Kumbukizi ya Mwl Nyerere na ''the torch on Kilimanjaro'' kitabu cha shule za msingi kinachoeleza historia ya Mwl Nyerere wakati wa kupigania uhuru

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,925
30,273
Wala haikuwa katika fikra yangu kuwa kitabu nilichoandika miaka 12 iliyopita na kuchapwa na Oxford University Press Nairobi (OUP) kama sehemu ya mradi wa vitabu vya kufundisha lugha ya Kiingereza kwa shule za msingi na katika kusoma vitabu hivi wanafunzi wajifunze uzalendo na historia ya viongozi wa nchi zao kitawavutia watafiti wa Kumbukizi ya Nyumba ya Mwalimu Nyerere kama kitabu kinachostahili kuwepo ndani ya nyumba ya Baba wa Taifa.

Tulikuwa katika kuchagua picha ndipo mmoja wa hawa watafiti akaona jina la kitabu hiki na akaniuliza hiyo ni picha gani?

Nikamfahamisha lakini akashangaa kuwa hajapatapo kukiona popote kitabu hiki kinachomuhusu Mwalimu Nyerere.

Nikamfahamisha kuwa juu ya juhudi za OUP kukifanyia uzinduzi Kilimanjaro Kempinski hafla ambayo ilihudhuriwa na maofisa waaandamizi wa Wizara ya Elimu, walimu wa shule za msingi, na wauza vitabu na kila aliyehudhuria hafla ile kutunukiwa nakala ya kitabu, kitabu hiki kimekuwa kama vile hakipendezi kwani kusudio la OUP kuwa kitabu hiki kitaingizwa katika mtaala wa shule za msingi Tanzania halikutimia.

OUP walialika waandishi wa Afrika ya Mashariki kupeleka miswada yao kwao kwa ajili ya mradi huu na vitabu karibu 15 vilichapwa kutoka Kenya na Uganda lakini kwa bahati mbaya hapakuwa na mswada hata mmoja ulioandikwa kutoka Tanzania.

Jambo hili liliwahudhunisha OUP.

Hapo ndipo waliponiomba niandike kitabu kuhusu harakati za Mwalimu Nyerere katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Niliwafahamisha kuwa sijawahi kuandika kitabu cha watoto lakini wao wakaniambia wako tayari kunielekeza ili kipatikane kitabu cha Mwalimu Nyerere kwa ajili ya shule za msingi za Tanzania na Afrika ya Mashariki.

Ndipo nikaandika kitabu hiki kwa muda mfupi na nikawapa mswada na wakachapa kitabu hiki, ''The Torch on Kilimanjaro,'' ambacho hakikufaulu kwa mwandishi na mchapaji ingawa kitabu hiki kinasomeshwa Kenya na Uganda na nchi nyingine za Afrika na sasa kimechachapwa mara ya pili mwaka wa 2015.

Kwa kuwa mswada huu haukufaulu Tanzania, OUP ambao waliniomba niwape mswada makhsusi kwa ajili ya Zanzibar waliamua kusitisha kuchapa kitabu hicho, ''The School Trip to Zanzibar,'' ambacho ingawa walisema ni kazi nzuri lakini bahati mbaya hakina soko kwa mlengwa wakiwa na maana Tanzania.

Kwangu mimi nitafarajika kwa kule tu kitabu hiki, ''The Torch on Kilimanjaro,'' kuwepo ndani ya nyumba ya Mwalimu Nyerere ingawa watoto wa shule za msingi waliokusudiwa kukisoma hakijawafikia kutoka mwaka wa 2007 kitabu kilipochapwa.

Picha: 1. Watafiti wa Kumbukizi ya Nyumba ya Mwalimu Nyerere wakikiangalia kitabu, ''The Torch on Kilimanjaro,'' (2007) First Edition 2.Mohamed Seif Khatib katika Uzinduzi wa Kitabu, ''The Torch on Kilimanjaro,'' Kilimanjaro Kempinski Hotel kulia kwake ni Sheikh Abdillah Nassir aliyepata kuwa Managing Director wa OUP 3. Mwandishi katika sherehe ya uzinduzi wa kitabu.4. ''The Torch on Kilimanjaro,'' (2015) Second Edition.


1570014424872.png

Second Edition (2015)
 

Attachments

  • 1570014177386.png
    1570014177386.png
    215.3 KB · Views: 11
Back
Top Bottom