Jenista Mhagama aongoza Kamati ya Kitaifa ya Maafa kutembelea maeneo yenye maafa ya mafuriko Mlimba, Kilombero Mkoani Morogoro

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,817
11,993
Moro.jpg

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSIANA NA MAFURIKO YA MLIMBA MKOANI MOROGORO

Mobhare Matinyi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali. Mlimba, Morogoro, Alhamisi, Aprili 11, 2024: Saa 10:30 jioni.

1. Leo Alhamisi ya tarehe 11 Aprili, 2024, Kamati ya Kitaifa ya Maafa ikiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu). Mhe. Jenista Mhagama, akiambatana na Mawaziri wengine watatu na Manaibu Mawaziri sita, iliendelea na ziara katika maeneo yenye maafa ya mafuriko kwa kuitembelea Halmashauri ya Mlimba, Wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro.

2. Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mlimba B, kata ya Mlimba, tarafa ya Mlimba, Mhe. Waziri Mhagama, kama ilivyokuwa jana alipozungumza na wananchi wa wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani, aliwafikishia salamu za pole kutoka kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan: na kuwahakikishia kwamba serikali itashirikiana nao katika kuzikabili changamoto za mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.

3. Mhe. Waziri Mhagama aliwaeleza wananchi kwamba mafuriko haya yanayoenea maeneo mengi nchini yanatokana na mvua kubwa za El Nino kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu mwezi Agosti 2023, huku akielezea hali ilivyo katika eneo la bonde la mto Kilombero baada ya kulikagua kwa kutumia helikopta za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

4. Mvua hizi zimesababisha bonde lote la mto Kilombero kujaa maji huku sehemu kubwa ya maji hayo yakiingia mto Rufiji na kuleta maafa ya mafuriko katika wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani. Ingawa mito mbalimbali nchini kutoka mikoa kadhaa huchangia maji kwenye mto Rufiji, lakini mto Kilombero pekee na matawi yake huchangia asilimia 62 ya maji ya mto Rufiji.

5. Wakiongea na wananchi wa Mlimba, Mawaziri na Manaibu Mawaziri waliwahakikishia waathirika wa mafuriko hayo kwamba serikali itahakikisha huduma za barabara, madaraja, maji, umeme, mbegu, chakula na afya zinapatikana mapema na kwa ufanisi.

6. Mawaziri waliokuwepo ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa; na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso. Aidha, Manaibu Mawaziri walikuwepo ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya; Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga; Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde; Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Molel; Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula; na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo.

7. Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa wizara hizi wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, nao walikuwepo ziarani. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya, Mbunge wa Mlimba, Mhe. Godwin Kunambi; Mbunge wa Ifakara, Mhe. Abubakar Asenga pamoja na viongozi wengine akiwemo Katibu Tawala wa Mkon wa Morogoro, Musa Ali Musa, walikuwa wenyeji wa Kamati ya Kitaifa ya Maafa.
 
Mafuriko kila sehemu kikubwa tuwe wawazi kwa watu kuhama mabondeni kuwatembelea hakuna tija kama watu kuachwa waishi mahala hatarishi na viongozi kutumia fedha na muda kuhalalisha kipato wasichostahili hata kidogo
 
Back
Top Bottom