Jaji Werema adaiwa kumtishia kifo Kafulila bungeni Dodoma

Nicholaus Kilunga

JF-Expert Member
Feb 15, 2014
1,188
567
Mwanasheria mkuu wa serikali jaji Fredrick Werema ametuhumiwa kumtishia kifo mbunge wa Kigoma Kusini mh David Kafulila,Imedaiwa kuwa jaji Werema alimtolea maneno hayo ya vitisho mh Kafulila jana asubuhi kwenye viunga vya bunge mjini Dodoma baada ya bunge kuahirishwa.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari hii,mh Werema alimtolea maneno hayo ya kitisho mbele ya mwenyekiti wa Bunge Mussa Hassan Zungu,mwandishi wa habari mmoja alietajwa kwa jina moja la Butare,akiwa na waandishi wa habari wenzake ambao hawakutajwa majina yao ,wakiambatana na mpiga picha ambaye pia ametajwa kwa jina la moja la Edwin na baadhi ya wabunge kadhaa waliokuwa wanapita,mh Werema amanukuliwa akimwambia mh kafulila kwamba "I will take your head,unless you apologize"ikimaanisha atamkata kichwa iwapo hatamwomba msamaha,

Kufuatia sakata hilo mh Kafulila amemthibitishia ukweli wa madai hayo mwandishi wa Bloghii ya " http://nicholauskilunga.blogspot.com/" na kwamba tayari ameshachukua hatua kwa kuiandikia barua ya madai ya kutishiwa maisha ofisi ya spika wa bunge,huku nakala ya barua hiyo akiipeleka kwa mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Mangu na nakala nyingine ameipeleka kwa kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma(RPC Dodoma)mh Kafulila aliendelea kuongea na mwandishi wa habari hii akisema"ni kweli nimetishiwa maisha na mwanasheria mkuu wa serikali leo asubuhi kwenye viunga vya bunge,na nimekwisha chukua hatua tayari,lakini watanzania wakumbuke kwamba nilipokuwa nikichangia hoja ya ufisadi huu wa Escrow wakati wa bajeti ya wizara ya nishati,nilisema,hata kifo cha Mgimwa kilipaswa kuchunguzwa, kwasababu aliugua na kufariki kipindi ambacho kulikuwa na pressure kubwa ya kuzitoa pesa hizi za Escrow na hivyo kuna mashaka sana kuhusu kifo cha waziri huyo hasa ikizingatiwa makosa yaliyofanywa na Hazina na BOT kwa kushirikiana na wizara ya nishati na madini na jaji Werema alihakikisha hizo Bilioni 200 zinatolewa"alimaliza kuongea mh Kafulila.

Mbunge Kafulila ambaye pia ni mbunge Kigoma kusini kupitia chama cha NCCR na waziri kivuli wa wizara ya Viwanda na Biashara,aliendelea kumweleza mwandishi wa habari hii kwamba jaji Werema anajua kila kitu kilichotokea kwenye mchakato huo,anasema jaji Werema ndiye aliyetoa ushauri wa kisheria na kuelekeza bank kuu kuruhusu utolewaji wa fedha hiyo na aliruhusu hayo akiwa kama mwansheria wa mkuu wa serikali,na hatua yake yake hiyo ya kuruhusu utolewaji wa fedha hiyo kufuatia wizara ya nishati na madini kuwa tayari ilikwisha saini makubaliano na kampuni aliyoiita ya kitapeli inayomilikiwa na mtu alieitwa na mh Kafulila kuwa Singasinga ijulikanayo kama PAP iliyopewa fedha hizo kama mmiliki halali wa wa fedha hizo wakti haikuwa na sifa hiyo.

Nae mh Werema alipopigiwa simu na mwandishi wetu na kutakiwa kuthibitisha ukweli wa taarifa hizi za madai ya kutishia kumwua mh Kafulila alijibu"Hilo jambo si jambo la kitaifa,tafadharini sana msilifanye kuwa la kitaifa,mimi nilifikiri umenipigia kwa ajili ya kuzungumzia mambo ya kitaifa,kwa hili sina majibu naomba uniache nipumzike"alimaliza kuongea mh Werema huku akikwepa swali la msingi alilokuwa ameulizwa na mwandishi hii,

Sakata hili liliibuka jana bungeni mjini Dodoma,kufuatia mwongozo uliokuwa umeomba na mh Kafulila kuhusiana na majibu ya waziri wa nishati na madini aliedai kwamba alilidanganya Bunge na kusema uwongo ndani ya bunge tena mbele ya waziri mkuu,pale alipokuwa akijibu hoja juu ya madai ya ufisadi kwenye akaunti ya Escrow na kusema kwamba fedha hizo zilitolewa baada ya kesi kuamuliwa,ndipo alipotaka muongozo katika suala hilo hali iliyomlazimisha mwanasheria wa serikali jaji Werema kuingilia kati na kujibu swala hilo kwa kusema taratibu zote zilifuatwa wakati wa utolewaji wa fedha hizo, na ni kweli kesi ilikuwa imekwisha amuliwa,wakati akiendela kuongea mh Werema alienda mbali zaidi kwa kulitolea mfano wa kabila lake kwamba wanamsemo mmoja kwamba Tumbili hana maamuzi ndani ya msitu hali iliyotafsiriwa kumlenga Kafulila ambaye nae alimjibu kwamba ni mwizi hali iliyompandisha hasira zaidi jaji Werema huku akivuka mstari na kutaka kwenda kumpiga mh Kafulila kabla wabunge kumzuia jaji Werema na baadae kutolewa nje na askari wa bunge.


Mheshimiwa Kafulila alisema kinachofanywa na serikali ni sawa na kile kilichotokea mwanzoni mwa miaka ya 2006 na 2007 pale katibu mkuu wa CHADEMA na aliekuwa mbunge wa jimbo la Karatu Dr Wilbroad Slaa pale alipoibua ufisadi mkubwa kwenye akaunti ya madeni ya nje yaani EPA,alisema mwanzoni mwa sakata lile serikali na chama cha mapinduzi walilipinga sana na kusema madai yale yalikuwa ya uzushi mtupu na kwamba hayana ukweli wowote,lakini baadae yalibainika kuwa madai ya kweli,

Tulijaribui kuwasiliana na ofisi ya spika kuthibitisha madai ya kupokea barua hiyo,lakini ilishindikana mpaka tunakwenda mtamboni,lakini tunawaahidi wasomaji wetu wapendwa kwamba kesho tutaweka hapa nakala ya barua hiyo,hivyo endelea kutusoma na kutufuatilia.

====================

mawaziri.jpg

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kushoto) akizuliwa na Mawaziri na Manaibu Waziri kutomfuata
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila baada ya kupandwa na hasira kufuatia mbunge huyo kumtuhumu
kwa kumuita mwizi kwenye ukumbi wa Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi


Kama siyo kuzuiwa na mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema jana angezua tafrani bungeni kutokana na kitendo chake cha kutaka kumpiga Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila. Sakata hilo lilitokea jana asubuhi baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kuahirisha kikao cha Bunge hadi jioni, ikiwa ni muda mfupi baada ya Werema na Kafulila kurushiana maneno bungeni.

Jaji Werema alichukia baada ya Kafulila kumwita mwizi, akijibu mapigo baada ya mbunge huyo kuitwa tumbili na mwanasheria huyo.


Mawaziri wamzuri Werema kumpiga Kafulina na wakamsindikiza nje ya ukumbi
Waliomzuia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Abdulla Juma Saadallah. Mawaziri hao walimsindikiza Werema hadi nje ya Ukumbi wa Bunge na kutoweka.


Ilivyokuwa
Hali ilianza kuchafuka wakati Jaji Werema alipokuwa akijibu mwongozo uliombwa na Kafulila kuhusu fedha za akaunti ya Escrow. Katika mwongozo huo, Kafulila alisema Wizara ya Nishati na Madini kupitia Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo alizungumza uongo mara mbili bungeni kuhusiana na fedha za akaunti ya Escrow. "Alisema uongo mbele ya Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maeneo mawili, kwamba uamuzi wa kutoa fedha za Escrow kwa IPTL ulikuwa wa Mahakama na Serikali isingeweza kwenda kinyume..." alisema. Alisema katika hukumu hiyo ya Septemba mwaka jana, hakuna mstari hata mmoja unaosema kuwa fedha za Escrow wapewe Kampuni ya IPTL.


"Profesa Muhongo aliliambia Bunge kuwa Serikali ililipa fedha hizo ili kuondokana na kesi hiyo lakini ninazo nyaraka za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuteua kampuni mbili za uwakili kwenda kuiwakilisha katika kesi nchini Uingereza," alisema Kafulila. Alisema kwamba aliomba mwongozo sababu huo umekuwa mwendelezo wa kuzungumza uongo bungeni... "Naibu Waziri (Nishati na Madini - Stephen Masele), alizungumza uongo bungeni tukaambiwa kuwa wamekutana katika sherehe za kuzaliwa yakaisha, haiwezekani, Bunge ni sehemu ya kuisimamia Serikali. "Haiwezekani Bunge ling'olewe meno liwe ni chombo ambacho mtu anaweza kuzungumza uongo bila kuchukuliwa hatua kwenye jambo hili ambalo linaligharimu taifa mabilioni ya fedha."

Baada ya madai hayo, Jaji Werema alisimama na kusema: "Bunge hili liliamua mambo mawili, kwanza kulikuwa suala la rushwa na CAG apewe kazi ya kuchunguza na kutoa taarifa bungeni. La pili kuna watu walitoa vipeperushi humu bungeni, miongoni mwao ni huyu anayetoa maneno machafu (Kafulila)," alisema Werema na kumfanya John Mnyika (Mbunge wa Ubungo-Chadema), kuomba mwongozo uliokataliwa na Mwenyekiti Zungu.

Hata hivyo, Mnyika na Kafulila waliendelea kuomba mwongozo, lakini Zungu aliwataka wamsikilize Jaji Werema kwa sababu naye alimsikiliza Kafulila. Werema aliendelea: "Suala la Escrow ni suala linalotokana na wanahisa wawili ambao ni IPTL na Mechmar… Pesa ya Serikali haikai kwenye Escrow."

Hata hivyo, alikatishwa na kelele za Mnyika ambaye alitaka mwenyekiti kumpa nafasi ya kutoa taarifa. "Sasa kama unataka kuleta mambo ya nje ndani ya Bunge ningojee pale nje," Jaji Werema alisema wakati wabunge hao walipokuwa waking'ang'ania kutoa taarifa. Alisema ugomvi huo ulitokana na wanahisa wawili hao kila mmoja akitaka IPTL ifilisiwe ili waachane. Alisema Serikali iliingia katika mgogoro huo kwa sababu ya mikataba ya udhamini na kwamba wakati wanagombana iliamua kufungua akaunti ya Escrow.

Hata hivyo, kuliibuka maneno tena kutoka upande wa Kafulila na Jaji Werema alitaka kusikilizwa hata kama yeye ni mtuhumiwa katika suala hilo. "… Wanyankole wanasema tumbili hawezi kuamua masuala ya misituni… sikiliza tumbili, sikiliza ‘please' (tafadhali)," alisema Werema. Sentensi hiyo iliamsha kelele kutoka upinzani na Kafulila alisikika akimwita Werema mwizi.

Zungu azuia vurumai
Hata hivyo, Zungu alizuia vurumai hizo kwa kumtaka Jaji Werema kukaa na kisha kuwataka wabunge hao wawili kupeleka ushahidi wao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru). Mara tu baada ya Zungu kuahirisha Bunge, Jaji Werema alisimama na kumfuata Kafulila lakini kabla hajamfikia, mawaziri hao walimzuia na kumsindikiza hadi nje.


Baadaye, Kafulila na Mnyika waliitisha mkutano na waandishi wakitaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda afute uongo huo bungeni ndani ya siku mbili na akishindwa, watakusanya sahihi za wabunge kumuondoa katika nafasi hiyo.

Alipohojiwa kama ni vyema kwa Wassira alisema walimsihi Werema kuachana na Kafulila na kuendelea na shughuli zake.



kafulila-june28-2014(1).jpg


Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (Kushoto), akieleza tuhuma za kutishiwa kukatwa shingo na Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema , huku spika wa bunge Anne Makinda akionyesha kutuliza munkari.



Spika wa Bunge, Anne Makinda amemzuia Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) kuendeleza sakata la tishio la kukatwa kichwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema.

Makinda, amefikia hatua hiyo jana baada ya Kafulila, kuomba mwongozo wa Spika kuhusu hatma ya shutuma za ufisadi unaoihusu kampuni ya Escrow, kufuatia hatua yake (Kafulila) na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuwasilisha ushahidi wao bungeni.

Wakati akiomba mwongozo huo, Kafulila alikumbushia namna alivyonusurika kutwangwa makonde na Werema, kisha tisho la Mwanasheria Mkuu huyo kutaka kuondoka na kichwa chake, ikiwa Kafulila hatamuomba radhi.

Pia, Kafulila alitumia fursa hiyo kuujulisha umma hususan wapiga kura wake, kwamba ikiwa jambo baya lolote litamtokea, mshukiwa wa kwanza anapaswa kuwa Werema.

Tayari Kafulila amewasilisha malalamiko yake kwa Spika Makinda na nakala zake kusambazwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu na Werema mwenyewe.
Pia amewasilisha nakala hiyo kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

Hata hivyo, kabla ya kutoa mwongozo, Makinda, alimlaumu Kafulila kwa kuwasilisha barua hiyo kwake, kisha taarifa zake kuchapishwa na kutangazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari jana.

Kuhusu hatma ya ushahidi wake (Kafulila) na Mnyika, Makinda alisema vielelezo hivyo vimefikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Makinda akatoa rai kwa wengine wenye vielelezo kama hivyo kuviwasilisha Takukuru na kwamba mjadala huo haupaswi kuendelezwa bungeni.

Kuhusu vitisho vya Werema kwa Kafulila, Makinda alisema Mbunge huyo wa Kigoma Kusini ndiye aliyeanza ‘kumchokoza' Werema na Mwanasheria Mkuu ‘akachokozeka'.
"Kafulila wewe uli-mprovoke (ulimkasirisha) na mwenzako ‘akaprovokika', hivyo kila mtu alikuwa na jazba zake," alisema.

Makinda, alisema kwa vile ofisi yake imeshapokea barua ya Kafulila kuhusu suala hilo, anapaswa kuwa na subira kwa vile lipo mahali panapohusika, kisha akahoji, "sasa unataka majibu yatolewe hapa bungeni, kama una vielelezo zaidi peleka panapohusika."

Jumatano iliyopita, Werema alitaka kumfuata Kafulila kwa kile kilichoaminika kutaka kumpiga, lakini akazuiwa na baadhi ya wabunge.

Habari zaidi zilieleza kuwa, juzi, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Azzan Zungu, alitaka kuwapatanisha lakini hakufanikiwa baada ya pande zote kutokubaliana.

Mzozo kati ya wawili hao ulianza baada ya Kafulila, kutaka ufafanuzi kuhusu Sh. bilioni 200 ‘zilizochotwa' katika akaunti ya Escrow zikihusishwa na njama za kifisadi.

Habari hii imeandikwa na Isaac Kijoti, Dodoma na Mashaka Mgeta, Dar es Salaam.


SOURCE: NIPASHE

 
nimemdharau sana werema na namtabiria mabaya sana , wito wangu kwa watz tuhakikishe mh kafulila analindwa , ukweli ni kwamba HAKUNA DHULUMA YOYOTE ILIYOWAHI KUISHINDA HAKI MAHALI POPOTE DUNIANI .
 
nimemdharau sana werema na namtabiria mabaya sana , wito wangu kwa watz tuhakikishe mh kafulila analindwa , ukweli ni kwamba HAKUNA DHULUMA YOYOTE ILIYOWAHI KUISHINDA HAKI MAHALI POPOTE DUNIANI .

Nimejiuliza sana swali hili,inakuwaje mtu anayeijua sheria vizuri anaongea vitu ambavyo anajua ni kinyume cha sheria?ama ndo anakamilisha ule usemi kwamba sheria zimewekwa ili zivunjwe?
 
Werema ni

1. Mwanasheria
2. Judge
3. Mwanasheria mkuu wa serikali
4. Mtu mzima
5. Kiongozi

Ametaka kumpiga mbunge Kafulila. Sasa najiuliza, iwapo mtu mwenye sifa zote hapo juu ametaka kumpiga mtu tena hadharani, je tuna viongozi kweli?
 
toa kinyesi chako hapa. hivi unataka hata watu wasitaniane? kwa akili ya kawaida tu kwa nini amuue? ujuwaji mwingi nao ni mzigo. unaonekana much know sana dogo. nakutabiria mwisho mbaya.
 
Kwa uteuzi wa Kikwete kuokoteza watu bila kufanyia vetting utaumiza kichwa chako kuwafikiria hao viongozi. Ukistaajabu ya Werema utayaona ya Sospeter Muhongo. Subiri tu muda wao uishe aje rais mwingine na watu wake.
 
toa kinyesi chako hapa. hivi unataka hata watu wasitaniane? kwa akili ya kawaida tu kwa nini amuue? ujuwaji mwingi nao ni mzigo. unaonekana much know sana dogo. nakutabiria mwisho mbaya.

Acheni vitisho nyie mburula!
 
Nadhani ni muda muafaka Kwa AG kujiuzulu kwani tayari amekiuka maadili ya utumishi wa umma.
 
Werema ni

1. Mwanasheria
2. Judge
3. Mwanasheria mkuu wa serikali
4. Mtu mzima
5. Kiongozi

Ametaka kumpiga mbunge Kafulila. Sasa najiuliza, iwapo mtu mwenye sifa zote hapo juu ametaka kumpiga mtu tena hadharani, je tuna viongozi kweli?

Hekima ya mtu huonekana mahali penye tatizo au pale alipochokonolewa! Kwa muktadha huu hakuna hekima pale hata robo kikombe
 
Back
Top Bottom