KUFUKUZWA KWA BENO MALISA - Malisa na Nape: Adui yao ni mmoja, bora wapatane

Malisa na Nape: Adui yao ni mmoja, bora wapatane
Mwandishi Maalum

Toleo la 239
16 May 2012


malisa.jpg



HABARI za kwamba Benno Malisa, Makamu na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM kufukuzwa ndani ya kikao cha Kamati Kuu na Mwenyekiti wa CCM, zilivuta hisia za haraka.


Kitendo cha Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM kuitisha kikao cha haraka sana akiwa na Malisa ili kukanusha habari hizo, kinathibitisha jambo moja tu. Kwamba, jambo lenyewe lilitokea, na kama ungekuwa ni uzushi, Malisa ndiye angeitisha na kukutana na wana habari.


Si mara ya kwanza kusikia Benno Malisa “akichafua” hali ya hewa ndani ya vikao vya CCM. Mimi nimetokea kumpenda na historia ni hakimu wa kweli, Benno Malisa awe ndani au nje ya CCM ataifaa CCM kuliko viongozi wa sasa wa CCM wanavyoweza kuelewa kwa sasa. Nijieleze.


Benno Malisa hamuogopi Mwenyekiti kama walivyo wengi ndani ya chama hicho. Mwenyekiti ndani ya CCM ni taasisi na “mungu mtu”. Hahojiwi, hapingwi, hakosolewi na haambiwi ukweli usiotiwa sukari kwanza. Matokeo ya tabia hii, ndiyo yanayoiangamiza CCM kwa kasi ya ajabu.


Tumewahi kusikia Benno Malisa akihoji dhana ya kujivua gamba ina maana gani na akaomba muasisi akieleze kikao cha Kamati Kuu ili wajumbe wote waelewe. Tumewahi kusikia au hata kushuhudia ndani ya vikao Benno Malisa akihoji uharaka wa kuwafukuza wanaoitwa mafisadi ndani ya chama bila kufanya uchambuzi wa kina kubaini nani si fisadi ndani ya CCM. Malissa kwa fikra za haraka na za ajabu, alisema hana pingamizi na kuwaita hao mapacha watatu kuwa ni mafisadi, bali angependa kujua nani si fisadi ikiwa hao watatu ni mafisadi.


Alipopuuzwa, kulitokea tishio la UVCCM kuasi na tayari vijana walisikika kutoka kila upande wa nchi wakijiandaa kuelekea Dodoma. Kikwete aliishia kufoka na kurusha vijembe. Mpango wa kuvuana magamba ukakwama, ukaibuliwa mkakati mwingine wa kupeleka masuala yote kwenye kamati za maadili. Wenye akili tukajua, hayo ndiyo mazishi rasmi ya dhana ya kuvuana gamba. Kama Kikwete ni muasisi wa dhana ya kujivua gamba, Benno Malissa ni muasisi wa kifo cha dhana hiyo.


Alipojiuzulu James Ole Millya na kujiunga na CHADEMA, watu wasiofikiri haraka walikejeli na kutukana. Benno Malissa alisema anasikitika kwa hatua aliyoichukua Millya, aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha. Malissa hakuona kama ni vema kupiga teke sufuria ulilowahi kupikia chakula kitamu. Malissa anatamani hekima na hatua za kisiasa zichukuliwe haraka kuliko kubezana na kuitana majina wakati huu chama kinapopoteza wanachama kwa kasi kubwa.


Tumewahi kumwona Benno Malissa wakati wa chaguzi ndogo za Igunga na Arumeru Mashariki akijitahidi kuonana na wapinzani kwa agenda zenye manufaa ya jamii nzima. Aliguswa na suala la vijana kujihusisha na uvurugaji wa mikutano ya vyama. Akaona njia ya haraka na ya kudumu ni kuongea na wapinzani ili vijana wa pande zote waonywe na kutulizwa ili wajifunze siasa. Alionekana muasi ndani ya chama chake, lakini kimsingi yeye alionyesha uongozi unaoonekana kukosekana ndani ya chama chake.


Suala la uteuzi wa wakuu wa wilaya ambalo inasemekana alilihoji na kusababisha afukuzwe ndani ya kikao ni la msingi. Wengi wamehoji uteuzi huu. Wengi wa walioteuliwa wanafaa zaidi kuwa makatibu wa CCM wa wilaya na mikoa kuliko kuwa wakuu wa wilaya. Malissa amekumbusha makubaliano ya mwaka jana kuhakikisha watendaji hawarundikiwi vyeo. Suala hili lilikuwa mwiba na kuibua mjadala mkali ndani ya chama wakati wa mapendekezo ya kuwaondoa wabunge katika NEC. Hata hatua alizochukua Mwenyekiti Kikwete kuwaondoa akina Membe katika sekretariati zililenga kutekeleza makubaliano haya ya awali.


Inakuwaje tena wabunge wanateuliwa kuwa wakuu wa wilaya? Inakuwaje makatibu na wenyeviti wa CCM na jumuia zake katika mikoa na wilaya wanateuliwa kuchukua wajibu mwingine wakati uhai wa chama unasuasua katika wilaya na mikoa yao?


Inakuwaje Mwenyekiti wa chama kinachotawala athamini zaidi kazi za Serikali kuliko za chama pale anapowaondoa watendaji wa chama kuwapeleka serikalini? Mbona tathmini ya akina Mukama iliyotumika kuasisi dhana ya kujivua gamba ilidai kuwa ndoa kati ya serikali na chama inakiponza chama zaidi?


Mbona watu wengi wanashangaa jinsi CCM inavyonywea mbele ya Serikali na kushindwa kuisimamia? Maswali haya, ndiyo aliyouliza Benno Malissa akaishia kufokewa na kuamriwa kutoka nje.


Kwa wanaoona mbali, watakubaliana nami kuwa mustakabali wa CCM uko mikononi mwa vijana kama Nape na Malissa. Ukitazama hata picha za vikao vya CCM utagundua kuwa chama hicho hakina uhai kikiwa mikononi mwa wazee wachovu. Asilimia zaidi ya 70 ya wanaofanya maamuzi ndani ya vikao vya CCM ni wazee walio zaidi ya miaka 50. Hawa wamelindwa na mfumo na wanaendelea kufaidi matunda ya mfumo lakini hawana njia ya kuubadili mfumo ili uwe na uhai mpya.


Damu na fikra za kina Nape na Malissa zinahitajika ili kuiokoa CCM. Hivi sasa si siri kuwa ndani ya CCM hakuna mtu mwingine nje ya Nape na Malisa mwenye uwezo wa kuongea na vijana akaeleweka.


Vijana wana hasira, wamekata tamaa na hasa wale wa vyuo vikuu. Sera na misimamo ya CCM ni mizuri kwenye makaratasi lakini haielezeki kirahisi kwa vijana. Wanaoweza kujaribu kama wangeacha unafiki, ni Nape na Malissa.


Tatizo ninaloliona ni kuwa hata hao vijana (Nape na Malissa) hawajaelewa kwa uzito suala ninalozungumzia. Nape alimburuta Malisa kuja kumuaibisha mbele ya kamera za waandishi. Ni sawa tu na Idd Amin alipodaiwa amemuua Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini Uganda, Janan Luwum, aliwaita waandishi wa habari Ikulu, akapiga picha naye na mkewe na watu wote wakaona. Idd Amin akawatukana waandishi wa BBC kuwa ni wazushi kwa sababu Askofu huyo ni rafiki yake kama wanavyoona wenyewe.


Askofu alipulizwa, alitabasamu tu. Usiku huo huo, Askofu aliuawa, gari lake likachomwa moto na kudaiwa alipata ajali na gari likaripuka na kumuua. Kwa hofu ya kugundua ujanja huo, mwili wa Askofu ulizikwa na jeshi kijijini kwao badala ya kuzikwa kanisani Kampala ambako umati ulikusanyika na kaburi likiwa tayari limechimbwa.


Kwa kukubali kuja na Nape mbele ya kamera ili kukanusha kuwa hakufukuzwa kutoka nje ya kikao, Malissa anaweza kuwa amefanya kosa kubwa la kisiasa. Muda utaamua.


Lakini kosa kubwa liko kwa Nape Nnauye. Adui wa Nape na CCM yake si CHADEMA, si waandishi habari anaowaita wazushi, si Benno Malissa. Adui wa Nape na Malissa kisiasa ni mmoja. Huyo ni uongozi wa juu wa chama chao, ambao ni mzito kusoma alama za nyakati, mwepesi wa kuchonganisha watendaji ili iwe rahisi kuwaongoza, na mwepesi wa kuwatosa wanapoingia katika mgogoro wakati wanautetea na kukitetea chama.


Nape anachelewa kujiunga na Malissa katika mapambano yenye maslahi mapana ya chama kuliko kuutumikia uongozi unaomaliza muda wake.


Mmoja wa vigogo wa CCM ambaye hutumiwa na chama katika ufumbuzi wa mambo mazito yanayokanganya, alipata kunon`gona: Ili CCM iweze kushinda katika chaguzi zinazokuja, haina budi kuwaruhusu wagombea wake waitukane hadharani.


Alimaanisha kuwa lazima aina fulani ya uasi iruhusiwe ili kukiokoa chama. Nilipoona Wilson Mukama akimkemea Edward Lowassa wiki iliyopita, hekima ya mjumbe huyo kigogo ikadhihiri.


Inahitajika semina elekezi ya mtu asiye wa CCM, asiye na maslahi ndani ya CCM, asiye na kundi, akae na Kamati Kuu na NEC, awaambie mambo haya kwa uwazi na ukweli. Kufukuzana na kutofukuzana kwa sasa, hakuisaidii CCM maana wanaofukuzwa na wanaobaki wote ni wale wale.












Malisa alimpa kiasi gani mwandishi wa hii stori yake?
 
Beno Malisa anapoteza muda wake kubakia CCM inayokufa. Beno na vijana wa aina yake wenye maono ya utaifa ndani ya CCM wanapaswa kufanya maamuzi magumu kabla mambo hayajaharibika zaidi. Kwa wajuzi wa historia ni kwamba CCM sasa hivi iko ktk awamu ambayo tukio dogo linaweza sababisha kishindo na kifo chake!
Labda wana imani kuwa ipo siku chama kitarudisha mvuto wake kilichokuwa nao hapo kabla.
 
Kubwa zaidi hapa ni kufukuzwa kwenye kikao kwa Beno Malisa,mbona magazeti hawakundika taarifa nzuri namna hii?
kwa nini alifukuzwa au anaonekana mkweli kila anapohoji kitu?
 
Kifo cha CCM ni moja kwa moja. Hiki chama hakifiki 2015 kikiwa imara. Na hakitakuwepo tena ulimwenguni baada ya kuachia nchi. Naomba mucopy na kupaste hii message yangu. Mutaikumbuka.
 
Beno Malisa ni mchezaji mzuri aliyevaa na jezi chafu
Joint venture yake na Serukamba inawezekana inamfanya awe mfuasi wa kambi nyingine yenye nguvu ndani ya CCM. Yeye kijana mdogo, hajui busara ya kutulia badala ya kuchagua upande bila kujua hatima yake itakuwaje?
 
Benno Malisa hamuogopi Mwenyekiti kama walivyo wengi ndani ya chama hicho. Mwenyekiti ndani ya CCM ni taasisi na "mungu mtu". Hahojiwi, hapingwi, hakosolewi na haambiwi ukweli usiotiwa sukari kwanza

Benno ni mpiganaji wa kweli aliye kwenye njia hisiyo sahihi, anguko la CCM litakuja kumpotezea weredi wake.
 
Benno Malisa hamuogopi Mwenyekiti kama walivyo wengi ndani ya chama hicho. Mwenyekiti ndani ya CCM ni taasisi na “mungu mtu”. Hahojiwi, hapingwi, hakosolewi na haambiwi ukweli usiotiwa sukari kwanza

Benno ni mpiganaji wa kweli aliye kwenye njia hisiyo sahihi, anguko la CCM litakuja kumpotezea weredi wake.
siku ccm inapigwa chini watu wataanza na ridhiwani manake wamempania ile mbaya atapata shida sana
 
Back
Top Bottom