Juu ya utumishi wangu kwenye "Taasisi" ile ninapohakikisha treni la EL linatema abiria wake

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,478
40,000
grunge_flag_of_tanzania_by_pnkrckr.png

Na. M. M. Mwanakijiji

Kumekuwa na tetesi nyingi kwenye hii mitandao juu ya utumishi wangu uliotukuka kwenye taasisi nyeti ambayo baadhi ya watu wamedokeza kuwa yawezekana ninaitumikia. Habari hizi si ngeni kwenye hii mitandao na kwa bahati mbaya wapo watu ambao habari hizi zinaweza kuwa zinawachanganya na kuwakwaza kwani wengine waliamini tu kuwa mimi nishabiki wa mabadiliko ya kisiasa kwa misingi ya kijuu juu bila kuwa na mahali hasa ninaposimamia. Kuhusishwa kwangu na "Taasisi" au wengine wamesema "Kitengo" kumenifanya ni lazimike - japo sijapenda sana - kutoa kauli juu ya hili.

Kwanza nawaomba radhi wale wote ambao kwa namna fulani watakwazika kwa kile nitakachosema hasa kwa vile wengi inawezekana walikuwa wanaamini miye ni muumini tu wa mabadiliko yasiyoelezeka na yasiyo na malengo au wale ambao walikuwa wanapenda kusoma maandishi yangu kwa muda wa miaka hii karibu ishirini sasa tangu nianze harakati hizi za kuliamsha taifa kifikra katika kile ambacho nilikiita wakati ule kuwa ni "mapambano ya kifikra". Wale ambao wanajua au wanafikiria wanajua juu ya utumishi wangu lakini wasijue mengi juu ya utumishi huo basi makala hii fupi itakuwa ni sababu ya wao kujua zaidi ya kile ambacho walifikiria au wanafikiria wanakijua.

Ni kweli kabisa kuwa mimi ni mtumishi wa kudumu wa Taasisi na kwa kweli siyo sahihi wala si haki kabisa kuita Taasisi ninayoitumikia kuwa ni "Kitengo" fulani. Kitengo ni sehemu ndogo tu ya Idara fulani, na Idara ni sehemu ndogo tu ya Taasisi au Shirika fulani kubwa. Mimi si mtumishi wa Kitengo au Idara fulani; mimi ni mtumishi wa Taasisi yenyewe. Nimekuwa mtumishi - siyo mwajiriwa - wa taasisi hiyo kwa takribani miaka ishirini sasa.

Na ni kweli kuwa kinyume na waandishi, wachambuzi au hata wanaharakati wengine wa mabadiliko mimi na wenzangu wachache (mnaowafahamu na msiowafahamu) ni waaminifu zaidi kwa Taasisi hii kuliko kitu kingine chochote kile. Tunaongozwa na mapenzi yasiyotetereka na yasiyopungua ya kuitumikia taasisi hii na kama mtu mmoja alivyosema huku kuwa sisi watumishi wa Taasisi ile ni "loyal" kwa taasisi kuliko kingine chochote. Katika utii na uaminifu wetu huo kwa kweli hatujali marafiki wa zamani au wapya, ndugu wa karibu au wa mbali, hofu ya sasa au ya mambo yajayo! Tunaitumikia taasisi hiyo na wengi wetu tunamwomba Mungu ikifika zamu yetu kutuita basi atuite tukiwa watumishi waaminifu na wasiotetereka wa taasisi hii. Na kwa sababu hii kututakia kifo au mauti hakututishi, hakutuogopeshi, na wale hatuangalii mauti kwa macho ya woga; tunaangalia tu kama ni zamu yetu kama ilivyo zamu ya wanadamu wote bila upendeleo.

Taasisi hii imenifanya niwe jinsi nilivyo. Tangu kujiunga nayo nikiwa kijana wa makamo hadi leo hii imenifanya nitambue mambo mengi na kujifunza mengi. Imenifanya niiangalie nchi yangu kwa macho ya mapenzi makubwa na watu wake kwa mapenzi makubwa zaidi. Taasisi hii imenifundisha kuona kuwa Watanzania wanastahili zaidi ya wanachopewa na kuwa WAtanzania hawajalaaniwa na Mungu au Shetani kupata madudu ambayo wamekuwa wakiyapata na ambayo wanaweza kuyapata tena endapo sisi tunaofanya kazi kwenye Taasisi hii (popote pale tulipo) tutaamua kukaa kimya. Taasisi hii kwa kweli ndio imefanya hata Watanzania ambao walikuwa hawajali nini kinaendelea wafunguke macho yao na kuanza kujali na wale ambao walikuwa wanafikiri wanaweza kutawala wapendavyo waanze kufikiria mara mbili na kuanza kutawala wanavyopaswa. Taasisi hii basi huwezi kabisa kuitenganisha na maandishi yangu, maono yangu na hata maoni yangu mbalimbali; vyote kwa kiasi kikubwa vimetokana na kuijua, kuipenda, na kuitumikia taasisi hii.

Siyo watu wote wanaweza kuitumikia taasisi hii au wanaweza kudumu katika utumishi wake hasa yanapotokea mabadiliko makubwa au changamoto ambazo zinaweza kumfanya mtu ahoji kama anataka kuendelea kuitumikia. Bahati mbaya sana katika miaka hii ishirini na katika wiki hizi chache za karibuni taasisi yetu imepoteza watu maarufu na waliokuwa na mvuto mkubwa na ambao waliaminisha umma kuwa na wao ni watumishi wa taasisi hii. Bahati mbaya pale sururu ilipolamba ardhi ndugu zetu hawa wakafumba macho yao na kusita; ndugu zetu tuliowapenda na kuwaamini walishindwa kuendelea kuwa watumishi na hawa tumewapoteza na ni vigumu sana kwa wao kurudi tena kuwa watumishi wa Taasisi hii. Hadi hivi sasa sijawahi kumsikia mtu aliyetoka kwenye Taasisi yetu kwa kukana au kubeza yale ambayo Taasisi inasimamia halafu akarudi na kuwa mtumishi tena; ukishatoka umetoka - milango yetu ya ofisi inafungukia nje! Ukiingia ndani umeingia na ukitoka umetoka.

Taifa letu limewahi kuwa na watu wachache sana ambao nao waliwahi kuwa watumishi wa Taasisi hii - wachache miongoni mwao ni kama Baba wa Taifa mwenyewe (Mtetezi kwa Kwanza Wa Taasisi Kitaifa), Edward Moringe Sokoine, Horace Kolimba, na wengine ambao majina yao yanajulikana na wengi ambao wametumikia taasisi hii bila kuimbiwa nyimbo za sifa na majina yao hayafahimiki. Hata katika mwaka huu wa uchaguzi, wachache wamejitokeza ambao wanaitumikia Taasisi hii na wanaendeleza yale yale ambayo wana Taasisi tunatakiwa kuyaendeleza nayo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inapata viongozi inaowastahili siyo wa kubambikiziwa.

NI kwa sababu hiyo, watumishi wa Taasisi hii kwa kweli hatujali sana nani yuko madarakani; hatujali nani anataka madaraka, lakini wakati wote yeyote tunayemtaka kuwa madarakani au yule ambao anafikiria anataka kuwa madarakani basi anachunguzwa kwa vigezo vile vile vya kitaasisi na ama tutamuunga mkono au kumpinga. Tunapofanya hivyo hatuchukulii mambo kijuu juu - tunafahamu kwa mfano mapungugu ya mtu au madhaifu yake na mazuri au ubora wake; hatutampinga mtu kwa vitu ambavyo tunajua kabisa ni vya ubinadamu wake au udhaifu ambao tunajua hautaingiliana utendaji kazi wake na hutasikia hata mmoja wetu akijaribu kumpinga mgombea au kiongozi kwa madhaifu au matatizo yake ya kibinadamu - kati ya yale Masharti Kumi ya vitu tunavyokatazwa kufanya hili ni namba tatu (3).

Taasisi hii inadumu, haifi, na haibadiliki bila kujali nani anaingia madarakani au nani anaondoka. Taasisi hii itaendelea kuwepo hata bila Mwanakijiji kuwepo kwani wapo watu wengi ambao wanapenda kuitumikia wengine rasmi na wengine siyo rasmi. Taasisi hii inavutia watu wengi na wenye kuthubutu kweli huweza kuitumikia tena kwa moyo kweli kweli na wengine (nimeambiwa) wamejikuta wakiitumikia taasisi hii bila kujua! Na wiki hizi chache mimi mwenyewe nimeshangaa; baada ya kuwapoteza baadhi ya watumishi wenzetu kwa upepo wa masaa makundi mengine mapya ya watumishi na wapenzi wa Taasisi hii wamejitokeza na kuniaminisha kabisa kuwa kazi ya Taasisi kujiuza na kuvutia watu - hasa vijana wake kwa waume - imefanikiwa sana!

Ni kweli mimi ni mtumishi wa Taasisi hiyo; nimeapa kuendelea kuitumikia na natumaini nitaendelea kuitumikia muda mrefu ili kuhakikisha kuwa Tanzania haiingizwi mjini na utapeli wa kisiasa wa kuuziwa kisichokuwepo na kuaminishwa kuwa kipo huku mtu akifurahia. Inanikumbusha miaka ile niliposafiri kwenda Zanzibar wakati huo na nikanunua Radio Kaseti yangu pale Darajani aina ya PANASONIG na kwa muda niliifurahia sana. Kwa miezi kadhaa niliifurahia radio hiyo hadi pale vidude vya kubonyezea kaseti vilivyopoanza kudondoka na radio kuanza kukoroma ndipo nilipoangalia vizuri nikakuta niliuziwa PANASONIG ambayo mimi nilifikiria ni PANASONIC! Baada ya kujiunga na Taasisi nilifundishwa mapema sana kuwa mdadisi wa kitu chochote ninachouziwa, kusikia au hata kuona kwa macho yangu - (sitoshangaa wengi hamkuona hiyo herufi G hapo au mlipuuzia na kufikiria ni 'typo').

Kwa wanaopenda kujua Taasisi hii ambayo ninaitumikia na ni mtumishi wa muda mrefu inajulikana kama UKWELI. Ni taasisi ambayo mvuto wake hudumu vizazi na vizazi na watumishi wake ni watiifu kwake kuliko kitu kingine chochote. Taasisi hii ya ukweli inavutia fikra za kile anayejiunga nayo na kile ambaye moyoni mwake imewasha moto Taasisi hii inahakikisha kuwa moto hauzimiki. Mtu yeyote anayependa ukweli - siyo hadaa - ni mtumishi mwaminifu wa Taasisi hii. Siyo kwamba hatofanya makosa au hatafanya jambo baya lakini kuwa lolote atakalofanya atafanya katika mwanga wa kuutafuta ukweli. Mtumishi wa Ukweli anatambua hadaa inapoonekana toka mbali au ikiwa imejibadili rangi kama kinyonga.

Naam, mimi ni mtumishi wa Taasisi hii na niwahakikishie tu kuwa sina mpango wa kusalimu kwa mtu yeyote, popote au kwa vyovyote. Hakuna vitisho, kejeli, dharau au hata maneno ya kukatisha tamaa ambayo yana nafasi katika kunifanya niache kuutafuta ukweli, kuupenda, na kuutetea mahali popote na kwa vyovyote. NI kwa sababu hii ndio maana kama nilivyowahi kusema nyuma naamini Watanzania wanajaribu kuingizwa mkenge na mgombea asiyefaa na asiyestahili kuwa Rais wa nchi yetu na kuwa kundi ambalo limemchukua lilikuwa na lengo moja tu - kuuvuruga ukweli (hata kama walikuwa hawajui). Bahati nzuri ukweli kama alivyosema Baba wa Taifa haupendi kupuuzwa; upuuzi kwa maangamizi yako mwenyewe!

Mwanafalsafa Mmoja Augustino wa Hippo aliwahi kusema "Ukweli ni kama simba, huitaji kumtetea. Unahitaji kumfungulia tu. Ukishamfungulia anajua kujitetea".

Kwa ajili ya UKWELI, Kwa ajili ya Taasisi ya UKWELI

Mtumishi Mdogo
MMM
 
Sina la kusema but umechelewa akili zetu kwa sasa ni kwa mabadiliko sio ccm kbsa
 
CV ndeefu, wapelekee CCM watavutiwa nayo sana! Tatizo unashindwa kusoma matakwa ya Watanzania walio wengi, ishu kwa sasa sio habari ya mtu binafsi, ishu ni kuitoa CCM as a whole!
 
Nilijiandikisha baada ya kupata matumaini pale Lowasa alipohamia upinzani. Sasa ni uvivu wa kufikiri, kufikiria kuwa unaweza kunibadilisha kura yangu iende ccm. Yaani aliyenihamasisha kujiandikisha, nisimpe kura?! Kwenda zako ... Subiri tupige kura then uje ulete hadithi hizi hata kama zina ukweli.
 
Ukweli maana yake Ni nini❔➖mkweli hajigambi,hajikwezi na wala hajitapi.Mkweli husifiwa,huonwa na pengine huwa hajitambui kama Ni mkweli.
Kama huwezi kujifahamu, utafahamu vipi hata mazingira yaliyokuzunguka?

Mimi nadhani unasumbuliwa na inferiority complex ndiyo maana unadhani amejigamba, amejikweza na kujitapa.

Kwangu mimi naona na kufikiria aliyoyaandika ni mambo ya kawaida sana katika dunia iliyojengwa kwa nguzo ya ukweli.
 
ADUI YETU SIO UJINGA,UMASIKINI,MARADHI,RUSHWA AU UFISADI!ADUI YETU NI CCM!
Ni kweli na mtanzania mwenye akili Timamu yeyote anayewaunga mkono HAJIELEWI.ADUI YA WANANCHI MAKINI KWA TAIFA LAO NI UMASKINI,RUSHWA,UFISADI,UKANDAMIZAJI,UNDUGULISATION,MARADHI na yeyote anapigana vita ya haya ni RAFIKI KWAO.
 
Umesomeka mkuu, kilo chako ndiyo kilio changu. Kuna watu wengi sana huu mkanganyiko umewaweka kwenye hali ya sintofahamu.

Binafsi Lowassa simtaki kama vile ambavyo wewe humtaki, ila napata ugumu mkubwa sana wa eti niipigie kura CCM?

Mkuu nikuombe maoni yako ya nani tumpigie kura?

Tusipige kura ya urais?
Mzee Mwanakijiji
 
Last edited by a moderator:
Ukweli usiozingatia sheria una maana gani ktk dunia ya kidemokrasia.

1. Chombo pekee chenye uwezo wa kuthibitisha mtu ana hatia na mahakama kwanini huyo mwizi hakupelekwa mahakamani?

2. Hivi ili jambo la kamati ya bunge kutokumhoji lowasa juu ya richmond ninyi mnaosimamia ukweli mnaliona ni jambo la kawaida? Kwanini hakusikilizwa?

Tumechoka kuishi kwa tetesi km tutafanya makosa kwa kumchagua anayehisiwa kuwa ni fisadi basi wakulaumiwa ni serikali ya ccm. Na vyombo vyake kwa kutotimiza wajibu wao.

Ukweli ni mmoja na haugawanyiki na ni wazi kuwa ccm na serikali yake walikuwa likizo kwa miaka kumi. Wacha tuwape muda zaidi wa kupumzika
 
Back
Top Bottom