Korona: Watanzania Tujilinde, Serikali inajali Uchumi kuliko Uhai wenu - Zitto

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,885
KORONA: HATUA ZA SERIKALI NA UMUHIMU WA KUJILINDA WENYEWE

UTANGULIZI

Ndugu wananchi wenzangu,

Kama mnavyofahamu, sisi ACT Wazalendo tumekuwa tukiuchukulia kwa uzito wa juu kabisa ugonjwa wa Virusi vya Korona (Covid 19). Sio tu kwa sababu tunaamini kwamba ugonjwa huu kama janga la dunia unahitaji jitihada za pamoja, bali pia kutokana na mwingiliano mkubwa miongoni mwa wananchi wetu na nchi za jirani (tunayo mipaka ya nchi kavu na nchi takriban 8).

Aidha, tunatambua kwamba, asilimia kubwa ya wananchi wetu wana magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari na presha. Vilevile, kutokana na ugumu wa maisha unaotokana na sera mbaya za kiuchumi, wananchi wengi wana sonona na msongo wa mawazo, kwa hiyo, kinga zao za mwili ziko chini sana na hivyo, wakipata maambukizi ya korona wanakuwa katika hatari kubwa zaidi.

Kutokana na ukweli huo, na uzalendo wetu kwa Taifa, kwa nyakati tofauti, viongozi wa chama cha ACT Wazalendo wakiwemo Mwenyekiti wetu, Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu Wenyeviti, ndugu Dorothy Semu na ndugu Juma Duni Haji, na Katibu Mkuu ndugu Ado Shaibu na naibu wake ndugu Nassor Mazrui,tumekuwa tukitoa maoni yetu kwa Serikali zote mbili (ya JMT na SMZ) kuhusu umuhimu wa kutanguliza Sayansi kwenye mapambano ya Kisayansi; kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za kujilinda na kuchapusha upatikanaji wa vifaa kwa watoa huduma za afya.

Mtakumbuka kwamba, mara ya mwisho kuzungumza nanyi kuhusu mapambano ya Korona, niliwafahamisha kuhusu Barua ya Chama chetu kwa Mheshimiwa Rais iliyokuwa na mapendekezo kadhaa kuhusu namna bora ya kupambana na ugonjwa huu, wakati ambapo maambukizi yalikuwa bado yako chini. Baadhi ya mapendekezo yetu ilikuwa ni pamoja na;

(i)Kuleta mshikamano katika nchi kwa kufanya kazi kwa pamoja na watu wote.​
(ii) Kuteua timu ya wataalamu ili kufanya uchambuzi wa kina wa madhara ya Covid 19 kwenye uchumi na maisha ya wananchi;​
(iii)Kuwa na Mfumo wa Mawasiliano kwa Umma ambao unazingatia Sayansi (kuwatanguliza mbele wataalam) badala ya maneno ya kupeana moyo tu na​
(iv)Kupunguza watu Magerezani kwa kuwapa dhamana watu ambao wana kesi zisizo na dhamana.​

Bahati mbaya sana maoni yetu yalitupiliwa mbali, na leo tunashuhudia hatari kubwa iliyo mbele yetu. Hata hivyo, tunafarijika sana kuona namna ambavyo, wananchi walivyohamasika kupitia kampeni zetu mbalimbali za kupambana na Korona. Tunaamini kama hamasa hiyo ingekutana na utashi wa kisiasa kwa waliopewa dhamana za Uongozi, tungekuwa na taarifa tofauti kuhusu Korona nchini Tanzania.

Leo, nimeona nirudi kwenu, nizungumze nanyi tena na kuwaasa, kwamba, kwa namna tunavyoiona Serikali hii na namna inavyolichukulia suala la Korona, hatuoni kama inazingatia Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoitaka Serikali kusimamia na kulinda ustawi wa wananchi. Hivyo, nitaacha maswali ya kufikirisha ili kila mmoja ayatumie kutafakari kesho ya Taifa letu, hatma ya familia zetu na ustawi wa nchi yetu.

DHANA YA HERD IMMUNITY

Ndugu Wananchi,

Katika sayansi ya utabibu hususan kuhusu kinga, zipo nadharia kadhaa, mojawapo ni ile ijulikanayo kama Herd Immunity. Hii ni nadharia kuwa ukiachia wananchi wote wapate maambukizi watajenga kinga mwilini na hivyo kuzuia tena virusi kusababisha ugonjwa.

Katika nadharia hii watu kadhaa watakufa na wengine wengi watapona. Kwa kimombo hii inaitwa Survival of the fittest, kwa maana watakaokuwa na kinga zaidi (vijana na watoto) watapona na wenye kinga dhaifu (watu wazima na wanaoishi na magonjwa kama vile kisukari, pumu nk) watafariki.

Maana yake ni kwamba, tunawatoa kafara wapendwa wetu, atakayekufa afe watakaobaki wabaki!. Katika hali ya kawaida hii sio nadharia ya Kiafrika na wala haina nafasi katika imani za dini mbalimbali tunazoziamini kwa mapokeo.

Kwa namna tunavyoona hatua zinazochukuliwa, na msisitizo mkubwa unaowekwa katika kudhibiti takwimu za maambukizi, vifo na athari za ugonjwa wa Korona, tunashawishika kuamini kwamba, pengine Serikali imechukua mkondo huo wa Herd Immunity.

Kama hivyo ndivyo, maana yake tutegemee asilimia 3 ya watanzania wote watafariki dunia kutokana na ugonjwa huu. Hii ni sawa na idadi ya wananchi wote waliokufa kwenye mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Hapa Tanzania idadi ya watu watakaokufa kwa kufuata nadharia hii ni sawa na idadi ya watu wote wa Mkoa wa Njombe. Sisi ACT Wazalendo hatukubali kamwe kupiga bomu kuua watu milioni moja (1,000,000) wa Mkoa wa Njombe.

MZAHA KATIKA SAYANSI

Ndugu Wananchi,

Serikali kupitia Mheshimiwa Rais, iliutangazia Umma kuwa vipimo vya kupima Korona katika Maabara yetu ya Taifa ni vibovu kwa kuwa vimepima Mapapai, Mbuzi, Kondoo, mafuta ya vilainishi ya magari nk.

Siku moja baada ya uasi huo kwa sayansi na maabara yetu ya Taifa, Waziri wa Afya alimsimamisha kazi Mkuu wa Maabara ya Taifa na kuunda Kamati ya Uchunguzi wa vipimo vya Korona. Licha ya kuwa tangazo la ubovu wa vifaa ilikuwa wazi, lakini mpaka leo Kamati ile haijaweka wazi Taarifa ya Uchunguzi wake. Kutokana na hatua hiyo Serikali (ya Jamhuri ya Muungano) haijatangaza taarifa za wagonjwa wa Korona tangu tarehe 29 Aprili, 2020.

Aidha, Maabara ya Taifa haijafanya vipimo vya COVID 19 tangu tarehe 4 Mei 2020.

Mbali na kwamba habari hiyo ya vipimo vya korona kuwa na kasoro haikuwa habari mpya, kwani kote duniani kasoro zimebainika; habari hiyo iliyopewa kipaumbele na Mheshimiwa Raisi imeidogosha nafasi ya sayansi katika jamii yetu, na matokeo yake wananchi sasa wanaamini kuwa “matokeo yote ya vipimo vya Korona si sahihi isipokuwa majibu yakiwa ni NEGATIVE”. Tunadhani hii ni hatari sana katika ujenzi wa Taifa la kisasa, ni kurudi katika enzi za Ujima na dunia ilipokuwa na maarifa machache!

Mheshimiwa Rais ambaye kitaaluma ni Mkemia, japo aliwahi kushiriki kikombe cha babu, haamini tena kwenye sayansi. Ameamua tujiendee tu kama gari bovu,hata wasaidizi wake wanaunga mkono mwelekeo wake wa “kuachana kabisa na utaratibu wa kupima”, uhimizaji mkubwa sasa umejikita kwenye kuondoa tahadhari zote zilizowekwa awali, kiasi tumeruhusu wageni watakaokuja nchini kutokukaa tena karantini ya siku 14. Ni hatari sana.

KORONA NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Ndugu Watanzania,

Kama nilivyokwishaeleza hapo awali, janga la Korona ni janga la dunia nzima, ni janga ambalo linahitaji nguvu ya pamoja katika kukabiliana nalo. Hauwezi kujifungia mwenyewe ukadhani utaweza kulimaliza peke yako. Bahati mbaya sana serikali hii, na Rais wa serikali hii, wanaishi katika ndoto hiyo! (ya kutokujali kuhusu Korona kwa imani kuwa tumepona kwa maombi tu). Katikati ya mapambano haya, pamoja na kutokuwa na mshikamano ndani ya nchi, Serikali pia imeamua kuvurugana na majirani zetu karibia wote kwenye Kanda zetu kubwa mbili, SADC na EAC. Tumeshindwa kushiriki vikao vya mipango ya pamoja ya kupambana na ugonjwa huu na wenzetu. Hali hii sio nzuri hasa ukizingatia nafasi ya Tanzania katika masuala ya Umajumui wa Afrika.

Kama hiyo haitoshi, Serikali ya Tanzania ambayo kwasasa ndiye Mwenyekiti wa SADC inaonekana dhahiri kukwepa jukumu lake na kufikia hatua ya kushindwa kuitisha mikutano ya kikanda ili kujadili suala hili linaloathiri uchumi wa nchi zote duniani. Mathalan, baada ya kuona Tanzania inasitasita, serikali ya Afrika ya Kusini iliamua kuchukua jukumu la kiuongozi, kuitisha kikao kwa ajili ya kujadili suala la korona na uchumi. Tanzania haikushiriki licha ya kwamba mkutano ulikuwa kwa njia ya mtandao.

Hali ni hiyo hiyo, hata katika Jumuiya ya EAC. Tunaalikwa na wenzetu ili tuweke msimamo wa pamoja, sisi tunakimbia. Hili ni jambo Mwalimu Nyerere,muanzilishi na aliyeweka misingi ya diplomasia ya Tanzania kupitia andiko lake maarufu la “Argue don’t shout” (yaani jenga hoja, usipige kelele) asingeweza kuamini lingetokea na lingekuwa na baraka za mkuu wa nchi, serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Serikali yetu imekuwa ni ya kupiga kelele badala ya kujenga hoja, kila jambo lawama ni kwa wanaoitwa mabeberu, kana kwamba ipo siku mabeberu wataisha!.

Wakati majirani zetu kama Zambia, Rwanda, Kenya na Uganda walichukua hatua za mwanzo kuzuia maambukizi kwenye nchi zao, Tanzania kupitia serikali ya Rais Magufuli tuliamua kutojali. Majirani zetu walipoamua kupima watu mipakani iligundulika kuwa Watanzania wengi ambao ni madereva wa magari ya masafa marefu wana virusi. Hii imesababisha mgogoro mkubwa ambao umesababisha baadhi ya nchi jirani kufunga mipaka yao kwa muda kwa kuogopa kuwa tutawaambukiza, na hata nchi zilizofungua mipaka kwa sasa, madereva wetu wanapitia wakati mgumu sana.

Jambo kubwa la kidiplomasia lililofanyika wakati wa kipindi hiki, ni kuwasha ndege ya Rais, kujaza mafuta, kulipa watu posho na kwenda Madagaska kutafuta kikombe cha kimataifa, ambacho kimeletwa kwa ajili ya uchunguzi!, hakika Balozi Mahiga (Mungu amalaze pema), amefariki dunia na maarifa yake!.


TUMEWADANGANYA WATANZANIA, NA SASA TUNAIDANGANYA DUNIA

Ndugu Wananchi,

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeomba msaada wa Mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani(IMF) wa jumla ya Dola za Marekani milioni 273 (sawa na Shilingi Bilioni 600) ili kukabiliana na athari za kiuchumi zitokanazo na janga la Korona, mikopo ya namna hiyo tayari imeshatolewa kwa nchi nyengine za Afrika Mahsariki za Kenya, Uganda, Rwanda pamoja na Sudan Kusini ambazo zimetimiza masharti ya jumla ya mikopo hiyo.

Tanzania mpaka sasa haijapata fedha hizo, kwa sababu mbili; Mosi, Serikali yetu imetoa taarifa zisizo za kweli kuhusu Bajeti ambayo wametumia katika kushughulikia janga hili la Korona kwa IMF, ikitaja kiwango kikubwa cha fedha ambacho imetumia kwenye sekta ya afya kwaajili ya janga la Korona wakati inajulikana kuwa kwenye bunge la Bajeti linaloendelea Dodoma, hakuna mahali popote serikali ilipotenga fedha kwaajili ya Korona. Uongo huo wa serikali kwa IMF ndio umesababisha kuchelewa kwa mkopo huu.

Pili, Serikali ya Tanzania imeandikiwa barua na Benki ya Dunia kujieleza kwanini imechukua mikopo mbalimbali ya kibiashara na kuficha taarifa za mikopo hiyo, kinyume na kanuni za Benki ya Dunia (IDA NCBP). Tanzania, chini ya Rais Magufuli, ilichukua mikopo ya kibiashara yenye gharama kubwa ya riba kutoka kwenye mabenki ya biashara ya Standard Chartered (USD 1.5 Bilioni), Eastern and Southern African Trade and Development Bank (USD 1 Bilioni) na Credit Suisse (USD 200 milioni).

Mikopo hii yote yenye thamani ya shilingi Trilioni Sita ilifichwa hapa nchini, hatukuijua, Serikali hii iliamua kudanganya ili kuonyesha kuwa deni letu la Taifa ni himilivu, nyie wananchi wa Tanzania mnaolipa deni hilo mlidanganywa, hamkuambiwa kuhusu mkopo huu, na hata sasa Serikali imekiri jambo hilo la mkopo huko kwawanaoitwa Mabeberu na sio kwenu nyie wananchi.

Kutokana na Serikali kutaka nafuu ya madeni kutokana na Covid 19 imebidi ieleze ukweli kwa Benki ya Dunia. ACT Wazalendo tuna barua kutoka serikali yetu kwenda Benki ya Dunia kukiri kutofuata kanuni za kuweka wazi mikopo hii ya kibiashara na hivyo kuomba isamehewe na sasa mikopo hiyo itambuliwe.

Mambo yote haya, yanawaonyesha nyie wananchi kuwaSerikali yetu sio tu inawadanganya nyinyi wananchi kuhusu Korona na athari zake kwenye uchumi wetu, bali pia inaidanganya dunia pamoja na washirika wa maendeleo, na hivyo kuhatarisha mapambano dhidi ya Korona pamoja na uchumi wetu. Ndio maana mpaka sasa Tanzania hatujapata nafuu ya kutolipa madeni kama ambavyo nchi nyengine zimepewa, kwa sababu tunaidanganya dunia, na hatuaminiwi na wenzetu pamoja na kutushangaa juu ya namna tunavyopambana na ugonjwa huu.

UCHUMI AU UHAI?

Ndugu Wananchi,

Tuna bahati mbaya sana kwamba Serikali ya Rais Magufuli kutokana na será mbaya za kiuchumi, imeangusha uchumi wa nchi yetu, hivyo baadhi ya mikakati ya kupambana na Korona inaweza ikaua kabisa uchumi na kuliangusha zaidi Taifa. Hivyo, wakati mwingine tunamuelewa pale anapoamua kuwa kama Mbuni kuficha kichwa chake chini ya ardhi wakati kiwiliwili chote kiko nje!. Ni kwa sababu uchumi uko ICU, zile tambo za makusanyo makubwa, akiba ya fedha za kigeni, uchumi kukua, zilikuwa ni ulaghai, kama ulaghai tunaoushuhudia kwenye mapambano ya Korona.

Kutokana na hali mbaya sana ya kiuchumi, Serikali imeamua kuwa uchumi na miradi ya serikali ni muhimu kuliko uhai wa wananchi!, ndio maana hakuna bajeti ndogo ya afya ya kupambana na Korona, hata hatua kiasi za sera za kibenki zilizotangazwa na Benki Kuu (BOT), ambazo tulishauri tangu awali, zimefanywa kwa lengo tu la kuombea mkopo IMF, ndio maana hakuna hatua za kikodi mpaka sasa za kupambana na Korona. Na Serikali yetu inaamini kuwa ikificha takwimu za watu wenye virusi pamoja na vifo vinavyotokana na korona basi itakuwa inalinda uchumi na miradi yake, jambo ambalo si sahihi. Hizi ni fikra ambazo hazina msingi wala ushahidi.

Ushahidi wa taarifa za serikali unaonyesha kuwa tayari uchumi wetu umeshaathiriwa na Korona na hivyo uwezo wa Serikali kutekeleza miradi yake ya Maendeleo utaathiriwa pia. Kwa mfano, mwezi Machi 2020 Serikali imeshindwa kukusanya Mapato ya Kodi ya VAT (Kodi inayotokana na Manunuzi ya Bidhaa – consumption taxes) kwa 50%.

Yaani wakati serikali ilipaswa kukusanya Shilingi Bilioni 460 kutoka kodi hii mwezi Machi, ilikusanya Shilingi Bilioni 224 tu. Kodi hizi ni kodi za matumizi - ‘consumption taxes’, ni kiashiria kikubwa kama Uchumi unakwenda vizuri au unachechemea, kwa sababu ni kipimo cha uwezo wa wananchi kutumia bidhaa na huduma sokoni. Mapato ya Serikali katika eneo hili, kwa mujibu wa Taarifa ya Mapitio ya Uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT), yamekuwa yanashuka kwa kasi kuanzia mwezi Februari mpaka mwezi Aprili mwaka huu.

Vile vile Watu 500,000 wamepoteza kazi kwenye sekta ya Utalii peke yake kwa muda wa miezi mitatu tu ya Januari mpaka Machi 2020, Tanzania imeshapoteza Shilingi Bilioni 800 katika fedha za kigeni ($340M). Sekta ya Utalii inayozalisha Ajira 1.5M nchini itaumizwa zaidi kwa mwaka mzima na kuathiri ukuaji wa Pato la Taifa na Mapato ya Fedha za Kigeni.

Katika hali kama hii Rais anaposema kuwa hatua za kuwalinda dhidi ya korona zitaathiri miradi yake ya Reli na Umeme, atatoa wapi fedha za kuendesha miradi hiyo wakati hakutakuwa na mapato ya kodi? Hatua ambazo Rais anachukua sio tu zitasababisha nguvu kazi ya taifa kupotea bali pia kusababisha kuchukua muda mrefu zaidi kurekebisha uchumi wetu huko mbele kwani tutapoteza wataalamu ambao taifa limewasomesha kwa muda mrefu na wenye uzoefu mkubwa katika kazi.

Watanzania hampaswi kukubali njia hii ambayo Serikali inatupeleka kwani ni hatari sana kwa nchi yetu na watu wake.

NINI CHA KUFANYA?

Ndugu Wananchi,

Mmesikia jitihada tulizokwishafanya kama Chama, mmekuwa mkituona tukihamasisha wananchi kuchukua hatua za kujiinda, lakini tunapokuwa na serikali kaidi, ambayo tayari imeshaamua kwamba tuendelee kuishi na korona kama tunavyoishi na UKIMWI, bila kuwa na jitihada za dhati; serikali ambayo haiamini kabisa kwenye sayansi, na imeamua kufunga maabara ya kupimia korona kama ndio njia ya kupambana na ugonjwa huu; Serikali ambayo kwao, suala la korona ni jambo linaloshughulikiwa na vyombo vya ulinzi na usalama badala ya wataalam wa afya; sisi kama viongozi mbadala tunabaki na maswali mengi bila majibu.

Baadhi ya maswali yetu ni,
(i) Je baada ya ukweli wote tuliouanika hapo juu,wananchi hamuoni kuwa CCM imeshajinyima imani yenu ya kuendelea kuwaongoza Watanzania?​
(ii) Wananchi hawaoni kuwa mkondo unaochukuliwa na serikali katika vita dhidi ya corona utasababisha kuiangamiza nchi yetu?​
(iii) Wananchi hamuoni kuwa nchi yetu kuchukua hatua za maksudi za kuitenga Tanzania na majirani zetu na dunia kwa jumla kutasababisha madhara makubwa kwetu na kwa vizazi vyetu?​

Sisi kama ACT –Wazalendo, tunadhani, maswali haya yabaki wazi kwa kila mwananchi kuyatafakari na kuchukua hatua, kwani Serikali yetu imeamua kutuacha yatima, na kwa kuwa yatima hadeki, basi ndugu zangu, tusijidekeze, tujiongoze maana hatuna uongozi.

HITIMISHO

“Ndugu Wananchi, ninajua kuwa Tanzania tutakuwa wa mwisho katika dunia kuondoa korona katika jamii yetu lakini wale ambao Mwenyezi Mungu atawajaalia kuwa hai lazima wawajibishe watawala wa sasa kama watakuwa hai kutokana na namna walishindwa kutumia mamlaka yao kulinda uhai wenu wananchi. Hivyo ninawasihi sana kuweka rekodi za wapendwa wetu ambao vifo vyao vimesababishwa na shida ya kupumua ili rekodi hizi zitumike katika kuwatendea haki wapendwa wetu

Wakati tunaendelea na tafakuri kuhusu maswali nilioainisha na katika kipindi hiki ambacho tunajiandaa na sherehe ya sikukuu ya Eid El Fitri; tunaendelea kuwasihi mzingatie M3 ambazo ni Miguu, Mikono na Mdomo; Miguu; kukaa umbali wa Mita 1-2 kati ya mtu na mtu na kuepuka misongamano, Mikono; kunawa mikono na sabuni kwa maji tiririka na Mdomo; kuepuka kugusa Mdomo, Pua na Macho na kuvaa Barakoa. Tunawasihi mchukue hatua moja kubwa zaidi, ya kuwalinda wale wenzetu walio katika hatari ya kupoteza maisha, hasa wazee, wagonjwa wa maradhi ya kisukari, pumu, presha, kansa nk. Ni muhimu sana kwa kila mtu ajilinde mwenyewe, wenye mamlaka wamechagua njia rahisi kwao na yenye maumivu kwetu wananchi.

Asanteni sana,
Eid Mubbarak!.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Alhamis, 21 Mei 2020
Dar es salaam

 
Ni kweli, na ndio maana hata kufunga anga walifunga wakiwa wamechelewa tena baada ya mashirika ya ndege karibu yote kusitisha safari.

Na hata Polepole alisema wazi kuwa hawawezi kuzuia ndege kwa sababu watalii watakosekana hivyo hawa watu uchumi kwao ndio kipaumbele na tushukuru tu hili gonjwa kwa Africa halijawa na madhara kama huko Ulaya na Marekani vinginevyo hali ingekuwa mbaya sana.

Hakuna aliekuwa na uhakika kuwa huu ugonjwa ukiingia nchini hali ingekuwaje hivyo mtu makini anapaswa kuchukua tahadhari kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu na sio ku-take chances kama walivyofanya huku kwetu(tahadhari zilichukuliwa ila kuna maeneo hazikuchuliwa kama kuzuia ibada,n.k).

Kwa kifupi,baadhi yao wanaongoza vita dhidi ya huu ugonjwa kama vile wanacheza mchezo wa pata potea na ndio maana hata kauli zao zinachanganya wananchi(baadhi wanawaambia watu wachukue tahadhari na hapo hapo wakionekana kupongeza/kusifu watu wasiochukua tahadhari kwa kuvaa barakoa!)

Museveni na Kagame japo huwa siwakubali,lakini katika hili kupambana na corona,wameonyesha uongozi kwa kujali raia wao na kutojali uchumi wala kuingiza siasa na hawakutaka ku-take chances kwani hakuna aliekuwa na uhakiki nini kingetokea iwapo hali ingekuwa kama tulivyokuwa tunaona huku Ulaya(Italy,France,n.k).

Mtu makini anapambana na corona kulingana na hali halisi huku muda ukiamua mapambano yaweje lakini sio kwa ku-take chances wakati ugonjwa unaua alafu unafanya mambo kwa kubahatisha.
 
"Serikali ya Magufuli kutumia mtindo wa 'Herd Immunity' kudhibiti Corona, ina maana 3% ya Watanzania wote (sawa na idadi ya watu wa mkoa wa Njombe) WATAKUFA. ACT wazalendo hatutaruhusu Watanzania wenzetu wafe kwa makusudi ya Serikali." Zitto Kabwe

IMG_20200521_122253.jpg
 
Corona haijaisha na haitaisha. Lakini nakuhakikishia hatutafika huko, virus tutamzoea na tutaishi naye kama Mende tu.

Eti watu idadi ya Njombe watakufa, yaani wafe watu laki saba (700,000+) Tanzania mara tatu ya fatalities ya dunia nzima hadi sasa.

Tuwe wakweli, that won't and will never happen.
Kwani Corona imeisha? He was maana yake umesha sio?


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Corona haijaisha na haitaisha. Lakini nakuhakikishia hatutafika huko, virus tutamzoea na tutaishi naye kama Mende tu.

Eti watu idadi ya Njombe watakufa, yaani wafe watu laki saba (700,000+) Tanzania mara tatu ya fatalities ya dunia nzima hadi sasa...
Huu ugonjwa utaua watanzania wengi na mbaya zaidi itakuwa mwendo wa kimya kimya! Nina uhakika aliyezembea wakwanza ambaye mnamuabudu atakufa kwa huu ugonjwa
 
Kwa hiyo? Mwanamke wa Tanzania anategemewa kupata watoto 5.2 hivyo 3% wakifa siyo ishu kitakwimu ukiachilia uchungu wa waliopoteza watu, tunarekebisha hiyo idadi fasta, wewe mwenyewe Zito Kabwe nina uhakika una watoto nje ya ndoa, ...
 
Huu ugonjwa utaua watanzania wengi na mbaya zaidi itakuwa mwendo wa kimya kimya! Nina uhakika aliyezembea wakwanza ambaye mnamuabudu atakufa kwa huu ugonjwa
Unamaisha mazuri ila umeruhusu vishambulizi vya Afya yako vikutie kashikashi, Hata hivyo hujachelewa kujisaidia, ondoa mapenzi makubwa yaliyopitiliza kwenye vitu vya kipumbavu, hii itakusaidia kuondoa presha nyemelezi ambayo ni hatari kuliko Corona,,. Zingatia hili mkuu..
 
Back
Top Bottom