Historia ya mageuzi nchini Tanzania kwa kifupi

Nicholas J Clinton

JF-Expert Member
Mar 13, 2014
877
486
HISTORIA YA MAGEUZI NCHINI TANZANIA KWA KIFUPI SANA

Binala. Nimerudi. Kama nilivyoahidi, nitarejea historia ya mageuzi ya kisiasa hapa nchini, japo kwa kudodosa kidogo tu. Ninayoandika hapa si magenni kwa kuwa huko nyuma, niliwahi kuyaandika/kuyasimulia kupitia jukwaa hili.

Vuguvugu la mageuzi ya kisiasa hapa nchini lilianza mwaka 1989; mijadala ya wazi na ‘uvunguni’ ilikuja kuhitimishwa kwenye kongamano la magauzi ya kisiasa na kikatiba la Juni 11-12/1991, katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Mojawapo ya maazimio (Tunachotaka Sasa) ya kongamano hilo ilikuwa kuundwa kwa Kamati ya Kuratibu Mageuzi ya Kisiasa na Kikatiba (National Committee for Constitutional Reform - NCCR). Kwa upande wa Zanzibar kamati ilijulikana kwa jina la KAMAHURU, ikongozwa na Mzee Shaaban Mloo (RIP) na wenzake. Kongamano lilimchagua Chief Abdalla Said Fundikira (RIP) kuwa mwenyekiti na wakili Mabere Nyaucho Marando kuwa Katibu wa NCCR.

Miongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo walikuwa Bwana James Mapalala, Mch. Christopher Mtikila (RIP), Mashaka Nindi Chimoto (RIP), mwandishi wa habari Ndimara Isaya Tegambwage, Mhadhiri wa sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Daktari Ringo Willy Tenga, Balozi Kasanga Tumbo (RIP), Mzee Kasela Bantu (RIP), na mwana diplamasia mahiri Prince Mahinja Bagenda. Kwa upande wa vijana walikuwepo akina James Francis Mbatia, Anthony Calist Komu, Idrisa Al-Nuru (RIP), na vijana wengineo. Akina Japhet Hassunga (Naibu waziri wa Maliasili na Utalii wa sasa) na rafiki yake Chimbombo baadaye walikuja kujiunga NCCR wakitokea IDM Mzumbe.

Kati ya Juni na Desemba 1991 kulitokea mabadiliko makubwa katika harakati za mageuzi ya kisiasa hapa nchini. Pengine kwa kutumia lugha ya kihandisi [majengo], tuseme kulitokea ‘expansion joints’ kwenye siasa za Tanzania. Ni katika kipindi hicho, Chief Abdulla Said Fundikira alisafiri bila kuaga Katibu na wajumbe wa NCCR (Kamati) kwenda nje ya nchi kuhudhuria kongamano la kimataifa la demokrasia na siasa za vyama vingi lililofanyika nchini Ujerumani/Hispania (sikumbuki vizuri).

Taarifa za kongamano hilo ziliripotiwa sana kupitia vyombo vya habari vya nje, hususan kupitia BBC na Deutsch Welle. Kongamano lilikuwa limeandaliwa mahsusi kwa ajili ya wanasiasa wa upinzani waliokuwa wanaibukia kudai mabadiliko ya kisiasa na kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi katika nchi zao barani Afrika. Miongoni mwa wanasiasa waliohudhuria kongamano hilo walikuwa ni pamoja na wanasiasa wa upinzani (Tanzania) waliokuwa wakiishi ughaibuni, wakati huo wakiitwa rebels – Bwana Salathiel Kambona na Bwana Ludovick Simon Mwijage.

Wakati wa kuhitimisha kongamano hilo, rebels wa Tanzania waliingia mgogoro na Chief Abdallah Said Fundikira juu ya nani afadhiliwe kuedeleza shughuli za kisiasa nchini. Akina Mwijage na Kambona wakitaka wapewe wao pesa wakati Chief Fundikira akitaka apewe yeye (mtu binafsi, siyo NCCR).

Mara baada ya kurejea nchini, Mabere Marando akiungwa mkono na vijana wenzake (Bagenda, Ndimara, Chimoto, Tenga) walitaka kumwajibisha mwenyekiti wao, Chief Fundikira. Hoja yao ilikuwa ni kwa nini alikwenda kuhudhuria kongamano hilo ‘kinyemela’ (bila kuaga wenzake) na alitakiwa eleze kikao kilichokuwa kimempatia mandate ya kukusanya pesa. Mwenyekiti Chief Fundikira hakujisumbua kujibizana na ‘vijana hao’, badala yake, kupitia Gazeti a Mfanyakazi wakati huo, tulisoma habari kuwa Chief Fundikira alikuwa ameanzisha chama ‘chake’ cha Union for Multiparty Democracy (UMD – sikumbuki mwezi, ila ilikuwa kati ya Oktoba na Desemba 1991). Akina Balozi Kassanga Tumbo, Mzee Kasela Bantu na baadhi ya wazee wengine waliamua kuondoka NCCR kwenda UMD, makao makuu yake yakiwekwa Magomeni [Mikumi] nyumbani kwa Chief Fundikira. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kumomonyoka kwa NCCR (Kamati).

Mara baada ya kuondoka kwa Chief Fundikira na Balozi Kassanga Tumbo, wana-Kamati walimteua Mabere Marando kuwa Mwenyekiti na Prince Bagenda kuwa Katibu wake. Mwandishi wa habari Stan Katabaro (RIP) akiandikia Gazeti la Mfanyakazi, aliandika na kushabikia sana [hata akijaribu kutengeneza] migogoro ndani ya NCCR. Baadaye ilikuja kugundulika kuwa maandishi ya Katabaro dhidi ya NCCR yalikuwa yakichagizwa na mgogoro binafsi uliokuwepo baina yake Ndimara.

Mparanganyiko wa NCCR haukuishia kwa kuundwa UMD/kuondoka kwa Chief Fundikira, la hasha. Kati ya Desemba 1991 na Februari 1992 James Mapalala naye aliondoka na kuanzisha Chama [chake]Cha Wananchi (CCW) – Mapalala akiwa mwenyekiti na Katibu Mkuu wake akiwa Dr. Alec Chemponda (RIP); Mch. Christopher Mtikila aliondoka NCCR akiambatana na Mwinjilisti Kamara Kusupa pamoja na Bwana Mahinbo Kaoneka na kisha kuanzisha Chama Cha Democrasia (CCD) – Kaoneka akiwa mwenyekiti, Kusupa Katibu Mkuu na Mch. Mtikila akiwa ‘Mlezi’. Viongozi wa CCD haikuwachukua muda kugombana na mlezi wa chama chao, kisha Mch. Mtikila akiungwa mkono na wafuasi wake akiwemo mlokole aliyeitwa Mwigandoshi, alitangaza kubadilisha CCD kutoka Kiswahili kuwa Kiingereza, yaani Democratic Party (DP), akiwaachia Kusupa na Kaoneka CCD yao. Ni wakati huo KAMAHURU walijitenga na NCCR kinyemela, kuungana na CCW na kisha kuunda chama cha The Civic United Front (CUF). Mwenyekiti akiwa James Mapalala na Katibu Mkuu Seif Sharif Hamad.

Hata hivyo, NCCR (Kamati) iliendelea kutandaa (networking) kupitia njia mbali mbali ikiwa ni pamoja na machapisho [Tunachotaka Sasa, Upinzani Siyo Uadui, Sera ya UZAWA]; kujitangaza kupitia magazeti [Radi (likimilikiwa na Ndimara Tegambwage), Mfanyakazi, Motomoto, Heko, Mshindi, Wakati ni Huu, Michapo, Family Mirror na kadhalika]; na kutembelea watu maarufu wenye mwelekeo wa kimageuzi kwa lengo la kuwashawishi, kuunga mkono NCCR. Hao ni pamoja na Bwana Wilfrem Mwakitwange (aliyekuwa mmiliki wa Rungwe Oceanic Hotels & Resort), Bwana Hillal Mapunda (aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Cha Siasa [Chama] Kivukoni), Mzee Mushendwa (mfanyabiashara aliyekuwa akiishi Morogoro), Daktari Walid Amani Kabourou (wakati akiwa likizo akitokea Marekani alikokuwa akiishi), Bwana Edwin Mtei na wengineo. Aidha, kupitia Prince Bagenda, Daktari Lingo Willy Tenga, waandishi wa habari Mbena Mwanatongoni (huyu sijui mahali aliko kwa sasa) na Anthony Ngaiza, Professa Mwesiga Baregu na Mashaka Nindi Chimoto, NCCR ilianzisha asasi ya kiraia ya African International Group of Political Risk Analysis (PORIS) ikiwa na dhima ya kuimarisha umahiri wa kiraia (civic competence) kwa watanzania, kueneza dhana ya mageuzi ya kisiasa miongoni mwa Watanzania.

Hadi kufikia Febriari 1992, wana-Kamati (NCCR) walikuwa wamebaini kuwa mwelekeo wa kisiasa nchini ulikuwa kuanzishwa vyama vipya vya siasa licha ya kutokuwepo kwa sheria. Kamati ilikuwa na hofu kuwa baadhi ya wana-Kamati (rogue elements) wangeweza kujitangazia isivyo rasmi kuwa NCCR ni chama chao hali ambayo ingesababisha mtafaruku kiasi cha kuua matokeo chanya ya kazi ya Kamati iliyokuwa imefanyika kwa miezi minane. Aidha ni wakati huo Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali ilikuwa imetoa ripoti na kupendekeza kwa Serikali kuwa Tanzania ianzishe mfumo wa siasa za ushindani wa vyama vingi. Serikali ya Rais Mwinyi na Chama Cha Mapinduzi chini ya Katibu Mkuu Horace Kolimba (RIP) iliitikia mapendekezo ya Tume ya Nyalali kuwa kunako mwezi Julai/ 1992, Tanzania ingeanza rasmi kuwa nchi yenye siasa za ushindani wa vyama vingi.

Februari 15/1992, wana-Kamati walikaa na kukubaliana rasmi kuwa NCCR ibadilike kutoka Kamati ya Mageuzi ya Katiba na kuwa chama cha siasa lakini kwa kubakiza jila la NCCR na kisha kuongeza mbele yake maneno MAGEUZI. Hivyo jina la chama likawa The National Convention for Construction and Reform (NCCR-MAGEUZI). Kabla ya hapo, wakati wa mashauriano, wajumbe walikuwa wamependekeza chama kipya kiitwe Chama Cha Demokrasia na Maendeleo. Hata hivyo, hofu ya kuachwa kwa jina la ‘NCCR’ kisha lije kutekwa na watu wenye nia mbaya na ku-water-down matokeo chanya ya kazi zake ilipelekea muafaka kuwa maneno ‘DEMOKRASIA NA MAENDELEO’ yabaki ila yawekwe na kuoonekana katikati ya logo/nembo ya Chama.

Mara baada ya NCCR-Mageuzi kutangazwa kuwa chama – Mabere Marando akiwa Mwenyekiti, Prince Bagenda akiwa Katibu Mkuu, Mashaka Chimoto akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Ndimara Tegambwage akiwa Katibu wa Habari na Uhamasishaji – chama kilienea nchi nzima kwa haraka sana, kikibebwa hususan na wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu nchini. Chama kiliunda na kuimarisha kamati za mikoa yote nchini. Chama kilipata misaada ya hali na mali kutoka kwa viongozi na watu mabalimbali – akina Gulam (huyu ni mtoto wa Mama Kero, mhindi aliyezaliwa na kukulia Bukoba), Alex Khalid (RIP) mmiliki wa Makondeko Holdings, Dr. Tenga, Prince Bagenda, Ndimara Tegambwage na Watanzania wengine waliokuwa wakiishi nje na ndani ya nchi. Mtanzania mmoja, Patrick Bamukunda (RIP), alijitolea gari lake na yeye mwenyewe kuendesha viongozi wa NCCR-Mageuzi muda wote na mahali popote ambapo wangetaka kwenda kwenye kazi za Chama. Wanafunzi kutoka vyuoni [vikuu] walifanya kazi za kueneza NCCR-Mageuzi kwa kujitolea.

Mwezi Mei/1992 uongozi wa NCCR-Mageuzi ulimkaribisha Mzee Edwin Mtei kujiunga na chama hicho. Prince Bagenda akiambatana na James Mbatia, walikwenda kwa Mzee Mtei, nyumbani kwake USA River, Arusha wakiwa na ujumbe rasmi wa chama kumkaribisha Mzee Mtei kujiunga na NCCR-Mageuzi. Mzee Mtei alitaka apelekewe andiko la Sera na Katiba ya NCCR-Mageuzi asome kwanza kabla ya kufanya uamuzi wa kujiunga na chama hicho. Alipendekeza apelekewe nyaraka hizo nyumbani kwake Dar es Salaam na kwamba baada ya kuzisoma angeitisha mkutano kukutana na uongozi wa NCCR-Mageuzi. Nyaraka zote ziliandaliwa na kuwasilishwa kwake kama zilivyokuwa zimeombwa.

Mwanzoni mwa Juni/1992, baada ya kusoma Sera na Katiba ya NCCR-Mageuzi, Mzee Mtei aliwaita viongozi wa NCCR-Mageuzi akutane nao nyumbani kwake Dar es Salaam kuwapa maoni na/au kujadiliana nao kuhusu pendekezo/kuombwa ajiunge kwenye cha NCCR -Mageuzi. Wakiwa nyummbani kwake, Mzee Mtei aliwaambia viongozi wa NCCR-Mageuzi kama ninavyonukuu, “vijana kuna watu wengi wenye ‘means and substance’ wanataka mimi nianzishe chama. ,,,kwa hiyo, nitaanzisha chama, ninawashauri mvuje chama chenu, ninawakaribisha mje kujiunga kwenye chama changu”, mwisho wa kunukuu. Marando alimjibu Mzee Mtei kwa kumwambia kuwa chama cha NCCR-Mageuzi kimekwisha kuanzishwa na kuwepo, hivyo hawakuwa tayari kuvunja chama hicho. Kwamba Mzee Mtei aendelee na jitihada zake za kuanzisha chama chake ila akisha kunyeshewa na mvua kama wao, ‘wangekutana wakati wa wakijikinga mvua’.

Wiki moja baadaye Mzee Edwin Mtei akiwa na marafiki zake; Bob Makani (RIP), Edward Barongo (RIP), Mzee Ngwilulupi (RIP) na wengineo, wakiwa wamevaa suti na suruali zikining’inia kwenye suspenders, waliitisha Press Conference pale Motel Agip, Dar es Salaam, kutangaza kuanzishwa chama kipya kikiitwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Ukweli wa kihistoria ni kuwa Mzee Mtei na wenzake hawakufanya mental work bali walitumia jina, sera na katiba ya NCCR-Mageuzi kuanzisha Chadema.

Baada ya expose’ hii sasa ninaamini kuwa taarifa ya kihistoria nilyoiandika kwenye Buriani ya Daktari Walid Amani Kabourou imeeleweka.

Niliandika yafuatayo, “....Hitoria ya Dr. Walid Amani Kabourou, katika siasa za upinzania hapa nchini haikuanzia Chadema, la hasha.
Mwaka 1992, akiwa safarini kwenda USA, Dr. Kabourou alipitia ofisi ya makao makuu ya NCCR-Mageuzi, mtaa wa Mchikichi Dar es Salaam. Dr Kabourou alinunua kadi (sikumbuki namba yake) ya NCCR-Mageuzi baada ya kukutana na viongozi wa chama hicho; Mabere Marando, Prince Bagenda, Ndimara Tegambwage na Mashaka Nindi Chimoto (RIP).

Itakumbukwa kuwa kifo cha Mh. Mbano kilitokea katika muda ambapo pia kulitokea kifo cha Mh. Stephen Kibona aliekuwa waziri wa fedha wakati huo katika serikali ya Rais Mwinyi. Kwa hiyo, kulikuwa na majimbo mawili - Ileje na Kigoma mjini - yaliyofanya uchaguzi mdogo kwa wakati mmoja mwaka 1993.

Katika jitihada za kutafuta wagombea, kwa kuwa wakati huo Chadema hakikuwa na watu zaidi ya old guards wake akina Bob Makani (RIP), Edward Barongo (RIP) na wengineo, mwenyekiti wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei, alisafiri hadi USA kumfuata Dr. Walid Amani Kabourou. Mzee Edwin Mtei alimwambia Dr. Kabourou ujumbe wa uongo kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi na Chadema vilikuwa vimekubaliana kugawanya majimbo - kwamba NCCR-Mageuzi kiweke mgombea jimbo la Ileje wakati Chadema kikiweka mgombea katika jimbo la Kigoma mjini. Kwamba safari ile alikuwa ametumwa na uongozi wa NCCR-Mageuzi (Mabere Marando) ampelekee ujumbe Dr. Kabourou ahamie Chadema ili aweza kugombea ubunge jimbo la Kigoma mjni; kisha akampatia kadi ya Chadema.

Ni bahati mabaya kuwa tangu awali siasa za upinzania nchini Tanzania zimeendelea kujengwaa kwenye misingi ya uongo. Na ni uongo huo uliopelekea safari ya Dr. Walid Amani Kabourou kujiunga na Chadema.

Mabere Marando, baada ya Kamati ya Utendaji ya NCCR-Mageuzi kumuagiza apige simu kwa Dr. Kabourou kumtaarifu kuwa chama kilikuwa kimemteua aje kugombea ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini, Dr. Kabourou alibaki midomo wazi na kumwambia Marando kuwa tayari alikuwa ameingia makubaliano/amesaini form za Chadema kugombea ubunge kupitia chama hicho [baada ya kuelezwa kuwa kulikuwa na makubaliano baina ya Chadema na NCCR-Mageuzi].”

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Waraka huu umenikumbusha mbali sana.

Vijana inabidi muusome ili muielewe Chadema na jinsi ilivyoasisiwa.

Motel Agip lilikuwa chimbo la wazee wajanja wajanja na mwenyeji wao alikuwa Tuntemeke Sanga rip aliyekuwa anaishi hotelini hapo huku akiwa ni mbunge wa porini huko Makete!

Ahsante mleta mada!
 
Ulianza vizuri ila umeharibu ulipojaribu kuiingiza CHADEMA hapo ionekane sio lolote sio chochote.

Wapinzani tukiendelea hivi hatutofika kokote. Hakuna anayepinga wanasiasa 80% wa upinzani walianzia NCCR ila haibadili ukweli kwamba wamefikia level za juu kuliko NCCR yenyewe.

CUF ilifika hadi kuwa na makamu wa Rais zenji pamoja na baraza la mawaziri. CHADEMA pia imefanikiwa kubeba hadi wabunge 70+ na halmashauri zaidi ya 20 na na kuweka rekodi ya kura nyingi zaidi ya Urais katika historia ya upinzani.

Mkubali mlikosea so mnajirekebisha ila kuanza kukashifu kina Maalim na Mtei haitowasaidia kitu afterall hta huyo Marando aliishia kuja CHADEMA!!

Leo hii CHADEMA imelea vijana wengi tu ambao hawaijui hta NCCR na wamefika bungeni je kuna mkono wa NCCR? Chadema umepata nguvu wakati wa Mbowe naye alianzia NCCR?

ACT ilianzishwa na 90% ya wanachadema na leo hii kimeenea Zanzibar yote so CHADEMA nao wachukue credit kwa hilo?

Kama tunataka kuitoa CCM tuwe wamoja tukianza kutunishiana misuli hatutofika kokote. NCCR mnawahitaji Seif na Mbowe ili kupata kura nyingi otherwise sioni political base yenu ilipo unless mnategemea wagombea wa CHADEMA waliofukuzwa!!
 
Asante kwa historia nzr kuhusu harakati za mabadiliko ndani ya nchi yetu...Nccr Mageuzi mkitaka mrudi kwenye ramani ya ushindani wa kisiasa bc jitengeni na ccm na njama zao..lkn mkitaka mbeleko toka ccm bc mjue ndo mtabakia jina tu..wananchi wa kipindi hk ni welevu wa Mambo tofauti na kipindi hicho, mnapotumika kuubomoa upinzani bc jueni mnajibomoa wenyewe na kamwe hamtasimama tena ..msitake kupambana na chadema bali pambaneni na ccm, hapo mtafanikiwa lkn c kwa wapinzani wenzenu...hakuna chama kwa sasa ambacho ni tumaini kwa watanzania na kwa wanaccm zaidi ya chadema..ukipambana na chadema ujue unapambana na watanzania kwa ujumla..nadhani hata serikali iliyoko madarakani hawajalitambua hilo... chadema ni mpango wa mungu
 
Unekosea Sana kuingiza CHADEMA. Nadhani CHADEMA ni self made haihitaji kuwa kwenye mgongo wa nccr. Hata Mwalimu Nyerere alikitabilia makubwa kipindi kikiwa chama kidogo Sana miaka hiyo.
 
Back
Top Bottom