Hongera wanasiasa

Tamu3

Member
Feb 17, 2023
25
16
HONGERA WANASIASA

1.
Waendapo majimboni, kuziomba hizo kura,
Utadhani wanadini, wenye za upole sura,
Magoti wapiga chini, mithili wataka pera,
Hongera wanasiasa, kudanganya wananchi.

2.
Hupita nyumba kwa nyumba, sera nyingi kimwageni,
Hudai kura waomba, wawakilishe bungeni,
Nguo zao hujipamba, zenye rangi ya kijani,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

3.
Fulana za bei ndogo, wanagawa mtaani,
Vijihela na majogo', watu wawagawieni,
Wanaupanua wigo, wao kuenda bungeni,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

4.
Lugha zile za asili, wajifanya kutumia,
Hawajui wakalili, kura nyingi kuzizoa,
Pamoja wala ugali, dhima ni kuwahadaa,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

5.
Kwa pombe za kienyeji, wote wawanunulia,
wapita vyote vijiji, ilani wakinadia,
Ahadi kuleta maji, na Safari kwenda jua,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

6.
Hutunga nyingi ngonjera, za kuvutia jukwani,
Lengo kuzipata kura, idhini kwenda bungeni,
Mshahara mshahara, wapate huko mbeleni,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

7.
Vitenge na hizo hela, ni nyingi uchaguzini,
Pia kanga na madela, hugawiwa mtaani,
Chakula pamoja hula, hongo ya kuwa diwani,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

8.
Kishashinda uchaguzi, kimbembe kinaanzia,
Wageuka kuwa wezi, kero wazipuuzia,
Vitenge na zile jezi, wanaacha kugawia,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

9.
Hawaendi majimboni, visingizio lukuki,
Wanahamia mjini, nyuma wameacha chuki,
Hawaendi vijijini, eti hakuna samaki,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

10.
Wanarudi majimboni, chaguzi kikaribia,
Nani awape idhini, awamu nayofwatia,
Heri wawekwe pembeni, mtu mpya kugombea,
Hongera Wanasiasa, kudanganya wananchi.

Denny Jeremias Kitumbika
Mtunzi wa Mashairi na ngano za Kiafrika
Mufindi TANZANIA

HONGERA WANASIASA
 

Attachments

  • 1710779238252.jpg
    1710779238252.jpg
    188.9 KB · Views: 1
Back
Top Bottom