendelea kuwa na udhaifu uleule wa zamani.Sababu ni nyingi sana,lakini moja kubwa ni mazingira ya sasa ya uwazi na utawala wa sheria ulioimarika. Mazingira ya sasa yamejaa wanaharakati kila kona ambao naamini hawatanyamaza kuona vitendo vya kishenzi vinafanyika makambini kinyume na malengo ya mafunzo.
Teknolojia iko juu sas hivi kiasi cha kuweza kuwabaini askari wataokuwa hawana maadili.Kumbuka enzi hizo hata siku za mkononi hazikuwepo.Lakini pia kuna suala zima la mapambano dhidi ya UKIMWI. Enzi zetu(operesheni vyama vingi) suala la Ukimwi halikuwa linapewa uzito sana kutokana na madhara yake kutokuonekana sana katika jamii kama wakati huu. Hivi sasa mtu anayetaka kuwa askari wa majeshi yote sharti la kwanza ni kutokuwa na maambuzki ya VVU.Sasa simanini kama nao askari watakubali kuchafua afya zao kwani wanajijua kuwa wako salama,hivyo ni imani yangu kuwa hata kama watakuwapo wasiojali, basi itakuwa kwa idadi ndogo kulinganisha na enzi zetu ambapo ilichukuliwa kama mshindano kwa maafande kujirusha na makuruta.
Lakini pamoja na mambo yote hayo,suala moja ambalo ni muhimu ni aina ya sheria ya mafunzo hayo itakavyokuwa. Wakati ule JKT kwa mujibu wa sheria ilkuwa na maana na nguvu kutokana na hali halisi ya wakati ule. Ilikuwa huwezi kupata ajira au kuendelea na elimu ya juu bila kuwa umepitia JKT. Lakini je, kwa mazingira ya sasa ambapo kila kitu,kuanzia elimu na ajira ni huria itawezekana kuwalazimisha watu kupitia JKT? Hapo mimi ndipo napata shida. Maana naamini haitakuwa rahisi kuwaambia wamiliki wa vyuo binafsi eti wasipokee vijana ambao hawajapitia JKT,itakuwa ngumu.
Hivyohivyo,kuwaambia waajiri binafsi wasiwaajiri vijana ambao hawajapitia JKT. Kwa miaka ile, ndio!,ilikuwa rahisi kwani elimu na masuala yote ya ajira yalikuwa chini ya dola,kwa hiyo penda usipende utakwenda tu JKT. Na ndio maana kuna Mh.Waziri mmoja katika serikali iliyopo madarakani anazongwa sana na hoja ya kukosa uzalendo kwa kukacha JKT. Mh huyu yeye alipomaliza kidato cha sita tu,na kwa kuwa ni mtoto wa kiongozi mzito,alifanya mipango akaenda kusoma nje ya nchi na akakaa huko hadi JKT ilipofutwa ndipo akarudi nchini.Na jambo hili ni moja ya mamabo machache sana yanayompunguzia credit katika harakati zake za urais 2015. Kwahiyo,ni mazingira kama hayo wapendwa!!
 
Back
Top Bottom