Hotuba ya kambi ya upinzani bungeni katika wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,895
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA MHESHIMIWA JUMA HAMAD OMAR (MB) AKIWASILISHA MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU BAJETI YA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17
  1. UTANGULIZI
    Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia muda huu kumshukuru Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb) kwa kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Ninamwahidi yeye pamoja na Kambi nzima ya Upinzani kwamba; nitafanya kazi kwa bidii katika kuibua mawazo mbadala ya kisera na kiutendaji ili kuboresha utendaji na ufanisi wa wizara hii kwa maslahi ya taifa letu.

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi za pekee kwa viongozi wote wakuu wa vyama vinavyounda UKAWA, kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaunganisha watanzania kupitia vyama hivyo katika kuyatafuta mabadilko na uhuru wa kweli katika ushiriki wao katika siasa na utawala wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa sio muungwana ikiwa sitawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Ole kwa imani kubwa waliyonayo kwangu kwa kunichagua kuwa mbunge wao na kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kunipatia katika kutekeleza majukumu yangu ya kibunge. Kwao wote nasema asenteni sana.

  1. UFANISI NA WELEDI WA JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua uwezo na weledi mkubwa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kulinda usalama wa mipaka ya nchi yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua pia mchango mkubwa wa Jeshi letu katika kupigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika zikiwemo Zimbabwe, Angola, Msumbiji, Zambia, Malawi, Afrika ya Kusini Uganda na nyinginezo.

Mheshimiwa Spika, Aidha Jeshi la Wananchi limekuwa likishiriki katika Operesheni mbalimbali za kimataifa za kulinda amani. Katika operesheni hizo Jeshi letu limetajwa kwamba ni la kupigia mfano katika uhodari wa kazi na nidhamu ya hali ya juu. Kwa sababu hizo, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeiletea nchi yetu heshima kubwa katika medani za kimataifa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jeshi letu kuwa na weledi na nidhamu kubwa inayopigiwa mfano duniani, watawala wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi letu la Ulinzi jambo linalolifanya lionekane kana kwamba halizingatii maadili yake ya kazi.

Mheshimiwa Spika, kumezuka tabia ya watawala kulitumia Jeshi la Wananchi katika masuala ya ndani ya kisiasa ili kutimiza matakwa yao ya kisiasa. Tabia hiyo ni mbaya kwa sababu licha ya kuliondolea Jeshi letu sifa ya maadili lakini ni kitendo kinachodumaza demokrasia katika taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kinapofika kipindi cha uchaguzi, Zanzibar inakuwa kama vile nchi iliyovamiwa kijeshi (invaded country). Kipindi chote cha uchaguzi Zanzibar, vikosi vya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi, na Mgambo kutoka Tanzania bara wanapelekwa Zanzibar na kupiga makambi kwenye viwanja vya ndege, bandarini na kwenye vituo vya redio. Aidha, vikosi hiyo vimekuwa vikipita mitaani na wakati mwingine kufanya mazoezi ya kijeshi katika maeneo ya makazi ya wananchi jambo ambalo huzua hofu kwa wananchi na kutoa taswira kama vile nchi inakabiliwa na vita.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba ulinzi wa raia na mali zao unafanywa na Jeshi la Polisi isipokuwa Jeshi la Ulinzi linaweza kuongeza nguvu ikiwa tu nchi iko vitani au kama hali ya hatari imetangazwa. Jambo tunalohoji hapa; ni kwa nini Jeshi la Wananchi wa Tanzania likafanye kazi ya Jeshi la Polisi huko Zanzibar wakati Jeshi la Polisi lipo, nchi haipo vitani na pia hakuna hali ya hatari iliyotangazwa?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalaani kitendo cha Serikali ya Muungano kutumia nguvu za kijeshi kutisha wananchi wa Zanzibar na kutumia mwanya huo kuchakachua mchakato wa kidemokrasia wa uchaguzi na kuiweka CCM madarakani kwa nguvu. Naomba ieleweke kwamba, unaweza kulazimisha utawala wa nguvu ya kijeshi lakini kushinda hisia za wananchi ni jambo jingine kabisa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutafakari upya matumizi sahihi ya Jeshi letu. Kulishirikisha Jeshi katika mchakakato wa kutwaa madaraka ya dola tena kwa njia za ujanjaujanja ni hatari kubwa sana. Ni vizuri demokrasia iachwe ichukue mkondo wake. Kwa maana hiyo, Jeshi libakie kulinda mipaka ya nchi yetu na kuilinda Serikali itakayowekwa madarakani na wananchi wenyewe.

  1. MIGOGORO YA MIPAKA YA ARDHI BAINA YA JESHI LA WANANCHI (JWTZ) NA WANANCHI
Mheshimiwa Spika, inakera na inaudhi pale ambapo Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa ushauri mzuri kwa Serikali kwa maslahi ya taifa na mustakabali mwema wa wananchi wetu halafu Serikali inapuuza ushauri huo.

Mheshimiwa Spika, nimeanza na kauli hii kwa sababu katika muda wote wa uhai wa Bunge la kumi, Kambi Rasmi ya Upinzani ililipigia sana kelele suala hili la migogoro ya mipaka ya ardhi kati ya jeshi na wananchi na kuitaka Serikali kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kupitia upya mipaka ya Jeshi na Wananchi katika maeneo yale yenye migogoro na kuiweka bayana ili wananchi watambue maeneo ya Jeshi na hivyo kutoyaingilia hayo maeneo, lakini mpaka sasa zoezi hilo halionekani likifanyika kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, wapo wananchi wengi sana ambao wameathiriwa na migogoro hii ikiwa ni pamoja na kubomolewa makazi yao, hivyo ni vema Serikali hii ya awamu ya tano ikamaliza na tatizo hili kabisa. Tunatambua kwamba Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Naibu wake wamekuwa wakishughulikia na kuipatia ufumbuzi migogoro ya ardhi baina ya wananchi wenyewe kwa wenyewe, ila haifahamiki bayana kwamba kunapotokea mgogoro wa mipaka ya ardhi kati ya wananchi na taasisi ya Jeshi unashughulikiwa na wizara ipi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kwa mara nyingine tena kulieleza Bunge hili kwamba; ina mpango gani katika mwaka mpya wa fedha 2016/17 wa kumaliza kabisa migogoro ya mipaka ya ardhi kati ya Jeshi na Wananchi?

  1. AJIRA KATIKA JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kwamba ajira katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania zinatolewa kwa upendeleo na kwa usiri na kwamba wanaonufaika na ajira hizo ni watoto wa maafisa wa ngazi za juu jeshini na mbaya zaidi kwa upande wa Zanzibar huwezi kupata ajira jeshini kama hujaunganishwa na kiongozi wa CCM.

Mheshimiwa Spika, jambo hili la ajira za upendeleo lipo katika baadhi ya taasisi za umma. Kwa mfano, mwezi Julai, 2014, Idara ya Uhamiaji katika Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi ilishawahi kulalamikiwa kutoa ajira 200 za upendeleo kwa ndugu na jamaa wa maafisa wa Uhamiaji, jambo lililosababisha ajira hizo kufutwa na kutangazwa upya baada ya kubainika kwamba zilikuwa ni za upendeleo.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba ajira za jeshi zinaanzia JKT kwa wale wanaofuzu mafunzo ya JKT, lakini kwa kuwa kumekuwa na malalamiko kwamba ajira zinatolewa kwa upendeleo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufanya uchunguzi wa tuhuma hii ya usiri na upendeleo katika ajira za Jeshi na kuchukua hatua stahiki ili kuwe na fursa sawa kwa kila raia wa Tanzania ya kupata ajira katika taasisi hii muhimu ya umma. Aidha, katika muktadha huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kufanya pia uchunguzi wa mchakato wa kujiunga na JKT ili kuhakikisha kwamba hakuna ukiritimba wowote unaofanyika katika kuwachagua vijana wenye nia ya kujiunga na JKT.

5. WASTAAFU WA JESHI LA WANANCHI

Mheshimiwa Spika, si nia yangu kuzungumzia kwa kirefu jambo hili kwa kuwa limesemwa sana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kila bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inapojadiliwa. Ila napenda kurudia tu neno moja kwamba “Wastaafu wa Jeshi, ni Jeshi la Akiba” (Reserved Army). Kama tusipolitunza jeshi hili la akiba hasara yake ni kwamba; tutakapofikwa na madhila ya kivita yanayohitaji msaada wa Jeshi hili la akiba tutakwama kwa kuwa wastaafu hao wa jeshi watakuwa hawana nguvu tena ya kutoa msaada wowote.

Mheshimiwa Spika, Inasikitisha sana kuona wanajeshi wastaafu waliotumikia taifa hili kwa muda mrefu na kwa uadilifu na uzalendo mkubwa wakisota mitaani kutokana na hali ngumu ya maisha inayosababishwa na kukosa kipato cha kujikimu maisha yao.

Mheshimiwa Spika,kutokana na Serikali kuwasahau wanajeshi wastaafu na kuwaacha mitaani bila kujua ni kitu gani cha kufanya, tayari wameanzisha umoja wao unaojulikana kama Muungano wa Wanajeshi Wastaafu Tanzania Bara (MUWAWATA) kwa upande wa bara na UMAWA kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha kwamba pensheni za wastaafu wa Jeshi zinalipwa kwa wakati, lakini pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa Serikali kutoa ruzuku kwa Muungano wa Wanajeshi Wastaafu ( MUWAWATA) na UMAWA ili Umoja waliouanzisha uweze kutekeleza miradi mbalimbali ya kijasiriamali kwa maslahi ya wanachama wa umoja huo.

  1. USHIRIKIANO WA KIJESHI NA MATAIFA MENGINE
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambaua Jeshi la Wananchi wa Tanzania linashiriki katika operesheni za kijeshi katika mataifa mengine kupitia katika Mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika na ule wa Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba ushiriki huo unaliongezea jeshi letu uzoefu wa kufanya kazi katika mazingira tofauti tofauti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutafakari upya faida hususan za ki-uchumi na ki-teknolojia ambazo kama taifa tunanufaika nazo kwa Jeshi letu kushiriki katika operesheni hizo.

Mheshimiwa Spika, mataifa yaliyoendelea kama vile Marekani na Uingereza hayapeleki majeshi yao kupigana vita au kulinda amani kama hakuna maslahi yoyote kwa mataifa yao. Na ndio maana sera zao za mambo ya nje ziko bayana kwamba ni maslahi ya nchi zao kwanza ndio mambo mengine yafuate.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza hivi kwa sababu kama taifa tusipojipanga kimkakati zaidi, tutaishia kupokea miili ya wanajeshi wetu waliokufa katika operesheni hizo huku taifa likibaki bila manufaa yoyote. Kwa sababu hiyo, tunapendekeza kwamba kuwe na malengo mahsusi na ya kimkakati Jeshi letu linapokwenda kushiriki operesheni katika mataifa mengine. Mikakati hiyo iwe ni pamoja na kufanya utafiti wa masuala ya kiuchumi na kiteknolojia ili baada ya operations hizo kuwe na faida iliyopatikana.

  1. UTEUZI WA WANAJESHI KATIKA NAFASI ZA KISIASA
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na utamaduni wa kuwateua maafisa wa vyombo vya dola waliopo kazini na wastaafu kushika nafasi za kisiasa kama vile wakuu wa mikoa na wakuu wa Wilaya.

Mheshimiwa Spika, baada ya uteuzi wao, wakuu hawa wa Wilaya na Mikoa hufanya kazi kwa mujibu wa chama kinachoongoza Serikali. Kwa maana hiyo, wakuu wa Wilaya wanafungwa na ibara ya 80(1) (c) ya Katiba ya CCM ya 1977 inayowataja kuwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM katika wilaya husika. Hali kadhalika wakuu wa mikoa wanafungwa na Ibara ya 94(1) (c) inayowataja kuwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM katika mikoa husika.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itambue kwamba Ibara ya 147 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka kwamba “Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chohote cha siasa, isipokuwa tu kama atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii”.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua hawa maafisa wa jeshi wanakuwa wamejiunga na CCM lini hadi kuteuliwa kushika nafasi za kisiasa za CCM, wakati wanakuwa wamefungwa na Katiba kutojiunga na chama chochote cha siasa?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina mtazamo kwamba; ili kulinda na kusimamia maadili ya kazi za Jeshi, wanajeshi wasihusishwe kabisa na kazi za siasa, iwe wapo kazini au wamestaafu. Tunashauri hivi kwa sababu kwa kuwateua kushika nafasi za siasa wanapostaafu, kunaweza kukawafanya wale wengine waliopo kazini kutozingatia maadili yao ya kazi na kuanza kujipendekeza kwa watawala kwa imani kwamba pengine na wao watateuliwa kuwa wakuu wa mikoa au wilaya watakapostaafu.

Mheshimiwa Spika, hatari kubwa zaidi ya kuwashirikisha wanajeshi katika mfumo wa utawala ni kwamba; itawavutia wanajeshi wengi kutaka kushiriki siasa moja kwa moja ilhali imekatazwa na katiba na matokeo yake utawala wa kiraia (civil governace) utapoteza thamani yake.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri kwamba wanajeshi waachwe wafanye kazi za Jeshi kwa mujibu wa taaluma na ujuzi wao wa kijeshi. Utawala wa nchi kwa mujibu wa Katiba ni wa kiraia. Hivyo, tusichanganye mambo ambayo yanaweza kutushinda kuyatafutia ufumbuzi ikiwa yataharibika.

6. JESHI LA KUJENGA TAIFA NA DHANA YA UJENZI WA TAIFA

Mheshimiwa Spika, ukisoma dhima ya Jeshi la Kujenga taifa utaona kwaba JKT pamoja na mambo mengine ina wajibu wa kuwafunza vijana wetu kufanya kazi za uzalishaji mali kwa ajili ya kujenga uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikishauri miaka nenda miaka rudi kwamba; Serikali itumie nguvu kazi iliyopo kwenye Jeshi la Kujenga Taifa katika kujenga uchumi wa kweli nchini. Tulishauri kwamba Serikali itenge mashamba makubwa ili vijana hawa wawapo mafunzoni, wafanye mafunzo kwa vitendo ya kilimo ili nchi iweze kujitegemea kwa chakula.

Mheshimiwa Spika, ni aibu kwa taifa hili kupata majanga ya njaa wakati Jeshi la Kujenga Taifa lipo na linamiliki mashamba yenye rutuba nzuri. Kwa sababu hii, tunashauri kwamba Serikali iwaagize wakuu wa makambi ya JKT kutengeneza programu maalum za uzalishaji mali katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, viwanda, ufundi, uvuvi nk kila mwaka. Tunapendekeza pia kwamba waziri mwenye dhamana awe anatoa taarifa ya uzalishaji uliofanywa na JKT na mapato (maduhuli) yaliyopatikana kutokana na uzalishaji huo katika kila bunge la bajeti.

  1. UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2015/16
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2015/16, Serikali imeweka rekodi mbaya ya kutoa fedha chini ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge kwa miradi ya maendeleo katika wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na katika mafungu mengine fedha hazikutolewa kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Bunge liliidhinisha jumla ya shilingi bilioni 220. 14 (katika fungu 57 – Wizara) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Lakini hadi kufikia mwezi Machi, 2016 fedha iliyokuwa imeshatolewa na hazina ilikuwa ni shilingi bilioni 40 sawa na asilimia 18 tu ya bajeti iliyoidhinishwa.

Mheshimiwa Spika, miradi iliyokuwa itekelezwe, mingine inawagusa moja kwa moja wananchi, hivyo kitendo cha kutotekelezwa kikamilifu kimewaathiri sana wananchi. Kwa mfano mradi mmojawapo ulikuwa ni upimaji na ulipaji wa fidia katika maeneo yaliyotwaliwa na jeshi. Mradi huu ulitengewa takriban shilingi bilioni 7.4, lakini fedha iliyotolewa hadi kufikia Machi, 2016 ni shilingi milioni 277.1 sawa na asilimia 3.7 tu ya bajeti iliyoidhinishwa.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha kutotoa fedha ya kutosha kutekeleza mradi huu kumeendelea kuchochea migogoro ya mipaka ya ardhi kati ya jeshi na wananchi ambayo ingeweza kuepukwa na hivyo kujenga uhasama kati ya Jeshi na Wananchi jambo ambalo lingeweza kuepukwa kama Serikali ingetoa fedha zote zilizoidhinishwa na kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, jambo la ajabu kabisa kuwahi kutokea ni kitendo cha kutopeleka fedha yoyote kutekeleza miradi ya maendeleo katika fungu 38 (Ngome). Fungu hili lilitengewa jumla ya shilingi bilioni 8 lakini hadi kufikia Machi 2016, hakuna hata senti moja iliyotolewa na hazina kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wowote wa maendeleo uliopangwa kutekelezwa chini ya fungu hili. Hivyo Bajeti ya Maendeleo katika fungu 38 Ngome haikutekelezwa kabisa.

Mheshimiwa Spika miradi iliyokuwa itekelezwe chini ya fungu hili ilikuwa ni ujenzi wa uwanja wa ndege Tanga, utafiti na ulinzi wa anga, ujenzi wa maghala ya mlipuko, ukarabati wa zana za ulinzi wa anga na ujenzi wa gati.

Mheshimiwa Spika, katika muktadha huo huo, fungu 39 (JKT) lilitengewa shilingi bilioni 4 kutekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa, lakini hadi kufikia Machi, 2016 hakuna hata senti moja iliyotolewa kwa ajili ya mradi huo.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaihoji Serikali; hivi kweli ina nia ya kujenga Jeshi la kisasa lenye ufanisi ikiwa haitekelezi bajeti ya maendeleo katika wizara hii iliyoidhinishwa na Bunge?

Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kutotekeleza bajeti ya maendeleo ya wizara hii, sio tu kunalifedhehesha Jeshi letu, lakini pia kinawaweka wananchi katika hali ya hatari kubwa. Kwa mfano wote tunafahamu jinsi matukio ya milipuko ya silaha katika maghala ya silaha za milipuko huko Mbagala na Gongo la Mboto – Dar es Salaam, yalivyosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa makazi ya wananchi. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali iliahidi kujenga na kukarabati maghala hayo ili kudhibiti ajali za milipuko. Lakini jambo la ajabu, Bunge limeidhinisha bajeti halafu Serikali haikutekeleza. Kambi Rasmi ya Upinzani inaionya Serikali kutofanya mzaha na masuala ya usalama, na kwa maana hiyo, tunaitaka Serikali kutoa maelezo ya kuridhisha mbele ya bunge hili; ni kwa nini haikutekeleza kabisa bajeti ya maendeleo katika fungu 38 na 39 kwa mwaka wa fedha unaomalizika wa 2015/16?

Mheshimiwa Spika, safari hii, katika fedha za maendeleo Serikali inaomba kuidhinishiwa shilingi bilioni 10 katika fungu 38 (Ngome) na shilingi bilioni 8 katika fungu 39 (JKT). Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji; kuna haja gani ya bunge kuidhinisha fedha hizi ikiwa fedha zilizoidhinishwa mwaka wa fedha 2015/16 hazikutumika kabisa? Serikali inalihakikishiaje bunge hili kwamba safari hii itatekeleza bajeti ya maendeleo kikamilifu kama itakavyoidhinishwa na bunge?

  1. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, nahitimisha hotuba yangu kwa kulipongeza tena Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa utumishi wao uliotukuka wa kuilinda nchi yetu kwa gharama ya uhai wao.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo,Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa viongozi wakuu wa Jeshi kuendelea kuwaelimisha wanajeshi walio chini yao kuzingatia maadili yao ya kazi, na kamwe wasikubali kutumika kisiasa kwa maslahi ya wanasiasa wachache wanaotaka kutimiza malengo yao ya kisiasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuacha kabisa kulitumia jeshi katika shughuli za kisiasa kinyume na Katiba ya chi na kinyume na kanuni zinazoongoza maadili ya kazi za Jeshi la Ulinzi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebaini pia kwamba, bajeti ya Wizara ya Ulinzi haitekelezwi ipasavyo. Tunataka Serikali itambue kwamba; kuchelewesha au kutopeleka kabisa fedha zilizoidhinishwa na bunge kwenye wizara hii ni kuuweka rehani ulinzi na usalama wa taifa hili. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, inaitaka Serikali kutofanya mzaha kabisa na bajeti ya wizara hii na kwa maana hivyo tunaitaka Serikali itelekeleze kikamilifu bajeti itakayoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

Juma Hamad Omar (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

KATIKA WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA

10 Mei, 2015
 
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia muda huu kumshukuru Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb) kwa kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mbowe alichaguliwa lini kuwa kiongozi wa upinzani ubungeni? Uchaguzi huo ulifanyika tarehe ngapi na ulihusisha wagombea gani? Alipata kura ngapi?

Kama haukufanyika kujiita kiongozi wa upinzani bungeni ni sahihi kisheria? Na kama hakuupata kwa uchaguzi nguvu ya kuteua anaitoa wapi?

Je hawa mawaziri vivuli wako kisheria kama aliyewateua hajachaguliwa kisheria kwa uchaguzi?
 
Mbowe alichaguliwa lini kuwa kiongozi wa upinzani ubungeni? Uchaguzi huo ulifanyika tarehe ngapi na ulihusisha wagombea gani? Alipata kura ngapi?

Kama haukufanyika kujiita kiongozi wa upinzani bungeni ni sahihi kisheria? Na kama hakuupata kwa uchaguzi nguvu ya kuteua anaitoa wapi?

Je hawa mawaziri vivuli wako kisheria kama aliyewateua hajachaguliwa kisheria kwa uchaguzi?

Swali hilo ungeenda kumuuliza Ndugai Spika wa Bunge na Waziri mkuu Majaliwa ambao wanamtambua na kumu address ka Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni.
Wewe ungeendelea kufanya kazi yako ya usafi hapo Lumumba haya mambo makubwa waache wakubwa zako wahoji kama wanaona kuna kasoro. Punguza kuwa na kiherehere dada yangu, heshima ya mwanamke utulivu na sio mapepe!
 
Mbowe alichaguliwa lini kuwa kiongozi wa upinzani ubungeni? Uchaguzi huo ulifanyika tarehe ngapi na ulihusisha wagombea gani? Alipata kura ngapi?

Kama haukufanyika kujiita kiongozi wa upinzani bungeni ni sahihi kisheria? Na kama hakuupata kwa uchaguzi nguvu ya kuteua anaitoa wapi?

Je hawa mawaziri vivuli wako kisheria kama aliyewateua hajachaguliwa kisheria kwa uchaguzi?


wimbo wa chris brown ule unaitwa zero zero zero zero mzuri sna.
 
Hili la wanajeshi kuteuliwa wakuu wa mikoa ni kizungumkuti cha makusudi kabisa .
 
Mbowe alichaguliwa lini kuwa kiongozi wa upinzani ubungeni? Uchaguzi huo ulifanyika tarehe ngapi na ulihusisha wagombea gani? Alipata kura ngapi?

Kama haukufanyika kujiita kiongozi wa upinzani bungeni ni sahihi kisheria? Na kama hakuupata kwa uchaguzi nguvu ya kuteua anaitoa wapi?

Je hawa mawaziri vivuli wako kisheria kama aliyewateua hajachaguliwa kisheria kwa uchaguzi?
Pole sana kijana , ukiona sabuni ina povu jingi sana ujue haitakatishi .
 
Eh hilo nalo neno anauliza swali la kizushi et mbowe kachaguliwa na nani ulitaka achaguliwe na nani ina maana hujui au kiherere chako tu.
 
Back
Top Bottom