kesho inaweza kuwa siku ya maafa makubwa arusha!
WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikiwa na furaha ya ushindi wa ubunge kilioupata katika jimbo la Arumeru Mashariki, furaha hiyo huenda ikaingia dosari endapo Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Arusha, itamwona na hatia mbunge wake, Godbless Lema.
Lema ambaye ni mmoja kati ya wabunge maarufu wa CHADEMA, anakabiliwa na kesi ya kupinga matokeo yake ya ubunge, iliyofunguliwa na baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika majumuisho ya utetezi wake, Lema ameomba shauri hilo litupiliwe mbali kwani madai dhidi yake ni uongo ndiyo maana Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowasa na Dk. Batilda Burian, waliodaiwa kukashfiwa hawakufika mahakamini kutoa ushahidi kukanusha au kuthibitisha maneno yaliyotamkwa dhidi yao.
Kupitia kwa wakili wake, Method Kimomogoro, Lema alidai iwapo kweli angetamka maneno ya kashfa, matusi na udhalilishaji dhidi ya Dk. Burian angefika mahakamani kama mlalamikaji au shahidi lakini hakufanya hivyo licha ya kupewa taarifa na walalamikaji katika shauri hilo baada ya kubaini ukweli kuwa hakuwahi kutamka maneno hayo.
"Wadai na mashahidi wao wameieleza mahakama kuwa miongoni mwa maneno yanayodaiwa kutamkwa na Lema ni uhusiano wa kingono kati ya Mheshimiwa Lowasa na Dk. Burian, lakini siyo Lowasa wala Dk. Burian aliyefika hapa mahakamani kuthibitisha au kukanusha uhusiano wao nje ya ndoa kati yao," alidai Wakili Kimomogoro.
Alidai hata mume wa Dk. Burian ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya akiwakilisha nchi za Pembe ya Afrika naye hakufika mahakamani kukanusha au kuthibitisha iwapo mtoto ambaye Lema anadaiwa kusema alizaliwa nje ya ndoa ni wa kwake au kueleza iwapo mimba aliyodaiwa kuwa nayo waziri huyo wa zamani ilikuwa yake.
Katika hati yake ya hoja za majumuisho, Wakili Kimomogoro alidai kitendo cha wote waliotajwa au kuguswa na ushahidi wa wadai na mashahidi wao kutofika mahakamani kutoa ushahidi kuthibitisha au kukanusha kinadhihirisha maneno yanayodaiwa kusemwa na mteja wake hayakuwahi kutamkwa na kuiomba mahakama kutupilia mbali shauri hilo.
Pamoja na kutupa shauri hilo, Kimomogoro pia aliiomba mahakama kuwaamuru wadai kulipa gharama zote ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kufungua kesi za uongo.
Wadai katika shauri hilo namba 13/2010 ni Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo ambao wanawakilishwa na mawakili, Alute Mughwai na Modest Akida wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mdaiwa wa pili akiwakilishwa na mawakili, Timon Vitalis, na Juma Masanja.
Kimomogoro alidai kuwa hata ushahidi wa mashahidi wote 14 wa walalamikaji umejikita katika maelezo ya mdomo bila kuongezewa uzito kwa vielelezo ikiwemo maandishi, magazeti au CD zenye kumwonyesha Lema akitoa kauli anazodaiwa kutoa kwenye mikutano yake ya kampeni ambayo wadai walieleza wanazo katika hati yao ya madai iliyoko mahakamani.
Alidai licha ya kushindwa kuwasilisha vielelezo kuthibitisha madai yao, wadai pamoja na mashahidi wao 14 waliofika mahakamani wametofautiana katika ushahidi wao kwenye mambo ya msingi yanayohusu tukio au jambo moja.
Alitoa mfano wa kutofautiana kwa shahidi wa tatu, Happy Kivuyo aliyedai kuvuliwa cheo cha katibu mwenezi wa CCM, kata ya Sokon I mwaka 2010 wakati shahidi wa nne, Salum Mpamba, aliyekuwa katibu wa CCM wilaya ya Arusha kipindi cha uchaguzi mkuu aliieleza mahakama kuwa alipohamishiwa wilaya ya Kyela Machi mwaka jana alimwacha Kivuyo akishikilia wadhifa huo.
Alidai ushahidi wa kimazingira unaonyesha kuwa Lema asingeweza kupuuza uwezo wa wanawake kiuongozi kwa sababu chama chake cha CHADEMA kilisimamisha wanawake wengi kugombea ubunge na udiwani sehemu mbalimbali nchini huku timu yake ya kampeni ikiwa na wanawake ambao alikuwa akiwanadi na kuwaombea kura.
"Wadai na mashahidi wao wameithibitishia mahakama katika ushahidi wao kuwa Lema alikuwa akiongozana na wagombea udiwani wanawake kupitia chama chake kwenye mikutano yake ya kampeni, hivyo isingekuwa rahisi yeye kusema Dk. Burian asichaguliwe kwa sababu ni mwanamke halafu papo hapo awaombee kura za udiwani wanawake wa chama chake," alidai Kimomogoro.
Kuhusu ubaguzi wa kidini na kikabila, wakili huyo alidai isingekuwa rahisi maneno ya kibaguzi kiimani na kikabila kutolewa na mgombea kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na watu wa dini na makabila mbalimbali.
Kwa upande wake wakili wa walalamikaji, Mughwai alipinga hoja ya kuwaleta Kimomogoro ya kushindwa kuwaleta mahakamani hapo Dk. Burian na Lowassa kwa madai kuwa Lema ndiye alipaswa kuwaleta mahakamani hapo kwani ndiye aliyeibua suala hilo.
Naye wakili wa serikali, Timon Vitalis, iliiomba mahakama kutupilia mbali madai hayo akidai kisheria mgombea kuelezea tofauti yake ya ukaazi na mgombea mwenzake hakuwezi kutafsiriwa kama kashfa, matusi wala udhalilishaji kwa sababu hiyo ni moja kati ya sifa anayotakiwa kuwa nayo kiongozi anayeomba kuongoza watu.
Vitalis alidai kuzuia wagombea kujinadai kwa tofauti zao kimakaazi ni sawa na kuwanyima kutaja sifa zao za kuchaguliwa na kusisitiza kuwa hata sheria ya uchaguzi haitaji kauli kuhusu ukaazi kama moja ya makosa kwenye kampeni za uchaguzi.
Akihitimisha hoja zake, wakili Kimomogoro anadai mlalamikaji wa kwanza, Mussa Mkanga, ndiye aliyeamua kutunga madai ya uongo dhidi ya Lema na kuwashirikisha wenzake kwa nia ya kulipa kisasi cha mbunge huyo kusababisha ajiuzulu nafasi yake ya udiwani kata ya Sombetini mwaka 2006.
Jaji Rwakibarila ambaye alijizolea sifa kutokana na aina yake ya uendeshaji wa shauri hilo anatarajiwa kusoma hukumu yake kesho kuanzia majira ya saa 3 asubuhi ambapo wasikilizaji wametakiwa kuingia kwenye chumba cha mahakama saa 2:30 asubuhi.
Source: Tanzania Daima
Arusha mjini tunasema: Wao wana pesa sisi tuna Mungu usiogope tutashindatulianza na mungu tutamaliza na mungu..
Ni kweli mkuu ni mahakama kuu kanda ya kazikazini....Nadhani hapo kwenye red Mahakama husika ni Mahakama kuu.
Vuteni pumzi Magwanda, leo Lema anapigwa chini.
Ni nani kakwambia uchaguzi ukirudiwa CCM itashinda? Hata bila Lema CHADEMA itapeta tuu
Hakuna kitu, Kesho Lema pigwa chiniiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii, SUBIRINI MTAONA
namwombea lema avuke mashetani yote yanayomwandama
Hakuna kitu, Kesho Lema pigwa chiniiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii, SUBIRINI MTAONA