BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,789
- 288,020
Edward Hosea awashambulia wabunge
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
Wabunge waja juu, wahoji uadilifu wake
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Edward Hosea, jana aliwashambulia wabunge katika semina ya kukabiliana na rushwa iliyoandaliwa na taasisi yake na kuwashirikisha wabunge wa Chama cha Kupambana na Rushwa (APNAC).
Akitoa mada katika semina hiyo, Dk. Hosea aliwashambulia wabunge hao hadharani, kwamba wamekuwa wakichangamkia posho za semina wakati hakuna uwajibikaji.
Katika mada hiyo iliyoonekana dhahiri kuwakera wabunge hao, Dk. Hosea alisema baadhi yao wamekuwa wakihudhuria na kusaini posho zaidi ya tatu katika semina tofauti kwa siku moja, huku wakishindwa kuwajibika, jambo ambalo alisema ni aina mojawapo ya rushwa.
Wapo wabunge wanaohudhuria semina zaidi ya tatu kwa siku moja na kusaini posho, lakini hata baada ya kuwezeshwa kwa posho hizo, hakuna uwajibikaji. Kwa kweli kuna mambo mengi yanayotokea, lakini tunayafumbia macho, alisema Dk. Hosea.
Mbali na kusaini posho kwenye semina tatu kwa siku, Dk. Hosea pia alisema wapo wabunge ambao wanatumia vibaya ubunge wao kwa kutokaa kwenye foleni wawapo sehemu za huduma kama benki.
Pia aliwapasha wabunge kuwa hivi sasa siri nyeti za serikali ziko wazi, na kwamba inatokana na ukosefu wa maadili miongoni mwao.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kutoa mada hiyo, baadhi ya wabunge walionekana dhahiri kukerwa na mada hiyo na kutaka kujibu mapigo kwa kuhoji utendaji wa taasisi hiyo na mafanikio yake tangu ilipoanzishwa.
Mbunge wa kwanza kutoa dukuduku lake, alikuwa Dk, Raphael Chegeni (Busega-CCM) ambaye alihoji utendaji wa TAKUKURU na kueleza kutoridhishwa kwake.
Dk. Chegeni alianza kujibu mapigo kwa kuhoji uwajibikaji wa Dk. Hosea na taasisi yake kuwa, iliwahi kuchunguza kashfa ya zabuni ya kampuni ya kufua umeme wa dharura, Richmond, na kuitangazia jamii kwamba hakukuwa na rushwa katika zabuni hiyo.
Kama hiyo haitoshi, Dk. Chegeni alisema TAKUKURU pia ilishindwa kuchunguza kashfa ya minara pacha ya majengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na badala yake Kampuni ya nje ya Ernest & Young ilibua ufisadi mkubwa na hatimaye leo baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge, Dk. Chegeni alihoji ujenzi wa gharama wa ofisi za TAKUKURU nchini pamoja na magari ya kifahari wanayotumia wakati haiwajibiki ipasavyo katika kukabiliana na rushwa.
TAKUKURU mnawajibika nini? Mlisema kwenye Richmond hakuna rushwa, lakini baadaye Bunge lilibaini kuwapo kwa rushwa, kwenye ujenzi wa minara pacha ya BoT mmeshindwa kuchunguza hadi kampuni ya nje ndiyo iliyokuja kuibua kashfa hiyo, alisema Dk. Chegeni.
Kutokana na hoja hiyo, Dk. Hosea alikuja juu na kuwataka wabunge hao kuacha kuhoji mambo hayo, kwani wakianza kuchambuana, hakuna atakayebaki salama.
Hapa hatukuja kulumbana, tumekuja kwenye semina, si mahala pake, lakini nyie wabunge ndio mlioamua kupitia Kamati Teule ya Bunge na mapendekezo yenu yapo, kwa hiyo iulizeni serikali, lakini hatuko hapa kushambuliana, alisema Dk. Hosea.
Hata hivyo, baada ya malumbano hayo makali, wabunge na maofisa wa TAKUKURU, waliendelea na semina yao inayofanyika katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, inayotarajia kumalizika leo.