Hitilafu ya umeme yakatisha uhai wa mtoto

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MTOTO Rahel Mathayo mwenye umri wa miaka 11 amekufa kwa kunaswa na umeme baada ya kugusa bomba la chuma la antena ya televisheni.

Inasadikiwa bomba hilo lilikuwa limegusana na nyaya za umeme.

Mtoto huyo, aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Kumbukumbu, wilayani Kinondoni alikutwa na mauti juzi saa 6:00 mchana katika eneo la Kinondoni Shamba.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema mtoto huyo aliyekuwa akicheza na wenzake, kwa bahati mbaya alishika bomba la chuma la antena la nyumba ya familia ya marehemu Mzaa Abdu, iliyo jirani na kwao.

Alinaswa na umeme na kutupwa chini na kupoteza fahamu na alikufa wakati akipelekwa hospitalini Mwananyamala.

Baba wa marehemu, Mathew Nassoro (60), alisema siku ya tukio, alitoka nyumbani kwake akaenda kwa mtoto wake wa kike anayeishi Kinondoni B kwa lengo la kumwangalia mjukuu wake aliyekuwa anaumwa.

Alisema wakati akiwa huko, alipigiwa simu saa 6 mchana na kuambiwa kuwa kuna hitilafu ya umeme na mtoto wake, ambaye ni kitindamimba kati ya watoto wake saba, amejeruhiwa.

Nassoro alisema kuwa kwa maelezo ya mashuhuda wa tukio hilo Rahel alikuwa ndani na ndugu zake lakini baadaye alisikia kelele za watoto wenzake wakimuita akaangalie hitilafu ya umeme katika nyumba ya jirani.

“Rahel alitoka ndani hajavaa hata viatu na mikono yake ilikuwa na maji na alipoenda moja kwa moja akashika ile nguzo alinaswa na kuna kijana aliyekuwepo maeneo hayo akamsukuma ili kumnasua lakini kijana huyu yeye alinusurika,” alisema Nassoro.

HABARILEO ilishuhudia nyumba hiyo ambayo wakazi wa eneo husika walisema nyaya za umeme zilikuwa zimegusana na mlingoti wa chuma ulioshikilia antena.

Wakati wa upepo mkali, inasadikiwa kulikuwa kukitokea hitilafu kutokana na nyaya hizo kugusana na chuma.

Mjumbe wa nyumba 10, Rashid Mohamed ambaye pia ni jirani wa nyumba hiyo, alisema msiba huo wameuona kama ajali zingine.

Alisema wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanesco (TANESCO) walifika katika nyumba hiyo yenye hitilafu na kukata umeme.

Walimwelekeza mwenye nyumba aunganishe nyaya vizuri. Kwa mujibu wa taarifa kutoka familia ya mtoto huyo, mwili wa marehemu unasafirishwa leo kwenda kijijini kwao Rubaya Chalinze Mkoa wa Pwani kwa ajili ya maziko.
 
ooh my god sijui wahusika walikuwa wamelaa au walikuwa wakisubiri mpaka madhara yatokee ndo wawajibike
Kuna vitu jamani inabidi tuwe tunavichukulia hatua mapema kabla madhara hayajatokea
RIP Rahel
 
KWeli hii ni hatari hasa kwa wabongo wanaopenda kutumia antena na kuzitundika kwenye mabomba ya chuma bila kuangalia athari zake.hata mimi ilishawahi kunitokea bahati nzuri nliwahi kuachia bomba la sivo na mm leo ningekuwa mbingu nyingine.watanzania waelimishwe madhara ya kutumia mabomba ya chuma badala yake watumie nguzo za miti au mabomba hayo ya chuma wayavike gamba la plastici tasaidia.RIP litle RAHEL
 
kuna umuhimu sana wa kujifunza elimu ya umeme na njia za kujikinga na hatari za umeme nadhani wataalamu wa mitaala waliangalie hili nakumbuka zamani tulikua na topics kama hizi mashuleni na baadae wakaziondoa!!wazazi wengi hawajui athari zinazoweza kujitokeza majumbani mwao hasa pale wanapoondoka kwenda makazini na kuwaachia nyumba mabeki 3 au mahousegirl ambao nao huwaacha watoto wakichezea cable za umeme bila kujua hatari yake ni nini!
 
Back
Top Bottom