HakiElimu yakemea tukio la ukatili wa Mwalimu Mkuu Kagera, yatoa mapendekezo kwa Serikali

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,813
11,991
Mkurugenzi wa HakiElimu, John Kalage amesema tukio la mtoto wa Shule ya Msingi Kakanja, Wilayani Kyera Mkoani Kagera kuchapwa katika njia ambayo ilionekana ni ya kikatili limewasikitisha kwa kiwango kikubwa.

Kalage.jpg


Ameeleza tukio hilo lililotekelezwa na Mwalimu Mkuu wa shule husika ambapo picha za video zinamuonesha akitoa adhabu kwa kukangaga miguu ya wanafunzi, kinakiuka haki ya mtoto na pia ni kinyume na maadili ya Ualimu, malezi na maadili bora ambayo mwalimu anatakiwa kuyatekeleza kwa Wanafunzi.

Kalage ameipongeza Serikali kwa uamuzi wa haraka iliouchukua mara baada ya video ya tukIo hilo kusambaa mitandaoni.

Amesema: “Tumeona jinsi ambavyo Waziri wa Elimu, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Waziri Gwajima wote wamekemea na kuchukua hatua.

“Tukio hilo ni sehemu ya matukio mengi ya ukatili na unyanyasaji kwa Watoto shuleni yanayotokea nchini.

“Mfano ripoti ya Polisi ya matukio ya Ukatili ilibainisha kuwa visa vya ukatili kwa watoto vilivyoripotiwa viliongezeka kwa 25.9% ambayo ni sawa na 26% kutoka visa 5,800 kwa Mwaka 2019 hadi visa 7,400 vilivyoripotiwa mwaka 2020.

“Kutokana na juhudi zinazoendelea za Serikali na tasisi mbalimbali kuhusu ukatili, tulitegemea hivi visa vingepungua lakini bado vinazidi kuongezeka.”

Akitoa mifano kwa kukumbushia matukio ya ukatili alitaja tukio la Mwaka 2006 katika Shule ya Sekondari ya Mbeya (kutwa), iliripotiwa tukio la Walimu watatu kumpa adhabu ya viboko, ngumi na mateke hali iliyosababisha mwanafunzi huyo kulazwa.

Pia, anasema Mwaka 2018 mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta, Bukoba Mkoani Kagera, alifariki kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa Mwalimu.

Kalage 2.jpg


TAFITI YA HAKI ELIMU
Kalage amesema “Taarifa yetu ya utafiti wa Haki Elimu ya Mwaka 2020 imeonesha takribani 88% ya Watoto wa Shule waliripotiwa kufanyiwa ukatili wa kimwili, huku takribani 90% ya watoto hao waliofanyiwa utafiti walieleza kuwa ukatili waliofanyiwa ulitokana na adhabu ya viboko shuleni.

“Pia katika utafiti huo, 55% ya Watoto walisema Walimu wao na walezi wamekuwa wakitumia ngumi na mateke kama sehemu ya kutoa adhabu kwa watoto."

Ameongeza kuwa pamoja na jitihada za Serikali, bado Taifa linaonekana kuendelea kukumbatia adhabu ya viboko kwa watoto shuleni.

“Kwa mujibu wa Muongozo wa Elimu juu ya Adhabu ya Viboko ya Mwaka 2002, inaeleza kuwa Mwalimu Mkuu anaruhusiwa kutoa adhabu hiyo au kukasimisha kwa mwalimu mwingine kwa maandishi.

“Pamoja na hivyo, muongozi huo unapewa nguvu na Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 na mabadiliko yaliyofanyika mwaka 2002, ambayo chini ya kipengele za 60 kinaruhusu utolewaji wa adhabu mbalimbali kama sehemu ya kuboresha nidhamu kwa Watoto

“Pamoja na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 ambayo inakataza vitendo vya kikatili kwa mtoto, lakini haitoi katazo la adhabu za kikatili kama adhabu ya viboko,” anasema Kalage.

Anaongeza kuwa “Madhara ya adhabu za kikatili yameelezwa vizuri katika mafunzo ya Walimu kama vile maumivu ya aina mbalimbali kwa mtoto au kujenga chuki kati ya mwalimu na mwanafunzi na inaweza kuchangia mtoto kutopenda shule.

“Tafiti zimeonesha Walimu wanapendelea adhabu ya viboko kuliko adhabu nyingine.

Tunajua wanashauriwa kutumia mbinu mbadala kutoa adhabu kwa Wanafunzi kuliko viboko, mfano kutumia vichocheo hasi ili kuwafanya wanafunzi kutoendelea na tabia mbaya, lakini kwa kuwa Sheria inaruhusu wao wanaona ni sahihi kuendelea kutumia viboko.

"Pia adhabu hizo zinatolewa pasipo kufuata muongozi kwa kuwa muongozo unaeleza kuwa Mwalimu Mkuu ndiye anatakiwa kutoa adhabu au kukasimu kwa maandishi na kuna idadi ya viboko, lakini kinachoendelea katika shule kadhaa ni uchapaji holela.

"Kutokana na matukio haya tunashauri Serikali kuchua hatua za kukomesha kabisa adhabu za viboko shuleni, badala yake zitafutwe namna bora za kuwaadhibu wanafunzi.

“Hatupingi kuwaadhibu watoto lakini tunaweza kutafuta namna bora ya kuwaadhibu, tunachopinga ni ukatili unaovaa sura ya adhabu.

“Tunashauri Serikali ipitie Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978, Muongozi wa Elimu wa mwaka 2002 na Sheria ya Mtoto ili kukwepa kushughulika na tukio mojamoja, kwa kuwa yapo mengi yanayotokea lakini hayajafika kwenye jamii.”

MAPENDEKEZO YA HAKI ELIMU
Tuweke utaratibu wa Shule zote 18,000 za Tanzania (12,000 Msingi na 5000 za Sekondari) kuwa na program ya Shule Salama hili liingie katika muongozo wa elimu.

Pili, mipango endelevu ya kuimarisha ulinzi rasmi wa watoto shuleni. Mwaka jana, Doroth Gwajima alianzisha muongozo wa kuwa na dawati la kuzuia ukatili, tunafikiri madawati hayo yaanzishwe katika kila shule.

Kutoa elimu kwa Wanafunzi, wazazi na wanajamii au wowote pale ambapo watoto wanakusanyika, tukishirikiana wote tutapunguza masuala ya kikatili wanayofanyiwa watoto.

Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wote wanaofanya ukatili kwa watoto

Mafunzo ya walimu yahusishwe utoaji adhabu chanya kwa watoto ili usihusishe ukatili, pia hii itasaidia watoto wenye changamoto ya tabia pindi wanapokabiliana na Walimu.

Miiko ya walimu iangaliwe ili wale wanaoshindwa kuzuia au wanashabikia matukio ya aina hiyo nao wanatakiwa kuwajibishwa, ukikaa kimya inamaanisha na wewe umeshiriki.

Masomo yanayohusu maadili yafundishwe na walimu wenye uwezo ili kuwawezesha wanafunzi kuwa na uelewa sahihi wa kitabia na kimaadili.

Haki Elimu.jpg
 
Back
Top Bottom