Justice delayed is justice denied!

Crucifix

JF-Expert Member
Feb 20, 2011
1,651
588
Sunday, 17 April 2011 20:32 (source mwananchi, usiulize kwa nini Sunday badala ya Jumapili)
James Magai

JAMHURI imegoma kujibu hoja za rufaa za muomba rufaa, Danford Anthorny katika kesi ya maombi ya rufaa namba 94/2010 kwa kile ilichoelezwa kuwa mahakama iliyosikiliza kesi ya msingi haikuwa na uwezo wa kisheria. Mrufani huyo alitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Kilosa na kuhukumiwa adhabu ya kifungo mwaka 2009 baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na nyara za serikali.

Hata hivyo hakukubaliana na hukumu hiyo, hivyo akakata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akitoa sababu nane za kupinga hukumu na adhabu hiyo. Lakini wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, mwishoni mwa wiki serikali ambayo ni mjibu rufaa hiyo ilikataa kujibu sababu hizo za rufani ikidai kuwa mahakama iliyosikiliza kesi ya msingi haikuwa halali.

Wakili wa serikali aliyejitambulisha kwa jina moja la Katuga alidai kuwa kwa kuwa haina uwezo wa kisheria kusikiliza kesi ya namna hiyo na kwamba kwa hali hiyo shauri hilo halikuwa halali kisheria.

"Mheshimiwa Jaji, mrufani alishitakiwa kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali kinyume cha kifungu cha 70(1) (2) cha Sheria ya Hifadhi ya Wanyama sura ya 283 kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambalo limo katika makosa ya uhujumu uchumi," alisema wakili Katuga.

Alisema mahakama za chini ya Mahakama Kuu, hazina uwezo wa kisheria wa kusikiliza shauri la uhujumu uchumi isipokuwa tu kama zimepata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) kwa mujibu wa kifungu cha 12(3). "Lakini mahakama ya Wilaya ya Kilosa ilisikiliza kesi hii bila kuwa na kibali hicho.Kwa hiyo ilisikiliza kesi ambayo haikuwa na mamlaka nayo, hivyo shauri halikuwa halali kisheria. Kwa sababu hizo Jamhuri haina sababu ya kujibu hoja za mrufani kwa sababu si halali mbele ya sheria," alidai Wakili Katuga.

Baada ya kusikiliza hoja za upande wa mjibu rufaa (Jamhuri) Jaji Fatuma Masengi alimuuliza mrufani iwapo alikuwa na jambo lolote la nyongeza, lakini mrufani huyo akajibu kuwa hana hivyo Jaji Masengi aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 4 kwa ajili ya uamuzi.

Akitoa maoni yake juu ya msimamo huo wa Jamhuri nje ya mahakama, Wakili wa kujitegemea Makaki Masatu baada ya Wakili wa serikali kubainisha kasoro hizo za kisheria zilizofanywa na mahakama ya chini, alisema jaji alipaswa kumwachilia palepale muomba rufaa.

"Wakili wa serikali anapokwenda kwenye kesi haendi kutetea tu upande wa serikali hata kama kuna makosa ya kisheria bali ni lazima asimame katika sheria; Hivyo baada ya wakili wa serikali kubainisha kasoro hizo mahakama ingeweza kumwachilia mpaka pale serikali kama ingetaka ingeweza kujipanga tena na kumshtaki upya ", alisema. Wakili Masatu.
 
Back
Top Bottom