Ijue historia ya eneo la Kisutu Dar—1

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
Na Alhaji Abdallah Tambaza

MKOANI Dar es Salaam, kwenye Wilaya ya Ilala kuna eneo linaloitwa Kisutu, ambalo historia yake inaanzia karne ya 1800 hivi wakati wa Utawala wa Kiarabu wa Seyyid Majid.

Seyyid Majid, aliyekuwa akitawala Dola ya Kiislamu akitokea Zanzibar, wakati huo wa ‘Ottoman Empire’, alijenga makazi yake pale Ikulu ya Magogoni (Kitongoji cha Mzizima), ili iwe kitovu cha kuenezea Uislamu kutokea hapo kuelekea maeneo mengine ya Mrima, Pwani na Bara hadi Kongo na Burundi.

Pamoja na Ikulu ile ya Magogoni, Seyyid Majid pia alijenga lile jumba la ‘Ocean Road Cancer Institute’ (ORCI) kwa sasa, ambalo mwanzoni lilikuwa ni Msikiti Mkubwa wa Ijumaa.

Wakoloni wa Kizungu walipokuja hapa kwetu baadaye, mahala hapo pakafanywa hospitali iliyojulikana kama ‘Ocean Road European Hospital’, iliyokuwa ikiwatibia Wazungu peke yao.

Ikulu ile ya Magogoni wakati huo, ilikuwa imezungukwa na misikiti mingine kama 40 hivi ambayo yote, katika Utawala wa Kijarumani, ilibadilishwa matumizi na kufanywa taasisi nyengine.

Misikiti mingine iliyobaki ikasambaratishwa na kutumiwa kwa shughuli nyengine, ukiwamo Msikiti mkubwa uliokuwa baharini pale Forodhani, jijini Dar es Salaam, ulipogeuzwa kutoka msikiti na kuwa Kanisa la Mtakatifu Joseph mpaka leo hivi.

Mwandishi Hussein Bashir Abdallah, katika kitabu chake alichokiita ‘Dola Kongwe ya Zanzibar, kutoka Omani hadi Kongo’, pamoja na mambo mengine anaandika:

“…Dar es Salaam ilifanywa ndio kituo cha kusafirishia ujumbe wa Uislamu na ustaarabu wake kwenda maendeo mbalimbali …ukiizunguka Ikulu ya Magogoni, Misikiti ilijengwa kutoa huduma mbalimbali ikiwemo Ibada na ‘llmu ya Dini’.

“Kulikuwa na Misikiti zaidi ya 40 iliyoizunguka Ikulu hiyo …ilijengwa kwenye ardhi aliyoitoa Sharif Attas na Jumbe Tambaza (machifu wa Kimashomvi), eneo hilo lilianzia Bustani ya Mnazi Mmoja karibu na Mnara wa Saa (Clock Tower) …na kuanzia Ferri Magogoni kwenda Daraja La Salender kutokezea Upanga lilikuwa ni Shamba la Jumbe Tambaza.” Angalia kitabu cha Bashir, Dola Kongwe ya Zanzibar, ukurasa 107.

Sasa, baada ya Wajerumani na Wamisionari wao kuwasambaratisha madiwani Sharif Attas na Jumbe Tambaza, mji huo uliokuwa na asili ya Magogoni wakauhamishia maeneo ya Kisutu, Dar es Salaam.

Makaburi ya kihistoria ya asili ya wakazi hao kule Magogoni, yapo ndani ya uzio wa majengo ya Wizara ya Utumishi mpaka leo, yakionyesha tarehe na wakati walipozikwa watu hao.Kwa namna hiyo, Kisutu ukawa ndio mji wa mwanzo wa wenyeji baada ya kuondoka kutoka Magogoni.

Kisutu hiyo, kwa mapana na marefu yake, ni eneo linaloanzia kwenye Jumba la Umoja wa Vijana wa CCM pale Barabara ya Morogoro na Lumumba, kwenda mbele mpaka kwenye Barabara ya Libya kwa upande wa magharibi; mahala ambapo siku za nyuma ilipokuwa stendi ya mabasi yaendayo Arusha na Moshi.

Mahala ambapo kwa sasa ndipo lilipojengwa jengo refu la ghorofa la Kitega Uchumi cha Vijana wa CCM (UVCCM), siku za nyuma, wakati wa ukoloni, kulikuwapo na nyumba nyingi za kuishi, mfano wake kama kota za serikali.

Kwenye nyumba hizo, zilizofikia idadi yake kama ishirini au thelathini hivi, walikuwa wakifikia watumishi wa serikali wa ngazi za juu, kutoka mikoani wanapokuja kikazi Dar es Salaam pamoja na watoto wa machifu wakati wakielekea masomoni Ulaya au kuja mjini kwa mikutano mbalimbali.

Nyumba hizo zilikuwa na wahudumu wa kupika vyakula (hasa vya Kizungu) na waangalizi wengine. Mahala hapo palitumika pia kuwafunza na kuwazoesha taratibu na mila za watawala (Wazungu), ikiwamo mafunzo ya kutumia visu na uma kwenye kula, ili wakifika Ulaya wasibabaike na kuonekana wajinga.

Mzee Baraka Msakara, alikuwa mmoja wa mababu zangu kwenye ukoo wetu wa Kimashomvi. Yeye alikuwa mfanyakazi wa mahala hapo akiwa kama mwangalizi mkuu mkazi (Resident Caretaker).

Nikiwa kijana mdogo kwenye miaka ile ya 50s kabla uhuru, mimi na ndugu zangu wadogo daima tulipenda kufika na kumsalimia Babu Mzee Baraka pale maskani kwake; bado ninakumbukumbu ya safari hizo, kwani kila tulipokuwa tunaoondoka kurudi nyumbani, Mzee Baraka alitujaza peremende mifukoni, pipi mikononi, keki midomoni na maputo ya kupuliza kwa wingi, tukawa tunakula njiani na vingine kuchezea tunapofika nyumbani.

Nyumbani kwetu hapakuwa mbali na mahala hapo. Ilikuwa ni Kisutu hiyohiyo, kwenye maeneo yale ambayo sasa kimejengwa Chuo cha Ufundi (DIT), Chuo cha Biashara (CBE); pamoja na Hosteli za Taasisi ya SIDO na zile za CBE na DIT.

Zamani hizo, sehemu hiyo ilisheheni nyumba za Kiswahili za miti na udongo na juu makuti ya minazi. Ni chache tu ya nyumba hizo ndizo zilizokuwa na umeme na huduma ya maji—maji ilikuwa ni ya kununua kwa ‘mzegazega’ (wachuuzi wa maji).

Eneo hilo la Kisutu lilijulikana kama Kisutu kwa Jamal Ismail; Muhindi aliyekuwa na biashara za aina nyingi yakiwamo maduka na mabasi ya kusafirisha abiria nje ya Dar es Salaam akisaidiana na wanawe.

Pamoja na Jamal Ismail, zilikuwapo biashara nyengine za maduka zikiendeshwa na wahindi, mabaniani na waarabu. Rhambai Patel, Jadu na Mohamed Abeid hawa pia walikuwa maarufu kwa maduka ya vyakula. Kisutu wakati huo, haikuwa na Mwafrika aliyemiliki biashara ya duka.

Kwa safari za kwenda kwenye miji kama Bagamoyo, Kibaha, Msata, Rufiji, Kisarawe na kwengineko, mabasi ya Jamal Ismail ndio yaliyokuwa tegemeo kwa wakazi wa Mzizima siku hizo na stendi kubwa ilikuwa ni pale Mwembetogwa (sasa Faya).

Babu yangu mzaa baba, Saleh bin Abdallah Tambaza, Zarara wa Shomvilali, alikuwa na shamba kubwa sana maeneo ya Upanga ambayo imepakana na eneo la Kisutu, wakishirikiana na kakake mkubwa Mzee Kidato bin Abdallah Tambaza.

Mwaka 1947 hivi, watawala wa Kiingereza waliamua kuwatoa maeneo hayo babu zangu, ili eneo hilo la Upanga yawe makazi ya Wahindi, raia wenye daraja la juu kuliko watu weusi. Ni ubaguzi wa kishenzi kabisa Wakoloni wale walitufanyia!

Kufuatia kadhia hiyo, Babu hakuwa na jinsi; alihamia shambani kwake Mabibo, lakini aliwanunulia wanawe ambao wakati huo walishafikia umri wa utu uzima, nyumba za kuishi pale Kisutu. Nyumba hizo mbili zilikuwa kwenye barabara moja iliyojulikana kama Wadigo Street.

Kwa hiyo nilipozaliwa mimi mwaka 1948, niliwakuta baba zangu wale wakiishi pamoja kwenye nyumba hizo wakiwa watumishi kwenye ofisi mbalimbali za serikali ya Kikoloni ya Kiingereza.

Eneo hilo la Kisutu lilikuwa na barabara mbili tu kubwa; moja ni hiyo Wadigo Street na nyengine ni Selous Street, ambayo ilikuwa imepakana na makaburi yale maarufu ya Kisutu.

Barabara hiyo Imeitwa Wadigo Street kwa sababu ni mtaa ambao wakazi wake wengi ni wa kabila la Kidigo; kabila ambalo wengi wa watu wake ndio waliokuwa wakiishi Kisutu pamoja na wenyeji Wamashomvi.

Makabila mengine kama Wachaga, Wapare, Wanyakyusa hawakuwapo siku hizo; si tu hapo Kisutu, lakini walikuwa ni wachache sana hapa mjini hata maeneo mengine. Wale waliokuwapo, basi walikuwa wakiishi kwenye kota za Serikali, maana wengi walikuja kufanya kazi za kiofisi serikalini.

Miongoni mwa wazee wa Kidigo waliokuwa wenyeji na maarufu pale Kisutu ni Mzee Salum Mboga, maarufu ‘Mdigo’. Huyu alikuwa mpigaji taarabu mashuhuri katika bendi ya Egyptian Musical Club, akipiga ala ya ‘violin’ kwa madaha sana.

Mzee Mdigo pia, alikuwa mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za Kihindi, akiimba kwa lafudhi ileile ya Kihindi; nyimbo za Latta Mangeshka, Raj Kappor na Ravi Shankar na nyenginezo—ilikuwa burudani tosha kumsikiliza Mzee Mdigo akiimba kihindi zama zile!

Wadigo wengine ambao walioa na kuoleana na wenyeji siku hizo ni pamoja na Mzee Mwinyibohari Kijongoo, Mzee Mwinyikombo na Mzee Zibe Kidasi Zibe, aliyekuwa na bendi yake— maarufu kama ‘beni bati’— iliyokuwa ikipiga kwenye sherehe za kusindikiza maharusi. Zibe Kidasi alikuwa mpiga tarumbeta asiye na mpinzani hapa mjini siku hizo.

Alhaji Mzee Mwinyikombo, yeye alikuwa ni mvuvi; mashuhuri sana kwa utengenezaji wa zana za uvuvi kama vile ngarawa, mashua, nyavu, majarife na makasia. Kazi hiyo ilimwezesha kumiliki nyumba zaidi ya tano maeneo ya Kariakoo, ikiwemo na moja ya ghorofa pale Upanga karibu na Faya.

Hali ya maisha ya Mzee Mwinyikombo wakati huo ilikuwa nzuri sana, hata akaweza kumudu kufanya safari ya kwenda kufanya Ibada ya Hijja, wakati huo ambao ilikuwa ni safari ngumu kwa watu wengi wa kipato cha chini— ilichukua takribani miezi mitatu na kugharimu pesa nyingi sana.

Selous Street, ni barabara ambayo Wahindi fulani kutoka nchi ya Ceylon walikuwa wakiishi hapo. Miongoni mwa Waceylon hao, ni vijana Abdul, Haji na Abdani. Hawa walikuja kuwa watu maarufu sana, si tu Kisutu peke yake, bali kote Dar es Salaam, kwani walikuwa mafundi wazuri sana wa kutengeneza mapikipiki (bodaboda) wakati huo.

Aidha, Abdani na nduguze, kwa kushirikiana na wakazi wengine wa Kisutu siku hizo, walianzisha timu ya Mpira wa Miguu iliyoitwa Bombay Football Club na wakawa na Bendi ya muziki wa Kihindi iliyokuwa ikiimba nyimbo za Kiswahili na Kihindi ikijulikana kama Bombay Musical Club.

Bombay Musical Club, ilikuja kubadilishwa jina na kuitwa Jamhuri Musical Band, pale nchi ilipojitawala ambapo sasa ilihamishia maskani yake Mtaa wa Aggrey na Kongo kule Kariakoo na hapo ikawa inapiga muziki wa taarabu na chakacha pia.

Barabara ya Selous, pia ndipo mahala alipokuwa akiishi mpigania uhuru mashuhuri wa nchi hii Mzee Haidar Mwinyimvua. Mzee Mwinyimvua, baba wa watoto kadhaa mashuhuri, akiwamo Imam Mkuu wa Masjid Mwinyikheir, Sheikh Ahmed Haidar Mwinyimvua, ambaye ni mmoja wa wanazuoni bobezi wa Dini ya Kiislamu hapa nchini.

Mzee Mwinyimvua, alikuwa ni Fundi Cherehani wa kushona kanzu za kiume na makoti, wakati huo hilo likiwa ndio vazi rasmi la wenyeji. Kwa kazi yake hiyo, aliweza kumiliki nyumba kadhaa maeneo mbalimbali hapa mjini, na hivyo kuweza kuwasomesha watoto wake kwa kiwango kizuri kabisa kutokana na kodi za nyumba hizo.

Aidha, Haidar Mwinyimvua pia, katika wakati fulani kwenye zile nyakati za kudai uhuru, alipata kuwa mwenyekiti wa baraza mashuhuri la wazee wa TANU hapa nchini.

Anakumbukwa zaidi kwa kule kuipenda nchi yake, pale alipoiuza moja ya nyumba zake na fedha akazipeleka kwenye harakati za ukombozi wa Tanganyika.

Mzee Haidar, ndiyo mfano mzuri wa namna ya watu walivyojitolea wakipigania nchi hii wakati huo—walitoa vyao vya thamani; walilaza watoto wao na njaa; ilimradi leo sisi tuwe huru!

Jirani, ama mita chache mbele ya Mtaa wa Selous, ndipo yalipo makaburi mashuhuri ya Kisutu panapozikwa Waislamu kwa wingi hapa jijini. Kwenye miaka ile ya kutawaliwa, na Kisutu ikiwa Kisutu hasa; makaburi yale yalitengwa mahsusi kwa ajili ya jamii ya watu wenye nasaba mbili, yaani Tanganyika na Arabuni— hasa Yemen, Oman na Persia.

Wenyeji siku hizo kila walipopatwa na vifo, basi walisafirishwa kupelekwa makwao kwenye asili yao, kama vile Kunduchi, Ununio, Mbweni, Kisiju na Kisarawe.

Wadigo ndio kabisa hawakukubali kuzikana hapa mjini wakisema,“amba! Huyu twenda mzika kwa babize na mamize! Hawezi asilan kulala na ‘majizaramu’ hapa, hawaaminiki hawa, mkimwacha waja mla nyama ndugu yetu,”kwa utani na mbwembwe nyingi wadigo walisema.

Aidha, wale ‘wajomba zetu’ ambao baba zao walikuja kutoka pande za Kiarabu wakaoa dada zetu hapa wakazaliwa wao, nao wakawa hawana sehemu ya kusitiriana hapa mjini, ukizingatia wanakotoka baba zao ni mbali Arabuni.

Kwa sababu hiyo, wazee wa Mzizima siku hizo, waliamua eneo hilo wapewe jamii hiyo wapate kuzikana hapo, maarufu pakijulikana Kisutu makaburi ya Waarabu; na si vinginevyo.

Hata hivyo, kwa maombi maalumu ruhusa ilitolewa kuzikwa jamaa wengine mahala hapo. Miongoni mwa watu mashuhuri waliozikwa Kisutu ni pamoja na familia nzima ya ukoo wa Sykes akiwamo Mzee Kliest Abdallah Sykes mwenyewe.

Wengine ni Abdulwahid Sykes, Ali Sykes, Kliest Sykes (aliyepata kuwa meya wa Jiji la Dar es Salaam wakati fulani) pamoja na mamake mpigania uhuru mashuhuri wa kike Bi Mwamvua Mrisho Mashu.

Kwenye makaburi ya Kisutu vilevile ndipo mahala alipozikwa mwanaharakati mwengine mpigania uhuru mwanamke, ‘Mama wa Taifa’ hili, hayati Bibi Titi Mohammed pamoja na Mzee Haidar Mwinyimvua.

Makaburi mengine ambayo mpaka leo yameendelea kuzikwa watu wa jamii moja tu ni yale yaliyopo palepale maeneo ya Kisutu, upande wa pili wa Barabara ya Bibi Titi Mohammed.

Mahala hapo wanazikwa jamii ya Waislamu wa kabila la Kingazija waliokuja hapa kwetu miaka mingi wakitokea Zanzibar, lakini asili yao hasa ni Visiwa vya Comoro. Hali ya hapo bado imebaki ileile; ni kwa Wangazija tu na si mtu mwengine.

Makaburi yanayofuata nyuma yake ni ya jamii ya Kibohora kutoka Pakistan na Bangladesh, ambayo nayo yamebaki kuwa ya kuzika jamii ya Kibohora peke yao mpaka leo.

Ukitoka makaburi hayo, ambayo yako mkabala na Hosteli ya SIDO, utayakuta makaburi ya Jumuiya ya Khoja Shia-Ithnasheri, ambayo wanazikwa madhehebu ya Shia peke yao mpaka leo hii.

Wakoloni Waingereza, katika kutawala kwao hapa, waliliacha Taifa hili likiwa halina mainjia wala wahasibu (accountants) wenye viwango vya NABAA, NABOCE au ngazi ya Shahada ya Kwanza. Kazi hizo zote zilitengwa kwa jamii ya Kihindi. Kazi yetu sisi kubwa ilikuwa ni ukarani mdogomdogo wa kuhesabu magunia, marobota na maboksi.

Serikali mpya ya Tanganyika, mara baada ya uhuru, wakataka kurekebisha hiyo hali. Hivyo, pakahitajika tuwe na wahasibu, mainjinia, mafundi umeme, mafundi mitambo na mafundi bomba.

Eneo la Kisutu likachaguliwa kwa kazi hiyo ya kujengwa vyuo hivyo. Nyumba zikavunjwa ikiwamo na ya kwetu; na mahala pake kikajengwa Chuo cha Biashara cha CBE na kile cha Ufundi cha DIT mnamo mwaka 1963. Kidogo kidogo tukawa tunapata wataalamu hao wa kizalendo.

Shule ya Sekondari ya Mzizima iko pale maeneo ya Kisutu karibu na hospitali ya Regency. Mahala hapo ilipojengwa shule hiyo, zamani za ukoloni palikuwa na kijihospitali kidogo kikiitwa ADH- Acquired Deseases Hospital.

ADH, ilikuwa ikilaza wagonjwa wenye magonjwa ya kuambukiza kama ukoma, ndui na labda kifua kikuu. Mfumo wa maisha wa siku zile uliyafanya magonjwa hayo miongoni mwa jamii ya Kiafrika kuwa mengi, kiasi cha kumfanya mtawala kuogopa na mwenyewe kuambukizwa magonjwa hayo.

Waliougua magonjwa hayo, wakati huo, waliwekwa karantini hapo ADH, wasije wakawaambukiza mabwana wakubwa pia!

Baada ya Uhuru kupatikana, hospitali ile dhalili, ikaondoshwa kabisa na mahala pake ikajengwa shule ya sekondari binafsi ikaitwa ‘H.H. Aga Khan Mzizima’, baada ya jamii ya Kihindi kupaomba mahala hapo wajenge shule hiyo.

Hii ilitokana na ukweli kwamba baada ya Uhuru, idadi ya Waafrika waliokuwa wakijiunga na elimu ya sekondari iliongezeka maradufu na hivyo kupunguza idadi ya watoto wa matajiri wa Kihindi kupata elimu hiyo.

Hivyo haraka haraka, zikajengwa shule mbili za sekondari hapa jijini za kulipia, wakati serikali ilikuwa ikitoa elimu hiyo bure kwenye shule nyengine inazozimiliki.

Shule nyengine binafsi kujengwa ilikuwa ni ile ya ‘Shaaban Robert Sekondari’ iliyopo pale Upanga. Pamoja na kwamba wamiliki wake ni Wahindi, mtu yeyote sasa alikuwa na fursa ya kujiunga bila ubaguzi, mradi awe na ada tu!

Tukutane Jumatatu ijayo tukiangazia eneo hilo la Kisutu sehemu ya pili.

Alamsiki!
 
Kwa kazi za Wahindi ni makubaliano na wewe 100%. Baada ya Uingereza kupoteza koloni la Marekani waliamua kuvamia India. Hiyo ilikuwa miaka ya 1700.

Walianza kutoa elimu kwa Wahindi. Walipogundua bara la Africa waliwabeba Wahindi kama skilled labour. Wahindi wengi waliishi na passport za Uingereza na baada ya Tanganyika kupata uhuru wengi walikwenda kuishi Uingereza. Kazi zote za u secretary, accountants, store keeping ect walifanya wao.
 
Kwa hakika jiji la Mzizima lina historia nzito sana. Shukrani kaka Rubawa kwa kushea nasi Historia hii ya Jiji letu pendwa.
Nasubiri sehemu ya 2 kwa shauku isiyo kifani.
Kila la kheri.
 
Tatizo mkoloni mwarabu na sultan wake alitangulia hapo pwani.

Kuja kwa mkoloni mzungu na kumwondoa sultan na kupurura utamaduni wake isiwe nongwa.

Ni principle duniani, tamaduni dhaifu hutawaliwa/humezwa na tamaduni zenye nguvu.
 
Nina wasiwasi mleta mada siyo mwana historia na alichoweka hapa ni masimulizi yasiyo na uhalali wa kihistoria,anasema Karne ya 1800,ninachojua mimi sasa hivi tuko karne ya 21,hiyo ya 1800 iliwadia lini? Anasema wakati wa Ottoman Empire ndipo aeneo la kisutu lilipoanza kujulikana?! What is this? Ottoman Empire ilitamalaki hadi Afrika ya Mashariki ?hii ni sawa na Gaddafi kuwa rais wa Kuwait.
 
Wahindi, wadigo, wamashomvi, wachaga, wanyakyusa, kanisa, misikiti, wazaramo, Tambaza, machifu, etc. duh! Asante Nyerere kwa social balance! Otherwise, shukrani kwa historia murua japo imekaa kiitikadi zaidi hata kama sio kwa makusudi haikupaswa kuachwa ibaki kama ilivyokuwa maana ilikuwa ni khatari kubwa!
 
Tatizo mkoloni mwarabu na sultan wake alitangulia hapo pwani.

Kuja kwa mkoloni mzungu na kumwondoa sultan na kupurura utamaduni wake isiwe nongwa.

Ni principle duniani, tamaduni dhaifu hutawaliwa/humezwa na tamaduni zenye nguvu.
Upo Sahihi ndugu yngu mradi ww ni mtu mweusi mwenzangu sina tatizo kbs maana kila siku nmekuwa sichoki kuomba radhi tusamehewe tu...
 
Nina wasiwasi mleta mada siyo mwana historia na alichoweka hapa ni masimulizi yasiyo na uhalali wa kihistoria,anasema Karne ya 1800,ninachojua mimi sasa hivi tuko karne ya 21,hiyo ya 1800 iliwadia lini? Anasema wakati wa Ottoman Empire ndipo aeneo la kisutu lilipoanza kujulikana?! What is this? Ottoman Empire ilitamalaki hadi Afrika ya Mashariki ?hii ni sawa na Gaddafi kuwa rais wa Kuwait.
Kweli kbs upo Sahihi ndugu yngu mradi ww ni mtu mweusi mwenzangu sina tatizo kbs maana kila siku naomba radhi sie wa kusamehewa tu...
 
Historia nzuri ina kuna baadhi ya mambo inaleta ukakasi. Mfano historia ya Kanisa Katoliki la St. Joseph, lilijengwa na Wamisionari wa shirika la Wabenediktini. Wewe ktk andiko lako lilikuwa msikiti
Anadai palikuwa na msikiti ukavunjwa ili kupisha ujenzi wa kanisa wakati mapori yalikuwepo kibao enzi hizo! Ukakasi mtupu Mkuu! And by the way kwanini wvunje msikiti kwa ajili ya kanisa na sio jengo au majengo mengine?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom