Hatuwezi kuendelea kwa kuiga na kuigiza.

Saint Ivuga

JF-Expert Member
Aug 21, 2008
54,363
58,386
Hatuwezi kuendelea kwa kuiga na kuigiza.

Kwa mujibu wa maandiko ya misahafu ya dini za mapokeo, tunaambiwa sisi Waafrika ni wa uzao wa Hamu mwana wa Nuhu, aliyelaaniwa na Baba yake baada ya kumchungulia alipokaa uchi akiwa amelewa. Kwa tafsiri hii ni kwamba, Mwafrika amelaaniwa, kama jinsi Ibil...isi alivyolaaniwa kwa kuwadanganya Adamu na Hawa, wakala tunda walilokatazwa shambani Edeni. Pengine ni kutokana na laana hii, Bara la Afrika limepachikwa jina la “Bara la Giza” lisilo na matumaini na lenye kuhitaji kustaarabishwa. Tunaambiwa, Shetani, yule mwovu adui wa Mungu, ni mweusi, ambayo ndiyo rangi ya Mwafrika. Hata Malaika ni weupe; Baba Mtakatifu (Papa) hachaguliwi kwa moshi mweusi; bali kwa moshi mweupe, ambayo ndiyo rangi ya Mungu na Malaika. Mwana wa Hamu ni mtu mwenye akili duni; wenzetu wa Ulaya na Marekani, ambao ni wana wa Shemu, wanadai wana akili kutuzidi sisi. Wao walituzwa kwa kupewa kipaji cha kufikiri na kutawala wengine, kwa sababu Baba yao Shemu, hakumtazama Mzee Nuhu katika hali yake isiyo rasmi, kama alivyothubutu Mswahili wetu Hamu. Ndiyo maana wana wa Shemu kama Sir Richard Burton, anavyodiriki kuandika bila aibu: “ Mwafrika afikiapo umri wa utu uzima, akili yake hudumaa; na kuanzia hapo hukua kiakili kwa kurudi nyuma, badala ya kwenda mbele” Naye Sir Anthony Ellis, anaandika katika kitabu chake “The People’s of the Slave Coast of West Africa”, ifuatavyo: “Mwafrika afikiapo umri wa kubalehe, akili yake hudumaa; hawezi kubuni wala kuunda kitu; hubakia kuiga na kuigiza kama Sokwe-mtu” Tumepachikwa sifa na majina ya kuchukiza na hawa hawa tunaofikiri ni wenzetu, wabia kwa fursa sawa katika maendeleo, chini ya dhana mpya ya utandawazi. Tunaweza kuyakataa majina haya, tukidai kwamba tumeendelea, na kwamba sifa tunazopewa ni za uongo, zenye lengo la kumdhalilisha Mwafrika. Lakini matendo yetu yanaweza kutusuta, pamoja na kwamba karibu tuna kila kitu cha asilia cha kujivunia. Tatizo letu ni kwamba hatujiamini. Tumejidekeza na kuwa watu wa kupokea tu, bila kutoa mchango katika maendeleo ya dunia, isipokuwa jasho letu kwa njia ya kunyonywa. Maneno ya Anthony Ellis, japo ni makali na yenye kudhalilisha Utu wetu, tutayakanaje, wakati sisi Waafrika bado tunawaua Ma-Albino na vikongwe kwa imani za kishirikina katika karne hii ya 21; wakati wenzetu wanajenga makao mapya mwezini? Kama huko si kudumaa akili kwa mtu mzima, ni nini? Tunakataaje kwamba sisi ni watu wa kuiga na kuigiza, kama sokwe-mtu, kama tunaweza kusafiri hadi Uingereza kuazima majina ya kidini – Johnson, Winterbottom, Wilberforce, George, Dickson; au Uarabuni kuazima majina – Mahmood, Haroub, Hussein na mengine mengi, eti kwa sababu tu yana ladha nzuri? Kuna kosa gani kuitwa Jidundufila, Magere, Maganga, Masalakulangwa au Mwakipesile? Afrika ilijua demokrasia kabla ya Wazungu. Kwa nini, kama si kuiga mithili ya Sokwe-mtu, tunakumbatia demokrasia ya kigeni, inayopwaya katika mazingira yetu na kutupa shida? Kwa jadi ya Kiafrika, watawala walichaguliwa na kutawala kwa njia ya haki. Walioondolewa madarakani sawia pale walipoonekana kukiuka maadili na misingi ya utawala. Wananchi hawakuwasubiri kipindi cha uchaguzi ndipo waweze kuwaondoa. Ni aina gani hii ya demokrasia kwa Afrika, kwa viongozi mafisadi kutoona haya, na kujiondoa sawia, mpaka wazomewe na wananchi kwa uchafu wao? Je, huku si kuwageuza wananchi wajinga wasio na macho wala akili ya kufikiri? Nimemsoma R. S. Rattray, katika kitabu chake: Ashanti Law and Constitution, jinsi watawala wa Ghana walivyoonywa waingiapo madarakani hapo kale, kwa maneno yafuatayo: “Mwambieni (mtawala) kuwa hatutaki awe mwenye tamaa; hatutaki atudharau, wala asiwe mgumu wa kusikia. Hatutaki atuite wajinga au wapumbavu; hatutaki atukashfu, wala kusababisha ghasia” Ni demokrasia gani hii leo Afrika, kwa viongozi wa watu kujali maslahi yao zaidi, kuliko maslahi ya watu wanaodai kuwaongoza, kama si akili kudumaa? Kwa nini viongozi wenye tamaa, dharau na wagumu wa kusikia, wameendelea kushikilia madaraka na kusababisha mfarakano katika jamii? Kitendo cha kuruhusu viongozi wahalifu kuendelea kushika madaraka kwa gharama ya umma, kunajenga kile kinachoitwa “Part–time democrasy” – Demokrasia ya muda, kinyume na “Full-time democracy” – Demokrasia ya wakati wote. “Part-time democracy” ina maana ya kuwanyima wananchi uwezo wa kuwashughulikia ipasavyo viongozi wabovu hadi uchaguzi unaofuata, hata kama uovu wao ni wa kuangamiza nchi na haki za wananchi. Kama huko si kudumaa akili ni nini? Kwa sababu ya kupenda kuiga na kuigiza kama sokwe-mtu, tumebeza na kukashifu ibada na jadi zetu kwa kukumbatia miungu wa kigeni. Tumekubali kupotoshwa kwamba Mwafrika hakumjua Mungu mmoja hadi Wazungu walipofika kumstaarabisha. Kama Mzungu Collingham Gardens (na wengine) ameamua kusema ukweli katika kitabu chake. “Ntu”, kwamba tangu kale Mwafrika aliamini dunia na binadamu waliumbwa na Mungu mmoja, na kwamba Mungu huyo anao wasaidizi, kama vile tu zinavyoamini dini zingine, kwa nini tunamwabudu Mungu wetu kwa tamaduni za kigeni, kama si kuiga na kuigiza? Hivi ni mpaka tusemewe na watu kama Benjamin C. Ray, katika “African Religions: Symbols, Ritual and Community”, kwamba “Kwa dini za Kiafrika, kule kutambua tu kuwapo kwa Wasaidizi wa Mungu ni kielelezo cha kuwapo Mungu”, ndipo tuthamini asili yetu? Ray anasema, na mimi nakubaliana naye, kwamba ni ujinga kutotambua nafasi ya Watabiri (wa kweli), na waganga wa jadi katika jamii za Kiafrika, kwani hakuna jamii isiyokuwa na wanasayansi wake, kwa kuzingatia mazingira ya kila jamii. Dini za jadi, kama ulivyo Ukristo, Uislamu na zinginezo, zinaamini kifo, ufufuo na maisha ya milele ijayo. Hebu angalia Placid Temple, katika kitabu chake “Bantu Philosophy”, anavyobainisha kwa usahihi, fikra za Mwafrika katika jambo hili: “Wafu wetu hawako kaburini, wako kwenye moto unaozimika, wako kwenye majani yanayojililia, wako kwenye miamba inayosota; wako porini, wako ndani ya nyumba; wafu hawakufa, wala hawatakufa milele” Zipo habari za kitheolojia kuhusu imani za kale za Mwafrika zinazopashwa kufanyiwa utafiti wa kina, na kuoanishwa na imani za dini za kimapokeo, ili kujenga imani imara na thabiti kwa Mwafrika. Kufanya hivyo, si kukana au kutengua imani za dini za sasa, Ukristo, Uislamu, Uhindu, Ubuddha, n.k. Inaaminika, Waafrika walikuwa na Biblia yao. Kitabu cha “The Book of Coming Forth, Day and Night” cha Waafrika kinaeleza karibu mambo yote ya msingi yaliyomo kwenye Biblia na Kurani, mambo kama vile, Amri 10 za Mungu, Uzazi kwa uweza wa roho Mtakatifu, ufufuo, Uumbaji na mengine mengi. Tunaambiwa juu ya Isis, Mwanamke wa Kiafrika aliyezaa mtoto kwa uweza wa ajabu, Horus, kama ilivyotabiriwa na Manabii. Tunaambiwa juu ya Osiris, Mwafrika anayesemekana kutumwa na Mungu kuuokoa Ulimwengu, na baadaye akauawa; na inasemekana alifufuka kusubiri hukumu ya mwisho. Kuna habari za kina Ng’wanamalundi, Gor Mahia na wengine, ambao habari za miujiza yao zinaweza kuandika matoleo tele ya vitabu. Matukio haya ni ya maelfu ya miaka kabla hata Bikira Maria hajazaliwa. Lakini habari hizi hazijaandikwa katika Biblia au Kurani kwa sababu Mwafrika ni wa uzao wa Hamu, aliyelaaniwa. Sir Anthony Ellis hajakosea, kwamba hatuna uwezo wa kubuni wala kuunda kitu; tumebakia kuiga na kuigiza tu. Alipobuni mashindano ya Mrembo wa Dunia mwaka 1951, Eric Morley na mkewe Julia, hawakuwa na rangi wala umbo la Mwafrika akilini mwao. Walibuni kwa ajili ya Wazungu wenzao. Lakini leo, dada zetu wa Kiafrika nao wamo, wakiiga na kuigiza visivyowalenga wao; hata rangi ya ngozi yao hawaitaki tena;. Wanaiona rangi nyeusi ni laana ya Hamu; ni rangi isiyo na hadhi. Wanataka kufanana na wale Wakoloni waliotutawala, na ambao wanarejea kwa mlango wa nyuma kwa dhana ya soko huria; wamejikana wenyewe, wakiuona Uafrika ni mzigo wa dhambi. Lugha ni kielelezo cha utamaduni wa jamii. Bara la Afrika ndilo pekee kati ya mabara matano duniani, lisilowakilishwa kwa lugha katika Umoja wa Mataifa kwa sababu utamaduni wetu hautikisi nyavu za Kimataifa. Na kuhusu sayansi na teknolojia, nakubaliana na Daniel F. Mccall na E. Bay, wanavyosema katika kitabu chao “African Images”, kwamba, “Hakuna jamii isiyo na wanasayansi wake; hakuna elimu ya sayansi na teknolojia katika jamii iliyo duni; kwani hata ile iliyoendelea ilikuwa na pa kuanzia”. Kinachotakiwa ni kuikubali, kuienzi na kuiboresha ili iweze kukidhi mahitaji ya jamii inayobadilika. Kosa kubwa tunalofanya ni kujikana wenyewe na kuchagua kuiga na kuigiza. Source; Raia Mwema News Paper By Joseph Mihangwa
 
Back
Top Bottom