BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,014
JK atuambie amechukua hatua gani
John Bwire Machi 18, 2009
Raia Mwema~Muungwana ni vitendo
John Bwire Machi 18, 2009
Raia Mwema~Muungwana ni vitendo
PAMOJA na gazeti hili, kupitia safu zake mbalimbali, kuitahadharisha serikali, kwa muda mrefu, kuhusu kuchukua hatua za kujihami dhidi ya anguko la uchumi wa dunia ambalo lilikuwa njiani, hakuna kope serikalini zilizopepesa.
Na hata athari za anguko hilo la uchumi zilipoanza kuzitafuna nchi tajiri za Marekani, Uingereza na Japan, watawala wetu nchini waliendelea kututia moyo kwamba tuko salama; kwamba hatutaathirika kwavile asasi zetu za fedha hazifungamani moja kwa moja na asasi za fedha za mataifa hayo tajiri zilizotetereka. Wakaonyesha hata takwimu kwamba uchumi wetu unakua!
Lakini, baada ya majuzi kuja nchini Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Dominique Strauss-Khan na kutuambia kwamba sasa ni zamu ya bara la Afrika kuanza kuathirika na anguko hilo la uchumi wa dunia, watawala wetu wakazinduka usingizini.
Wakati mwanzoni walituambia kwamba hatuwezi kuathirika kwa kuwa asasi zetu za fedha hazifungamani moja kwa moja na asasi za fedha za mataifa tajiri zilizosambaratika, sasa wanakiri kwamba dunia ni kijiji na kwamba kinachowaathiri walioko Ulaya kitawaathiri walioko Tanzania.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na BBC, yaliyosikika alfajiri ya Ijumaa iliyopita (Machi 13), Rais Kikwete alisema kwamba nchi zetu duniani zimefungamana (interlinked), na kwamba kinachotokea na kuathiri London pia kitaathiri Dar es salaam.
Tuonavyo, hicho alichokisema Rais Kikwete ndiyo ukweli wenyewe, na ndiyo maana, kwa mara nyingine, tunaihimiza serikali kuchukua hatua haraka za kujihami, maana kuchelewa kwao kutakuja kuleta kilio na kusaga meno kwa Watanzania wakati athari za anguko hilo la uchumi zitakapoanza kututafuna kikweli kweli.
Kama watawala wetu walikuwa wanasubiri kuamshwa, basi, kengele ya kuwaamsha imeshapigwa na Strauss-Khan. Tunachokitarajia sasa kutoka kwao ni kututangazia ni hatua gani wanazichukua kukabiliana na athari za anguko hilo la uchumi wa dunia.
Tunasema hivyo kwa sababu, mpaka sasa, Rais wetu Jakaya Kikwete hajautangazia umma namna serikali yake inavyopambana/ itakavyopambana na athari za anguko hilo la uchumi wa dunia. Haitoshi tu kwenda London kuhudhuria mkutano wa G20 wakati nyumbani hajachukua hatua zozote kubwa.
Ijumaa ya wiki iliyopita tuliisikia serikali ya nchi jirani ya Kenya ikitangaza kwamba imeishiwa fedha kutokana na anguko hilo la uchumi wa dunia, na kwa sababu hiyo imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kusimamisha ajira zote serikalini, kusimamisha safari zote za nje kwa maofisa wa serikali na kusimamisha semina na makongamano kwa asasi zote za serikali.
Je, sisi hatuwezi kufuata nyayo za wenzetu wa Kenya kabla mambo hayajaanza kutuharibikia kabisa? Au tuamini kwamba bado tuko salama?
Tunajua kwamba ni jambo gumu kusimamisha ajira katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi; hasa kwa chama kilichoahidi kuongeza ajira, lakini je, hata safari za nje, semina na manunuzi yasiyo muhimu navyo hatuwezi kuvisimamisha kwa muda huu?
Wakati tukiisubiri serikali yetu itutangazie inachukua hatua gani kukabiliana na athari za anguko hili la uchumi wa dunia, wito wetu kwa wananchi ni kuwa makini na matumizi ya vipesa kidogo walivyonavyo; kwani kipindi kugumu cha maisha kinakaribia kupiga hodi.