nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,862
- 5,797
25 NOVEMBER 2011
*Wamshangaa kauingilia mambo yao, kupotosha umma
*Wamtaka awataje wabunge wachanga wasiojua sheria
*Mnyika amshukia Makinda, asema alipuuza wabunge
Na Benjamin Masese
SIKU moja baada ya Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilila, kudai mazungumzo kati ya Rais Jakaya Kikwete na Kamati teule ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hayatabadili maamuzi yaliyopitishwa na Bunge, chama hicho kimeibuka na kusema kuwa, kiongozi huyo hana msaada wowote kwa bunge bali anaeneza sumu, chuki na kuchonganisha makundi ndani ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam, ambaye pia ni Katibu wa wabunge CHADEMA, Bw. John Mnyika, alisema wameshangazwa na kitendo cha ofisi ya bunge kuwa mstari wa mbele kupotosha umma juu ya muswada wa mabadiliko ya katiba mpya 2011.Alisema juzi Dkt. Kashilila alitoa taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa, baadhi ya wabunge wa Bunge la Muungano ni wachanga na hawajui sheria ambazo walipaswa kuzitumia kujenga hoja.
"CHADEMA inamtaka Dkt. Kashilila awataje wabunge hawa kwa majina na kueleza kwa nini alishindwa kuwashauri mapema ili waweze kutimiza lengo la muswada huo kutosomwa bungeni kwa mara ya pili," alisema.
Alisema kitendo cha kusema majadiliano kati ya Rais Kikwete na kamati teule ya chama hicho hayawezi kubadili maamuzi ya bunge ni kutaka kupotosha Watanzania na dhamira ya Kamati Kuu ya CHADEMA kutaka muafaka kwa njia ya majadiliano.
"Hili suala ni bichi, upo uwezekano wa kutolewa maamuzi makubwa yasiyotarajiwa, Dkt. Kashilila anapaswa kusoma ibara ya 62(1) na 62(3) ya katiba ya Tanzania.
Alisema Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda aliwapuuza wabunge waliojitokeza kuonesha jitihada za kupinga muswada huo usisomwe kwa mara ya pili lakini si kweli kwamba wabunge hawajui sheria.
Bw. Mnyika alisema alikusudia kutumia kanuni ya 86(3)(a) kupinga muswada usisomwe kwa mara ya pili lakini alipuuzwa hata alipotumia kanuni ya 55 (3)(b) ili kutoa hoja ya kuahirisha mjadala.
"Huyu Dkt. Kashilila ndiye hajui sheria, alishindwa kulisaidia Bunge na kumshauri Spika wake, umma uliona yaliyokuwa yakitendeka, hata kanuni ya 86 (3) (b) ilipotumika, wabunge walisimama ili kuunga mkono hoja lakini haikusikilizwa.
"Kimsingi suala la kupitisha muswada huu lilikuwa limepangwa, nawaomba wananchi mpuuze kauli za Dkt. Kashilila, jambo la msingi tupiganie haki yetu ya kushirikishwa katika mchakato wa kupata katiba ambayo itatuongoza miaka 50 ijayo," alisema.
Aliongeza kuwa kama Dkt. Kashilila atashindwa kuwataja wabunge wasiofahamu sheria na kueleza sababu za kushindwa kumshauri spika, watakutana na kutafakari hatua za kuchukua.