Jifunze kutofautisha watu hawa wawili wanaokuja kwako kimahusiano

Feb 4, 2024
67
204
Mahusiano sio kitu kigeni na hasa mahusiano ya kimapenzi yamekuwa yakiimbwa kwa ubaya na uzuri kila uitwao leo, kwenye hii Dunia kila mtu ni lazima ahusiane kama hutofanya hivyo kwenye mahusiano ya kimapenzi basi utafanya hivyo kwenye mahusiano ya kijamii hivyo hakuna namna unaweza kukwepa kuhusiana.

Kwenye mahusiano kuna kufaana na kushindwana ndio maana kila siku tunashuhudia matukio makubwa mawili ambayo ni watu kuendelea kuhusiana na huku wengine wakiafiana kuachana, Kwenye kuendelea kuhusiana haimaanishi kuwa wameendana kwa sababu kuna wengine wafanya hivyo kwa sababu tu wanajiona wamekosa pakwenda na kwenye kuachana yawezekana mnaendana ila mmoja tu kushindwa kuwa na subira ama kushindwa kujifunza kuishi na mwenziwe.

Kuna makundi makubwa mawili ya watu ambao wanakuja/watakuja kwako kimahusiano hivyo ukiyafahamu hutopata shida ya kukabiliana na matokeo ya kila kundi.

Kundi la kwanza ni yule MTU ANAYEKUJA KUKUANGALIA KWELI WEWE NDIYE?
Huyo ni yule ambaye hajui nani anamtafuta hivyo atakuja kwako kama kubahatisha tu ukiwa ndiye atakaa na ukiwa siye ataondoka, hili ni kundi lenye watu wengi sana na kwa ufupi mimi huwa naliita kundi ambalo linajifuta kwenye mahusiano yaani bado wanachama wake hawajui kipi wanataka hivyo wanapoingia kwenye mahusiano wanakuwa mguu mmoja nje na mwingine ndani, utalitambuaje kundi hili? Huwa wana sifa zao zinazo fanana kwa kiwango kikubwa.

TABIA YA WANAKIKUNDI HIKI NI KAMA ZIFUATAZO:
1. Wanakuwa kama waamuzi wa mpira tu muda mwingi wanatafuta makosa yako.
2. Hawana subira hivyo changamoto inayohitaji utatuzi wa pamoja wao ndio wanaichukulia kama mlango wa kutokea.
3. Hawasamii lengo moja ipasavyo hasa la kwanini wanahusiana yaani ukimuuliza kuhusu kesho yenu kwenye suala la pamoja anakuwa na maelezo mengi yanayokingana yenyewe, wapo hivi kwa sababu wanakuwa hawana uhakika kweli wewe ndiye?
4. Huwa hawatulii na mtu mmoja kwa sababu hawajui nani wanamtafuta hivyo hujikuta kwenye mahusiano na watu wengi
5. Muda mwingi wanakuwa kama wapelelezi.
6. Kuachana kwao sio jambo dogo na muda mwingi watatishia hivyo hasa changamoto inapojitokeza.
7. Hawapendi kutafuta suluhisho bali wanakuwa kishari zaidi pindi amani inapotakiwa.
8. Wanakuwa na haraka sana na utalijua hilo kwa kuona wanataka mambo yawezekane bila kughairishwa kwa mfano mmepanga kukutana na bahati mbaya ukakutwa na changamoto na ukatoa taarifa ila kwake anaweza kutumia changamoto hiyo kama fimbo ya kukuadhibu na mkaachana.

Kundi la pili katika eneo hili ni MTU AMBAYE ANAKUJA KWAKO KUKAA.
Huyo anajua nani anamtafuta hivyo haji kwako kwa kubahatisha bali kajiridhisha kabla hajaja kwa lugha nyepesi hawa ni wale ambao hawapo kwenye majaribio labda wakukute wewe ndio upo kwenye majaribio uwakimbize ila ukiwa nawe upo tayari basi watajenga kibanda kwako na maisha yataendelea.

Hili ni kundi lenye wanachama wachache kwa sababu ili uwe mwanachama sifa ya kwanza lazima ujitambue vilivyo na ujue nani unamtaka.

Hili kundi ndio linafanya watu wasifie mahusiano na kuyaimba kwa uzuri wake , wanachama wake wana tabia zinazofanana na sio tabia nyingi hata.

SIFA ZA WANACHAMA WA KUNDI HILI.
1. Hawana mambo mengi hivyo wakija kwako hawaji kama waamuzi wa mpira bali wanakuja kujifunza kuishi na wewe na kufundishana pale mnapopishana.
2. Ni kundi ambalo halifichi lengo lao kuu na kupitia matendo utawaona hivyo pia.
3. Ni watafuta suluhu kwenye changamoto sio wepesi wa kutishia muachane.

Hizo ndio sifa za kila kundi na mpaka kufikia hapo natumai umejitambua upo kundi gani ama una uhusiana na mtu wa kundi gani , ikiwa upo kwenye kundi la kwanza ni bora uachane na mahusiano kwanza na uwekeze nguvu kubwa kwenye kujitafuta ili ujue nani hasa unamtafuta.

Makala hii imeandikwa na Mwanasayansi Saul kalivubha
#fikia ndoto zako
+255
 
Back
Top Bottom