Kaka ukipata muda ukasoma tafakari

Daddo

JF-Expert Member
Jan 17, 2013
1,434
1,020
Nawashangaa wanaoshangaa.hivi ni kweli haya mambo yanatokea bila kujua chanzo? Au kwa kuwa wazawa wamejitia upofu na kutokusikia ndiyo maana inakuwa bora liende?

Kaka ebu kaa chini jitafakari tena. Nakumbuka kabisa ulikabidhiwa mamlaka ya kuungoza ukoo kwa heshima kubwa sana. Kila mmoja aliweza kuimba tena kwa kuinua mikono juu huku akiwa ameipamba kwa kuipaka rangi ya kijani na manjano kuashiria amani, mshikamano na maisha mazuri.


Kwakweli ilipendeza sana maana wazee wa kijiji walikula na kunywa huku watoto wakicheza na kufurahi kwa pamoja. Haikuwahi kutokea hapo awali nadhani hata yule aliyekutangulia aliona wivu kwa namna moja au nyingine.


Lakini kaka ebu turudi nyuma tutafakari furaha ya hawa watu ilikuwa imesababishwa na kitu gani? Je si zile ahadi nzuri zenye manukato mazuri ulizowaahidi?. Ukadiriki kuwaambia kwamba wewe kama kiongozi wa ukoo utahakikisha kaya zote zimepata maisha mazuri. Eti hatutakuwa tunafuata maji ya kunywa kwenye vijito vile vichafu tulivyo vizoea. Shule litakuwa siyo tatizo tena kwa wanaukoo, Barabara za kuunganisha mitaa yote na nyumba bora kwa kila familia.


Kwauelewa wangu japo sijawahi kwenda shule, kama ungetekeleza haya uliyoyahidi sidhani kama tungesikia harufu mbaya kwenye huu uko. Kaka sijui kama unapata muda wa kutembelea mitaa ya kila kaya iliyoko kwenye ukoo huu. Kuna harufu mbaya sana ambayo haivumiliki tena.


Wanandugu wanajiuliza chanzo cha hii harufu hasa ninini? je inawezekana ni panya wanaofia ndani na hakuna anayeonesha juhudi ya kuwatoa na kuwatupa? au kaya zimeshindwa usafi wa mazingira? Ama inawezekana hivi vyoo tunavyovitumia na tulivyokuwa tunavitumia tangu enzi za marehemu babu ndiyo vinavyotoa harufu?


Kipindi cha uongozi wa marehemu babu hivi vyoo vilikuwa vikitumika kwa umakini mkubwa. hakuna aliyethubutu kwenda kujisaidia akaacha tundu la choo likiwa wazi asisemwe. Ilikuwa lazima baada ya mtu kutumia choo akifunike kwa mfuniko ule wa mbao.


Lakini sitaki kujiridhisha moja kwa moja juu ya hili maana harufu hii ni kali kuliko hata ile ya choo. Labda nitakuwa wa mwisho kuamini hilo maana hata mimi ni binadamu.


Kaka usinikazie macho sana maana si mimi tu ninayelalamika juu ya hili swala. Labda tu ni kwakuwa umekuwa mvivu wa kutembelea kaya zako pengine ungeweza kuyasikia haya na kuyashuhudia mwenyewe.


Wapo waliofikia hatua ya kupoteza matumaini na wewe kabisa na kila wakuonapo wanatema mate japo kwa kujificha sana. Wahenga wanasema ''Huwezi kugombania sime kwa kushika kwenye makali huku adui akiwa ameshika kwenye mshikio'' hilo linawafanya wateme mate kwa kuangalia pembeni la sivyo nadhani wangekutemea usoni.


Wengine wanatamani sana kukuondoa kwenye kiti uichokalia ili ukoo uongozwe na mtu mwingine. Mwaka juzi ilikuwa utolewe kwenye kiti lakini huruma iliwajia watu baada ya kulia sana eti muda uliokuwa mfupi kwako kutekelaza mipango yako.


Kwa makusudi au kutokujua dhamira yako wakaacha uendelee kushikiria usukani. Kaka mimi naomba nikutaarifu kwamba sasa watu wamechoka.

Wengine wameanza kukaa vikao na kujadili mambo makubwa tena ya ndani kabisa. Hawaoni kilichofanyika mpaka sasa japokuwa kweli muda uliongezewa.

Haiingii akili kwa mtu kama wewe kuruhusu koo za majirani kuja kufuja mali za ukoo wako huku ukiwachekea bila kuchukua hatua yoyote. Mashamba yaliyoacha na marehemu babu yetu sasa yamekuwa hayana faida kwenye ukoo huu tena.


Kama kweli wewe ni mtu makini unashindwaje kusimamia kaya ili kuzalisha mali kwa manufaa ya ukoo? Kwa sasa hata wanandugu nao wameanza kugawanyika hawaelewani tena. Hakuna anayemjali mwenzake zaidi ya kujijali mwenyewe.


Kweli ukoo uliokuwa imara enzi za babu yetu ndio huu ambao leo unashinda kiguu na njia kwenda kuomba unga wa mlo wa siku kwa watu wengine? Unafikiri wanapotuambia kwamba kabla ya kupewa huo mlo wa siku tukubali kwanza kuwapa mashamba ili wao walime wanachokitaka wanakosea?


Ona sasa tumekubali kutoa mashamba kwa wageni. Wageni kwa roho mbaaya au kwa makusudi kabisa wameng'oa kabisa miti ya matunda iliyokuwa kwenye mashamba, na kuamua kupanda tumbaku ambayo hata ukiwa na njaa huwezi kuchuma ukala. Je nani wakulaumiwa?

Alinichekesha juzi mmoja wa watumishi wako aliposema kwamba ni kweli hatuna unga wala mboga za kutoosheleza kwa mlo wa wote ila bado tunasifa ya kukopeshwa kutoka kwenye koo zingine. Hivi kweli kaka hiyo inakuingia akilini?

Tuachane na hayo basi tuzungumzie maswala mengine. Unajua kuwa baadhi ya familia zimeshachoka kusubiria treni uwanja wa ndege? kama ulikuwa hujui basi huku kwetu hali si shwari.

Wanafamilia hao wanazunguka huku na kule kujaribu kuamsha hamasa ya familia zingine. Nakweli juu ya hilo naona mambo yanakwenda kama wanavyotaka. Ila kuna watu ambao bado wanaangalia upepo maana hawajawa na imani kubwa juu ya kinachohubiriwa na hao.

Usidhani kwamba wanamisamiati mikubwa wanayoitumia kupata watu, bali wanatafsiri kila harufu mbaya inayofukuta kwenye ukoo huu. Wengi wameamini kwamba harufu haitoki kwenye kaya zote za ukoo bali ni kwenye familia yako.


Wanatembea kifua mbele kusema kwamba familia yako haifai tena kutoa kiongozi wa ukoo maana hata choo chenu hakisafihwi tena huku kila anayejisaidia akiondoka bila kufunika tundu la choo.


Kwa ufupi kila mtu anafanya anavyotaka na hakuna wa kumkemea. Inasemekana hata usimamizi wa mali za ukoo haupo tena maana mali za ukoo mnachuma na kuficha huku wengine wakifa na njaa na hakuna anayejali.


Wewe mwenyewe umekaa kimya hata kuwanyoshea kidole wanafamilia wenzako hutaki matokeo yake ndiyo haya ya kuchokwa.

Pamoja na haya yote wapo wanaokusifia kwamba pengine unashindwa kuwanyoshea kidole kwakuwa muongozo aliouacha babu ni wakizamani sana na hauwezi kukidhi matakwa ya sasa, swali ni je babu alikuwa anatumia muongozo gani kuwakemea walie waliokuwa wanataka kuchuma na kupora mapera, machungwa na mananasi yaliyokuwepo na kuweza kuyagawa kwa usawa kuhakikisha kila kaya inapata?
Wewe mbona hata wageni wanakuja wanachuma na kuondoka nayo huku wanaukoo wakibaki kulalamika bila hatua za makusudi kuchukuliwa? tena wanadiriki na kusema eti wanakuja kuchuma kwenye shamba la bibi, kweli hili ni shamba la bibi?

Nikupongeze kwa kufikiria kuanza kutafuata mbadala wa muongozo aliouacha babu ila sina uhakika kama hili wazo lilitoka kwenye kaya yako au ulishinikizwa na yale maneno ya kusutwa kutoka kaya ya jirani. Hilo mimi si jukumu langu kujua cha msingi tu ni kwamba nakushauri uangalie upya jinsi ya kuiondoa hii harufu mbaya ili kila mtu arudishe imani yake kwako.


Kaka naomba nikukumbushe tu kwamba kama unatamani kaya yako iendelee na kuongoza ukoo basi huna budi kufuata kurudisha sifa za mwanzo za ukoo yaani kujaliana, kupendana na kuthaminiana.
 
Thread ndefu namna hii maana nimeisoma mpaka macho yanatoa machozi lakini sijaelewa chochote!
 
Tulio watoa kucha,kuwatesa kuwatoboa macho na kuwang'ata tuliwaachia uhai wao.sasa wewe subiri utamfata babu yako!.
 
Kaka! Safi ujumbe mzuri kwa hali halisi iliopo sasa! Na watanzania wanavyoongelea hali hiyo sehemu mbalimbali! Wasioelewa ni wavivu wa kusoma na kutafakkari! Na hao wakipata madaraka kwa sababu ya uvivu wao wa kutopenda kusoma na kutafakari ndio wanatiaga sahihi kwny mikataba mibovu! Kwa sababu ya uvivu wao! Big up!!! BRAvO!!

Sent from my BlackBerry 9700 using JamiiForums
 
Safi sana mleta uzi,Laiti kama viongozi wetu wangekuwa na uchungu na rasilimali za nchi hii yetu maisha yangekuwa mazuri sana,

Ila kwa uchu wa madaraka na kujilimbikizia mali hakuna anaye mjali mwezie,maskini anazidi kunyang'anywa hata kile kidogo alicho nacho na viongozi wetu wamekaa kimya kama hakuna kinachoendelea,Lakini ipo siku tutaamka kutoka usingizini na kujua kudai haki zetu
 
I-copy na ukaipesti kwenye gazeti linalojitambua, ni bonge la andiko, lugha rahisi na ya kueleweka, haihitaji tafsiri.
MR.NOMA anasema inafanana na mjomba ni kweli; Wana kaya tulimtuma Mpwa wa Mkuu wa Kaya kumweleza yanayotusibu, akapata nauli akaenda kumwambia hakusikiliza.

Tukamtuma Mwanae kwenye "Ridhiwani Ongea na Mshua (Ongea na baba yako)", hatuna uhakika kama alimfikishia baba yake ujumbe wetu.

Sasa tunamtuma kaka wa Mkuu wa Kaya napo tuone, tukishindwa basi tena, ni kufanya lolote tu.
 
Last edited by a moderator:
I-copy na ukaipesti kwenye gazeti linalojitambua, ni bonge la andiko, lugha rahisi na ya kueleweka, haihitaji tafsiri.
MR.NOMA anasema inafanana na mjomba ni kweli; Wana kaya tulimtuma Mpwa wa Mkuu wa Kaya kumweleza yanayotusibu, akapata nauli akaenda kumwambia hakusikiliza.

Tukamtuma Mwanae kwenye "Ridhiwani Ongea na Mshua (Ongea na baba yako)", hatuna uhakika kama alimfikishia baba yake ujumbe wetu.

Sasa tunamtuma kaka wa Mkuu wa Kaya napo tuone, tukishindwa basi tena, ni kufanya lolote tu.

Nashukuru kwa ushauri.
 
Last edited by a moderator:
Well written, pamoja na mengine, nimependa jinsi ulivyoiwakilisha hiyo sehemu ya rasilimali za nchi zinavyofaidisha nchi za nje na kutuacha wenye nazo masikini. Shame on us!!

Sent from BlackBerry 9900.
 
Kweli fanani umetamba vema na kwa mkutadha huu umefanya hadhila wenye upeo kusoma kwa raha.
Umetumia fasihi yenye lugha raini.
 
Back
Top Bottom