Mama Amon
JF-Expert Member
- Mar 30, 2018
- 2,021
- 2,479
Hivi, katika mazingira ambako mabaki ya mtu aliyekufa hayawezi kupata huduma za mazishi zinazotolewa na dini za kigeni kama vile Ukristo, Uislamu, Uhindu, na Ubuda, utaratibu gani wa kisheria unapaswa kutumika katika kuendesha mazishi ya mabaki ya mwili wa marehemu?
Nauliza swali hili kutokana na tukio la tarehe 26 Desemba 2020. Siku hiyo walifariki watu wanne wa familia moja, akiwemo baba, mama na watoto wao wawili, kutokana na ajali ya moto iliyotokea katika Mtaa wa Sahare Majengo Mapya, Kata ya Mzingani jijini Tanga.
Waliofariki ni baba wa familia, Sigfrid Kimbi (44), mkewe Aurelia Shayo na watoto wao, Samweli Kimbi (9) na Ezra Kimbi (7). Miili yao ilisafirishwa hadi Moshi, nyumbani kwa Kimbi kwa ajili ya mazishi. Walizikwa tarehe 29 Desemba 2020 kwenye Kitongoji cha Kisomboko, Uru Mawella, Moshi Vijijini, Mkoani Kilimanjaro.
Tukio hilo limeleta majonzi kwa wengi kwa sababu mbili. Kwanza, siku zote kifo kinahuzunisha watu wengi.
Na pili, siku zote kifo huzalisha majukumu kwa watu waliobaki hai kuhusiana na kazi ya kuhifadhi mabaki ya mwili wa marehemu. Kuna wafiwa, maafisa wa ustawi wa jamii, na viongozi wa dini, japo kila kundi linabeba majuku kwa sababu tofauti na malengo tofauti.
Safari hii, utekelezaji wa majukumua haya uliambatana na utata baada ya watoto wawili kuzikwa kwa heshima zote za Kikristo wakati wazazi wao wakinyimwa heshima hiyo.
Jambo hili lilimfanya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, kutoa kauli ambayo ilionyesha kuwa pale viongozi wa dini wanapojitoa kwenye jukumu la kuendesha ibada ya mazishi, basi, Taifa halina utaratibu mbadala kisheria kuhusiana na suala zima la mazishi ya raia.
Kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971, inafahamika kuwa kuna ndoa za aina tatu hapa nchini Tanzania:
- Ndoa zinazofungwa kwa kufuata utaratibu wa dini za kigeni kama vile Ukristo, Uislamu, Ubuda na Uhindu;
- Ndoa zinazofungwa kwa kufuata utaratibu wa dini za kimila (ATR); na
- Ndoa zinazofungwa kwa kufuata utaratibu wa kiserikali bomani.
- Utaratibu wa mazishi ya wana ndoa ambao ndoa zao zilizofungwa kwa kufuata utaratibu wa dini za kigeni kama vile Ukristo, Uislamu, Ubuda na Uhindu;
- Utaratibu wa mazishi ya wana ndoa ambao ndoa zao zilifungwa kwa kufuata utaratibu wa dini za kimila (ATR); na
- Utaratibu wa mazishi ya wana ndoa ambao ndoa zao zilifungwa kwa kufuata utaratibu wa kiserikali bomani.
Utaratibu huu ni muhimu na lazima kwa kuwa, kila kundi la wanandoa linastahili kupata ibada ya mazishi ya kipekee.
Kwa mfano, katika macho ya Kanisa Katoliki, ndoa ambazo hazijafungwa Kikristo zinakuwa hazijakidhi viwango fulani, na hivyo wahusika hawana haki ya kupata huduma ya ibada ya mazishi yanayolingana na heshima ya Kikristo.
Padre wa parokia walikokuwa wanasali baba, mama na watoto alithibitisha ukweli huu aliposema kwamba, kwa mujibu wa taratibu za Kanisa Katoliki, hakuwa na jukumu la kuwazika baba na mama kwa vile walikuwa wanaishi kama mke na mume bila kufunga ndoa kulingana na taratibu za ndoa ya kikristo.
Mwongozo Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kuhusu mazishi uliomo katika Kitabu Kilichaandikwa na Marehemu Askofu wa Moshi Amedeus Msarikie, unasema yafuatayo:
Kwamba, Sheria ya Kanisa Katoliki namba 1177 hadi 1185 inasema kuwa ni haki ya kila muumini mkatoliki kufanyiwa Ibada ya mazishi ya Kikristo isipokuwa kama amepoteza haki hiyo kutokana na ukaidi wake mwenyewe.
Kwamba, haki hiyo inatokana na jinsi marehemu wakati wa uhai wake alivyotimiza wajibu wa Kikristo kwa mamlaka ya Kanisa na jumuiya nzima ya Kikristo.
Kwamba, kwa kuwa ibada ya mazishi ya Kikatoliki kama tendo lolote la Kiliturujia ni alama na ishara wazi ya mshikamano wa kikristo, basi, inamaanisha kwamba, ibada hiyo inapotolewa lazima umoja wa Kanisa uonekane wazi, na kwamba, wanaopokea mazishi hayo ni lazima wawe wameonyesha umoja wa Kanisa kwa maisha yao.
Kwamba, kwa wakristo waliojitahidi kuishi vizuri maisha yao ya Kikristo wanapaswa kupatiwa huduma ya mazishi ya Kikristo katika parokia yake na mazishi hayo yanapaswa kuongozwa na Paroko au Paroko msaidizi au Katekista au muumini mwingine aliyeidhinishwa na paroko kutekeleza wajibu huo.
Kwamba, Wakristo waliojitenga na mshikamano wa Kikristo wanapoteza haki zao katika kanisa ikiwa ni pamoja na haki ya kupata mazishi ya Kikristo, ambapo wafuatao wanahusika: Wale walioasi kanisa kwa kufuata mafundisho ya dini nyingine; Wale waliojitenga na kanisa kwa kutosali kinyume cha amri ya tatu ya Mungu na Amri ya kwanza ya Kanisa; Wazushi katika mafundisho ya imani, kwa maana ya watu wanaojiita wakristo wakatoliki lakini wanafundisha kinyume na viongozi wa kanisa katoliki wanavyofundisha; na watu wanaokataa utaratibu sahihi ulioanzishwa na viongozi wa kanisa katoliki, kwa mfano utaratibu wa kusali katika Jumuiya ndogo ndogo ulioanzishwa na kanisa.
Kwamba, Wakristo waliojitenga na kanisa kwa kuukataa ukweli unaofunuliwa na Mungu au ukweli uliotangazwa na viongozi wa kanisa, wanapoteza haki zao katika kanisa ikiwa ni pamoja na haki ya kupata mazishi ya Kikristo, ambapo wafuatao wanahusika: Waliobatizwa lakini baadaye wakatenda dhambi ya heresia (heresy) kwa kukaidi ukweli ambao ni lazima kuusadiki kwa mujibu wa imani ya kanisa katoliki; Wale wanaotenda dhambi ya apostasia (apostasy) kwa kukana dini Katoliki mbele za watu; Wale wanaotenda dhambi ya skisma (schism) kwa kukataa mamlaka ya Kanisa, yaani kukataa kukiri mamlaka halali ya Baba Mtakatifu, Maaskofu, Mapadre na Mashemasi;
Kwamba, Wakristo wanaohusishwa na dhambi za waziwazi na zenye kuwakwaza wakristo wengine (public scandal), wanapoteza haki zao katika kanisa ikiwa ni pamoja na haki ya kupata mazishi ya Kikristo, ambapo wafuatao wanahusika: Wakristo wenye ndoa za mitara; Majambazi wanaotishia maisha ya watu kwa kutumia silaha; Wale wanaofuata mila zenye upotofu mkubwa unapingana na kanisa kwa mfano kurithi wajane, kukubali kurithiwa kama mjane, kutambikia mizimu, na kufanya kufunga ndoa ya jinsia moja; Wale wenye imani za ushirikina, mfano mganga wa kienyeji, mchawi anayefahamika, kupiga ramri, na kumkaribisha mganga wa kienyeji nyumbani.
Kwamba, Wakristo wanaopotosha mafundisho ya viongozi wa kanisa kwa makusudi, wanapoteza haki zao katika kanisa ikiwa ni pamoja na haki ya kupata mazishi ya Kikristo, ambapo wafuatao wanahusika: Wale wanaokufuru Ekaristi takatifu, mfano kuiba Ekaristi Takatifu, kuitupa, kuichezea; Wale wanaotupilia mbali wajibu wa kutunza familia; Wale wanaowatesa wanafamilia wenzao kwa ukatili mkubwa; Wale wanaodharau desturi takatifu za kanisa Katoliki mfano kuiba vitu vya kanisa, kuchoma au kuharibu vitu vitakafu kwa makusudi kama vile rozari na visakramenti vingine; Wale wanaochochea kuzuka kwa madhehebu potofu miongoni mwa wakatoliki; Wale wanaojihusisha na vitendo vya kuua watu, mfano kwa kuwadhania kuwa ni wachawi, kuwaua walemavu wa ngozi.
Na kwamba, Jumuiya ndogo ndogo zinayo “mamlaka ya kushauri” (consultative power) kwa vyombo vya Kanisa vyenye mamlaka ya “kutoa uamuzi” (deliberative power) juu ya nani apewe ibada ya mazishi na yupi asipewe, kwa kuwa, ni wana jumuiya ndogo ndogo wanaoweza kuonyesha kuwa huyu mtu aliishi imani yake vizuri au alikuwa na vizuizi vilivyotajwa hapo juu au hapana.
Kimsingi, hizi ni taratibu za kidini kwa ajili ya kujiimarisha kitaasisi kwa kuchora mstari unaoweza kutenganisha watu wote waliobatizwa na kupata kibali cha kuitwa wkristo katika kundi la "sisi wakristo bora" dhidi ya kundi la "wao wakristo duni."
Hata hivyo, naona kuwa, Sheria ya Kanisa Katoliki namba 1177 hadi 1185 ni batili kwa kiwango kile ambacho zinapingana na Katiba ya Kanisa Katoliki iitwayo Mwanga wa Mataifa (Lumen Gentium). Kwa mujibu wa ibara ya saba ya Katiba hii, tunaambiwa:
"Maana kwa ubatizo tumefananishwa na Kristo: “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja” (1Kor 12:13). Katika ibada hii takatifu ushirikiano wetu na kifo cha Kristo na ufufuko wake huonyeshwa kwa ishara na kutekelezwa: “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake”; na “kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake” (Rum 6:4-5)." (Lumen Gentium 1968, ib.7)
Ni kwa sababu hii, wakati wa mazishi ya Kikatoliki, kuna sala muhimu inayosema kuwa, kama ambavyo marehemu alivyoshiriki ubatizo wa Kristo, vivyo hivyo, anaombewa ili upate fursa ya kushiriki ufufuko wake siku ya mwisho.
Kwa hiyo, kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa tajwa, kigezo kilicho cha lazima na chenye kutosheleza mahitaji ya kutofautisha kati ya Mkristo na mtu asiye Mkristo ni sakramenti ya ubatizo, isipokuwa kama muumini amewahi kukana imani yake baada ya kupokea ubatizo huo.
Yaani, "unless recanted after its administration, baptismal sacrament is a the only indelible, necessary and sufficient criterion of Christian membership and the pertinent rights and obligations."
Hayo masharti mengine yote ni nyongeza inayoweza kuhojiwa na mtu yeyote makini, kwa sababu kadhaa, moja ikiwa kwamba, masharti haya yanaweza kuchochea uvunjifu wa amani katika jamii.
Lakini hii sio hoja yangu kuu kwa sasa. Hoja yangu kuu hapa ni kwamba, katika Taifa ambalo linaongozwa na serikali isiyofungamana na dini yoyote, kanuni hizi haziwezi kuwa kanuni za jumla kwa kuwa, katika Taifa la aina hii, kuna watu wasiofuata dini yoyote na wanaopaswa kuzikwa baada ya kufa; kuna watu wa dini moja lakini walio katika madhehebu tofauti wanaozikwa kwa kufuata desturi tofauti; na kuna watu wanaopinga kwa hoja halali baadhi ya mafundisho ya viongozi wa kanisa, na hasa yale yasiyokubalika kisayansi na kimantiki, na wanapaswa kuzikwa baada ya kufa.
Kwa hiyo sasa, swali pana linalozuka hapa ni kwamba, katika mazingira ambako mabaki ya mtu aliyekufa hayawezi kupata huduma za mazishi zinazotolewa na dini za kigeni kama vile Ukristo, Uislamu, Uhindu, na Ubuda utaratibu gani wa kisheria unapaswa kutumika katika kuendesha mazishi ya mabaki ya mwili wa marehemu?
Kama utaratibu huu ungekuwa bayana, RC Mghwira asingejikuta anakwaruzana na paroko wa Kanisa Katoliki.
Nimeangalia sheria ya kusajili Vizazi na Vifo (birth and death registration act) pamoja na sheria ya kutunza Afya ya Umma (public health act) lakini sikuona mwongozo mzuri juu ya jambo hili.
Ni kama vile siku zote Taifa limekasimu madaraka ya kuzika mabaki ya raia wake kwa taasisi za kidini bila kuona hatari iliyoko mbeleni, na hasa pale, sheria za kidini zinapozalisha ubaguzi holela unaoweza kuwa chimbuko la "public nuisance" inayoongelewa kwenye sheria ya utunzaji wa afya ya jamii.
Hivyo naomba kuwauliza enyi learned fellows: Ni sheria gani zinapaswa kutumika kuratibu haki na majukumu yanayohusiana na mazishi ya marehemu ("burial rights and duties") hapa Tanzania?
Nyumba iliyoteketea kwa moto huko Kilimanjaro juzi na kuua watu wanne