Hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Makadilio ya bajeti 2015-2016

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,895
HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS, MAHUSIANO NA URATIBU, MHESHIMIWA DKT. MARY M. NAGU (MB.) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MATUMIZI
YA FEDHA ZA OFISI YA RAIS, TUME YA MIPANGO (FUNGU 66) KWA MWAKA 2015/16

UTANGULIZI


1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala iliyochambua bajeti ya Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango (Fungu 66), Bunge lako sasa lipokee na kujadili mapitio ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Mipango kwa mwaka 2014/15 na likubali kupitisha makadirio ya matumizi ya fedha ya Tume ya Mipango kwa mwaka 2015/16.

2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninapenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu mapitio ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Mipango kwa mwaka 2014/15 na makadirio ya matumizi ya fedha za Tume ya Mipango kwa mwaka 2015/16. Aidha, naomba kuishukuru Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba vijijini na Makamu wake Mheshimiwa Gosbert Begumisa Blandes, Mbunge wa Karagwe, kwa ushirikiano, maelekezo na ushauri mzuri iliyotupatia wakati wa kujadili makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2015/16, hatua ambayo ilitusaidia kuandaa na kuwasilisha hotuba hii.

3. Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi ya Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ni: (i) Kutoa dira na mwongozo wa uchumi wa Taifa; na (ii) Kubuni sera za uchumi, Mikakati na Mipango ya Maendeleo ya Taifa, na pia usimamizi wa uchumi na kufanya tafiti za kiuchumi na kijamii.

4. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia majukumu hayo ya msingi, naomba sasa niwasilishe kwa muhtasari utekelezaji wa: (i) bajeti kwa mwaka 2014/15; (ii) ahadi za Serikali Bungeni; (iii) miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Tume ya Mipango; na (iv) utekelezaji wa maagizo ya Kamati yako. Aidha, taarifa ya utekelezaji itafuatiwa na mapendekezo ya mpango na makadirio ya matumizi kwa mwaka 2015/16.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA ORTM, 2014/15

5. Mheshimiwa Spika, bajeti ya Tume ya Mipango kwa mwaka 2014/15 ni shilingi 13,042,514,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 1,518,726,500 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 6,633,898,500 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Miradi ya maendeleo ilitengewa shilingi 4,889,889,000 ambapo shilingi 3,814,670,000 ni fedha za ndani na shilingi 1,075,219,000 ni fedha za nje.

6. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 30, 2015, Tume ya Mipango ilikuwa imepokea shilingi 4,878,520,955 sawa na asilimia 37.40 ya bajeti yote. Kati ya fedha zilizopokelewa: mishahara ni shilingi 1,474,306,480 sawa na asilimia 97.08 ya bajeti ya Mishahara; Matumizi Mengineyo (OC) ni shilingi 3,257,844,475 sawa na asilimia 49.11 ya bajeti ya

Matumizi Mengineyo, na Matumizi ya Maendeleo ni shilingi 146,370,000 sawa na asilimia 3 ya Matumizi ya miradi ya maendeleo. Mtiririko huu wa fedha umeathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa shughuli za Tume ya Mipango, hususan miradi ya maendeleo.

UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI BUNGENI

7. Mheshimiwa Spika, ahadi zilizotolewa Bungeni chini ya Fungu 66 kwa mwaka 2014/15 ni:-
i. Kufuatilia Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo 2014/15;
ii. Kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2015/16;


iii. Kuanza maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21);
iv. Kuendesha tafiti za kiuchumi na kijamii; na v. Kujenga Uwezo wa Tume ya Mipango.

Kufuatilia Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo 2014/15

8. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Tume ya Mipango ilifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 52 katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Kagera, Katavi, Kigoma, Mara, Morogoro, Mbeya, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Dar es Salaam na Pwani. Miradi iliyofuatiliwa ilijumuisha ile ya Umma na Sekta Binafsi katika maeneo ya barabara, madaraja na vivuko, bandari, nishati, maji, kilimo, umwagiliaji, viwanda, utalii, elimu, afya, viwanja vya ndege, mifugo na madini. Lengo kuu lilikuwa ni kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi husika pamoja na kuainisha mafanikio na

changamoto za utekelezaji ili kuishauri Serikali ipasavyo. Aidha, kwa miradi ya sekta binafsi, lengo pia lilikuwa ni kupata taarifa za uwekezaji, ajira na mipango ya baadaye ya mradi husika.

9. Mheshimiwa Spika, Changamoto kuu zilizoonekana katika miradi iliyofuatiliwa ni pamoja na miradi mingi ya maendeleo kutopata fedha za kutosha na kwa wakati hali iliyosababisha utekelezaji kuwa nyuma ya ratiba. Vilevile, baadhi ya miradi unasuasua au kusimama kabisa kutokana na malimbikizo ya madeni ya wakandarasi. Aidha, ilionekana kuwa maeneo mengi ya miradi ya maendeleo hayana hatimiliki hususan miradi ya bandari na viwanja vya ndege. Hali hiyo inasababisha uvamizi wa maeneo hayo na migogoro na wananchi, hivyo kuathiri uwekezaji. Hata hivyo, Serikali inafanya kila kinachowezekana kutatua migogoro hiyo inapojitokeza ili kutowakatisha tamaa wawekezaji, kulipa fidia pale inapolazimu na kuepusha usumbufu kwa wananchi.

10. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto zilizobainishwa, Serikali inakusudia kuimarisha vyanzo vya mapato vya kodi na visivyo vya kodi. Vilevile, Serikali imehakiki madai ya wakandarasi ili kuweka utaratibu wa kulipa malimbikizo husika moja kwa moja kutoka Hazina. Aidha, Wizara, Idara, Taasisi, Wakala za Serikali, Sekretariati za Mikoa na Halmashauri zimeelekezwa kupata hatimiliki ili kudhibiti uvamizi na gharama za ulipaji fidia usio wa lazima.

Kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa, 2015/16

11. Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango iliandaa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2015/16 ambayo yalijadiliwa na kuridhiwa na Bunge, Novemba 2014. Mapendekezo hayo yalizingatia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16), MKUKUTA II (2011 - 2015), Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2010, na sera na mikakati ya kisekta. Aidha, Tume ya Mipango imekamilisha rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2015/16 kwa kuzingatia Mapendekezo ya Mpango yaliyoridhiwa na Bunge, Novemba 2014. Rasimu hiyo iliwasilishwa kwa Wabunge wote tarehe 29/4/2015 katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere – Dar es Salaam. Aidha, rasimu ya Mpango ilijadiliwa katika Kamati ya Bunge ya Bajeti tarehe 5 Mei 2015. Maoni ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti yametumika katika kuboresha rasimu ya Mpango itakayowasilishwa Bungeni Juni 2015.

Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21)

12. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Tume ya Mipango imeanza maandilizi ya kutayarisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano utakaoongoza usimamizi wa uchumi na mipango ya maendeleo kwa kipindi cha 2016/17 – 2020/21. Kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango Elekezi wa Maendeleo (2011/12 – 2025/26) ya kujenga uchumi ambao una maendeleo ya viwanda yaliyo karibu sawa na nchi

zenye hadhi ya kipato cha kati, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano utalenga katika kujenga uchumi wa viwanda. Mpango huu utajielekeza kuendeleza viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na viwanda vyenye kutumia teknolojia ya kati, hasa viwanda mama kama vya chuma na vile vinavyotumia makaa ya mawe na magadi soda. Aidha, viwanda vyenye kutumia gesi asilia na mafuta navyo vitapewa msukumo.

13. Mheshimiwa Spika, pamoja na kulenga viwanda vinavyotumia utajiri mkubwa wa rasilimali zilizopo nchini, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano utajielekeza katika kujenga viwanda vitakavyotuwezesha kutumia vizuri fursa za nchi, hususan nafasi ya kipekee ya Tanzania kijiografia inayotuwezesha kuwa lango kuu la biashara na huduma kwa nchi za maziwa makuu, na soko kubwa la kikanda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC.

Tafiti za Kiuchumi na Kijamii

14. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2014/15, Tume ya Mipango iliendelea kutekeleza tafiti ambazo hazikukamilika mwaka 2013/14, ambazo ni:-
i) Maendeleo ya ujuzi utakaoiwezesha Tanzania kuwa na uchumi imara ifikapo mwaka 2025: taarifa ya utafiti huu iko katika hatua ya kutolewa maoni na wadau kabla ya kuandaa mapendekezo ya kisera yatakayowasilishwa katika mamlaka za maamuzi Serikalini;

ii) Muundo taasisi (institutional Framework) kuchochea uwekezaji na maendeleo ya teknolojia viwandani:

Utafiti huu umekamilika pamoja na mapendekezo ya kisera kwa ajili ya kujadiliwa na wadau kabla ya kuwasilishwa kwenye mamlaka za maamuzi Serikalini.

15. Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Tume ya Mipango imeanza maandalizi ya awali kwa ajili ya kuendesha tafiti hususan katika eneo la maendeleo ya viwanda na ukuaji wa miji. Lengo la tafiti hizo ni kupata taarifa muhimu zitakazosaidia katika maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21).

16. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) kwa kipindi cha kuanzia Julai 2011 hadi Desemba 2013. Mapitio hayo yalifanyika ili kupima mafanikio yaliyopatikana na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji; kubainisha maeneo ambayo yanahitaji msukumo zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa; na kupata taarifa zitakazosaidia katika maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2015/16 – 2020/21) ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Kazi ya kuboresha mapitio hayo inaendelea ili kujumuisha kipindi chote cha Mpango na taarifa kamili itawalishwa kwa wadau sambamba na Mapendekezo ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano itakapofika Novemba 2015.

Kujenga Uwezo wa Tume ya Mipango

17. Mheshimiwa Spika, katika kujenga na kuimarisha ujuzi wa kiutendaji, Tume ya Mipango iliajiri watumishi

wapya 26 ambapo Wachambuzi Sera waliopangiwa kazi katika Klasta za Tume ya Mipango ni 18, na watumishi wengine 8 walipangiwa katika Idara na Vitengo Saidizi. Aidha, watumishi 7 walihamia katika idara za utawala kwa utaratibu wa kawaida wa utumishi wa umma. Hadi sasa, Tume ina jumla ya watumishi 149, ambapo wanaume ni 91 na wanawake ni 58.

18. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kuimarisha weledi, Tume ya Mipango imewezesha watumishi 8 kushiriki katika mafunzo ya muda mrefu katika maeneo yafuatayo:- shahada ya uzamivu katika uchumi; na shahada ya uzamili katika: uchumi; sera na mipango; menejimenti ya fedha; uhasibu; utawala; sheria; na teknolojia ya habari na mawasiliano. Aidha, watumishi wawili waliwezeshwa kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi. Vilevile, kwa upande wa mazingira mazuri ya kazi, Tume ya Mipango imeweza kuongeza vitendea kazi na kukarabati vilivyopo kadri upatikanaji wa fedha ulivyoruhusu.

Shughuli Nyingine Zilizotekelezwa katika Mwaka 2014/15

Kukamilisha Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma


19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Tume ya Mipango imekamilisha uandaaji wa Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma (Public Investment Management Operational Manual) ambao umeanza kutumika katika mwaka 2014/15. Mwongozo huu unatoa maelekezo ya utaratibu na hatua zinazohitajika


katika kuandaa andiko la mradi na kutekeleza miradi yote inayotumia fedha za umma. Mwongozo huo pia unatoa maelezo na ufafanuzi juu ya vigezo mbalimbali vinavyotumika katika uchambuzi wa miradi ya maendeleo kiuchumi, kifedha na kijamii.

Kuratibu Mazungumzo ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Serikali ya Japan



20. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Tume ya Mipango iliendelea kuratibu uchambuzi wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Japan. Shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na kubainisha maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano kati ya Tanzania na Japan na kuainisha miradi itakayoombewa ufadhili kutoka Serikali ya Japan kwa mwaka 2015/16. Miradi iliyowasilishwa Kwa Serikali ya Japan kupata ufadhili kwa mwaka 2015/16 ipo katika sekta za kilimo, viwanda, usafirishaji, ujenzi, nishati, maji, afya na fedha.

Kuratibu Maandalizi ya Mchango wa Tanzania katika Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs)

21. Mheshimiwa Spika, Tanzania imepata mafanikio mbalimbali katika kufikia Malengo ya Milenia, hususan katika maeneo ya elimu na afya. Pamoja na mafanikio hayo, changamoto za umasikini, vifo vya mama wajawazito na upatikanaji wa chakula na lishe zimeendelea kuzikabili nchi zinazoendelea. Changamoto hizo na nyingine zimepelekea Umoja wa Mataifa kuandaa malengo mengine ya maendeleo baada ya mwaka 2015 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi washiriki. Katika kutimiza adhma hiyo,

Tume ya Mipango imekuwa ikiratibu na kushiriki katika majadiliano kuhusu Malengo Endelevu ya Maendeleo (Sustainable Development Goals). Mapendekezo yaliyowasilishwa na Tanzania kuingia katika SDGs ni pamoja na: kuondokana na umaskini uliokithiri; kuwa na elimu bora na afya nzuri hasa kwa kinamama na watoto; kuwa na uchumi imara na maendeleo endelevu; kulinda mazingira; kuwa na uwiano sawa wa kijinsia; utawala bora; na kuongeza kasi ya ushirikiano endelevu na nchi mbalimbali.

Mpango Mkakati wa TEHAMA wa Tume ya Mipango na Mwongozo wa Kudhibiti Vihatarishi

22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Tume ya Mipango imekamilisha uandaaji wa Mpango Mkakati wa TEHAMA wa Tume ya Mipango utakaoongoza namna bora ya kujenga uwezo wa wataalam wa Tume ya Mipango katika matumizi ya TEHAMA na ununuzi wa vifaa na mifumo ya kielektroniki. Mkakati huo utasaidia kuipunguzia Tume ya Mipango gharama za ununuzi na kuendesha mifumo hiyo. Aidha, Tume ya Mipango imeandaa mwongozo wa kudhibiti vihatarishi kwa lengo la kuweka viwango na namna Tume ya Mipango itakavyodhibiti vihatarishi ili visiikwaze kufikia malengo yake ya kila mwaka. Vilevile, Tume ya Mipango imeandaa daftari la mali za kudumu pamoja na kuzifanyia tathmini yake kwa lengo la kujua thamani na kuweka kumbukumbu ya mali za Serikali zilizopo Tume ya Mipango.

MIRADI YA MAENDELEO 2014/15

23. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Tume ya Mipango ilitekeleza miradi mitatu ya maendeleo ambayo ni: (i) Mradi wa Kujenga uwezo wa Kuratibu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo; (ii) Mradi wa Kupanga Masuala ya Idadi ya Watu (Population Planning Project); na (iii) Mradi wa Kuhamasisha Ukuaji Uchumi ili Kupunguza Umasikini bila Kuathiri Maendeleo Endelevu ya Mazingira (Pro-Poor Economic Growth and Environmentally Sustainable Development).

24. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2014 hadi Aprili 30, 2015, mradi wa Kujenga uwezo wa Kuratibu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na ule wa Kupanga Masuala ya Idadi ya Watu haikupata fedha. Hata hivyo, Tume ya Mipango ilifanya kazi za kupitia maandiko ya miradi ya maendeleo ya baadhi ya Wizara, Idara, na Wakala za Serikali na kutoa ushauri na maelekezo ya kuboresha maandiko hayo.

25. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2014 hadi Aprili 30, 2015, shughuli zilizotekelezwa katika mradi wa Kuhamasisha Ukuaji Uchumi ili Kupunguza Umasikini bila Kuathiri Maendeleo Endelevu ya Mazingira ni pamoja na kuendesha utafiti ili kubaini mafanikio katika juhudi za kupunguza umaskini na kuongeza kipato kwa namna ambayo haiathiri mazingira katika wilaya za Nyasa, Bunda, Sengerema, Bukoba na Ikungi. Kwa ujumla, kuna mafanikio dhahiri ya kupungua kwa umasikini kutokana na
kuinuka kwa kipato na kuongezeka kwa tija kwa bei katika shughuli msingi za wananchi.
na kuimarika Aidha, hili pia

limechangiwa na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma kama vile za elimu, afya, maji, na usafiri. Katika baadhi ya maeneo wananchi wamejitahidi sana kuboresha nyumba na makazi na pia kuongeza umiliki wa vyombo na zana za kudumu. Familia nyingi pia zimedhihirika kubadili au kuchanganya shughuli za kiuchumi kama vyanzo msingi vya mapato. Pamoja na Mafanikio haya, katika sehemu nyingi ilibainika kuwa ongezeko la kipato limeendana na matokeo hasi ya utunzaji wa mazingira, hususan, uvunaji holela wa misitu, kilimo kuendeshwa katika maeneo oevu na vyanzo vya maji, uharibifu wa mazalia ya samaki, na ukuaji wa miji midogo kiholela. Kutokana na matokeo ya utafiti huu, viongozi na wananchi wanahimizwa kuongeza jitihada katika kutunza mazingira na kusimamia matumizi ya ardhi ili kuwezesha ukuaji endelevu wa uchumi.

MAAGIZO YA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA

26. Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Bajeti la mwaka 2014/15, Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ilihoji na kushauri yafuatayo:-
i. Suala la kutolipwa kwa muda mrefu posho maalum (top-up allowance) kwa watumishi wa Tume ya Mipango litafutiwe ufumbuzi wa haraka; na
ii. Tume ya Mipango iongezewe wataalam.

27. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa kwamba hatua zifuatazo zimechukuliwa na Tume ya Mipango katika mwaka 2014/15:-
i. Wizara ya Fedha imeendelea kutoa fedha za posho maalum (top – up allowance) kwa watumishi wa

Tume ya Mipango wanaostahili kulipwa posho hizo na kuwezesha malipo hayo. Aidha, madeni ya nyuma yanayofikia shilingi 916,579,200 yamekaguliwa na yanaendelea kupunguzwa katika bajeti ya 2014/15 kulingana na upatikanaji wa fedha. Uchambuzi wa kuwezesha wachambuzi sera wote kulipwa posho ya ziada na malimbikizo umekamilika kwa ajili ya utekelezaji kwa awamu; na
ii. Kuajiri watumishi wapya 26, na kupata watumishi wengine 7 waliohamia katika utaratibu wa kawaida ndani ya utumishi wa umma.

MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2015/16

A. Shughuli za Kipaumbele, 2015/16



28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, shughuli za kipaumbele zitakazotekelezwa na Tume ya Mipango ni:-
i. Kukamilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21);

ii. Kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17;

iii. Kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2015/16;

iv. Kuendesha tafiti za Kiuchumi na Kijamii; na v. Kujenga Uwezo wa Tume ya Mipango.

Kukamilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21)

29. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, Tume

ya Mipango inatarajia kukamilisha utayarishaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 -2020/21). Kama nilivyoeleza awali, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano utalenga katika kujenga uchumi wa viwanda. Serikali itahakikisha kwamba Mpango huo unaoandaliwa unatoa matumaini kwa Watanzania hasa katika kukabiliana na umaskini, kuongeza ukuaji shirikishi wa uchumi na kupanua fursa za ajira hasa kwa vijana.

Kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17

30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango itaandaa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17. Mpango huo utakuwa wa kwanza katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 - 2020/21).

Kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo

31. Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyobainishwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kuchambua maandiko ya miradi na taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kwa kila robo mwaka; na kufuatilia utekelezaji wa baadhi ya miradi ya Kitaifa ya kimkakati.

Tafiti za Kiuchumi na Maendeleo ya Kijamii

32. Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango itaendelea kukamilisha tafiti kuhusu maendeleo ya viwanda, hususan,

viwanda gani vipewe kipaumbele kwa kuzingatia fursa za Tanzania, kubaini malengo ya maendeleo ya viwanda kwa miaka 5 (2016/17 – 2020/21); uhusiano kati ya ukuaji wa miji na maendeleo ya viwanda; maendeleo ya sayansi na teknolojia; na kubaini vyanzo vya kugharamia utekelezaji wa Mpango huo. Kama nilivyosema awali, lengo la tafiti hizo ni kusaidia maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21).

Kujenga Uwezo wa Tume ya Mipango

33. Mheshimiwa Spika, Tume ya Mipango itaendelea kuwajengea uwezo watumishi wake na kuboresha vitendea kazi vya ofisi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake. Maeneo yatakayopewa umuhimu mkubwa ni pamoja na mafunzo kwa wataalam wa kada zote na ununuzi wa vitendea kazi.

B. Miradi ya Maendeleo Itakayotekelezwa 2015/16


34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango itatekeleza miradi ifuatayo: (i) Mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuratibu Utekelezaji wa Bajeti na Miradi ya Maendeleo; (ii) Mradi wa Maboresho katika Usimamizi wa Fedha za Umma; (iii) Mradi wa Kupanga Masuala ya Idadi ya Watu; na (iv) Mradi wa Kuhamasisha Ukuaji Uchumi ili Kupunguza Umasikini bila Kuathiri Maendeleo Endelevu ya Mazingira.

35. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mradi wa Kujenga Uwezo wa Kuratibu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo shughuli zilizopangwa ni:-

i. Kujenga uwezo wa watumishi katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali katika kuandaa, kusimamia, na kutekeleza mipango ya maendeleo;
ii. Kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo; na
iii. Maandalizi ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dodoma.

36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, shughuli zitakazotekelezwa katika mradi wa Maboresho katika Usimamizi wa Fedha za Umma ni kuwezesha uchapaji, usambazaji na kuendesha mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya Umma kwa Maafisa Mipango Serikalini katika ngazi za wizara na mikoa. Lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa na ujuzi katika kuandaa maandiko ya miradi na uchambuzi wa miradi ya maendeleo.

37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, shughuli zitakazotekelezwa katika mradi wa Kupanga Masuala ya Idadi ya Watu ni:-
i. Kuratibu mapitio ya Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu (2006);
ii. Kuendesha utafiti kuhusu hali ya Nguvukazi Nchini ikiwa ni moja ya makubaliano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
iii. Kujenga uwezo wa watumishi katika uchambuzi wa masuala ya Idadi ya watu na Maendeleo.

38. Mheshimiwa Spika, shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika mradi wa Kuhamasisha Ukuaji Uchumi ili Kupunguza Umasikini bila Kuathiri Maendeleo Endelevu

ya Mazingira kwa mwaka 2015/16 ni pamoja na:-

i. Kuwezesha kufanyika mijadala ya kitaifa kuhusu masuala ya umaskini, jinsia, ukuaji endelevu wa uchumi na mazingira;
ii. Kuingiza masuala ya jinsia na mazingira katika mipango ya sekta za kilimo, uvuvi, na misitu;
iii. Ununuzi wa vitendea kazi na mafunzo juu ya nyenzo mbalimbali za utayarishaji mipango na uchambuzi wa sera na taarifa za kiuchumi; na
iv. Kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za kusini (South South Cooperation).

C. Makadirio ya Bajeti kwa Mwaka 2015/16

39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16, Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango inaomba kutengewa shilingi 11,588,052,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 7,871,896,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, na shilingi 3,716,156,000 kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Mchanganuo wa maombi hayo ya fedha ni kama ifuatavyo:-
attachment.php


HITIMISHO

40. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Fungu 66 - Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kwa mwaka 2014/15 na Mpango na Makadirio ya Matumizi kwa mwaka 2015/16.

41. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
 

Attachments

  • bajeti1.png
    bajeti1.png
    17.1 KB · Views: 178
Back
Top Bottom