Kesi ya mjane wa bilionea Msuya: Kampuni ya CMC Motors ilivyomtetea mjane wa Bilionea Msuya

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
428
996
[Kampuni ya uuzaji magari ya CMC Automobiles Limited imeieleza Mahakama kuwa gari aina ya Ford Rangers yenye namba za usajili T307 CBH, inayohusishwa katika kesi ya mauaji ya Aneth Elisaria Msuya iko kwenye gereji yake tangu Mei 9, 2016.

Maelezo hayo yametolewa na Meneja Utawala na Matengenezo wa kampuni hiyo, Ernest Msuya (65), wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo, inayowakabiri Miriam Steven Mrita, mjane wa Erasto Msuya maarufu kama, Bilionea Msuya; na mwenzake Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray.

Miriam na Muyella wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji, wakidaiwa kumuua, Aneth ambaye alikuwa wifi yake Miriam.

Aneth aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam.

Alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, ambaye alikuwa mfanyabiashara wa madini mkoani Arusha, na aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.

Kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Miriam na mwenzake walikwenda Kigamboni kwa marehemu Aneth mara ya kwanza Mei 15, 206, wakiwa na gari aina ya Ford Rangers (T307 CBH) kwa ajili ya kufanya mipango ya mauaji hayo.

Ushahidi huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na shahidi wa 22, Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Arusha, Mrakibu Mwandaimizi wa Polisi (SSP) David Mhanaya kutokana na maelezo ya aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa marehwmu Aneth, Getruda Peniel Mfuru.

Getruda ambaye ni shahidi wa 25 na wa mwisho wa upande wa mashtaka pia alirudia maelezo hayo katika ushahidi wake, akidai kuwa washtakiwa walikwenda huko na akaonana nao mara tatu kwa siku tofauti yaani Mei 15, 18 na 23, 2016 wakiwa na magari tofauti likiwemo gari hilo.

Hata hivyo shahidi wa pili upande wa utetezi, Karim Mruma aliyejitambulisha kuwa ni dereva wa Miriam na familia yake, aliieleza mahakama kuwa yeye ndiye amekuwa akimuendesha Miriam na kwamba mwezi Mei wote Miriam hakutoka nje ya Arusha.

Pia alidai kuwa gari hiyo iliyotajwa washtakiwa kwenda nayo kwa Marehemu Aneth Mei 15, 2016, iko katika gereji ya CMC tangu Mei 9, 2016 alipoipeleka kwa matengenezo na kwamba tangu tarehe hiyo mpaka sasa iko katika gereji hiyo ya CMC Arusha.

Msuya, ambaye ni shahidi wa nne upande wa utetezi katika ushahidi wake jana aliunga mkono maelezo hayo ya Mruma kuwa gari hiyo iko katika gereji yao tangu Mei 9, 2016 mpaka sasa.

Katika ushahidi wake akiongozwa na wakili wa mjane huyo wa Bilionea Msuya; Peter Kibatala, shahidi Msuya alilieleza Mahakama kuwa analitambua gari hilo kwa kuwa liliuzwa na kampuni yao kwa mteja wao Arusha na kwamba limekuwa likipelekwa katika gereji yao mara kwa mara kwa matengenezo.

Mbali na maelezo yake ya mdomo pia aliwasilisha vielelezo viwili kikiwemo kitambulisho chake cha kazi kuthibitisha kuwa ni mwajiriwa wa kampuni hiyo na wadhifa wake.

Pia aliwasilisha mahakamani fomu ya usajili wa gari hilo kuonesha kuwa limekuwa likipelekwa katika gereji hiyo mara kwa mara kwa matengenezo, ikionesha tarehe mbalimbali za kupokelewa na kutoka, na tarehe hiyo ya mwisho ya kupokelewa hapo mpaka sasa.

Katika ushahidi wake, Msuya kwanza alianza kuielezea kampuni hiyo na namna inavyofanya shughuli zake, ili kujenga msingi wa ushahidi wake.

Alisema kuwa kampuni hiyo, makao makuu yake yako Kisutu Dar es Salaam na kwamba inajishughulisha na uuzaji magari mapya na kuyatengeneza yakiwa na matatizo mbambali na kwamba inawahudumia watu binafsi pamoja na Serikali na taasisi zake.

Alieleza kuwa aliajirwa katika kampuni hiyo kuanzia nafasi ya chini ya ufundi tangu mwaka 1984, na kupanda madaraja mpaka kufikia wadhifa alio nao sasa na kwamba kwa sasa ana uzoefu wa kutosha wa miaka zaidi ya 41.

Alieleza kuwa kampuni hiyo ina matawi yake Arusha, Dodoma Mbeya Tanga, na kwamba ofisi hizo zinafanya kazi kwa kuratibiwa na makao kwa kuwa kila kinachofanywa kwenye matawi hayo kinajulikana makao makuu kupitia mfumo wa mtandao wa kompyuta.

Shahidi huyo alielezea kuwa gari likipelekwa katika ofisi zao kwa matengemezo hupokewa na wataalamu ambao husajiliwa katika fomu maalumu ya kuonesha kumbukumbu za kupokelewa na kuorodheshwa katika kadi maalum (job card) inayoelezea tatizo lake na tarehe iliyopokewa, dereva aliyelipeleka na namba zake za simu.

Job card ni nyaraka maalumu kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za kupokela gari la mteja na ni mali ya CMC, lakini mteja pia anapewa ya kwake na zote zinakuwa halisi.

"Kazi ya register ni kupokea gari na kurekodi muda na tarehe gari lilipoingia na umbali ambao limetembea (kilometa) wakati linaingia na zile inazokuwa nazo wakati linatoka, lengo likiwa ni kuwa na kumbukumbu za kuhakikisha usalama wa gari la mteja", alisema Msuya na kuongeza;

Hivyo alisema kuwa ni suala ambalo halipo la gari kuingia na au kutoka bila kuwekwa kumbukumbu alisisitiza kuwa haliwezekani kabisa kwa CMC.

"CMC ni kampuni kubwa ambayo imeingia hapa nchini tangu mwaka 1954 wakati ilikuwa inaitwa Coopermotors Corporation ikiuza magari aina ya Land Rover tu na kwamba biashara yake kubwa ni kuuza magari hayo mapya ya kilometa 0 ambayo inaendelea nayo," alisema na kuongeza:

"Sasa hivi tunauza magari aina tatu, Ford, Land Rover na Renault. Wateja wetu ni watu binafsi na Serikali pia."

Kuhusu gari aina ya Ford Ranger T307CBH, inaohusishwa katika kesi hiyo alisema kuwa hiyo gari anaifahamu, kwa kuwa kampuni yao iliiuza gari hiyo kwa mteja mwaka 2012, huko Arusha na kwamba toka waiuze wao ndio wanaifanyia matengezo mara kwa mara kila inapotokea hitilafu.

Baada ya kuwasilisha mahakamani fomu ya usajili wa gari hilo (Revista) iliyopokewa kama kielelezo cha upande wa utetezi, shahidi huyo alianza kuisomea mahakama tarehe mbalimbali zinazoonesha jinsi gari hilo lilivyokuwa likiingia katika gereji hiyo kwa matengenezo na kutoka mpaka tarehe hiyo ya mwisho.

"Gari hii liliingia CMC tarehe 9, mwezi wa 5 na ilitoka tarehe 10 Agosti, 2016, lakini likarudi tena tarehe hiyohiyo," alisema Msuya.

Alieleza kuwa wakati linatoka Agosti 10, 2016 ilikuwa na kilomita 30, 569 (ilizokuwa imetembea) na kwamba wakati inarudi tarehe hiyohiyo ulirudi ikiwa na kilomita 30573, zikiwa zimeongezeka kilomita nne na kwamba haijatoka tena mpaka leo.

Akifafanua kuhusu gari hiyo kutoka Agosti 10, 2016, takribani miezi mitatu baada ya mauaji ya Aneth, shahidi huyo alisema:

"Walikuja Polisi wa upelelezi Arusha wakataka kuichukua hiyo gari tukawaambia hii gari halina uwezo wa kutembea mahali parefu. Hali hiyo ya kushindwa kutembea umbali mrefu ilianza tangu ilipoletwa Mei 9, 2016", alidai na kuongeza;

"Wao Polisi walilazimisha tukawaruhusu wakalichukua hawakufika mbali wakalirudisha kwa sababu ni bovu wakatoa maagizo kwamba litengenezwe lipelekwe.

Alipoulizwa na Wakili Kibatala kama gari hilo liliweza kuwa nje ya gereji hiyo ya CMC, Mei 15, 18, 20, 23, 25 na 26, 2016, tarehe zinazotajwa na upande wa mashtaka kuwa ni miongoni mwa magari waliyoyatumia washtakiwa kufanya mipango na kutekeleza mauaji alijibu:

"Gari hilo lilikuwa Arusha. Kwa rekodi hizi na ugonjwa wa gari lenyewe haiwezi kutoka (kuwa nje ya CMC) kwa tarehe hizo."

Alihitimisha ushahidi wake kwa kuieleza mahakama kuwa gari hilo likipelekwa katika gereji hiyo kwa mara ya mwisho likiwa na tatizo la injini kugonga na kwamba likipelekwa na dereva Mruma ambaye mara zote ndiye amekuwa alilipeleka kwa matengenezo.

Kesi hiyo imehirishwa mpaka Jumatatu Novemba 6, itakapoendelea kwa ajili ya upande wa mashtaka kumhoji maswali ya dodoso shahidi huyo, kuhusiana na ushahidi wake na maswali ya kusawazisha kutoka kwa Wakili Kibatala.

Credit: MWANANCHI
 
Back
Top Bottom