Kama hata Kuendesha Sensa Imekuwa Mgogoro, Serikali Hii Itaweza lipi...?

Mtoboasiri

JF-Expert Member
Aug 6, 2009
5,101
1,946
Sensa njia panda
• Waislamu wanaoipinga mbaroni, Polisi yaonya tena

na Waandishi wetu


amka2.gif
ZOEZI la kuhesabu watu na makazi (sensa), huenda lisifanyike kwa ufanisi uliotarajiwa kutokana na kukumbwa na dosari lukuki katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Miongoni mwa watu wanaotoa upinzani mkubwa, ni baadhi ya makarani waliopangwa kulisimamia zoezi hilo kudaiwa kupanga njama za kulivuruga kwa madai ya kupunjwa posho zao.
Wakati makundi hayo yakitishia kuvuruga sensa, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu wameonya kuwa, atakayeendesha harakati za kulipinga zoezi hilo, atakumbana na mkono wa sheria.

Dar mambo mazito


Jumuiya na taasisi za Kiislamu Tanzania, limewasisitiza Waislamu nchini kutoshiriki katika zoezi hilo kwasababu limegubikwa na propaganda na matumizi ya mabavu.


Katibu wa Jumuiya hiyo, Ponda Issa Ponda, alisema zoezi hilo halina misingi ya haki na ukweli, hivyo Agosti 29, mwaka huu watafanya maandamano makubwa kupinga matumizi ya nguvu dhidi ya wale wanaolipinga. Ponda aliitaka serikali kuahirisha zoezi hilo ili kuepusha ufisadi mkubwa wa fedha za umma na wajiandaa kulifanya upya kwa kuweka misingi bora itakayozingatia mahitaji ya wananchi.


Wakati jumuiya hiyo ikiwasha moto, makarani zaidi ya 70 wameandamana katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kufuatilia hatima ya malipo yao ya mafunzo ya semina ya zoezi hilo. Licha ya kuandamana, makarani hao walieleza kuwa kuna hati hati ya zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi na lengo kufikiwa kutokana na kuwepo kwa utata wa malipo.


Kampeni ya Sensa ya Watu na Makazi ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Agosti 17, mwaka huu katika viwanja vya Mnazi Mmoja na inatarajia kufanyika usiku wa kuamikia kesho. Wakizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, baadhi ya makarani waliohudhuria mafunzo ya siku saba walisema, wanashangazwa na hatua inayofanywa na Idara ya Taifa ya Takwimu kushindwa kutoa malipo hayo.


Walisema kuwa makarani ni kundi muhimu katika kufanikisha zoezi hilo, hivyo wanaona ajabu idara hiyo kushindwa kuwathamini. Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Judith Adam, alisema kuwa mkanganyiko uliojitokeza unaweza kuleta matokeo mabaya katika zoezi hilo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. “Hapa kuna mambo ya uchakachuaji yamejitokeza maana kuna waliolipwa malipo ya semina kwa siku hizo saba sh 105,000 wakati malipo halali yanatakiwa yawe sh 245,000,” alisema.


Huku akiangua kilio, Judith aliutupia lawama uongozi wa Kata ya Makumbusho na kueleza kuwa baadhi ya kundi lao wameshindwa kulipwa kutokana na majina yao kutoonekana katika orodha ya malipo. Alisema kutokana na utata huo, kuna uwezekano wa kundi lililoondolewa katika malipo hayo kuyahamasisha makundi mengine kupinga zoezi hilo. “Tuwe wazi viongozi wa serikali wasifanye mchezo kwani hawa walioondolea na kunyimwa haki yao wana hasira sana na wanaweza kwenda kushawishi watu wengine wasikubali kuhesabiwa na hilo linaweza kujitokeza,” alisema.


Akizungumzia malalamiko hayo, Msaidizi wa Idara ya Taifa ya Takwimu, Japhet Maiga, alisema anatambua kuwepo kwa matatizo katika baadhi ya maeneo, hivyo kwa sasa wanajipanga kuweza kuyatatua. Alisema kuwa, wanakutana na waratibu na maafisa watendaji wa maeneo yaliyopata matatizo kujua ukweli kutokana na baadhi kuonekana kama ni wavamizi.



Masheikh watano mbaroni


Masheikh watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Tanga, kwa kosa la kukutwa na vipeperushi, na vitabu mbalimbali walivyokuwa wakivigawa kwa wananchi vikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi wasishiriki zoezi la sensa. Waliokamatwa ni Chambo Ramadhani (37) mwalimu wa dini ya Kiislamu na mkazi wa chuda jijini Tanga, Kassim Mbaraka (31), mwalimu wa dini mkazi wa Chuda, jijini Tanga.


Mwingine ni Hamad Mohamed, mwalimu wa dini mkazi wa Mabawa, jijini Tanga, Fadhili Chambo (26) mwalimu wa dini mkazi wa magomeni, jijini Dar es Salaam na Hussein Idd (36), dereva mkazi wa Mabawa, jijini Tanga. Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Tanga, Japhari Mohamed, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 22 saa mbili na nusu usiku katika eneo la Mtimbwani, Wilaya ya Mkinga. Alisema, awali watuhumiwa hao walitumia spika za misikiti ili kutangaza msimamo wao wa kudai haki za Waislamu zinazokiukwa na serikali na baada ya kumaliza kutoa agizo hilo kwa njia ya matangazo walitawanyika maeneo mbalimbali kijijini hapo kwa ajili ya kugawa vitabu na vipeperushi.


Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, alisema uongozi wa mkoa huo umejipanga vizuri katika kuimarisha ulinzi na usalama sehemu zote, hivyo kuwataka wananchi wasiwe na wasiwasi.


Sensa yamng’oa sheikh


Mkoani Mbeya, Sheikh Yassin Bambala wa Wilaya ya Mbarali amevuliwa wadhifa wake kwa kosa la kuwahamasisha waumini wa dini ya Kiislamu kususia sensa. Tamko hilo la kumvua wadhifa huo, limetolewa na Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Mbeya, Sheikh Juma Kila, katika ofisi ya Bakwata iliyopo eneo la Sokomatola, jijini Mbeya mara baada ya kukamilika kwa maamuzi ya Baraza hilo.


Katibu huyo alisema hatua hiyo imetokana na Sheikh Bambala kushiriki na kuhudhuria vikao vya baadhi ya waislamu wanaopinga zoezi la sensa kufanyika kwa kuwataka waislamu wasijitokeze kuhesabiwa. Alisema baraza hilo limebaini kuwa wapo baadhi ya viongozi wenzao ambao walikuwa wakionekana kufanya kampeni za chini chini kuungana na taasisi nyingine kuwataka waislam wasishiriki sensa ya mwaka huu. Alisema, kitendo hicho kinapingana na msimamo wa BAKWATA na kiongozi mkuu wa Waislamu (Mufti), kuhusu kuhakikisha waislamu wanashiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.


Killa alisema, wahusika hawa wamekiuka maagizo ya pamoja ya Waislamu kwani awali mashehe wa ngazi za wilaya na wale wa mikoa nchini, waliitwa na Mufti mjini Dodoma kwenye kikao cha Tume ya dini na kupeana msimamo wa pamoja kuhusiana na zoezi la Sensa na wakakubali kurudi kwenye maeneo kuwahamasisha waislamu wenzao juu ya umuhimu wa Sensa.
Aliongeza kuwa, wamebaini kuwa baadhi ya Masheikh, akiwemo Sheikh Bambala baada ya kurudi kutoka Dodoma, wameanza kufanya kazi tofauti na makubaliano ya pamoja yaliyofikiwa.


Katibu huyo wa BAKWATA mkoa, alisema kufuatia hali hiyo, wameanza kuchukua hatua kali kwa viongozi waliodhihirika na ushahidi kupatikana kuwa wamekuwa wakienda kinyume na maagizo ya Tume ya Dini hiyo.


Mwanza shwari


Wakati mambo yakionekana kutokuwa shwari kwa baadhi ya maeneo, mkoani Mwanza Jumuiya ya Kuendeleza Qur'an na Sunna Tanzania (JUQUSUTA), imeitaka Serikali kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote wakiwemo viongozi wa dini ya Kiislamu, wanaohamasisha kuzuia zoezi la sensa.


Kauli hiyo imetolewa jana jijini Mwanza na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo nchini, Sheikh Hassan Kabete wakati alipokuwa akizungumza kwenye ufungaji wa mkutano wa siku mbili wa kuzungumzia masuala ya Kiislamu, uliofanyika Mwanza Hotel jijini hapa. Alisema, zoezi la sensa halipaswi kukwamishwa na kundi au mtu yeyote, kwani ni jambo jema na linaloiwezesha Serikali kupanga mikakati yake ya kimaendeleo kwa taifa na wananchi wake kwa ujumla, hivyo viongozi au Waislamu wanaochochea kukwamishwa kwa zoezi hilo ni vema wakakamatwa kisha kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo. "Juqusuta tunataka serikali iwakamate Waislamu wanaotaka kuvuruga zoezi hili la sensa. Mwislamu mwenye nia njema hawezi kuzuia jambo jema kama hili. Tunahoji inakuwaje viongozi wanaohamasisha wanaonekana kwenye tv, lakini hawakamatwi na serikali, badala yake wanaokamatwa ni watu wa chini?", alisema Sheikh Kabete na kuongeza: "Hivi ni nani anayeweza kuandaa chakula nyumbani kwake bila kujua idadi ya watu waliopo nyumbani hapo? “Ni nani anayeweza kufanya jambo bila kuwa na takwimu? Mimi nadhani kuzuia sensa ni mambo ya kihuni", alisema mwenyekiti huyo wa Juqusuta nchini, shekh Kabete.


Akifunga mkutano huo, Mlezi wa Jamii ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha St. Augustine SAUT (SAMUCO), Altaf Hiran Mansoor aliwaomba waislamu kote nchini kufuata maadili mema kwa kila jambo wanalolifanya, kwani hiyo ndiyo nguzo na msingi mhimu wa kila muumini wa dini hiyo.


Iringa


Viongozi wa dini mkoani Iringa wametoa rai kwa waumini wao kushiriki kikamilifu zoezi la sensa ya watu na makazi linalotaraji kuanza leo majira ya saa 6 usiku kuamkia siku ya jumapili . Wakizungumza na Tanzania Daima, jana viongozi hao walisema kuwa zoezi hilo la sensa ya watu ili liweze kufanikiwa linahitaji ushiriki mzuri kutoka kwa wananchi wote bila kujali itikadi zao za dini .


Mohamed Rafiki ambaye ni Rais wa Jumuiya ya Waislamu Wahamadiya mkoa wa Iringa alisema jamii inapaswa kutambua kuwa ili serikali iweze kupanga bajeti yake ushiriki wa wananchi wote unahitajika katika zoezi la sensa.
Hata hivyo, alikemea tabia ya baadhi ya watu wanaotishia kukwamisha zoezi hilo kwa kutazama maslahi yao binafsi .


Mwakilishi wa madhehebu ya Kikristo mkoani Iringa, mchungaji Bryceson Mbogo kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, alisema Kanisa lake limekuwa likihamasisha zoezi hilo katika ibada mbali mbali . Mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesema kuwa hadi sasa maandalizi kwa ajili ya zoezi hilo, yamekamilika na kuwataka wananchi wote wakiwemo watu wenye ulemavu kushiriki katika zoezi hilo.



Zawadi ya nyamapori kutolewa


Uongozi wa wilaya mpya ya Mkalama mkoani Singida, umeahidi kutoa nyama pori kwa Wahadzabe wa kitongoji cha Kipamba kata ya Mwangeza ili washiriki sensa. Mkuu wa wilaya hiyo, Edward Ole Lenga, alisema ugawaji wa nyama pori hiyo utasaidia jamii ya Wahdzabe kubaki kwenye kaya zao kipindi chote cha sensa.


Akizungumza muda mfupi kabla ya kumkaribisha mkuu wa mkoa wa SIngida, Dk. Parseko Kone, awahamasishe Wadzabe na wakazi wengine wa kata ya Munguli, kushiriki sensa, Lenga alisema msaada huo wa nyama pori, unatokana na ombi liliotolewa na jamii hiyo ambayo chakula chake kikuu ni nyamapori, mizizi, matunda pori na asali.


Alisema, Wahdzabe hao wanaokadiriwa kufikia 227, wametoa ombi hilo ili wakati wote wa sensa wasiende porini kuwinda na badala yake wabaki kwenye kaya zao wakisubiri kuhesabiwa. Lenga, alisema ombi hilo tayari limeishakubaliwa na maandalizi yote muhimu ya kuwinda wanyama pori siku moja kabla ya siku ya sensa, yamekwisha kamilika.


Naye Dk. Kone, alisema atatoa msaada wa chakula wenye uzito wa zaidi ya tani moja ambao anaamini utakidhi mahitaji ya watu katika kipindi chote cha zoezi la sensa. “Nimewaletea chakula hiki ambacho ni mchele uliochangwa na vyakula mbali mbali ikiwemo mboga mboga kutoka shirika lisilo la kiserikali la International Africa Outreach la nchini Marekani. Chakula hiki ni kizuri mno, kina virutubisho vingi”alisema


Wengine waunga mkono


Mkurugenzi wa Jumuiya ya Tanzania Isalamic Peace Foundation, Shehe Sadiki Godigodi akishirikiana na Jumuiya, Taasisi na Mabaraza ya Kiislam Tanzania, wamewataka wanancho wote bila kujali dini zao kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo. Shehe Godigodi alisema kwa kutambua umuhimu wa Sensa, Taasisi hizo zimeamua kuwaomba na kuwahamasisha waumini wa Kiislamu kote nchini kushiriki katika zoezi hilo kwa kuwa litakuwa na faida kubwa kwa umma wa Waislaamu na kwa vizazi vijavyo.


Alisema, hakuna serikali yoyote inayoweza kufikia malengo yake katika maendeo bila kujua idadi halisi ya watu inaotakiwa kuwahudumia katika huduma mbalimbali.


Polisi watoa tamko


Jeshi la Polisi nchini, limeapa kuwachulia hatua kali watu wote watakaolihujumu zoezi la sensa. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jeshi limejipanga katika kuhakikisha zoezi la sensa linafanyika katika hali utulivu pasipokuwepo na uvunjifu wa amani wa kutaka kuhujumu zoezi hilo.


Chagonja alisema kuwa watu ambao watafanya uhalifu ikiwemo kuchana karatasi za makarani wa sensa, watachuliwa hatua kwa kuwafikisha mahakamani kutokana na sheria ya sensa. Alisema kuwa, kususia sensa ni kosa huku akiwataka wenye malalamiko kutekeleza zoezi katika hali usalama na baadaye baada ya kazi hiyo kukamilika ndio wafuatilie madai yao.

“Jeshi halitaweza kuwaacha watu ambao wanataka kuhujumu zoezi la sensa ambalo liko kisheria kwa madai yao wanatumia taasisi katika kushawishi wananchi wasijitokeze katika zoezi ambalo watendaji wetu wametekeleza hadi kufikia hapo” alisema Chagonja .

Kwa Upande wa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, alisema kuwa tayari jeshi la polisi linawashikilia watu kutokana na kutaka kuhujumu zoezi hilo. Alisema bado wanaendelea kufuatilia kwa karibu juu ya watu ambao wanashawishi wananchi kugoma katika kuhesabiwa kwa sababu zao ambazo haziko kisheria.



Takwimu wafunguka


Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS), Adelgunda Maro, amewataka wenye nia ya kukwamisha zoezi la sensa, kutii sheria na mamlaka zilizopo kwa kukubali kuhesabiwa. Wito huo aliutoa jana jana asubuhi wakati akihojiwa na Redio Tumaini kuhusu zoezilinalotarajiwa kufanyika usiku wa kuamkia kesho. “Ni kitu ambacho kipo kisheria na kama tunavyojua ni kwamba sheria huwa zinasimamiwa na dola na tumeamriwa kisheria tuhesabiwe kwahiyo watu watii sheria na mamlaka zilizopo kwa kukubali kuhesabiwa,” alisema Maro.



Waongo waonywa Bukoba


Aidha, wananchi wameonywa kuhusu kutoa taarifa za uongo kwa makaranai wa sensa ambazo sio sahihi na wanaotumia vipeperushi kuzuia zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika kesho Agosti 26, watakuwa wamekwenda kinyume na taratibu za sheria za nchi na kupanga maendeleo ya taifa.


Tahadhari hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Bukoba, Ziporah Pangani wakati akizungumza kwenye kikao cha madiwani wa halamashauri mbili zote za Bukoba kilichokuwa na Madhumini ya mkutano kuwawezesha madiwani kufahamu hatua iliyofikiwa na manispaaa katika kuwezesha zoezi hilo la hesabu ya watu na makazi ( SENSA).


Alisema, taarifa za Sensa zitasaidia kutambua mahitaji halisi ya wananchi kulingana na idadi ya watu katika eneo husika sanajari na kutoa huduma zakiuchumi ikiwemo miundo mbinu ya barabara na utoaji wa huduma za matibabu na elimu. Alisema, utaratibu huo wa kuwa na takwimu utawasidia kupanga na kutekeleza mipango muhimu ya maendeleo kwa jamii husika na taifa kwa ujumla.



Source: Tanzania Daima Jumamosi 25 Agosti 2012.

MAONI YANGU:
Kama kuendesha sensa tu kumeishinda serikali hii sijui ni kipi cha manufaa wanaweza kukifanya.
 
Back
Top Bottom