Kauli ya Damu ni nzito kuliko Maji ni Uongo

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,892
Anaandika, Robert Heriel
Mtibeli.

Misemo na kauli za kilaghai imekuwa ikitumiwa kujenga jamii ya kinafiki katika jamii na Ulimwengu huu. Moja wapo ya misemo au kauli za Uongo au kilaghai ni pamoja na kauli isemayo, Damu ni nzito kuliko Maji.

Hiyo dhana au kauli hiyo haina ukweli wowote. Isipokuwa ni Imani ya kizamani yenye Uongo ambayo Kwa wakati huo labda iliundwa Kwa nia nzuri, kuleta umoja wa kindugu.

Sina tatizo na Nia nzuri, Ila ninatatizo na mchakato wa kuifikia Nia hiyo, mchakato ukishakuwa wakilaghai au kiuongo Uongo madhara yake ni makubwa kuliko Nia nzuri iliyotarajiwa.

Wazee wa zamani walitumia nguvu kubwa isivyohalali katika kulazimisha Kupata mambo mazuri, Mema.

Kwa mfano, wazee wa zamani walitumia misemo na hadithi za Uongo kutishia Watoto au Vijana wao ili tuu wapate kutiiwa, kuheshimiwa. Wakati wangeweza Kutumia njia njema kuifikia Nia njema ambayo ni kuipata heshima yao.

Wazee wa zamani walitumia nguvu kupiga Wake zao ili kuheshimiwa, Kupata heshima Jambo ambalo ilikuwa ni ukatili na hiyo heshima hawakuipata isipokuwa kudharauliwa.

Wazee wa zamani waliwalazimisha Watoto wao kuolewa au kuoa pasipo kuangalia uchaguzi wa Watoto wao. Na kama ungekaidi basi wangekutishia kupatwa na mabalaa, Jambo ambalo lilikuwa ni Uongo na hata sasa ni Uongo.

Hiyo ni mifano michache Kati ya mingi inayothibitisha kuwa Misemo na nguvu za kilaghai na Uongo zilivyotumiwa na Wazee wetu. Suala la kusema Damu ni nzito kuliko Maji ni Jambo la Uongo wa kizamani ambao hauna ukweli wowote.

Mahusiano ya damu, undugu au hata kuwa mapacha haina nguvu yoyote kama ilivyoripotiwa. Nguvu ya mahusiano ya Watu hujengwa na ukaribu na Matendo baina ya Watu hao kuliko Damu.

Kadiri mnavyokaribiana na kuhusiaña mara Kwa mara au Kwa ukaribu ndivyo nguvu yenu inavyozidi kuongezeka. Mtu anaweza kuwa ni ndugu yako, damu yako lakini kusiwe na nguvu yoyote baina yenu inayowaunganisha.

Kusema Damu inanguvu ni kauli ya kisiasa tuu kujenga Imani au itikadi itakayowaunganisha Watu.

Ni Sawa useme utaifa ATI unanguvu kisa mnatoka taifa moja. Huo ni Uongo Mkubwa. Utaifa utakuwa na nguvu ikiwa ndani ya taifa kuna mahusiano mazuri baina ya wananchi.

Watu wanapendana, wanaheshimiana, hakuna kudharauliana, kila mmoja anapata riziki yake kulingana na Majaliwa yake pasipo kudhulumiwa, kama Makosa yatatokea basi sheria yeyote ataadhibiwa bila kujali nafasi yake na hakuna upendeleo. Nchi ya hivyo lazima iwe na nguvu, umoja na ushirikiano.

Utaifa, au undugu, au ukabila sio chochote ikiwa hakuna mahusiano mazuri baina ya watu. Ni kauli za kilaghai zilizokaa kiujanja ujanja.

Damu sio chochote katika mahusiano baina ya watu. Ni ishu ya kiimani na kimtazamo. Damu ni sehemu tuu ya mwili Kwa kiumbe yeyote ili aweze kuishi lakini haina nguvu katika masuala ya mahusiano ya MTU na MTU mwingine. Chenye nguvu kwenye mahusiano ni Mtazamo, upendo, na Imani, full stop.

Kama damu ingekuwa na nguvu kama inavyoelezwa basi familia nyingi zingeishi Kwa Upendo.
Kama kweli damu ingekuwa na nguvu basi mataifa yanayoundwa na jamii zenye uhusiano wa kidamu zingeishi Kwa Upendo.

Kama kweli damu ingekuwa na nguvu basi Dunia nzima tungeishi Kwa kupendana wala kusingekuwa na vita, dhulma, Ufisadi, Ukoloni, n.k. Kwa sababu inadaiwa wanadamu wote wametoka Kwa Baba na Mama mmoja. Yaani Sisi damu yetu imetoka sehemu moja. Yaani Sisi ni ndugu.

Kauli ya kusema Damu inanguvu ni kauli ya janjajanja, kilaghai isiyo na mashiko. Hujawahi sikia mtu akimuua Ndugu yake, hujawahi? Hujawahi kusikia Baba akimuua Mtoto wake wa kumzaa au kinyume chake? Labda kwenu hujawahi kuona hayo.

Hapo kwenu au kwenye familia yenu, Ndugu zako au wewe unapendana na Ndugu zako? Vipi hujawahi kuona Ndugu wakizipigania Mali za Ndugu Yao aloyefariki na kudhulumu Watoto wa Marehemu?

Huko hujawahi kusikia, Majambazi yamevamia na kuua alafu nyuma ya hao Majambazi kuna mkono wa Ndugu WA karibu wa waliovamiwa? Labda hizo hujawahi kusikia.

Hujawahi kusikia Kaka akilala na MKE wa mdogo wake au kinyume chake? Hujawahi nakuuliza?
Hujawahi kusikia Ndugu akimbaka au kumlawiti mtoto wa dadaake au mjombaake? Hujawahi?
Hiyo damu ni nzito Kwa namna ipi?

"Labda Taikon Akili yako haijatulia, lakini ukikaa ukifikiria damu ni nzito kuliko Maji"

Wewe ndio Akili yako haijatulia. Ni mara ngapi umesikia Ndugu yako anamatatizo mazito lakini umemlia buyu licha ya kuwa na uwezo wa kumsaidia kifedha? Au ni mara ngapi wewe imekuwa na shida ambayo ulijaribu kuomba msaada Kwa Ndugu zako ambao unauhakika wangekusaidia lakini walikulia Buyu? Huo uzito wa damu uko katika nini?

Je, ni kufanana Kwa Sura na maumbile? Au je ni kufanana kijenetiki?

Kama damu ni nzito kuliko Maji unafikiri ni Kwa nini Watu wanaogopa Kufa wakiwa na watoto Wadogo? Unajua ni kwanini wanahisi Watoto wao watapata shida siku wao wakiondoka Duniani? Kama kweli damu ni nzito.

Majibu yapo wazi wala huhitaji kuwa Polopesa ama profesa kujibu swali Hilo. Hakuna uzito wowote kwenye Damu.

Namna ya kujenga uzito kwenye Maisha yako;

1. Ipende Familia yako, Mkeo/Mumeo na watoto.
Acha ubinafsi. Penda Mkeo au Mumeo kama unavyojipenda wewe. Kama ni familia "pendaneni haswa" kisha upendo huo utahamia Kwa Watoto wenu. Watoto hawafundishwi kupenda Bali wana-adapt upendo wanaouona Kwa wazazi wao.

Sio mzazi unasema "ninyi ni ndugu, mpendane wanangu" wewe chizi nini! Kama Baba na Mama mmeshindwa kupendana Watoto watawezaje? Watu hawapendani Kwa sababu wamezaliwa pamoja, Bali wanapendana Kwa sababu wameukuta na kukulia kwenye mazingira yenye Upendo.

Acheni kuishi Maisha ya kuviziana, Maisha ya kitapeli Tapeli, Maisha ya mguu ndani mguu nje kila mmoja akijitega kuwa siku mkiachana mzani usilalie upande wake. Hapo mnafanya Watoto NAO wawe vivyohivyo.

2. Tenda Haki Kwa familia yako.
Kila mmoja ndani ya familia awe Chini ya sheria. Ingawaje Baba ndiye kichwa cha nyumba lakini hiyo haitamaanisha kuwa yeye yupo juu ya sheria.

Mgawanyo wa majukumu uwe Kwa upendo na Haki kulingana na Akili, mwili na hisia za mwanafamilia.
Mume upewe majukumu kulingana na ulivyo, na MKE apewe majukumu kulingana na alivyo, lakini hiyo haitamaanisha kuwa hamtaweza kusaidiana. Kupeana au kugawana majukumu ni kwaajili ya kufanya mambo yaende Kwa upesi.

Mfano, wote mpo nyumbani, wikiendi kuna kazi za nyumbani labda kupika, Usafi, kufua n.k Kuliko Mkeo afanye kazi zote ambapo ni lazima atachelewa tuu basi unaweza kumsaidia, Wakati yeye anasafisha nyumba wewe unaweza ukawa unafua, Wakati yeye anapika wewe unaosha vyombo. Lengo ni kazi ziishe upesi mpate muda wa kupumzika na pia mmoja asielemewe.

Au jukumu la mwanaume labda ni kutafuta Pesa za kulisha familia, kusomesha Watoto, Pesa za ujenzi na kununua Mashine kama magari n.k. Mshahara au kipato kinaweza kisiwe kikubwa kutosheleza hayo yote.

Hivyo MKE hata kama jukumu lake kuu ni malezi lakini anaweza kumsaidia mumewe majukumu ili kufikia malengo Kwa uharaka.

Mfano, MKE anaweza kumsaidia mumewe kusomesha Watoto ili Pesa nyingine zitumike kwenye ujenzi, lakini pia MKE anaweza kusaidia kulisha familia Wakati Mume anatafuta Pesa ya usafiri WA nyumbani (kununua Gari).

Haki ni kuhakikisha kila mmoja analinda furaha na maslahi ya mwingine. Jambo hilo Watoto wataiga, huo ushirikiano na umoja ndio utakaoleta nguvu ya hao Ndugu Wawili au hiyo familia. Kinyume na hapo hakuna kitakachowezekana.

3. Imani na kuheshimu Familia yako
Mume lazima uwe na Imani na umheshimu Mkeo. Halikadhalika MKE naye lazima awe na Imani na heshima Kwa Mumewe. Heshima ubora na udhaifu wa mwenzako. Udhaifu wa Mkeo au Mumeo unazibwa na ubora wako.

Nazungumzia udhaifu wa kimaumbile na silika (Tabia aliyozaliwa nayo mtu mathalani hasira, usahaulifu) na sio uovu au uhalifu.

Mwenzako labda anaupeo mdogo lakini wewe unaupeo mkubwa, mheshimu Kwa Upeo wake mdogo ambao wewe utauziba Kwa Upeo wako mkubwa.

Mwenzako anahasira, ziba pengo lake Kwa upole au busara zako. Ikitokea ishu ambayo unajua kabisa mwenzako Kwa jinsi hasira zake zilivyo ataharibu, basi mwambie utasimamie ishu hiyo wewe.

Ukimheshimu Mkeo au Mumeo hata Watoto wataheshimiana bila kujali utofauti wao wa kimaumbile, kimapato, kielimu n.k

Sasa Mume kisa unakijimshahara cha milioni tano kutwa kichwa kutoa maneno ya kejeli, dhihaka, na unyanyasaji Kwa Mkeo. Hiyo sio Tabia nzuri na itajibu tuu Kwa Watoto. Au Mwanamke kisa unauwezo wa Pesa au fikra kuliko Mumeo unamletea maneno ya kashfa, unafikiri Watoto wenu watafanya tofauti na wanayoyaona kwenu?

Usije ukadhani damu imewaunganisha, thubutu! Hakuna kitu kama hicho.

Mimi acha nipumzike, mwenye kuelewa aelewe. Mwenye kutukana atukane, mwenye kukaa kimya akae kimya, lakini ujumbe ndio huo.

Robert Heriel,
Taikon wa Fasihi,
Kwa sasa Dar es Salaam.
 
Akili mtu wangu, akili tu

Haki huimarisha familia

Haki huinua taifa

Haki

Hii tabia inajiakisi kwenye ile eti mpigieni kura msanii wetu kwenye tuzo za kimataifa. Bila hata kujua wapinzani wake wameimba nn basi tu kapige kura kisa tuna 'udugu' wa utaifa

Au mpigie kura classmate kisa tu tunasoma nae. Ujinga tu.

Na hata udugu ni hivyohivyo, tunakuwa close kama tuko close sio kwa sababu tu tumezaliwa hapo. Au tumefunga ndoa gdmnt
 
Back
Top Bottom