SoC03 Kukuza Kiwanda Bunifu cha Muziki wa Singeli Kupitia Biashara ya Urithi wa Utamaduni

Stories of Change - 2023 Competition

Kijava Martin

Member
Jul 23, 2023
5
2
UTANGULIZI.

Hatupaswi kulalama kuhusu ajenda ya uchumi wa viwanda na mchango wa kisekta ikiwa tunu ya utamaduni ya muziki adhimu wa Singeli haujengewi mpangokazi mahsusi ili kuboresha katika namna ya maudhui na mapokeo katika hadhira ya ndani na nje ya nchi, misingi ya kuutambua na kulinda kwa sera na sheria, pia kutoa kipaumbele kama zao la kiwanda bunifu cha utamaduni wa mtanzania.

Kupitia umoja wa Afrika 2015, kwamba kizazi cha sasa kipo imara kwamba hatma ya afrika ipo mkononi mwao, na ni lazima kuchukua hatua sasa ili kutengeneza kesho wanayoitaka.

Ajenda ya kuhuwisha fikra za sanaa zalishi katika safari ya kufikia maendeleo ya kiwanda bunifu ni swali linalijibika kikamilifu na uwepo wa muziki wa Singeli nchini ukiwa sehemu ya uzalishaji kutoka urithi wa utamaduni.

Si hivyo tu, uchambuzi na tafsiri kuhusu mashiko ya kihistoria na muendelezo wa utamaduni katika fikra za kiafrika kwamba maendeleo hutokea pindi mipango na sera zote kutegemea uwezo wa kila mtu katika jamii kutokana na mjumuisho wa mfumo wa kuishi unaodhihirishwa katika eneo husika. Zaidi ya hapo, Walter Rodney alinukuliwa akieleza kuwa maendeleo ya binadamu ni namna ambayo uelewa, uthibiti, na maboresho ya utu huzingatia mabadiliko ya mazingira ya ndani na yanayomzunguka mtu katika maisha yake kwa kutumia nyenzo atakazo buni au asilia.

MUZIKI WA SINGELI NI NINI?
Muziki wa Singeli ni zao la Urithi wa sanaa ya ngoma za asili kutoka makabila mbali mbali ya Tanzania ambayo mila na desturi zake huendana. Muundo wa Singeli umezaliwa kutoka Ngoma hizi za asili ikiwemo Sindimba, Vanga, Chakacha, Mdundiko, Dumange, Beni, Vugo, Baikoko, na Lelema. Hata hivyo mtindo wa Singeli umebeba vionjo kadhaa kutoka katika aina fulani ya muziki wa ndani na nje ya nchi ikiwemo Taarabu, Mchiriku, Segere, BongoFlava, na Raggae.

Balaza la Sanaa la Taifa (Act No.23, 1984) hutafsiri muziki kama muundo na mtindo wa ala za sauti na vyombo zilizo katika mpangilio fulani katika namna ya kuandikwa au kurekodiwa. Kulingana na takwimu za BASATA ni zaidi ya watanzania milioni sita ambao wanajishughulisha katika sekta ya sanaa.

SOKO LA MUZIKI WA SINGELI
Hapo awali soko la muziki wa Singeli limekuwa likibezwa mno huku muziki huo ukihusishwa na kutokustaarabika, wa uswahilini, wa kishamba. Mbali na hapo, umekuwa ukichorwa kama jukwaa la kueneza mihemko ya kihuni. Kufikia mwaka 2015 BBC iliripoti mlipuko mkubwa wa soko la muziki wa Singeli katika miji hadi vijiji nchini Tanzania. Kuanzia hapo muziki wa Singeli umekuwa ukishika hatamu kila kona ya nchi na nje ya nchi kutokana na mguso wa kipekee wa burudani katika jamii. Imekuwa deni kubwa la kimsisimko wa sherehe yoyote ikiwemo kampeni na matamasha ya serikali, matamasha ya burudani, matangazo ya biashara, harusi na sherehe mbalimbali za kijamii ikiwa muziki wa Singeli haupo.

BIASHARA YA URITHI WA UTAMADUNI
Biashara ya Urithi wa utamaduni ni namna ambayo jamii inanufaika kutokana na utengenezaji wa faida kutokana na Tunu ya kitamaduni inayodhihirisha utu wao katika eneo husika. Mfano ni Utalii wa utamaduni katika Maasai Boma na jamii ya Wasandawe. Mtindo wa biashara ni namna ambayo mtengeneza faida hutambua na kutumia vyanzo vya mali na kuweka sokoni kwa thamani ili ajipatie pesa. Kwa namna hii, kukuza kiwanda bunifu cha Muziki wa Singeli ni kuchochea biashara kimataifa kutokana na uzalishaji wa ndani ya nchi katika ajenda ya uchumi wa viwanda nchini.

MUZIKI WA SINGELI NA MAADILI YA JAMII
Taharuki juu ya udhibiti wa maadili ni suala mtambuka na lenye kuibua hofu kubwa kutokana na mvutano wa Usasa, Mila na Desturi, Utaifa na Uraia wa Ulimwengu. Hofu ya maadili hutokea ambapo hali fulani, tukio, mtu au kipindi cha watu huibuka na kutambulika kuwa tishio dhidi ya taratibu za maisha katika eneo fulani. Japokuwa katika hali ya hofu ya maadili jinsi jambo hilo huwa linaendewa na kuchakatwa kupitia vyombo vya habari, mamlaka ya udhibiti wa sheria, wanasiasa na umma kwa ujumla huwa ni kinyume na zaidi ya uhalisia wa hatari au tishio hilo la maadili katika eneo husika hivyo hofu hukuzwa zaidi.

Uchambuzi yakinifu juu ya taharuki ya maadili inayotokana na sanaa ya utamaduni kwa mfano, mtindo wa kucheza Kangamoko, Baikoko, na Chura ambapo kwa sasa vyote vinahusishwa moja kwa moja na tasnia ya muziki wa Singeli, hivyo muziki huu huchorwa kama pango la kufuga taharuki hii kwa umma. Lakini, vichochezi vinavyopelekea maonesho ya wazi ya uchezaji wa mitindo hiyo kinyume na maadili ya jamii ni kutokana na hali ya sitofahamu ya kiuchumi na kijamii ikiwemo ukosefu wa ajira, Umasikini, Ujinga, na kutojitambua. Hoja hii hujazilizwa sambamba na hotuba ya aliekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni ma Michezo -2013, Dr. Fenella Mkangara "Mheshimiwa Spika, Sekta ya maendeleo ya utamaduni ilikabiliana na changamoto kubwa ya kuendelea kumomonyoka kwa maadili miongoni mwa vijana kutokana na athari za utandawazi. Aidha, katika zoezi la kurasimisha tasnia za filamu na muziki baadhi ya wadau hawakuwa na uelewa kamili wa sheria na kanuni za tasnia hiyo...."

UMUHIMU WA KUKUZA KIWANDA BUNIFU CHA MUZIKI WA SINGELI.
Kukuza kiwanda bunifu cha muziki wa Singeli huchagiza maendeleo mbalimbali kitaifa ikiwemo ongezeko la ajira rasmi katika sekta ya utamaduni, ongezeko la mapato serikalini, kuingia katika jukwaa la mashindano ya kiuchumi kimataifa kupitia kazi za muziki wa Singeli, kurahisisha kusambaa kwa lugha ya Kiswahili kimataifa, kuvutia zaidi vivutio vya utalii wa utamaduni visivyo hamishika, kuwezesha kurasimisha mdundo wa Taifa kwa hisia za kimuziki pamoja na kuimarisha uhifadhi na kuthamini Tunu nyingine za utamaduni ndani ya nchi.

HITIMISHO.
Hivyobasi, tafiti mahsusi zifanyike kimkakati, mpangokazi wa kitaifa utengewe bajeti ya kutosha, mabingwa wabobezi katika kiwanda bunifu cha muziki wa Singeli na biashara ya Urithi wa Utamaduni wahusishwe katika kukuza bidhaa hii. Wizara ya mipango na sera inasubiriwa kwa hamu katika mpangokazi na dira ya kitaifa kama hii.
 
DJ miso missondo kadhihirisha tena kuwa Mnanda/Mchiriku au Singeli haiwezi kufa hata ikihujumiwa vipi
 
Aliyekuambia kinachoitwa singeli ni muziki ni nani? Hayo si Yale mangoma ya kienyeji ya waramo wanayopita mitaani wakikatika na kusomba watunyaitwayo mdundiko?
 
Aliyekuambia kinachoitwa singeli ni muziki ni nani? Hayo si Yale mangoma ya kienyeji ya waramo wanayopita mitaani wakikatika na kusomba watunyaitwayo mdundiko?
Ni mchanganyiko wa mangoma mengi ya asili sikia ngoma inaitwa Hauna imeimbwa na Man Fongo
 
Back
Top Bottom