Msanii
Platinum Member
- Jul 4, 2007
- 22,606
- 29,754
- Rais ambaye ndiye mlinzi namba moja wa KATIBA ya nchi anasema ni KIJITABU.... na hakuna uwajibikaji wowote kwenye hilo (Ibara ya 26.-(1) Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii nasheria za Jamhuri ya Muungano.)
- Bunge letu linapokea na kupitisha kwa mbwembwe miswada yote ambayo ina viashiria vyote vya kugawa maliasili zetu kwa wageni bila kuzingatia umiliki wa umma wa maliasili hizo. Nazungumzia Loliondo na maeneo mengine ambayo yanagawiwa kwa kivuli cha uwindaji na uwekezaji (Ibara ya 27.-(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuriya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yotei nayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu maliya mtu mwingine. (2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali yamamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifuna ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.)
- Tumeshuhudia sakata la MoU kati ya Tanzania na Dubai kugenisha bandari zote za bara huku Bunge likipitisha kwa mbwembe mkataba huo, huku likiwakejeli wananchi wanaoukosoa na kuulalamikia, hali ilifika baadhi ya wakosoaji walibandikwa kesi ya UHAINI. Katiba imevunjwa kwa kiwango cha kutisha (Ibara ya 28.-(1) Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi nakudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa taifa.)
- Sheria mbalimbali zilizotungwa na Kupitishwa na Bunge ambazo zinakizana na Sehemu ya Tatu ya Katiba ya JMT (Haki na Wajibu Muhimu). Sheria za kuwawekea kinga ya kutoshtakiwa mkuu wa mhimili wa Bunge, Sheria ya Kinga ya kutoshtakiwa kwa Wanausalama, Sheria ya Makosa ya mitandao, Sheria ya Hadhi za Viongozi, Kanuni zitokanazo na MAAGIZO ya watawala kwa viongozi kwenda kwa Jeshi la Polisi, Sheria mpya ya Bima ya Afya kwa wote, Sheria ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa n.k. (Ibara ya 13.-(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki,bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele yasheria. (2) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlakayoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambaloni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake. ).
- Serikali imeshindwa kudhibiti wizi wa mali za umma. tumeshuhudia ripoti ya CAG ikianika uchotwaji mkubwa wa fedha za umma kupitia miradi mbalimbali kwenye ngazi mbalimbali lakini mkuu wa nchi amekuwa akitoa kauli za kuwakemea wahusika bila kuchukua hatua yeyote ya kulinda maadili ya umma.
- Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kutumika kisiasa ambapo ushahidi upo wazi kabisa. Katiba inakataza askari wetu wa vikosi VYOTE kutokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa. Lakini ukweli upo wa askari wengi kumiliki kadi za uanachama wa Chama tawala. Jambo hili linafanyika kwa wazi bila hofu wala utii kwa Katiba (Ibara ya 147 - (3) Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga nachama chohote cha siasa, isipokuwa tu kama atakuwa na hakiya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii.)
Itapendeza sana iwapo Ofisi ya Mwandishi wa Katiba na sheria itawekwa chini ya Katibu wa Bunge ili kutimiza takwa la Kikatiba la Bunge kutunga sheria. Leo tunashuhudia wajibu wa utungaji wa Katiba na sheria vikifanywa na wale ambao sheria inapaswa kuwasimamia na kuwawajibisha kwenye utendaji wao wa kila siku serikalini.
Mpaka sasa tuna Taasisi tatu pekee nchini ambazo Kikatiba hakuna mwenye mamlaka ya kuzihoji
- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
- Baraza la Mawaziri
- Tume ya Uchaguzi ya Taifa
Rais afahamu kwamba, sisi wananchi ndiyo matokeo ya yeye kuwa mkuu wa nchi, pia akumbuke kwamba yeye ni zao la jamii hiyo hiyo anayoiita kwamba haina uelewa wa Katiba na inafaa kuelimishwa. Sisi wananchi wengi tunapata mashaka sana endapo rubani wetu ana ufahamu stahiki wa Katiba ya nchi. Kauli zake zinatupa mashaka kwenye hilo
Wapo Watanzania wenzetu ambao wameamua kuweka akili na fikra zao kapuni kwa kuamini na KUTULAZIMISHA kuamini kwamba Haki na Wajibu Muhimu ni fadhila ya mkuu wa nchi kwa wananchi sisi. Lakini tunaamini sasa kuwa hazina kubwa ya thinktank wa nchi wameelemewa na upumbavu na kufilisika kwa fikra, mtazamo na hoja.
Ninaamini kwamba siyo kila mmoja anapaswa kuwa kiongozi ili kuleta mabadiliko bali Watawala wa nchi hii wamefanya eneo la uongozi kuwa DUKA LA FURSA kwa kila anayewania/ kupata nafasi hiyo.
Ni muhimu sana kuelewa kwamba; Ukimya na utulivu wa nchi yetu umejengwa kwenye UTU, UZALENDO, UPENDO na MSHIKAMANO ambavyo ni sehemu ya tunu za taifa letu hususani kwenye kujenga Taifa moja imara lenye malengo chanya. Tumeanza kupoteana kwa sababu walioshika madaraka wamejipa umungu wa nchi hii kwa kutumia vikosi halali vya Serikali kujimilikisha nchi na maamuzi yake yote. Bado nafasi ya kujisahihisha ipo na tukaanza upya. Muda utafika ambapo hizi hoja zetu zitageuka mjukuu wa majuto kwani supu ikishawekwa tui si supu tena
NB
Tuweke viwango vya utungaji wa Katiba ya Nchi yetu ambapo Mtanzania yeyote atakaye shiriki kwenye Bunge la Katiba anakubaliana na sharti la kutoshiriki uchaguzi wowote ngazi ya Ubunge ama kuteuliwa nafasi yeyote kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa kwa muda wa miaka 15 au 20. Hii itatupatia waadilifu na wenye nia safi ya kutuletea Katiba inayokidhi viwango vya Taifa letu. Hivyo hata sasa Serikali inaweza kuandaa utaratibu wa kupata Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba bila kuathiri taratibu za Bunge la JMT linaloelekea ukingoni.
Msanii