Fahamu mbinu mbalimbali za kuongeza mauzo ya biashara yako

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Jana tuliona kwamba mzunguko wa fedha ndio damu ya biashara yako. Kama mzunguko huu usipokuwa vizuri basi biashara yako itadhurika. Na kama mzunguko huu utasimama basi biashara nayo itakufa. Tuliona baadhi ya njia za kuhakikisha mzunguko wako wa fedha upo vizuri.

Leo tutaangalia eneo muhimu sana la kuhakikisha mzunguko wa fedha kwenye biashara yako unakuwa mzuri. Eneo hili ni mauzo. Mauzo ndio yanaleta fedha kwenye biashara yako na hivyo kama ukiongeza mauzo maana yake unaongeza fedha zinazoingia. Japokuwa hili halimaanishi kwamba ukiongeza mauzo umeongeza faida, la. Tutaangalia kwenye makala zijazo jinsi ya kuhakikisha unapata faida ya kukutosha. Leo tuangalie kwanza kuhusu mauzo ya biashara yako na jinsi ya kuyaongeza.

Kabla hatujaona mbinu tano ambazo unaweza kuzitumia kuongeza mauzo kwenye biashara yako naomba nijibu swali muhimu sana ambalo unaweza kuwa unajiuliza, je inawezekana mauzo ya biashara yangu kuongezeka? Jibu ni ndio, haijalishi biashara yako ipo kwenye hatua gani, bado una nafasi ya kuongeza mauzo zaidi ya unayofanya sasa. Kikubwa ni kujua mbinu sahihi za kutumia ili uweze kuongeza mauzo yako.

Kwa kuwa tuko sawa sasa ya kwamba mauzo ya biashara yako yanaweza kuongezeka, sasa unayaongezaje? Hapa ndio zinakuja mbinu tano muhimu unazoweza kutumia kuongeza mauzo yako.

Mbinu ya kwanza: Uza bidhaa zinazoendana kwa pamoja

Mteja anapokuja kununua bidhaa kwako, tayari amejipanga atanunua bidhaa au huduma fulani. Unaweza kumuuzia bidhaa hiyo na akaondoka, unakuwa umepata mauzo ya kile alichotaka na mambo yanaishi hapo. Ila ukiwa mfanyabiashara mjanja unaweza kumuuzia ile bidhaa anayotaka na pia ukamjulisha kwamba kuna bidhaa nyingine ambayo inaweza kutumika kama hiyo. Au kama zikitumika pamoja basi zitaboresha maisha yake kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano kama mtu amenunua nguo muuzie na viatu, na begi la nguo. Kama mtu amenunua kompyuta, mwambie kuna vitu muhimu anahitaji kununua ambavyo vitafanya matumizi ya kompyuta yake kuwa mazuri. Kwa mfano kuweza kuhifadhi data zake sehemu tofauti ili zisipotee kompyuta inapopotea. Kama mtu akinunua kitabu kimoja mwoneshe na vitabu vingine ambavyo vitampatia maarifa zaidi.

Kwenye biashara yoyote unayofanya, kuna bidhaa nyingi unazoweza kuuza kwa pamoja. Fanyia kazi hili.

Mbinu ya pili: Uza bidhaa yenye uhitaji mkubwa

Ni rahisi mtu kununua tiba kuliko kununua kinga. Ndivyo binadamu tulivyo, kama hakuna tatizo kubwa linalotusumbua basi hatuhangaiki kutafuta suluhisho.

Ni kazi yako kama mfanyabiashara kuangalia biashara yako vizuri na kuangalia matatizo ya watu, ni matatizo gani ambayo yanawaumiza na wanatafuta sana suluhisho. Kisha wapatie suluhisho la matatizo yao kupitia biashara yako.

Kwa mbinu hii utapata wateja wengi ambao wana matatizo na wanatafuta suluhisho la matatizo yao.

Mbinu ya tatu: Toa punguzo na weka muda wa kuisha kwa punguzo hilo

Tengeneza aina yoyote ya ofa kwenye biashara yako ila weka muda maalumu ambapo ofa hii itakuwepo. Sio lazima ofa yenyewe iwe kubwa na ya kuathiri biashara yako. Kikubwa ni kutengeneza mazingira ya utofauti kwenye biashara yako ambayo yatamvutia mteja kununua zaidi.

Na unapoweka tarehe ya mwisho wa ofa yako na ukawa unawakumbusha wateja mara kwa mara kwamba ofa inakwisha watasukumwa kufanya maamuzi haraka kabla nafasi hiyo haijaisha.

Mbinu ya nne: Weka bei zako vizuri

Bei zako inaweza kuwa sababu ya watu kununua au ikawa kikwazo cha watu kununua. Sio mara zote ukiweka bei ndogo ndio unapata wateja wengi, kuna wakati ukiweka bei kubwa ndio unapata wateja bora zaidi.

Kwa kuwa hili la bei linahitaji mbinu zake pia, tutalijadili kwa undani kwenye makala inayofuata.

Mbinu ya tano: Boresha huduma unazotoa kwa wateja wako

Hakuna kitu ambacho kila mtu anapenda kama kupata huduma bora, kama kuona anajaliwa na kama kuona kwamba yeye ni muhimu. Ukijenga biashara yako kwenye misingi hii ya kumjali na kumpatia huduma nzuri mteja wako, mteja ataridhika na hataweza kukaa kimya. Atawaambia wengi zaidi na hivyo utakuwa na wateja wengi na mauzo yako kuongezeka.

Wateja ulionao sasa ni sehemu nzuri sana ya kukuza biashara yako kwa sababu ni wao ambao wataisema biashara yako vizuri. Na pia wanaweza kuwa sehemu ya kuiua biashara yako kama watapata huduma mbovu na kuanza kuisema biashara yako vibaya.

Fanyia kazi mbinu hizi tano na utaona mabadiliko makubwa kwenye mauzo yako.

===========

Wateja


Haijalishi huduma au bidhaa yako ni kubwa kiasi gani, biashara yako haitazalisha pesa kama wateja hawatakuwa tayari kununua bidhaa au huduma yako. Hakuna wateja, hakuna biashara.

Tatizo la kukosa wateja hukabili sana biashara ndogo, na hata kusababisha biashara hizo kufa. Siyo kwamba wateja hawapendi kununua bidhaa za biashara hizi, bali tatizo kubwa ni mbinu duni za kujitangaza na masoko.

Katika makala hii nitakueleza mbinu 10 rahisi na za gharama nafuu ambazo unaweza kuzitekeleza na ukaongeza au kuvutia wateja zaidi kwenye biashara yako.

1. Lugha nzuri
Katika mambo yanayowapotezea wafanyabiashara wengi wateja ni lugha mbaya kwa wateja. Hakuna mteja anayependa kupokelewa au kujibiwa vibaya. Hakikisha unazungumza na wateja wako kwa namna bora ambayo wataona unawajali, unawathamini na kuwaheshimu.
Mimi mwenyewe ninapenda kwenda kwenye biashara ambayo wahusika wana lugha nzuri; huwa nawashauri pia rafiki zangu kwenda kwenye biashara za aina hiyo. Hivyo hakikisha unatumia mbinu hii ili kuongeza wateja.

2. Huduma au bidhaa za bure

Wateja wengi wanapenda vitu vya bure au zawadi. Siyo lazima ufanye jambo kubwa la bure ili kuwavutia wateja; hata jambo dogo tu linaweza kuwavutia sana. Ili kuwavutia wateja unaweza kutoa huduma au vitu vya bure kama vile kalamu, mifuko, shajara (diary) au hata maji ya kunywa. Kwa njia hii utawavutia wateja wengi zaidi.

3. Punguzo
Punguzo ni njia bora sana ya kukabiliana na ushindani wa kibiashara na kupata wateja. Ikiwa mwenzako anauza sabuni kwa shilingi 2,100, wewe uza 2,050. Unaweza usipate faida kubwa kwenye bidhaa moja lakini utapata faida kubwa kwenye mauzo ya jumla. Kwa mfano ikiwa faida kwenye sabuni hapo juu ni sh. 100, muuzaji wa kwanza akauza sabuni 5 kwa sh. 2,100 atapata faida ya sh. 500. Lakini wewe ukauza sabuni 20 kwa sh. 2,050 utapata faida ya sh. 1,000. Je huoni kuwa umeuza na kupata faida zaidi kutokana na kuvutia wateja wengi kupitia punguzo? Weka punguzo sasa.

4. Shindano
Siyo lazima uwe na pesa nyingi ndipo uweze kuendesha shindano. Unaweza kuendesha shindano lenye zawadi ndogo kama vile vocha, kalamu, mikoba, shajara au hata vinywaji.
Kwa njia ya kuweka shindano watu wengi watavutiwa kununua bidhaa au huduma zako ili wawe washindi. Unaweza pia kuweka bidhaa au huduma zako kama kitu cha kushindaniwa badala ya zawadi nyingine.

5. Anzisha tovuti au blog
Watu wengi hawafahamu umuhimu wa tovuti au blog. Wengi hufikiri kuwa ni mahali pakuweka matangazo ya watu wengine ili wakulipe.Ukweli ni kuwa blog au tovuti ni muhimu sana kwa ajili ya kuongeza wateja kwa njia ya kutangaza biashara yako.Ukiwa una blog nzuri yenye watembeleaji wa kutosha, unaweza kuitumia kutangaza na kuuza bidhaa zako wewe mwenyewe na ukajipatia pesa nyingi.

6. Tumia mitandao ya kijamii
Kama ilivyo kwa blog na tovuti, vivyo hivyo mitandao ya kijamii inaweza kutumiwa kuzalisha pesa nyingi. Ikiwa unataka kuongeza wateja, basi wafahamishe watu kupitia mitandao ya kijamii juu ya huduma au bidhaa zako. Hakikisha wanazielewa na kuweza kuzifikia kwa urahisi.

7. Matangazo

Biashara nyingi hupuuza nafasi ya kujitangaza ili kuongeza wateja na hatimae kupata faida zaidi. Siyo lazima utumie njia za gharama kubwa kujitangaza kwani zipo njia nyingi sana.
Unaweza kutumia mitandao (rejea mbinu ya 5 na 6), vifungashio, saini ya barua pepe (email signature), card ya utambulisho wa biashara (busness card), vipeperushi n.k.

8. Toa misaada
Je umeshawahi kujiuliza kwanini biashara na kampuni nyingi hutoa misaada mbalimbali? Je ni kwa kuwa wana pesa za ziada au wanawapenda sana wale wanaowasaidia?
Ni wazi kuwa hii ni mbinu nzuri sana ya kujitangaza na wala si vinginevyo. Kwa njia ya kutoa misaada wateja huongezeka zaidi kwani watu huifaahamu biashara husika, pia huichukulia kama biashara inayowajali zaidi. Kumbuka siyo lazima utoe misaada mikubwa au ya pesa nyingi. Unaweza kutoa hata bidhaa zako au huduma yako kama msaada kwa watu au taasisi fulani.

9. Lenga changamoto
Watu wananunua bidhaa au huduma fulani ili itatue changamoto zao. Hivyo kuendesha biashara isiyolenga changamoto za wateja haitapata soko. Hebu fikiri mtu anaanzisha duka la kuuza dawa za Ebola Kenya au Tanzania, je atapata wateja kweli? Ni wazi kuwa hatapata wateja kwani tatizo la Ebola kwa Tanzania na Kenya ni dogo sana. Hivyo ili kuongeza wateja hakikisha unakuwa mbunifu na kulenga changamoto na mahitaji ya wateja.

10. Shirikiana na biashara au kampuni kubwa
Hebu fikiri kampuni kama Vodacom au Airtel wakikutaja kwenye matangazo yao kuwa wewe ni wakala wao; je unafahamu ni nini kitatokea? Moja kwa moja utafahamika zaidi pamoja na kile unachokifanya na utaongeza wateja zaidi. Kumbuka kushirikiana na kampuni au biashara nyingine kubwa hukufanya pia uaminike zaidi kwa wateja.

Hitimisho
Naamini sasa umeona jinsi unavyopoteza wateja na faida bila sababu yoyote ya msingi. Fanyia kazi mbinu jadiliwa hapo juu nawe kwa hakika utaweza kuongeza wateja na hatimaye kupata faida zaidi.

Michango ya wadau:
Endapo una mtaji mdogo na unataka kuanza na kukuza biashara yako. Fanya yafuatayo;

1. JIPE MUDA, BIASHARA HAITAWEZA KUKUA HARAKA KAMA UNAVYOFIKIRI
Uzuri wa kuanza biashara na mtaji kidogo ni kwamba kila mtu anaweza kufanya hivyo. Lakini pia urahisi huu wa kuanza biashara kwa mtaji kidogo unafanya ukuaji wa biashara kuwa wa taratibu sana. Hivyo unapofanya biashara yoyote ambayo unaanza na mtaji kidogo ni muhimu ukajipa muda ili kuweza kukuza mtaji wako.

Usiwe na tamaa ya kutaka kukuza biashara hii haraka, unaweza kuingia kwenye maamuzi ambayo yatakugharimu zaidi. Endelea kufanya biashara yako huku ukijifunza zaidi na kuangalia kila fursa ambayo unaweza kuitumia kukuza biashara yako.

2. KUZA MTAJI WAKO TARATIBU
Kwa mtaji huo mdogo ambao umeanza nao biashara, endelea kuukuza kila siku. Usiendeshe biashara kwa kula kila kipato unachopata, badala yake tenga sehemu ya akiba irudi kwenye biashara yako.

Fanya hivi kwa nidhamu ya hali ya juu sana na unahakikisha kila unapopata faida sehemu inarudi kwenye biashara yako.

Pia endelea kuangalia kwa mazingira uliyonayo na kwa biashara unayofanya ni kwa jinsi gani unaweza kukuza mtaji wako zaidi. Kama utafikiria hili kila siku, hutakosa majibu ambayo yatakusaidia.

3. PUNGUZA GHARAMA ZA BIASHARA NA ZA MAISHA PIA
Kuwa kwenye biashara haimaanishi kwamba ndio una uhuru wa kufanya chochote unachotaka na fedha za biashara hiyo, kwa sababu tu ni zako. Wewe sasa upo kwenye wakati mgumu wa kukuza biashara yako huku ukiwa huna njia nyingi za kufanya hivyo.

Hebu kwa sasa punguza kabisa gharama zako za kibiashara na za maisha pia. Kama kitu sio muhimu sana basi usikigharamie. Punguza matumizi yote ambayo ni ya anasa tu na sio kwa ukuaji wa biashara. Katika kupunguza gharama zako za biashara na maisha, jijengee nidhamu nzuri sana ya fedha. Usitumie fedha kiholela tu, kuwa na mahesabu na sababu kwa nini umetumia fedha fulani, hasa kwa matumizi ambayo sio ya kawaida.

4. ANGALIA WATU AMBAO UNAWEZA KUSHIRIKIANA NAO
Baada ya kuiendesha biashara yako vizuri na ukaona inaenda kwa faida, unaweza kuangalia watu ambao unaweza kushirikiana nao kwenye biashara hiyo. Kuna watu wengi ambao wanaweza kuwa na mtaji lakini hawana muda wa kufanya biashara.

Lakini pia watu hawa wanataka mtu ambaye wanaweza kumwamini. Hivyo kama unaweza kuaminika angalia watu unaoweza kushirikiana nao kibiashara.

Andaa mpango mzuri ambao utamshawishi mtu ni jinsi gani yeye atafaidika kama atawekeza kiasi kidogo kwenye biashara yako. Ikiwa unaendesha biashara yako kitaalamu itakuwa rahisi zaidi kushawishi watu kushirikiana na wewe.

5. RASIMISHA BIASHARA YAKO ILI KUJIWEKA KWENYE NAFASI NZURI YA KUPATA MKOPO
Hata kama biashara yako ni ndogo kiasi gani, irasimishe. Iendeshe kisheria kwa kuwa na namba ya mlipa kodi na hata leseni pia. Hivi vitakuwezesha wewe kutambulika na taasisi za kifedha pale utakapohitaji msaada zaidi wa kifedha.

Mkopo kwenye taasisi za kifedha ni chanzo muhimu ila usikimbilie kama bado hujaweza kuiendesha biashara yako kwa faida. Hakikisha umeiweka biashara yako vizuri kwanza na inajiendesha kwa faida ili unapochukua mkopo unajua unauweka wapi na kuendelea kupata faida zaidi.

Kuikuza biashara pale ambapo umeanza na mtaji kidogo ni kitu ambacho kinawezekana. Ila unahitaji kujitoa na kujenga nidhamu kubwa. Unahitaji kufanya kazi zaidi ya wafanyabiashara wengine, unahitaji kuwa mbunifu wa hali ya juu na pia unahitaji kujijengea uaminifu.

Ukishajua wewe biashara yako ni ndogo na inahitaji kukua, basi hakikisha kila mara unaumiza akili yako ifikirie njia zaidi za kuikuza. Na kama utaweza kufanya hivi basi utaziona fursa nyingi zilizokuzunguka za kuikuza biashara yako.
----
Habari rafiki?
Changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, hivyo ujanja siyo kuzikimbia changamoto, bali kukabiliana nazo na kuzishinda ili kuweza kusonga mbele zaidi. Hii ndiyo sababu kupitia AMKA MTANZANIA tuna kipengele cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia malengo makubwa tunayojiwekea kwenye maisha yetu.

Karibu kwenye makala yetu ya leo ambapo tunakwenda kupeana ushauri juu ya changamoto zinazowazuia watu kuanza biashara. Kwa zama hizi tunazoishi sasa, biashara ni kitu muhimu mno, iwe umeajiriwa au hujaajiriwa, unahitaji kuanzisha na kukuza biashara yako ili kuweza kujitengenezea uhuru wa kifedha. Na siyo lazima uache kazi yako ndiyo uanzishe biashara, kama ambavyo nimeeleza kwenye kitabu hiki; kukipata) unaweza kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa.

Imekuwa ndoto ya wengi kuanza biashara, lakini maswali ya awali kabisa ni nifanye biashara gani? Nianzie wapi? Nipate wapi mtaji? Nipate wapi soko la uhakika? Sasa leo kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto, tunakwenda kuangalia pa kuanzia, namna ya kupata soko, mtaji na hata jinsi ya kuikuza biashara yako. kabla hatujaingia kwenye ushauri wenyewe, hebu tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Mimi ni mpambaji, nadarizi ila nasumbuliwa na mtaji na soko na ni mfugaji mzuri wa kuku wa mayai ila kwa sasa nipo nipo tu sijui hata pakuanzia naomba ushauri wenu na msaada wenu. Amina S. A
Hiyo ndiyo changamoto kubwa inayomsumbua msomaji mwenzetu, na nina hakika wapo wengi ambao wana changamoto kama hiyo. Swali ni je unatokaje hapo ulipo? Moja kwa moja tunakwenda kuangalia hatua unazoweza kuchukua, tukitumia mfano wa msomaji mwenzetu na mingine kwenye hali kama hizo.

HATUA YA KWANZA; Anzia hapo ulipo, hiyo ndiyo biashara uliyonayo tayari.

Kitu kimoja ambacho nataka kukuambia mwanzo kabisa ni kwamba hapo ulipo tayari una biashara, ni wewe kuijua na kuanza kuifanyia kazi. Je kuna kitu ambacho unapenda kufanya? Au kuna kitu ambacho una ujuzi nacho? Je kuna uzoefu wowote umepitia kwenye maisha yako ambao wengine hawajaupitia? Je kuna elimu uliyopata ambayo wengine hawana au wanaihitaji? Au je umeajiriwa au kuna watu walishakulipa kutokana na kitu ulichokifanya? Kama umejibu ndiyo kwenye swali lolote kati ya hayo hapo juu, basi tayari biashara unayo.

Kwa mfano wa msomaji mwenzetu hapo juu, ana ujuzi wa kupamba na wa kudarizi. Tayari ana biashara, tena nzuri sana ya kupamba na kudarizi. Kwa mwingine inawezekana ni ujuzi wa afya, au kilimo. Mwingine anaweza kuwa anapenda kuandika, mwingine kuimba. Mwingine anapenda kufuatilia michezo, au kutumia mitandao ya kijamii. Vyote hivi unaweza kuvigeuza na kuwa biashara.

HATUA YA PILI; Angalia ni nani mwenye uhitaji wa kile unachofanya au unachotaka kufanya.

Ukishajua kile ambacho unacho, ambacho ndiyo unakigeuza kuwa biashara yako, angalia ni watu gani watahitaji huduma au bidhaa yako. Angalia ni watu gani ambao wana shida au mahitaji ambayo wewe unaweza kuyatimiza kupitia kile ambacho unakifanya.

Kwa msomaji wetu aliyetuandikia, wateja wake ni watu wanaofanya sherehe mbalimbali kama harusi au mahafali. Wateja wake pia ni watu wanaopenda mavazi yaliyodariziwa.
Kama vitu unavyofanya wewe ni vingine, angalia watu gani wanaweza kunufaika navyo.

Kama unapenda kufuatilia michezo, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika kupitia yale unayofuatilia leo. kama unapenda kutumia mitandao ya kijamii, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika kupitia wewe kuwa kwenye mitandao ya kijamii. Kama unapenda kuandika, angalia ni watu gani wanaweza kunufaika na kile unachoandika. Kila unachofanya, wapo watu ambao wanakitafuta kwa hamu, ni jukumu lako kuwajua na kuwafikishia kile unachofanya.

HATUA YA TATU; Wape watu kile unachotoa bila ya malipo.

Hapa ninachukulia kwamba unaanzia chini kabisa, ambayo ni sehemu nzuri sana kuanzia kwa sababu sasa hivi huna namna ambavyo unatengeneza kipato. Hivyo unaweza kutoa huduma zako kwa wengine bila hata ya kulipwa. Kama unachotoa ni bidhaa basi anza kutoa kwa bei ya chini sana, ambapo hupati faida yoyote. Lengo ni watu wakujue wewe ni nani kwanza, hapo ulipo sasa hakuna anayekujua na hata ukiwaambia kuna kikubwa unaweza kufanya hakuna anayeweza kukuamini, hivyo unahitaji kujijengea uaminifu.

Kwa msomaji mwenzetu aliyetuandikia hapa, anaweza kuanza kutoa huduma zake za upambaji bure kabisa. Angalia sherehe mbalimbali zinazofanyika pale unapoishi na omba kujitolea kupamba bure kabisa, wao wanunue tu mapambo. Au kama hizi hakuna, tafuta watu wanaofanya upambaji, ambao tayari wameshajijengea majina, waombe kujitolea kuwasaidia kazi bure kabisa, wasikulipe chochote. Lengo hapa ni wewe ujifunze, pamoja na kuwaonesha wengine kile ambacho unacho. Pia kwenye kudarizi hivyo hivyo, anza kudarizi vitu vya nyumbani kwako/kwenu na wasaidie watu kudarizi. Kadiri watu wanavyoona kazi zako ndivyo wanavyotaka kufanya kazi na wewe.

Kwa shughuli nyingine kama uandishi, tafuta njia ya kuwafikishia watu maandishi yako kwa bure kabisa. Anza kwa kuwa na blog, na andika mara kwa mara, kwa kuanza fanya kila siku, andika hata kwa siku mara mbili au mara tatu, andika sana, andika vitu ambavyo mtu akivifanyia kazi maisha yake yatakuwa bora.
Kama unachofanya ni kufuatilia michezo, anza kuwapatia watu uchambuzi wa ile michezo ambayo unafuatilia, toa historia za ile michezo ambayo unaifuatilia, hakikisha watu wanapotaka taarifa kuhusu michezo hiyo, wanakuja kwako kwanza.

Hatua hii ya tatu ni hatua muhimu kwani hapa ndipo watu wanapokujua na kuanza kuwatengenezea utegemezi. Wafanye watu wakutegemee wewe kupitia kile ambacho unawapatia. Kumbuka kwenye hatua hii hakuna faida yoyote unayotengeneza, unatengeneza jina kwanza.

HATUA YA NNE; Anza kutoza gharama kwa wale wanaotaka zaidi ya unachotoa.

Ukishatengeneza jina lako, na watu wakaanza kukutegemea kutokana na matokeo bora unayotoa, sasa unaweza kuanza kuwatoza watu kwa kile cha ziada wanachotaka uwafanyie. Ni wakati gani w akufanya hivi utaona tu inakuja yenyewe, watu wataanza kukuuliza wenyewe kama unaweza kuwasaidia kwenye mambo yao yanayohusika na unachofanya, na wao wenyewe watakuuliza wakulipe kiasi gani. Hii ndiyo hatua muhimu kwako kujenga msingi sahihi na imara wa kibiashara.

Kwa mfano ambao msomaji mwenzetu ametuandikia, hapa ndipo unapoanza kutoa huduma yako ya upambaji kwa gharama. Hapa umeshatengeneza jina lako, umeshashiriki kwenye sherehe nyingi na watu wameanza kuambiana kuhusu wewe. Hapa umeshawaangalia wengine wanaofanya wana mapungufu gani na wewe unakuja na suluhisho bora kabisa.

Kama ni uandishi watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwapa ushauri wa moja kwa moja, au kama kuna vitabu umeandika ambapo watu wanaweza kujifunza zaidi. Kama ni matumizi ya mitandao, watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwatangazia biashara zao kupitia mitandao ya kijamii. Kama ni ufuatiliaji wa michezo, watu wanaanza kukuuliza kama unaweza kuwaelimisha zaidi kuhusu michezo hiyo, au kuwasaidia kutabiri michezo hiyo. Yapo mengi ambayo watu watahitaji kutoka kwako.
Unapofikia kwenye hatua hii ya nne, unahitaji kuwa umepitia biashara za wengine na kuona ni vitu gani unahitaji kufanya tofauti ili uwe bora zaidi ya wengine.


HATUA YA TANO; Kuza biashara yako.

Unapofika hatua hii ya tano sasa una biashara ambayo ina wateja, ambao wapo tayari kukulipa ili kupata bidhaa au huduma unayotoa. Hapa sasa ndiyo unaweza kusema una biashara, na unachohitaji kufanya hapa ni kuikuza biashara yako. unaweza kuona ndiyo sehemu rahisi, lakini ukweli ni kwamba hii ni sehemu ngumu, kwa sababu kila siku unahitaji kuja na mbinu mpya na bora za kukuza biashara yako.

Katika hatua hii ndiyo unaweza kuchukua mkopo wa kibiashara, kwenye hizo hatua nyingine za nyuma kamwe usichukue mkopo, utajipoteza. Chukua mkopo ukishakuwa na biashara ambayo tayari ina wateja wanaokulipa kwa kile unachofanya.
Hizi ndizo hatua tano muhimu ambazo mtu yeyote anaweza kuzitumia kutoka chini kabisa mpaka kufikia kumiliki biashara kubwa na yenye mafanikio.

Maswali ya haraka haraka na majibu yake;

Swali
; je hatua hizi tano ni rahisi?

Jibu; hapana siyo rahisi hata kidogo, unahitaji kuweka juhudi kubwa sana, unahitaji kujifunza kila siku, unahitaji kuacha uvivu na unahitaji kubadili maisha yako moja kwa moja.

Swali; itanichukua muda kiasi gani kuanzia hatua ya kwanza mpaka hatua ya tano?

Jibu; ukiweka juhudi vizuri, ukajifunza vyema na kufanyia kazi yale unayojifunza, itakuchukua mwaka mmoja mpaka miwili. Ukiwa mzembe itakuchukua muda mrefu zaidi na hivyo utakata tamaa haraka. Ukitaka kufanya haraka zaidi ya hapo utashindwa kabisa.

Fanyia kazi hatua hizi tano kwenye biashara unayotaka kuanzisha kwenye maisha yako, na utajijengea biashara kubwa na yenye mafanikio. Muhimu ni uwe mvumilivu na ujitoe sana kwenye kile unachofanya. Usikate tamaa na jifunze kwa wengine ambao wamefanikiwa kwenye kile unachoanza kufanya wewe.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea ,
----
Kama wewe ni mjasiriamali au mfanyabiashara unaehangaika kupata wateja kutokana na ushindani basi naomba unisikilize kwa umakini sana, kwani katika makala hii nataka nikuonyeshe mbinu ambayo itakusaidia:-

  1. Kuua ushindani kwenye soko lako na
  2. Kuwafanya wateja wavutiwe kuja kununua bidhaa/huduma unayotoa kutoka kwako badala ya washindani wako.

Tofauti ya stretejia (mbinu) hizi mbili inatokana na mfano ambao ametoa wa mapapa wenye kutafuta samaki.

Anasema mfanyabiashara ni kama papa mwenye kutafuta eneo lenye samaki samaki kwa ajili ya kula. Na samaki ni mteja wa mfanyabiashara yule.

Papa huyo akigundua eneo lenye samaki na kuanza kula wale samaki, baada ya muda fulani atapita papa mwengine kuja kula samaki katika eneo lile.

Na baada ya muda atakuja mwengine na mwengine hadi itafika wakati papa hao wanakuwa wengi kuliko idadi ya samaki na wanashtukizia kuwa wanatafunana wenyewe kwa wenyewe hadi damu kumwagika na kufanya rangi ya ile bahari kuwa nyekundu, na ndio maana ikaitwa red ocean strategy.

Huo ndio mfano wa wafanyabiashara wengi.

Utakuta mtu anaanzisha duka lake. Mambo yake yanaenda vizuri na anaanza kupata wateja.

Mtu mwengine anaona ile biashara na kusema “Kumbe biashara ile inalipa! Wacha na mimi nianzishe duka langu.”,

Anaanzisha duka lake na kuingia kwenye ushindani na yule aliyefungua duka la mwanzo. Baada ya muda, mwengine nae anaanzisha duka lake na kuingia kwenye ushindani na wale wawili.

Inafika wakati mlolongo wa watu wanafungua biashara kama ile na wanaingia katika ushindani hadi wanafikia 20, 30 hali ya kuwa idadi ya wateja bado ni ileile.

Inafika wakati wanajikuta wapo katika ushindani na biashara zote zinakuwa zinaumia.

Lakini Blue Ocean Strategy inakufanya wewe kujichomoa katika eneo lile la bahari na kuenda katika eneo jengine ambalo halina mapapa na kuwavuta samaki kuja kwako.

Na kwa vile lile eneo ni lako na ushaweka bendera yako hata papa mwengine akija hawezi kushindana na wewe kwa sababu eneo lile unalifahamu vizuri na samaki wale wamevutiwa na wewe kuliko mapapa wengine.

Vipi unaanzisha Blue Ocean Strategy?

Kwanza unatakiwa kufahamu kuwa kuna aina mbili za wajasiriamali au wafanyabiashara ambao ni
  1. Generalist na
  2. Specialist
Generalist ni mfanyabiashara anayewalenga wateja wote na Specialist ni mfanyabiashara anayelenga kundi fulani tu la watu na anafanya hivyo kwa sababu anajuwa kuwa hakuna mtu mwengine kama yeye anayeweza kutatua matatizo ya kikundi hilo kama yeye.

Ingawa watu wengi wanaona ni bora kuwa generalist kwa sababu soko lake ni kubwa, kitu wasichokifahamu kuwa kuwa generalist haitaji taaluma kubwa na soko lenye taalum ndogo linakuwa na ushindani mkubwa kuliko soko lenye taaluma ndogo.

Lakini ukiwa specialist unakuwa na uwezo wa kuwanasa watu wengi kwa sababu wewe unaonekana kuwa ni mtaalamu mbele ya macho ya soko lako na watu wanakufata wewe na wapo tayari kukulipa pesa zaidi kuliko yule mtu ambaye anaonekana anafanya kila kitu (generalist).

Na mfano mzuri ni kama madaktari.

Daktari ambaye anatibu wagonjwa wote ni generalist (MD) na daktari ambaye ni specialist anaona wagonjwa wachache lakini analipwa pesa nyingi na super specialist analipwa pesa nyingi zaidi kuliko wote.

Na kama wewe unataka kuua soko lako basi huna budi kuwa specialist au hata super specialist.

Mfano mimi (Dr Said) nilivyoanza biashara yangu niliingia katika soko la web design ambalo lilikuwa na ushindani mkubwa.

Nilianza kuwatengenezea tovuti wafanyabiashara, lakini nikaona nikijiweka kama Web Designer watu watanifananisha na Web Designer wengine na kunihoji kuhusu bei zangu kuwa juu kulinganisha na web designers wengine.

Hivyo sikujiweka kama Web Designer, na hata nilipokuwa nawapigia simu nilikuwa nikiwaambia

“Hello! Kwa jina naitwa Dr. Said Said, ninawasaidia wafanyabiashara kama wewe kutumia tovuti kunasa wateja kwenye mtandao. Na sasa hivi natoa consultation ya bure ya saa 1. Je ungependa kupata consultation ya bure kujifunza namna unavyoweza kutumia tovuti yako kunasa wateja?”

Wengi walikuwa wanajibu kuwa wangependa kupata consultation hiyo.

Na mimi nikienda kule nawaonyesha njia wanazoweza kutumia kupata wateja kwenye biashara zao kupitia website (tovuti) na sio jinsi wanavyoweza kumiliki website yenye kupendeza.

Najua wateja wangu hawajali sana kuhusu kumiliki website nzuri kama wanavyojali kupata wateja kupitia website zao.

Kujiweka kwangu kama Specialist (Online Marketer) kumenisaidia sana kupata projects nyingi zenye thamani (Blue Ocean Strategy) badala ya kujitangaza kama web Designer ambayo ni Red Ocean fani yenye ushindani mkubwa.

Mbinu hiyo na wewe unaweza kuitumia katika biashara yoyote ile.

Tuchukulie mfano wa biashara ya tour:

Muda si mrefu nimetoka kupigiwa simu na mmiliki wa kampuni ya tour na anataka ushauri vipi aitumie website yake kupata wateja.

Kitu cha mwanzo nilichomwambia ni kujiposition vizuri kwenye soko kama specialist badala ya generalist, ushauri huohuo ambao niliokupa wewe nilimpa yeye.

Badala ya kusema sisi ni tour company ambao tunapokea wageni kutoka nje sema sisi tunaspecialise kuwasaidia kundi fulani la watu kupata jambo fulani.

Kwa mfano nina rafiki yangu ambaye yeye amejikita kwenye motorbike safari.

Anasema “Sisi tunashughulika na Adventure safari za Motorbike tu! Kama wewe hujui kuendesha pikipiki hapa sio kwako”.

Kwa haraka haraka unaweza kuona kuwa atapata wateja wachache lakini kwa vile hana ushindani, wateja anaowapata wanamtosha sana na anatengeneza pesa nzuri sana na anaweza kuweka chaji ambayo washindani wake hawawezi kuweka kwa sababu washindani wake hawafanyi motorbike safari.

Swali unalotakiwa kujiuliza nia nijiweke vipi kwenye soko kama mtaalam wa kitu fulani ili niwavute watu waje kwangu?

Siku zote angalia wateja wako wana matatizo gani na kitu gani maalumu utafanya.

Usijaribu kufanya mambo mengi . Chagua kitu kimoja tu cha kufanya.

Muhimu hilo tatizo liwepo katika soko na watu wachache waweze kutatua hilo tatizo. Kama wewe ni miongoni mwa hao wachache ambao wanaweza kutatua tatizo hilo basi nakuhakikishia utapata wateja wengi na utakuwa huna ushindani katika biashara yako.

Ifanyie kazi na unijulishe umefaidika vipi na mbinu hiyo.

Ni mimi mwenye kujali mafanikio yako,

Dr. Said Said
Mkurugenzi wa Online Profits

[Makala hii imechapwa na Abdallah Hemedi - Content Manager | Online Profits] .
----
Hapa tanzania, karibia Biashara 1000+ huanzishwa kwenye Mwezi ya January na Kufikia mwezi wa November, Karibia 85% ya hizo biashara hufeli.

Wengi wetu tuliwahi kuwa kweye hiyo 85% ya biashara zinazo feli. Na wengine tuko kwenye ile 15% ya wanaondeleza biashars kwa bahati au kwa kuwa tuna elewa tunachokifanya.

Kuna mambo kadhaa ambayo tunayafanya vibaya na hivyo kutufanya kuwa wale wale, kufanya biashara zetu zisitofautiane na wengine kwa kuwa tunaona matokeo ni yale yale.

Ukitambua Kosa liko wapi, na hata kama bado biashara yako inasonga; Kutambua nini kinakufanya uwe yuleyule itasaidia kukuza biashara yako kwa kiasi kikubwa.

Ukifanya yafuatayo, nakuhaidi utapata matokeo mazuri na kwa mda mfupi.

1. "Kama Huwezi Nunua Vyote Kwa Pamoja, Huwezi Kununua Kimoja Wapo!"

Uliwahi kuanza kupungukiwa bidhaa dukani na pesa iliyopo mfukoni haitoshi? Mfano unauza Madaftari, Michele, Sukari, Mafuta , Na mengineyo ila ukaishiwa Madaftari na Mafuta labda na Unga. Kama hutoweza kuvinunua vyote kwa pamoja, huwezi kununua kimoja wapo.

Namaanisha kwamba; Umeishiwa madaftari, mafita na unga; Ukasema ngoja uanze kununua Unga kwa kuwa hela uliyo nayo haitoshi, basi ukinunua unga ukianza kuuza pesa utakayoipata utanunua Mafuta...Na ukianz kuuza mafuta ndipo utanunua Madaftari.Ina maana kwamba kila pesa itakayokuwa inaingia inatumika na sio Kuhifadhiwa.

Je, unafanya nini ili kukwepa hali hii?

2.Matumizi Yasizidi Mapato.

Unaweza kuwa umeweka vitu vya Laki Tano Dukani(Ni Mfano) Ukiaanza kuuza. sasa ukaanza kuagiza Vitu vya Ziada ambavyo Bei yake itazidi ile uliyoingiza mda huo, Basi utakuwa umejiingiza kwenye mzunguko ambao utafanya Ufunge Duka; Madeni!

Inamana kila hela utakayopata Utaanza luitumia kulipia bidhaa ulizoagiza mwanzo na bado hizi zitaanza kuisha na huna hela ya kununua nyingine maana imetumika kulipia bidhaa za awali hivyo utaendelea kujikopa ili uendelee kuwa na vitu Dukani. Process itajirudia na huyokuwa na Faida jivyo utafunga Duka

Nacho jaribu kukwambia ni kuwa usifanye matumizi yakazidi mapato.Numua Vile Unavyoweza kununua Na kubaki na Faida ya awali!

3.Epuka Mikopo

Hakuna litu ambacho kinaonelana kirahisi kama kupokea mkopo kutoka kwa rafiki au benki ili uendelee kukuza biashara yako. Jambo hili uonelana jema kwa kuwa wengi uahidi Kuweka riba chache na wengine kukupa mda mrefu wa marejesho.

Kadri siku zitakavyoenda...ndipo uatakapo gundua kuwa huwezi tena kuingiza faida au kulipa mkopo kwa wakati kwa kuwa labda wateja ni kidogo ila / au mahitaji yanaongezeka kila kukicha.

Badala ya Mikopo unaweza kuchagua Crowd Funding. Hapa jamii inayo kuzunguka itakupa Hela (Labda kuanzia 10,000/ Kila Mtu) Na In Return watapokea Punguzo la kiasi fulani wakiwa wana nunua vitu kutoka Dukani mwako na Pumguzo litaendelea kwa mda gani.

Hii ni rahisi maana sio mkopo, huto warudishia pesa bali huduma ya.kipekee labda punguzo la asilimia fulani mpaka kiasi alichokupa kikiishia kwenye hayo mapunguzo na kuongeza kidogo tu!

Faida nyingine ni kuwa utajipatia wateja wa paop kwa papo..Kwa kuwa hawato nunua kwingine bali kwako ili wapate punguzo.

Shida ni kwamba luwapata watakao fanya hivyo mara nyingi ni ngumu.

Unaweza kusambaza Offer yako kwa Vipeperushi au kutoa tangazo kwenye Local Radio Station.

4." Mteja Huwa Sahihi Wakati Wote!"

Ili biashara yako kuwa ya kitofauti na za wengine utahitaji kumuondolea mteja kitu kinachoitwa "No Money Out" Syndrome...Hichi kila mtu anacho. Kumshawishi mtu kunua bidhaa kwako kila mara na kila siku ni jambo ambalo unapaswa kufanya ili kufanikiwa. Na njia rahisi ya kufanya hivyo ni kwa kumfanya ajisikie huru, na anae thaminiwa. Hapa ni kwa kumsikiliza na kuepuka mabishano.

5.Tenga Fungu La Matangazo

Itimisho.

Natumai kuwa baadhi ya njoa hizi ulikuwa huzifahamu. Na kama umefunguka Share na unao wapenda...Na soma makal nyinhine za Ujasiriamali.
 
Endapo una mtaji mdogo na unataka kuanza na kukuza biashara yako. Fanya yafuatayo;

1. JIPE MUDA, BIASHARA HAITAWEZA KUKUA HARAKA KAMA UNAVYOFIKIRI
Uzuri wa kuanza biashara na mtaji kidogo ni kwamba kila mtu anaweza kufanya hivyo. Lakini pia urahisi huu wa kuanza biashara kwa mtaji kidogo unafanya ukuaji wa biashara kuwa wa taratibu sana. Hivyo unapofanya biashara yoyote ambayo unaanza na mtaji kidogo ni muhimu ukajipa muda ili kuweza kukuza mtaji wako.

Usiwe na tamaa ya kutaka kukuza biashara hii haraka, unaweza kuingia kwenye maamuzi ambayo yatakugharimu zaidi. Endelea kufanya biashara yako huku ukijifunza zaidi na kuangalia kila fursa ambayo unaweza kuitumia kukuza biashara yako.

2. KUZA MTAJI WAKO TARATIBU
Kwa mtaji huo mdogo ambao umeanza nao biashara, endelea kuukuza kila siku. Usiendeshe biashara kwa kula kila kipato unachopata, badala yake tenga sehemu ya akiba irudi kwenye biashara yako.

Fanya hivi kwa nidhamu ya hali ya juu sana na unahakikisha kila unapopata faida sehemu inarudi kwenye biashara yako.

Pia endelea kuangalia kwa mazingira uliyonayo na kwa biashara unayofanya ni kwa jinsi gani unaweza kukuza mtaji wako zaidi. Kama utafikiria hili kila siku, hutakosa majibu ambayo yatakusaidia.

3. PUNGUZA GHARAMA ZA BIASHARA NA ZA MAISHA PIA
Kuwa kwenye biashara haimaanishi kwamba ndio una uhuru wa kufanya chochote unachotaka na fedha za biashara hiyo, kwa sababu tu ni zako. Wewe sasa upo kwenye wakati mgumu wa kukuza biashara yako huku ukiwa huna njia nyingi za kufanya hivyo.

Hebu kwa sasa punguza kabisa gharama zako za kibiashara na za maisha pia. Kama kitu sio muhimu sana basi usikigharamie. Punguza matumizi yote ambayo ni ya anasa tu na sio kwa ukuaji wa biashara. Katika kupunguza gharama zako za biashara na maisha, jijengee nidhamu nzuri sana ya fedha. Usitumie fedha kiholela tu, kuwa na mahesabu na sababu kwa nini umetumia fedha fulani, hasa kwa matumizi ambayo sio ya kawaida.

4. ANGALIA WATU AMBAO UNAWEZA KUSHIRIKIANA NAO
Baada ya kuiendesha biashara yako vizuri na ukaona inaenda kwa faida, unaweza kuangalia watu ambao unaweza kushirikiana nao kwenye biashara hiyo. Kuna watu wengi ambao wanaweza kuwa na mtaji lakini hawana muda wa kufanya biashara.

Lakini pia watu hawa wanataka mtu ambaye wanaweza kumwamini. Hivyo kama unaweza kuaminika angalia watu unaoweza kushirikiana nao kibiashara.

Andaa mpango mzuri ambao utamshawishi mtu ni jinsi gani yeye atafaidika kama atawekeza kiasi kidogo kwenye biashara yako. Ikiwa unaendesha biashara yako kitaalamu itakuwa rahisi zaidi kushawishi watu kushirikiana na wewe.

5. RASIMISHA BIASHARA YAKO ILI KUJIWEKA KWENYE NAFASI NZURI YA KUPATA MKOPO
Hata kama biashara yako ni ndogo kiasi gani, irasimishe. Iendeshe kisheria kwa kuwa na namba ya mlipa kodi na hata leseni pia. Hivi vitakuwezesha wewe kutambulika na taasisi za kifedha pale utakapohitaji msaada zaidi wa kifedha.

Mkopo kwenye taasisi za kifedha ni chanzo muhimu ila usikimbilie kama bado hujaweza kuiendesha biashara yako kwa faida. Hakikisha umeiweka biashara yako vizuri kwanza na inajiendesha kwa faida ili unapochukua mkopo unajua unauweka wapi na kuendelea kupata faida zaidi.

Kuikuza biashara pale ambapo umeanza na mtaji kidogo ni kitu ambacho kinawezekana. Ila unahitaji kujitoa na kujenga nidhamu kubwa. Unahitaji kufanya kazi zaidi ya wafanyabiashara wengine, unahitaji kuwa mbunifu wa hali ya juu na pia unahitaji kujijengea uaminifu.

Ukishajua wewe biashara yako ni ndogo na inahitaji kukua, basi hakikisha kila mara unaumiza akili yako ifikirie njia zaidi za kuikuza. Na kama utaweza kufanya hivi basi utaziona fursa nyingi zilizokuzunguka za kuikuza biashara yako.
 
Back
Top Bottom