Jaji Kiongozi, Dr. Eliezer Mbuki Feleshi afanya ziara mkoa wa Mbeya

Ally YK

Member
Feb 25, 2015
26
89
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mahakama Kanda ya Mbeya huku akitoa wito kwa Uongozi wa Kanda hiyo kutoruhusu mlundikano wa mashauri.

Akizungumza na Viongozi na baadhi ya Maafisa wa Mahakama katika kikao chake cha majumuisho ya ziara yake kilichofanyika Aprili 10, 2019 katika Ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu-Mbeya, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliwaelekeza Viongozi hao kuainisha mashauri yote yenye umri wa miaka mine (4) lengo likiwa ni kutoruhusu mashauri hayo kuvuka miaka mitano (5).

“Nimeridhika na suala la usikilizwaji na umalizwaji wa mashauri katika Kanda hii kupitia taarifa mbalimbali zilizotolewa, hivyo ni rai yangu kuwa mashauri yote yaliyo na umri kuanzia miaka mitatu na minne (4) yaainishwe na kufanyiwa kazi kabla hayajafikia umri wa miaka mitano (5) Mahakamani,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.

Mhe. Jaji Kiongozi alisema kuwa lengo la Mahakama ya Tanzania ni kutokuwa na mashauri yanayokaa kwa muda mrefu kuanzia miaka mitano (5) na kuendelea huku akisema kuwa nia iliyopo mashauri yasikae zaidi ya miaka miwili (2) Mahakamani kabla ya kumalizika.

Mbali na agizo hilo, Mhe. Jaji Kiongozi aliwasisitiza Wahe. Majaji, Wasajili, pamoja na Mahakimu kuheshimu nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Viongozi wa Mhimili huo kwa ustawi bora wa uondoshwaji wa mashauri.

Aidha; Mhe. Jaji Kiongozi alionyesha kufurahishwa kwake na juhudi za Majaji na Mahakimu wanaochapa nakala zao za hukumu na kuwapatia Wadaawa kwa wakati.

“Katika Kanda hii nimefurahishwa na jitihada za baadhi ya Mahakimu wanaochapa nakala zao za hukumu, hivyo nitoe wito kwa Majaji na Mahakimu ambao hawajaanza kuiga mfano huu ili kutopelekea ucheleweshaji wa upatikanaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliagiza Mahakama katika Kanda hiyo kuhamasisha wanafunzi katika shule za Sekondari kusoma masomo ya sheria ili kuwajengea upendo wa fani ya uanasheria/uhakimu.

Kabla ya kuhitimisha rasmi ziara yake katika Kanda hiyo, Mhe. Jaji Kiongozi alitembelea na kupata taarifa za utendaji za Mahakama ya Watoto, Mahakama ya Mwanzo Uyole, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya Mbeya ambapo sehemu zote Mhe. Jaji Kiongozi alionyesha kuridhishwa na kasi ya uondoshaji wa mashauri na kusisitiza kuendelea na kasi hiyo.

Mhe. Jaji Kiongozi amefanya ziara ya kikazi katika Mahakama Kanda ya Iringa na Mbeya lengo likiwa ni kujua hali ya maendeleo ya utekelezaji wa maboresho ya huduma mbalimbali za Mahakama na vilevile kuwakumbusha Watumishi wa Mhimili huu kuendelea kutekeleza jukumu la msingi la utoaji haki nchini kwa ubora wa hali ya juu kwa manufaa ya wananchi.

IMG_7027.JPG
IMG_7028.JPG
IMG_7108%20(1).JPG
IMG_7043.JPG
IMG_7055.JPG
IMG_7123.JPG
IMG_6953.JPG


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom