Karibu Kwenye Programu Iitwayo Mbeya Real Estate Workshop Namba 01

Aliko Musa

Senior Member
Aug 25, 2018
156
240
Tutakayojifunza:

(A) Sehemu Ya Kwanza; Kuhusu Taarifa Tatu (3).

✓ Lengo kuu la programu.

✓ Shabaha/Fokasi ya programu ya leo.

✓ Chanzo cha taaarifa.

✓ Ufafanuzi wa Fokasi ya programu.

✓ Sababu za uwepo wa fursa kwa kila taarifa.

(B) Sehemu Ya Pili: Kuhusu Fokasi Ya Programu

✓ Maana ya vibanda vya biashara.

✓ Makadirio ya mtaji fedha.

✓ Makadirio ya kodi ghafi ya mwezi.

✓ Gharama za uendeshaji/usimamizi.

✓ Faida na changamoto za mabanda ya biashara.

✓ Dondoo muhimu kuhusu vibanda.

SEHEMU YA KWANZA: KUHUSU TAARIFA TATU.

(a) Lengo kuu la programu ya Real Estate Workshop.

Ni kujifunza kwa undani zaidi kuhusu soko mahalia (local real estate market) la mwanachama anayeleta taarifa. Nimeanzisha programu hii kwa sababu haiwezekani kujenga mafanikio kwa muendelezo kupitia ardhi na majengo endapo mwekezaji na timu yake hawafahamu hali ya soko.

Matokeo chanya ya programu hii yanategemea sana ushirikiano wa sisi wanachama. Tunatakiwa kujadili kwa uwazi. Tunatakiwa kubadilishana maarifa na taarifa kuhusu somo husika.

(b) Shabaha/Fokasi Ya Programu Ya Leo.

Ni kujifunza kwa undani zaidi kuhusu MABANDA YA BIASHARA. Kupitia taarifa hizi tutachambua mambo ya msingi kuhusu faida na changamoto za umiliki wa mabanda ya kukodisha kwa wafanyabishara wadogo na wa kati.

(c) Chanzo cha taaarifa.

Ni mimi rafiki yenu, Aliko Musa kutoka Mbeya, Tanzania.

Taarifa tatu (3) za Mbeya Real Estate Workshop ni:

✓ Fursa ndani ya soko la kabwe (Soko la SIDO).

✓ Fursa ndani ya stendi mpya ya magari ya Tunduma, Ileje na Chunya.

✓ Eneo la mlango wa chuo kikuu cha Mzumbe tawi la Mbeya.

Kwenye taarifa zote hizi tatu, tutalenga UMILIKI WA MABANDA YA BIASHARA kwa ajili ya kukodisha kwa wafanyabishara wadogo na wa kati

(d) Ufafanuzi wa mabanda ya biashara.

Mabanda ya biashara (vioski, kontena, vibanda) ni nyumba za kuhamishika. Nyumba hizi za kuhamishika zinaweza kutengenezwa kwa kutumia:

✓ Mbao

✓ Maturubai au Kapeti imara na nzito.

✓ Mabati.

✓ Vyumba.

✓ Miti au mianzi.

Makontena.

Makontena ya kutoka nje ya nchi yana changamoto nyingi kutoka serikalini. Hivyo, sishauri kuanza na eneo hili endapo bado mtaji wako ni chini ya milioni tano.

Kontena hizi huuzwa kati ya milioni moja hadi milioni tatu. Haya ni makadirio ya bei endapo unanunua kwa mtu au kampuni.

Bei ya kununua kontena mpya inaweza kuwa zaidi ya milioni mbili kutegemea na gharama za usafirishaji na vibali vyake.

Kontena za aina hii hufaa sana kwa biashara za kati kama ifuatavyo:

✓ Biashara ya miamala ya fedha (mobile money transfer).

✓ Duka la vifaa vya ujenzi na malighafi ya ujenzi.

✓ Duka la pembejeo za kilimo.

✓ Duka la dawa na vifaa vya mifugo.

✓ Stoo/bohari kwa ajili ya bidhaa mbalimbali.

✓ Biashara ya nyingine yoyote ya biashara isipokuwa zile zenye usimamizi mkali kutoka mamlaka husika mfano duka la dawa za binadamu.

Banda la mbao.

Hili linahitaji ukarabati wa mara kwa mara. Litahitaji ukarabati wa mara kwa mara hasa kama unahamisha mara kwa mara. Banda hili la mbao linahitaji uhamisho si zaidi ya mara moja kwa mwaka mmoja.

Kwa uhamisho wa mara moja kwa mwaka mmoja, banda la mbao litaweza kulipa endapo lilikuwa na wapangaji kwa miezi 10 au zaidi kwa mwaka husika.

Lakini pia zipo mbao ambazo huduma zaidi na zinahitaji ukarabati kwa nadra sana. Endapo unaweza kupata mbao za aina hii kwenye eneo unapowekeza unaweza kujenga banda la mbao.

Endapo utafuata ile kanuni ya 4% ya mabanda ya biashara. Banda la mbao (hata mbao za kawaida) unatakiwa kulikodisha kwa angalau miaka minne (4) tu.

Banda la chuma.

Hili ni banda ambalo hutengenezwa kwa kutumia vyuma kwenye ofisi za kuchomelea vyuma. Haya ni mabanda namba mbili kwa uimara baada ya makontena ya chuma.

Haya ni mabanda yanayolipa zaidi ukilinganisha na makontena na mabanda ya mbao. Sababu za kulipa sana kwa mabanda ya chuma ni kama ifuatavyo:

✓ Huhitaji kiasi kidogo cha mtaji fedha ukilinganisha na makontena.

✓ Hudumu zaidi ukilinganisha na mabanda ya mbao.

✓ Huhamishika kwa urahisi zaidi ukilinganisha na mabanda ya mbao na makontena.

✓ Mabanda ya chuma ni rahisi kuyabadilisha kulingana na mahitaji ya wapangaji au mpangaji tarajiwa.

Mabanda ya chuma ndiyo chaguo namba moja kwa mwekezaji anayetaka kutengeneza kiasi kikubwa cha kipato endelevu ndani ya miaka mitano (5) tu.

Kwa mwaka wa kwanza, huwa ninashauri mwekezaji kumiliki si zaidi ya mabanda 6 ya chuma. Hii ni kwa sababu zifuatazo:

✓ Kujifunza kwa undani zaidi kuhusu soko mahalia (hapa unajifunza kwa vitendo).

✓ Kujifunza na kutambua hatari za biashara ya kukodisha mabanda ya chuma hatua kwa hatua.

✓ Kujifunza changamoto za biashara ya kukodisha mabanda ya chuma.

✓ Kutafuta njia za kukabiliana na changamoto za biashara ya kukodisha mabanda ya chuma.

Hivyo, utatakiwa kumiliki (kununua/kutengeneza) banda moja la chuma ndani ya siku sitini (60). Kwa mwaka utakuwa na mabanda 6 (sawa na siku 360).

(e) Sababu Za Uwepo Wa Fursa Ya Mabanda Ya Biashara.

Soko kabwe (SIDO).

Hili ni eneo la kibiashara maarufu sana hapa Jijini Mbeya. Ni eneo ambalo mgeni yeyote kutoka nje ya jiji la Mbeya ni lazima ajisikie vizuri kutembelea eneo hili.

Ni eneo ambalo wafanyabishara wadogo na wa kati kutoka mikoa tofauti tofauti huja kununua bidhaa kwa bei ya jumla. Mikoa ambayo wafanyabishara wake huja hapa ni:

✓ Mkoa wa Songwe.

✓ Mkoa wa Njombe.

✓ Mkoa wa Songea.

✓ Mkoa wa Katavi.

✓ Wilaya wa Sumbawanga (Rukwa).

Wafanyabishara na wafanyakazi kutoka wilaya zote za mkoa wa Mbeya hutegemea soko hili kwenye bidhaa nyingi sana. Ni eneo ambalo limejaa msongamano wa watu wengi sana kuliko masoko yote hapa jijini Mbeya (Kwa sasa, pengine kuliko masoko yote ya Nyanda za juu kusini).

Asubuhi sana (kuanzia saa 11 kasoro) wafanyabishara wa mitumba hufungua biashara zao. Muda wa jioni tena (kuanzia saa 11 kasoro) wafanyabishara wadogo wa mitumba humwaga bidhaa zao eneo hilo hilo la soko la kabwe.

Hivyo kulifanya eneo la soko la kabwe liwe na msongamano mkubwa sana wa watu.

Daladala kutoka maeneo yote ya karibu na Mbeya mjini haziwezi kupita bila kusimama eneo hili. Na ni eneo ambalo abiria wengi wa daladala hupanda daladala. Na abiria wengi wa daladala hushukia eneo hili.

Mabanda ya biashara ya chuma na mabanda ya aluminium eneo la kabwe yanakodishwa kati ya 50,000 hadi 300,000.

Hapa ni eneo la kisasa sana, haiwezekani uweke banda la mbao au makontena marefu kwa sababu ya uwepo wa nafasi ndogo ya kuegesha mabanda au makontena.

Mabanda yanayofaa kwa eneo la kabwe ni kama ifuatavyo:

✓ Mabanda ya plastiki ya kampuni za mitandao kama yale Airtel.

✓ Mabanda ya aluminium.

✓ Mabanda ya chuma.

Haya unaweza kupambana kutafuta eneo la kuegesha pale soko la kabwe. Kisha ukaanza kutengeneza kipato kizuri sana kulingana na fedha uliyowekeza.

Wapangaji wako wa eneo la kabwe watakuwa ni;

✓ Wafanyabishara wadogo wa urembo.

✓ Wafanyabishara wa miamala ya kifedha.

✓ Na biashara nyingine zinazochukua nafasi ndogo.

Nani Anaweza Kukupa Taarifa Za Kupata Eneo La Kuegesha Soko La Kabwe?.

Moja.

Madalali wa nyumba za kupangisha.

Mbili.

Madalali walioshikilia fremu au maeneo kuzunguka soko la kabwe.

Tatu.

Wafanyabishara wa fremu za soko la Kabwe.

Stendi Mpya Ya Airport Ya Zamani.

Hii ni stendi mpya ya magari ya kwenda Wilayani Ileje, Mkoani Songwe na maeneo yote ya wilaya ya Chunya.

Ujenzi wa awali wa stendi hii umekamilika mwezi wa nane (8) mwaka huu. Eneo hili hufaa kwa mabanda ya kukodisha kwa wafanyabishara kwa sababu:

✓ Ni njia kuu ya kuingilia soko kuu la Mwanjelwa (kutoka Duka la Vunjabei). Soko la pili kwa kuwa nguvu baada ya Kabwe hapa Jijini Mbeya.

✓ Ni karibu sana sana na hospitali ya kisasa ya Maranatha.

✓ Ni stendi ya abiria kutoka wilaya ya Chunya ambayo ni moja ya wilaya nzuri sana kwa biashara hapa Jijini Mbeya.

✓ Ufunguzi wa tawi la Chuo Kikuu Cha Iringa (The University Of Iringa) karibu kabisa na eneo la stendi hii mpya.

✓ Ni karibu sana na masoko ya maziwa na miwa kwa wafanyabishara wote hapa Mbeya.

Mlango Wa Kuingilia Chuo Kikuu Cha Mzumbe.

Hili ni eneo la kuingilia chuo kikuu cha Mzumbe. Ni moja ya maeneo ambayo yana msongamano mkubwa wa magari na watu. Wewe pita na gari kuanzia saa 12 jioni eneo hili, uwezekano wa kusubiri foleni ni mkubwa sana.

Eneo hili lina sifa mbili tu. Nazo ni:

✓ Msongamano wa watu wengi muda wa mchana.

✓ Msongamano wa watu wengi zaidi muda jioni mpaka saa nne usiku.

Eneo hili ni fursa kubwa kwa kuegesha mabanda ya biashara kwa sababu hizi:

✓ Uwepo wa Chuo Kikuu Huria (The Open University Tanzania) karibu sana na Chuo Kikuu cha Mzumbe.

✓ Uwepo wa hosteli mlangoni mwa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania (The Open University Tanzania).

✓ Uwepo wa Greenhill College karibu na Chuo Kikuu Huria Tanzania.

✓ Uwepo wa Chuo Cha Biashara Cha Moshi karibu na Chuo Kikuu Huria na Greenhill College.

✓ Uwepo wa Chuo Cha Gresi (Grace College) karibu na mlango wa nyuma wa nyuma wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.

✓ Uwepo wa Jengo Benki Kuu Ya Tanzania Kanda Ya Nyanda Za Juu Kusini.

✓ Mbele kidogo ni Jengo la la Mahakama kuu ya kanda.

✓ Uwepo wa jengo la TAKUKURU nyuma ya jengo la BENKI KUU (BIOT).

Hizi ni sababu ambazo zimenifanya nivutiwe sana sana na eneo hilo. Hakika ni eneo ambalo unaweza kuegesha mabanda ya biashara na kuendelea kuvuna kipato endelevu.

Uzuri ni kwamba upande mmoja ni majengo ya miradi na upande wa pili ni makazi ya watu. Hivyo, kuifanya sehemu moja ni kitovu cha biashara kuzunguka miradi hii mikubwa ya serikali na binafsi.

SEHEMU YA PILI; KUHUSU FOKASI YA PROGRAMU.

(a) Maana ya vibanda vya biashara.

Hizi ni nyumba za kuhamishika ambazo hutumika kwa ajili ya biashara za huduma au biashara za bidhaa. Mabanda yanaweza kutumika kwa ajili ya:

✓ Makazi pekee.

✓ Makazi na biashara.

✓ Biashara pekee.

Kwa hapa kwetu Tanzania, mabanda haya ni kawaida kutumika kwa ajili ya biashara pekee. Kwenye shughuli za utalii na kijeshi, mabanda haya yameonekana yakitumika kwa ajili ya makazi.

Kwa lengo kuu letu la kutengeneza fedha, mabanda ya biashara ya kukodisha itakuwa ni chaguo kwa sasa. Lakini ikiwa umepewa tenda kwenye vituo vya utalii unaweza kufikiria mabanda kwa ajili ya makazi.

Mabanda ya mbao, makontena na mabanda ya chuma hufaa zaidi kwenye eneo hilo la stendi mpya ya Airport zamani.

Mabanda ya aluminium na mabanda ya makampuni ya mitandao ya simu kama Airtel ni uwekezaji usio lazima. Ni uwekezaji usio lazima kwa sababu sio mahitaji ya soko husika.

(b) Makisio Ya Mtaji Fedha.

Mabanda ya biashara huhitaji mtaji wa kuanzia 250,000 na kuendelea. Hivyo ikiwa una kiasi hiki cha fedha, unaweza kunishirikisha mimi tusaidiane kwenye uchaguzi wa kibanda, uchaguzi wa eneo la kuegesha na jinsi ya kupanga kiasi cha kodi.

Kwa Eneo la Kabwe na Mlango wa chuo kikuu cha Mzumbe unatakiwa kuwa na angalau Laki nne (400,000). Kwa sababu ya uhitaji wa mazingira ya maeneo tajwa.

(c) Makisio Ya Kodi Ghafi Ya Mwezi.

Unatakiwa kukusanya kodi halisi (net monthly rent) ya 4% ya gharama zote za umiliki wa kibanda chako. Mfano umetengeneza au umenunua kibanda kwa laki tano (500,000).

Unatakiwa kuchukua 4% unazidisha na 500,000 na kupata Tshs.20,000 (elfu ishirini tu). Hii ni kanuni rahisi sana kuifanyia kazi. Sitamuelewa yeyote ninamsimamia kwenye aina hii ya uwekezaji akishindwa kuendena na spidi ya kanuni hii.

Hiyo laki tano (500,000) inayojumuisha gharama zifuatazo:

✓ Gharama za kutengeneza kibanda au kutengeneza kibanda.

✓ Gharama za usafiri wa kibanda.

✓ Gharama za kumlipa mwenye eneo au kiwanja (Kodi ya maegesho).

✓ Gharama za usimamizi wa kibanda chako ikiwemo ukarabati na usafiri wako binafsi.

(d) Gharama Za Usimamizi/Uendeshaji.

Gharama za uendeshaji wa mabanda ya biashara kwa ajili ya kukodisha zinaweza kujumuisha:

✓ Kodi ya maegesho.

✓ Gharama za udalali.

✓ Nauli ya msimamizi kutoka eneo anapoishi mpaka eneo la kuegesha kibanda.

✓ Kuingiza umeme au sola paneli kulingana na mahitaji ya wapangaji tarajiwa.

✓ Gharama za kuchora maandishi ya matangazo au kununua stika za matangazo ya biashara itakayokuwa inafanyika.

✓ Gharama za kutengeneza kibao cha " KINAPANGISHWA".

✓ Gharama za kusafirisha kibanda.

✓ Gharama za kujenga mtandao wa maofisa serikali za mitaa.

(e) Dondoo Tano (5) Za Mabanda Ya Biashara.

Moja.

Orodha Ya Biashara Zinazoweza Kufanyika Kwenye Mabanda Ya Chuma, Mbao Na Makontena.

Biashara zinazoweza kufanyika kwenye nyumba za kuhamishika ni kama ifuatavyo;-

✓ Biashara ya kutoa huduma mbalimbali kama vile uwakala wa bima, uwakala wa viwanja na nyumba, ushauri wa kitaalamu, na kadhalika.

✓ Biashara ya chakula maarufu kama migahawa.

✓ Biashara za kuuza bidhaa za urembo, duka la vifaa na malighafi za ujenzi, duka la bidhaa muhimu za nyumbani, duka la vifaa na dawa za mifugo na kilimo, fremu ya kushonea nguo na viatu, fremu ya kuingiza nyimbo na kukodisha CD, DVD, na kadhalika.

✓ Biashara ya kuhamisha fedha kama vile M-pesa, Tigopesa, Airtel money, halopesa na TTCL pesa.

✓ Biashara ya vifaa vya shuleni na maofisini maarufu kama stationary.

✓ Biashara ya kuuza bidhaa za teknolojia na mawasiliano kama vile mifuniko ya simu, mabetri ya simu, chaja za simu na kadhalika.

✓ Biashara ya vinywaji baridi na vya moto.

Mbili.

Falsafa Ya Kujenga Utajiri (Wealth-building Platiform).

Falsafa hii imejengwa kwenye kipato endelevu. Kipato endelevu ndiyo falsafa pekee ya kujenga utajiri kupitia uwekezaji kwenye ardhi na majengo. Falsafa nyingine ya kutengeneza fedha, tafadhali rejea darasa namba 7 lilofanyika kwenye makundi yote ya whatsapp TZ REAL ESTATE TEAM (TRT).

Mabanda ya biashara ni eneo linalofaa sana kwa wawekezaji ambao hawana mtaji wa kumiliki mali zisizohamishika (ardhi na majengo).

Mabanda ya biashara yanaweza kukutengenezea mkondo mzuri sana wa kipato endelevu.

Tatu.

Asilimia 4 (4%) Ya Kipato Cha Mabanda Ya Biashara.

Mabanda ya biashara yanatakiwa kuingiza 4% ya jumla ya gharama zote za matengenezo (au manunuzi) na gharama za uendeshaji.

Hii 4% ni kipato endelevu ambacho ni kipato halisi. Ni kipato ambacho kinabaki baada ya kutoa fedha yote ya matumizi.

Kufanikiwa kwa biashara ya wapangaji wako ndiyo kufanikiwa kwako wewe. Kwa sababu mpangaji ataendelea kukulipa kodi kwa kila mwezi.

Nne.

Maeneo Mazuri Kwa Ajil Ya Kuegesha Mabanda Ya Biashara Ya Kukodisha.

(i) Mtaa wa stendi ya mabasi ya wilaya (stendi ya mabasi ya mikoani).

Ni muhimu sana kutafuta kona ambayo biashara ya wapangaji wako itaendelea kustawi. Labda mpangaji ashindwe kukuza biashara yake kwa sababu zake mwenyewe.

(ii) Kituo kikubwa cha mauzo na manunuzi ya bidhaa (shopping centers).

Pia, unatakiwa kutafuta kona ya mtaa ambayo wapangaji wako wanaweza kufanya biashara na wakapata wateja wa biashara zao.

(iii) Mtaa wa chuo na chuo cha ufundi.

Hapa unatakiwa kutafuta kona ambayo wanavyuo wengi wanaweza kufika kwa urahisi zaidi kufuata mahitaji yao.

(iv) Mtaa wa chuo kikuu.

Kama unaishi karibu na chuo kikuu, hongera sana. Pia, unaweza kusogea kufuata fursa ya kuegesha mabanda ya biashara karibu na chuo kikuu.

Hapa wengi wa wapangaji wako watakuwa ni wanachuo wenyewe. Wanachuo watahitaji fremu kwa ajili ya biashara kama kuongeza kipato cha pembeni.

(v) Mtaa wa kiwanda.

Hiki inatakiwa kiwe ni kiwanda ambacho kinakuwa na waajiriwa wengi kiasi kwamba biashara zinakuwa na wateja sehemu hiyo.

(vi) Mtaa wa kiwanja cha mpira wa vilabu vya ligi ya NBC (NBC Premier League).

Kama kuna uwanja ambao upo mjini na unakutanisha timu za ligi kuu ya Tanzania inayodhaminiwa na NBC unaweza kuangalia uwezekano wa kuwekeza banda au kontena kwenye mtaa huo na kuipangisha.

(vii) Soko kuu la wilaya yako.

Karibu na maeneo ya kuzunguka soko la wilaya kunaweza kufanyika biashara tofauti tofauti. Kwenye mitaa hii, mara nyingi fremu za biashara zinakuwa zimejaa na kodi haipungui tshs.100,000.

Kitu ambacho ukiweka banda au kontena lako ukapangisha kwa tshs.20,000 hadi tshs.50,000/= inatosha kukuingizia kipato endelevu.

(viii) Soko kuu la mkoa wako.

Kama jiji ilivyo Mbeya, kuna kunakuwa na masoko zaidi ya mawili ambayo yana wateja wengi.

Kwa majiji ya Dodoma ambayo yana soko moja tu, utalazimika kukaribia eneo la kuzunguka soko husika.

Ukipata eneo zuri unaweka nyumba yako ya kuhamishika na kuanza kupangisha.

(f) Faida Na Changamoto Za Mabanda Ya Biashara.

Utangulizi

Mabanda ya biashara hayahitaji uwe na kipande cha ardhi ili upate umiliki wake.

Mabanda ya biashara ndiyo aina ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo ambao hukidhi mahitaji ya wapangaji wa asilimia kubwa.

Mpangaji anaweza kuitumia nyumba ya aina kwa biashara aipendayo na mahali popote atakapochagua.

Nyumba za aina hii huhitaji kiasi kidogo cha mtaji fedha ukilinganisha na nyumba zisizohamishika.

Nyumba za kuhamishika ndiyo nyumba pekee ambazo hutofautiana na nyumba zingine katika vitu vifuatavyo;-

Moja, zinahitaji kiasi kidogo sana cha fedha kwa ajili ya ukarabati.

Pili, huhitaji kiasi kidogo cha mtaji fedha ukilinganisha nyumba zisizohamishika.

Tatu, kodi ya pango la majengo toka serikalini. Mara nyingi, hakuna tozo ya kodi ya pango la majengo.

Faida Za Kutengeneza Pesa Kupitia Kupangisha Nyumba Za Kuhamishika

Moja, kiasi kidogo cha mtaji fedha. Unaweza kuwekeza katika nyumba za aina hii ata kama una kiasi kidogo cha mtaji fedha.

Pili, ni rahisi kumiliki. Hii ni tofauti na umiliki wa nyumba zisizohamishika.

Nyumba zisizohamishika huhitaji uwe na umiliki wa kipande cha ardhi.

Lakini pia unaweza kuingia ubia na mwenye ardhi ukajenga nyumba katika ardhi ya mbia wako kwa kufuata sheria za Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania.

Tatu, huhamishika kwa urahisi sana. Unaweza kuhamisha wakati wowote pale unapopata wapangaji wenye mahitaji tofauti na wapangaji wa mwanzo.

Pia unaweza kuhamisha muda wowote kufuatana na mahitaji ya wapangaji kwa wakati huo.

Nne, hazina changamoto ya eneo lisilofaa kwa shughuli fulani. Nyumba za kuhamishika zinaweza kuhamishwa na kutumika sehemu yoyote ile.

Hii inaifanya nyumba ya kuhamishika kuondoa changamoto ya eneo lisilo na wateja.

Tano, gharama ndogo za ukarabati katika nyumba za kuhamishika.

Sita, nyumba za kuhamishika ni rafiki wa mazingira. Hii ni kwa sababu matilio yanayotumika kujengea hayaharibika kwa urahisi.

Changamoto Za Mabanda Ya Biashara.

Moja, kipato cha msimu hasa kwa mabanda ya biashara kwa ajili ya biashara ndogondogo.

Pili, wapangaji wako kubadili mawazo ya biashara mara kwa mara.

Hii inaweza kuathiri kipato chako pia, kwa nao watakuwa wanashindwa kutengeneza kipato endelevu kwa kila mwezi.

Tatu, huwezi kupata mikopo kwa urahisi kutoka katika taasisi za kifedha kama vile benki, vyama vya ushirika (credit unions), na mashikrika ya akiba na mikopo (savings and loans associations).

Nne, unaweza kuanzisha huduma kubwa kwa ajili ya mabanda ya biashara.

Nyumba za kuhamishika zinaweza kutumika katika shughuli maalum kama vile burudani na starehe (Recreational Vehicles, RV Homes).

Kumbuka kuwa mbao, mabati, vyuma na makapeti mazito yanatosha kutengeneza (manufacturing) nyumba zinazohamishika.

Rafiki yako,

Aliko Musa.

Mbobezi majengo.

Whatsapp; +255 752 413 711
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom