Idd Simba: Nchi yetu ipo hatarini

Saint Ivuga

JF-Expert Member
Aug 21, 2008
54,363
58,386
By admin
–January 20, 2011Posted in:
Habari Mchanganyiko

Na Salehe Mohamed
MSHAURI wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Iddi Simba, amesema nchi ipo hatarini kwa sababu amani na utulivu wa Tanzania vimeanza kutoweka.
Simba aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya Awamu ya Tatu, aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya utoaji wa vibali vya sukari, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati jopo hilo likizungumza na waandishi wa habari kuhusu mustakabali wa taifa.
Alisema kuwa ni vema amani na utulivu uliopo vikaenziwa badala ya watu kutoa kauli za kuchochea vurugu za kisiasa na kidini.
“Kila neno linalotolewa na wanasiasa au viongozi wa dini lina uzito wake, tunaonya amani na utulivu vimeanza kutuponyoka ni vema tukawa makini,” alisema.
Alibainisha kuwa jopo hilo si kundi la wababishaji au lenye kutafuta madaraka katika jamii bali ni la watu makini wasiopenda kubezana, kukejeliana na vitendo vingine vyenye lengo la kuigawa jamii.
Awali kabla ya Simba kutoa kauli hiyo, mratibu wa jopo hilo, Sheikh Mohamed Idd Mohamed, alitoa tamko la kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kutomkebehi na kumkejeli Rais Jakaya Kikwete.
Sheikh Mohamed alisema kejeli na kebehi hizo hazisaidii kuimarisha amani na demokrasia bali zinavunja.
Alisema wananchi hawana budi kuzingatia utawala wa sheria na kutii amri za mamlaka zilizoundwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
“Jopo la masheikh linawaasa Watanzania kuzingatia utawala wa sheria na kutii amri za mamlaka zilizoundwa kwa mujibu wa sheria za nchi na linatabanaisha kuwa kupinga amri za mamlaka za kisheria ni kupinga amri za Mwenyezi Mungu aliyeziweka,” alisema.
Sheikh huyo aliongeza kwamba ni kosa kutoitii mamlaka hiyo, ni kusababisha uvunjifu wa amani na kupoteza roho na mali kama ilivyotokea Arusha hivi karibuni.
Katika maelezo yake, alisema wamesikitishwa na kauli ya maaskofu zilizoonyesha kuunga mkono matakwa ya chama cha siasa na kufikia kutomtambua kiongozi wa kisiasa kwa misingi ya kisiasa.
Alisema viongozi hao wanasahau wao ni viongozi wa dini yao na wala si viongozi au wasemaji wa vyama vya siasa.
Jopo hilo limewataka maaskofu kuacha mara moja mwenendo huo mbaya unaoweza kuwagawa viongozi wa vyama vya siasa, wanasiasa na watendaji wa serikali kwa misingi ya dini na kuisambaratisha nchi.
Aliwataka maaskofu kuacha mara moja mwenendo huo mbaya unaoweza kuwagawa viongozi wa kisiasa na watendaji wa serikali kwa misingi ya kidini, na kusambaratisha nchi vipande vipande.
Aidha, kwa upande mwingine linampongeza Rais Kikwete kwa kuona umuhimu wa kuunda Tume ya Katiba.
Sheikh Mohamed, alisema jopo hilo linampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuona umuhimu wa kuunda Tume ya Katiba ambayo wanaamini itafanya kazi itakayokidhi matarajio ya Watanzania.

Mshauri wa kikao cha Jopo la Masheikh na Wanazuoni, Idd Simba (chini) akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu matamko yaliyotolewa katika kikao cha viongozi hao wa Dini ya Kiislamu, Dar es Salaam, ambapo waliwataka viongozi wa dini kuacha kuingilia masuala ya kisiasa na utawala wa nchi yanayoweza kuipeleka nchi pabaya. Kutoka kulia ni Katibu wa Jopo hilo, Sheikh Mohamed Mtulia, Mwenyekiti Sharif Hasim na Mohamed Idd (juu)ambaye ni Mratibu. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA)
Source: Tanzania Daima
 
Kaamua akimbilie kwene dini, kwa mashehe amewapata sio maaskofu
 
Back
Top Bottom