Je, tatizo la Zanzibar ni vurugu za kijinai (Criminal Violence) au ni vurugu za kisiasa (Political Violence)?

Jamhuri ya Zanzibar

Senior Member
Jul 17, 2012
126
195
images.jpeg

Sambamba, je, kusaidia kumaliza au kupunguza uhasama, mizozo na mpasuko, Zanzibar inahitajia haki ya kijinai (criminal justice) au inahitajia zaidi haki ya kisiasa (political justice)?

Na, Khalid Said Suleiman.

Jumapili, Disemba 6, 2020.


Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, naomba kueleza mtazamo wangu. Na katika hili, tukubali kutofautiana katika fikra na mitazamo, lakini tuvumiliane, tuheshimiane na tubaki kuwa wamoja.

Nini khasa kinachofautisha baina ya dhana mbili hizi: vurugu za kisiasa (political violence) na vurugu za jinai (criminal violence)? Tofauti muhimu ni hii. Vurugu za kisiasa zinahitaji zaidi ya wakala wa jinai tu; inahitaji eneo la kisiasa. Zaidi ya wahusika tu, inahitaji wafuasi. Zaidi ya vurugu za jinai, vurugu za kisiasa husababishwa na masuala mengi ikiwemo historia, jiografia, ubaguzi, tofauti za kiitikadi, kutoaminiana, nakadhalika.

Kwa maoni yangu, busara ni kutafsiri na kufafanua upya kiini cha tatizo ni nini na ni upi utatuzi wa kudumu na/au alau wa muda mrefu. Kwani kama maradhi; matatizo huzidi kila yanapochelewa kutatuliwa na hayaondoki kwa kuondoa tu dalili (symptoms) zake. Aidha, tusitafute dawa ya ugonjwa mdogo itakayozua magonjwa makubwa zaidi na yasiyokuwa na tiba.

Ipo skuli ya fikra (school of thought) inayoamini kuwa tatizo ni unyanyasaji uliokithiri na uovu wa utesaji uliopindukia. Kwao wao, utatuzi na suluhisho, ni kufikiria vurugu hizi kama vurugu za jinai, na kutaka uwajibishwaji wa wahusika (perpetrators) kwa upande mmoja; au kususia kwa upande wa pili. Lakini kwa yanayotokea Zanzibar khasa wakati wa chaguzi, je yanapaswa kuzingatiwa kama masuala ya kijinai kuliko kuwa ni ya kisiasa?

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba kususia na/au kutafuta suluhisho la kuwawajibisha tu wahusika katika Mahakama za jinai iwe za kitaifa au za kimataifa huenda yakawa ni matokeo ya kutofaulu kwa namna mbili: moja ni kiuchambuzi (analytical) na pili ni kisiasa (political). Kiuchambuzi ni kwamba, tunachanganya vurugu za kisiasa na vurugu za jina. Kisiasa, tunawekeza nguvu nyingi zaidi kutaka kususia au kwa kutaka wahusika wawajibishwe tu badala ya kuzingatia masuala yanayosababisha uhasama na vurugu zinazotokea. Kwa hivyo kususia au kutafuta utatuzi katika Mahakama tu kunaweza kukuza badala ya kupunguza vurugu katika jamii kwa vile wahusika (perpetrators) na waathirika (victims) bado wanalazimika kuendelea kuishi ndani ya jamii moja tena iliyoingiliana sana na inayotegemeana mno.

Muhimu zaidi ni kukubali ukweli kwamba migogoro ya Zanzibar ni mapinduzi kati ya matabaka (revolution between classes) ya wenyewe kwa wenyewe na sio mizozo au vita kati ya nchi na nchi (not wars between states). Kama hivyo ndivyo, basi somo la Maridhiano bila ya shaka yo yote limetufundisha kutafuta suluhisho na utatuzi ndani ya tatizo na sio nje yake na kwamba kunahitajika jitihada katika mageuzi ya ndani (internal reform), na sio kususia au tu kuingiliwa kutoka nje (external intervention).

Mazungumzo na Maridhiano ambayo wengi tutakubaliana kuwa yalisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhasama, mgogoro na vurugu Zanzibar yanatosha kuwa ni kielelezo cha kutupatia malighafi ya fikra kuwa dhana ya kususia na siasa tenganishi kwa mazingira ya Zanzibar sio tu hazina msaada; bali huenda zikawa ni zenye kuzidisha tatizo.

Kwa maoni yangu, njia mbadala ya utatuzi na suluhisho la maana zaidi ni ile ya mageuzi ya kisiasa (political reform) na hii haiwezi kupatikanwa bila ya kushirikiana na kuwa sehemu ndani ya serikali. Hii inatokana na ukweli kwamba upande mmoja kufikiria kuendelea kususia na/au kuazimia kuupeleka upande wa pili katika Mahakama za jinai itawia vigumu kuweza kupatikana nia ya mageuzi ya aina yo yote hata kwa kiwango kidogo na badala yake tutatoka katika vurugu, uhasama na mateso ya wakati wa uchaguzi na kuingia katika majanga ya visasi, kushamiri kwa vitendo vya ubaguzi na kukomoana wenyewe kwa wenyewe katika maisha ya kila siku.

Sote ni mashahidi kuwa siasa za kususia Zanzibar zishafanyika. Jaribio la kufungua kesi za uhalifu dhidi ya ukiukwaji wa haki za binaadamu pia limewahi kufanyika na bado tatizo lipo na ni lenye kujirudia. Suali la kujiuliza: kama Wazanzibari, tunawezaje kumaliza mzozo ambao haujaisha? Je! tunawashawishi vipi tunaotofautiana nao kuwa ni kwa masilahi yao pia kumaliza mzozo unaoendelea? Hakika, mgogoro wa Zanzibar wa zaidi ya nusu karne ni vigumu kupatiwa utatuzi kwa ima kususia au kutanguliza haki ya jinai kwa sababu watu ambao tunataka kuwapeleka katika Mahakama au kwasusia ni watu wale wale tunaowahitaji kumaliza mzozo.

Kwa mtazamo wangu, tufikirie njia mpya juu ya haki yenye mafanikio mawili. Kwanza, itakayotusaidia kutofautisha kati ya aina tofauti za haki ikiwa ni pamoja na haki ya jinai, haki ya kisiasa, na ile ya kijamii. Pili, itatusaidia kuweka kipaumbele katika haki ya kisiasa (political justice) ambayo ni mageuzi ya mfumo wa kisiasa (reform of the political system) dhidi ya hizo mbili (haki ya jinai na ya kijamii). Tofauti kati ya haki ya kisiasa na haki ya jinai ni mbili: Moja, haki ya kisiasa inalenga jamii yote kwa mapana yake; wakati haki ya jinai inalenga watu binafsi na wachache. Pili, lengo la haki ya jinai ni adhabu, wakati lengo la haki ya kisiasa ni mageuzi ya kisiasa (political reform) ya kimfumo na kiutendaji kuanzia ngazi za juu za uongozi wa serikali, taasisi na idara zake, hadi watendaji, nakadhalika.

Mapendekezo:
Kwa pande zote mbili (ile ya chama tawala na ile ya upinzani) kunahitajika nia njema, yenye shabaha ya dhati katika kujenga utengamano wa kijamii na kuamini kivitendo kwamba uongozi ni dhamana na upo kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi wote bila kujali itikadi za kisiasa wala za kimaeneo. Sambamba na hayo, kunahitajika kujenga utamaduni wa kuaminiana, kuachana na siasa za kubaguana kuwa hawa sio wazalendo zaidi ya hawa na kuona kwamba maridhiano na kuwa sehemu ya serikali sio lengo (destination) bali ni nyenzo muhimu na mwanzo mzuri wa safari ya Zanzibar tuitakayo.

Kwa hivyo, kama hatua ya mpito, wahusika wa pande zote wakubaliane kuweka safu ya kanuni za Kikatiba ambazo zitafafanua vigezo vya kuajiri kwa mujibu wa sifa na uwezo katika kugawana madaraka (power sharing) kati ya pande mbili kwa ngazi zote kuanzia juu hadi chini, kuachana na urasimu wa zamani na kuvifanyia maboresho vyombo vya ulinzi na usalama khasa vikosi vyote vitano kwa kuvifanya viwe vyombo huru, vinavyojitegemea na vyenye kutumikia na kuajiri raia wote kwa usawa na uadilifu.

Halikadhalika, kuanzisha mageuzi ya uchaguzi (elecroral reform) ambayo yatakuwa shirikishi na kuachana na utamaduni mbaya wa kuonana maadui na badala yake kuwa wapinzani wa kisiasa.

Aidha, kuwepo kwa muswada wa Haki (Bill of rights) utakaojumuishwa kama sehemu ya ukaguzi na mizani ya Kikatiba (constitutional checks and balance). Muswada huo wa Haki pia uingize suala la ujumuishwaji wa Wazanzibari wa asili zote katika kuajiriwa bila ubaguzi wa aina yo yote kama haki ya msingi ya binadamu. Ajira zitegemee sifa na uwezo wa mtu badala ya itikadi za kisiasa au eneo analotoka. Na hapa panahitaji mkazo wa aina yake. Ili Zanzibar ipige hatua za kimaendeleo iwe ya kielimu au kiuchumi, inahitajia mabadiliko makubwa ndani ya mfumo wa serikali, mashirika na jamii kwa ujumla ambapo watu watachaguliwa na kuhamishiwa katika nafasi za juu za ufaulu (position of success), mamlaka (power), na ushawishi (influence) kwa misingi ya uwezo, upeo, vigezo na sifa zao (meritocracy).

Wakati umefika wa pande zote za vyama kubadili misimamo. Lengo isiwe kutafuta ushindi kwa gharama ya maisha ya watu. Wala isiwe kususia kwa gharama ya kuendeleza tatizo na kukithirisha madhara kwa Wananchi — badala yake iwepo dhamira ya dhati ya mabadiliko ya sheria ambayo ingewajumuisha pande zote kuwa jamii ya kisiasa iliyofanyiwa marekebisho. Mafanikio katika hili ni kuwaleta wapinzani wa pande mbili pamoja na kukubaliana juu ya mageuzi ya kisiasa ambayo yataondoa ubaguzi wa kisheria na kisiasa na kufafanua tena uraia unaojumuisha. Wala shabaha isiwe kulipiza kisasi kwa waliokufa, lakini kuwapa walio hai nafasi ya pili.

Upatanisho unahitaji maono ya muda mrefu. Upatanisho ni njia ya maisha. Bado kuna machungu, lakini ndio safari ya uponyaji. Tuwatakie ahueni kamili na ya haraka majeruhi. Tuzitambue na kuzifariji familia zilizoathirika na tuwaombee hasanati waliokufa. LAKINI pia tuwape waliohai (kutoka pande zote) nafasi ya kurekebisha makosa kwa upande mmoja; na kuwanusuru wasiendelee kuteseka kwa upande wa pili.

Katika dunia ya leo ya siasa za vyama vingi uhusiano kati ya vyama ni muhimu, lakini uhusiano na utengamano kati ya watu ndio msingi halisi wa demokrasia, diplomasia, uongozi makini na ustawi mwema. Uhasama, dhulma na chuki hazilingani na haki; na hazielekezi kwenye uadilifu wala njia ya amani; na kwa hivyo, hatupaswi kuruhusu cho chote kusimama kati ya watu wa Zanzibar na mustakabal wa upatanisho na matumaini kwani Zanzibar itastafiid zaidi kupitia ushirikiano kuliko "ushindi" na itapata zaidi kutoka kwa ushirikiano kuliko "kususia".

Matarajio na athari ya mabadiliko haya yanaweza kuwa na msaada mkubwa katika kutatua matatizo yetu ya muda mrefu kwa ufanisi zaidi. Wakati tunatazama nyuma kwa yaliyopita, kazi yetu iwe kutafuta usawa na mizani kati ya yazamani na ya siku zijazo (balance between the past and the future) kwa upande mmoja; na kurekebisha kasoro za zamani na upatanisho wa siku zijazo (redress for the past and reconciliation for the future) kwa upande wa pili; kwani hatuwezi kamwe kufikiria mawazo ya kwenda mbele kwenye mema na mafanikio kama jamii moja ikiwa tutaendelea kuishi kwa mabaya ya zamani yaliyopita.

Zanzibar ni Nchi yetu sote, watu wa mirengo tofauti. Na ni ukweli usiofichika kwamba Zanzibar ina utajiri mkubwa wa mchanganyiko wa makabila na asili za watu na kwa hivyo Wazanzibari tutakuwa na nguvu na sauti licha ya udogo wa nchi yetu ikiwa tutakuwa na mfumo shirikishi badala ya tenganishi na kwamba tunaweza kuyafikia kwa UMOJA wetu mengi ambayo hatukuweza kuyafikia kwa kugawanyika kwetu.

Tukiwa na busara, tutawajengea watoto wetu Nchi nzuri yenye utengamano wa kijamii, maendeleo ya kielimu na kiuchumi na kuweza kuzitumia vyema raslimali zilizopo na fursa nyenginezo kwa maslahi mapana yetu sote.

Mungu Ibariki Zanzibar.

Mungu Wabariki Wazanzibari WOTE.

Aamiin.
 
Maneno yako ni ya kizalendo na yenye kuonesha mapenzi makubwa kwa nchi yako pendwa Zanzibar.

Lakini Masikini ,Zanzibar ilivamiwa na watu wenye nia ovu tangu zamani, na wanaendelea kusimamia mfumowao huo ovu kwa watu wa nchi hii.

bali hata kupindisha Historia na kujidai eti nchi hii wao ndio wenyewe na ndio waliostahiki kuitawala.

IMG-20190704-WA0001.jpg IMG-20190704-WA0003.jpg IMG-20190704-WA0005.jpg

Nakala hizi tatu zitakupa kiini cha ubaya na wanaousimamia . Kuna watu Hapa Zanzibar wanaaminishwa kuwa wao ndio wenye nchi hii wengine wote ni wageni na hawastahiki kutawala au hata kuwa na sauti,bali kuwa ni halali kwao tuu wakiaminishwa kuwa ''zanzibar ni sehemu ya Tanganyika'' na kwa hiyo ni lazima itawaliwe na watu wenye ASILI YA TANGANYIKA.

Mzizi huu wa fitina unahitaji suluhu,lakini si ya kidiplomasia tuu ,hata nguvu ya kidola itumike kuuzima ubaya wa aina hii. Bahati mbaya zaidi ni kuwa Huenda ikawa Mfumo huu unasimamiwa na watu werevu na wenye Nguvu za kidola.

Sikushangaa kumsikia ,Lukuvi wakati wa mchakato wa katiba mpya kusema kuwa Hatuwezi kuiacha Zanzibar ijtawale, na pia kumsikia Samul Sita aliposema Hawako tayari kuruhusu Uraia wa Nchi Mbili kwa kuwa Kuna wazanzibari wengi wako nje ya nchi, wao watakuwa wafaidika wakubwa wa fursa hii na wanaweza Kuja kuipindua tena Zanzibar na Kuirudisha mikononi mwa Waliopinduliwa.

Yamkini Fitna hizi ndizo zinazoleta uhasama wa kumwagwa damu za watu wasio na hatia. Ukweli ni kwamba
SUK ni mwiba kwa watu hawa ambao wamo ndani ya CCM na wameihodhi, na kimsingi wakipata mwanya humimina kikombe cha fitina kwa Mkuu wa nchi ili azidi kutegemea dhana yao potofu kuwa wapinzani ni Maadui wa Zanzibar na wao ndio wanaoipenda na kuitakia maslahi nchi hii ilhali wengi wao wanaasili ya akina Lukuvi.

Niishie hapo
 
Back
Top Bottom